Nikiwa kama mjukuu kipenzi wa bibi yangu, huwa napenda sana kutumia
muda wangu wa mapumziko kujadiliana naye mambo mbalimbali yanayohusu
jamii, iwe yaliyokuwa yanatokea hapo awali au yanayoendelea kutokea.
Ilikuwa ni siku ya jumapili baada ya kutoka kwenye mihangaiko, niliingia
ndani na kumuita bibi kwa jina lake la utani ‘Nyaksi’ ili twende nje
tukapunge upepo na mazungumzo ya hapa na pale.
Kama ilivyo ada yangu, huwa napenda sana kutafiti mambo
mbalimbali, nikamuuliza bibi, eti bibi nimewahi kusikia kuwa wakati wa
enzi zenu mlikuwa hamruhusiwi kula mayai wakati wa ujauzito kwa kuwa
mtoto atazaliwa bila nywele? Bibi Nyaksi huku akitabasamu akanigeukia na
kusema, "umeshaanza, kwanza usikumbushe enzi zile bado nipo mbichi"
akimaanisha wakati yupo msichana. Wote tukatabasamu kwa pamoja. Nyaksi
akaendelea kusema sio mayai tu, bali vyakula vyote nyenye virutubisho
kwa wingi ambavyo ninyi vijana wa leo mnaviita ‘purotini’, akiitamka
protini kwa lafudhi ya kizee. Nyaksi alisema tulizuiliwa kula vyakula
hivyo kwa mlengo wa mwiko, akaendela kusema, unajua Babu (jina langu
alilopenda sana kuniita Nyaksi) wazee walitumia mwiko ili kututisha
lakini ukweli ni kuwa wakati ule hakukuwa na tekenolojia (akimaanisha
teknolojia) hivyo kama utakula vyakula vyenye virutubisho sana
vitamfanya mtoto awe mkubwa, na hivyo kama utashindwa kujifungua kwa
njia ya kawaida basi hakutakuwa na njia nyingine ya kukusaidia. Nyaksi
akaendelea ninyi vijana wa siku hizi mna raha, hospitali nyingi,
madaktari wengi huku mna njia nyingi mbadala ikiwemo ya upasuaji na
nyinginezo.
Nilimuacha Bibi Nyaksi amalizie maneno yake, halafu nikamuuliza,
kama sisi tuna teknolojia na njia nyingi za kisasa, sasa inakuwaje urefu
wa maisha wa vizazi vyetu unazidi kupungua kadri teknolojia inavyozidi
kukua? Nyaksi alicheka sana, huku akipigapiga makofi ili kuvuta hisia
alisema " hakuna kizuri kisicho na kasoro". Baada ya hapo tukaacha
kuongelea masuala ya afya na kuketi chini ili kupunga upepo uliokuwa
ukivuma kwa kasi kutokea Kinyanyiko.
Kipindi chote naburudika na upepo uliokuwa unavuma ukitokea kwenye
mabonde ya Kinyanyiko nilikuwa natafakari mambo mengi kuhusu maneno ya
Nyaksi. Misemo yake ilikuwa inazungukazunguka kichwani kwangu , huku
maneno "Hakuna kizuri kisicho na kasoro " na " ninyi mnaishi kwenye
ulimwengu wenye tekinolojia" vikijitokeza mara kwa mara. Lakini je, hizi
teknolojia zinatunufaisha vipi? Zipi faida na hasara zake? Hivyo nikawa
nachorachora chini nikiainisha viambatanishi vyote vya hii tunayoiita
teknolojia, nikarudi haraka nyumbani na kuchukua iPad yangu kuanza
kuandika makala hii ambapo tutaiangalia teknolojia kwa mapana na jinsi
gani teknolojia inavyoweza kuongeza ufanisi katika medani ya afya.
Teknolojia ni nini?
Teknolojia ni utengenezaji,matumizi,maarifaya
vifaa,machine,mitambo,uashi ili kutatua tatizo au ketenda kazi husika,
iwe ni kwenye matibabu au kwenye michezo. Katika makala yetu ya leo
tutaangalia sana hii teknolojia ya mawasiliano ya mtandao yaani ICT. Kwa
wale maveterani kama mimi mtakumbuka teknolojia hii ilianza kuibukia
kwa kasi sana nyumbani katika miaka ya tisini, katika wakati huo
teknolojia hii siyo tu ilionekana kuwa ni kitu cha anasa bali pia ni kwa
wenye nazo tu. Teknolojia hii ilihusishwa na viashiria chungu mzima
kama kwenda na wakati, usomi, umjini n.k. kitu ambacho kimetufikisha
hapa tulipo.
Mtazamo wa jamii juu ya teknolojia
Kama nilivyoelezea hapo juu, asili na historia juu ya ujio wa
teknolojia hii ya mawasiliano ya mtandao inachangia sana katika
ujengekaji wake, kwa mfano hapa kwetu wengi bado wana mtazamo hasi kuwa
teknolojia hii ni kwa ajili ya wasomi au wenye uwezo, ingawa dhana hii
inaendelea kubadirika siku hadi siku, lakini tatizo bado lipo. Nani wa
kulaumiwa? Ni wanajamii au sisi wana mawasiliano? Jibu ni fupi. Hakuna
wa kulaumiwa bali hatuna budi kutafakari juu ya namna ya kuliboresha na
kulihalisisha kwa jamii yetu.
Muundo wa teknolojia kwenye karne ya 21
Katika makala yake ya sababu za watoto wachanga kulia,
Dk Paul Mwanyika amefafanua
kwa undani hatua ambazo mtoto hupitia katika ukuaji, kwa muktadha
huohuo nami naufananisha ukuaji wa teknolojia na ule wa mtoto. Kwa
ufupi, teknolojia imepitia hatua nyingi. Kwa mfano hapo zamani
teknolojia ilikuwa ni kwa ajili ya kurahisisha kazi au utendaji, lakini
leo hii teknolojia imegeuzwa kuwa sehemu ya kazi na siyo tena kitendea
au kirahisisha kazi.
Si kitu cha kushangaza kusikia mtu anauza madawa mtandaoni
(online) bila kuwa na duka nje ya mtandao (
brick shop).
Aidha leo hii madaktari wanaweza kupata muongozo au kushiriki kwenye
upasuaji bila kizuizi cha umbali. Huu ndiyo muundo wa teknolojia ya
sasa, tunatumia teknolojia kama huduma/kazi
(Technology As A Service) na siyo tu kitendea kazi.
Faida/Matumizi za teknolojia kwenye Afya
Lengo la makala hii ni kuwaamsha (kumbusha) wanajamii umuhimu au
njia mahususi za kutumia teknolojia katika kujenga afya bora. Msukumo wa
makala hii umekuja kutokana na matokea ya utafiti
niliyofanya kwenye tovuti ya TanzMED.com. Ndani ya tovuti hii kuna
sehemu ambayo mtumiaji anaweza kujisajiri akawa anapokea taarifa
mbalimbali kuhusiana na afya (milisho ya afya). Nilichogundua ni kuwa
uwiano wa wanaojisajili kwa wanaotembelea ni chini ya 1%. Baada ya
kuwauliza watembeleaji wengi kwanini hawajisajili, karibu 20% walisema
hawafahamu jinsi ya kutumia njia hiyo, wengine 20% hawajui uwepo wa
programu hii na waliobaki ni kutotambua umuhimu wa kufanya hivyo. Hii ni
sehemu ndogo tu ambayo matumizi ya teknolojia yanaweza kukurahisishia
kujenga afya bora.
Hivyo tuangalie kwa kila kundi ni jinsi gani linaweza kunufaika na teknolojia.
Madaktari
Wakiwa ndio watendaji wakuu, ni dhahiri kuwa madaktari ni moja ya
watu wenye heshima kubwa sana kwenye jamii yetu. Wengi tumekuwa
tukiwaamini na kuwakubali madaktari kwa kiwango kikubwa zaidi. Leo hii
kuna mitandao jamii kama Facebook, Twitter na hata TanzMED.com
(Jumuiya), kwa kutumia mtandao jamii daktari anaweza kuwasiliana na
wanajamii akawapa mustakabali wa masuala ya afya, kwa mfano nimewahi
kuona vipachiko kadhaa vya
Dk Fabian Mghanga kwenye
Facebook,
akiwa anapachika mambo yaliyo motomoto kwenye jamii yetu kwa sasa,
wanajumuiya wote wanaomfuata huweza kuona vipachiko vyake na
kubadilishana naye mawazo au kutolea maoni. Si hayo tu daktari pia
anaweza kutumia programu za mawasiliano kubadilishana mawazo
(kuchat) na
wagonjwa walioruhusiwa ili kufuatilia hali zao na kuwafariji. Vilevile
daktari anaweza kutumia simu kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa wagonjwa
walio hospitali akiwakumbusha kunywa dawa na kufanya mazoezi ya asubuhi
au jioni. Wagonjwa watafarijika sana endapo wanapokea ujumbe toka kwa
daktari unaomsisitizia jambo fulani. Hivyo muda umefika sasa kwa
madaktari wetu kubadirika na kuanza kutumia fursa hizi ambazo
zinawezekana na kupatikana kwenye mazingira yetu ya Tanzania.
Chukulia mfano, kwanini mahospitali yasichukue namba za simu za
wagonjwa wote na kuzipanga kulingana na aina ya magonjwa yao halafu
wakawa wanawatumia ujumbe au taarifa mbalimbali zinazohusu maendeleo au
tahadhari muhimu juu ya magonjwa yao?
Vyombo vya habari & Wasanii
Hii ni moja ya sehemu ambazo zina ushawishi na upenzi mkubwa mno
kwenye jamii. Katika baadhi ya nchi zilizoendelea, unaweza kukuta uwepo
wa televisheni au redio zinazohusu masuala ya afya pekee. Kwa nchi kama
Tanzania wamiliki wa hizi televisheni, magazeti au redio wanaweza
kutumia vituo vyao kufikisha maarifa, ufahamu na hata ujumbe juu ya
afya. Kwa kushirikiana na watu maarufu na wasanii dhana hii inaweza
kukubalika na kufika mbali zaidi.
Makampuni ya teknolojia
Makampuni yanayojihusisha na mawasiliano ya mtandao, kuanzia
makampuni ya simu, watengeneza programu nk, yanatakiwa kushirikiana na
wadau wa medani ya afya katika kuhakikisha wanainufaisha jamii. Kwa
mfano kampuni ya Dudumizi Solutions imejiunga na kundi la madaktari na
kuanzisha mtandao wa Afya ujulikanao kama
www.tanzmed.com. Hii
ni chachu na changamoto kwa wadau kuonesha kuwa sasa teknolojia ni
sehemu ya jamii hivyo tunatakiwa kujihusisha zaidi, tubadilishe utendaji
au mfumo wa teknolojia. Kwa mfano makampuni ya simu yanaweza kuja na
programu ambazo zitawawezesha wanajamii kutuma namba fulani halafu
wakapata elimu au taarifa fupi za masuala ya afya (kama ile inayofanya
kwa mama wajawazito). Aidha wataalamu wa programu wanaweza kuja na
programu inayoweza kutumika kwenye simu kumuwezesha mtu kukokotoa afya
yake (BMI Calculator), kujua siku ya kujifungua nk, hii ni mifano
michache ambayo wadau wa ICT wanaweza kuitumia kujenga jamii yenye afya
njema. Nimeongelea kwa ufinyu wake kutokana na hali halisi ya maendeleo
ya ICT kwa nchi yetu ingawa tunaweza kwenda mbali zaidi ya hapo.
Wanajamii
Wakiwa ndio walengwa namba moja, wanajamii wanatakiwa kuanza
kutumia teknolojia kama sehemu ya kujenga afya yao. Kwa mfano unaweza
jiunga kwenye milisho
(Subscription) ya tovuti mbalimbali za
afya ambapo utakuwa unapokea taarifa mbalimbali za afya kama; mabadiriko
ya hali ya hewa, magonjwa ya milipuko, kinga na mengineyo. Mara nyingi
makala hizi huwa zinachujwa kuhakikisha unatumia taarifa inayojieleza.
Hivyo jijengee mazoea ya kutumia teknolojia kwa ajili ya afya yako, iwe
kuuliza maswali juu ya afya au kusoma dalili na kinga za magonjwa
mbalimbali. Mtandao wa
www.tanzmed.com una yote haya kwa ajili ya afya yako.
Nilipomaliza kuainisha
baadhi ya faida za teknolojia, kuna maneno ya Bibi Nyaksi yakawa
yaniumiza," Hakuna kizuri kisicho na kasoro". Hivyo tuangalie athari za
hii teknolojia.
Kuvunja maadili na mipaka ya teknolojia
Kutokana na ujio wake, wengi wamekuwa wakitumia teknolojia bila
mipaka. Maadili ya teknolojia yamepigwa kumbo. Kwa mwandishi wa TanzMED
Dk Fabian Mghanga ameeleza
jinsi gani dawa za kuongeza makalio zinavyoshabikiwa, huku zikiwa
hazina maelezo ya kuridhisha juu ya matumizi na namna zinavyofanya kazi.
Ushabiki huu pia huchochewa sana na matumizi ya mitandao jamii kama
vile Facebook, ambapo baadhi ya watu hutuma matangazo au picha zenye
mvuto na kuwafanya akina dada wengi wahamasike kwa kutaka kuwa na mvuto
kama waliouona kwenye picha. Si hayo tu, tumeona pia jinsi mwandishi
Dk Henry Mayala alivyotuelezea
jinsi vumbi la viwandani linavyoweza kukusababishia pumu au magonjwa ya
mfumo wa hewa, haya yote ni kwa sababu ya kuvukwa kwa mipaka ya maadili
ya teknolojia kwa watoa huduma. Uvukaji wa mipaka siyo tu kwa
watengenezaji (watoa huduma) za teknolojia bali pia kwa wanajamii. Kwa
mfano katika makala yake ya kupungua kwa hamu ya kufanya mapenzi
Dk Khamisi Bakari amesema
sababu mojawapo ni matumizi ya intaneti kwa muda mrefu, hii ni
inatuonesha mifano dhahiri ya athari zinazosababishwa na utokaji nje ya
maadili ya teknolojia kwa mtumiaji. Hivyo maadili ya teknolojia ni
lazima yaheshimiwe.
Maadili na mipaka ya kazi
Nakumbuka kuna wimbo mmoja wa wanamuziki wa kizazi kipya wanaoitwa
Wagosi wa Kaya uitwao
wauguzi kuna
kipande cha mstari kinasema; "...nesi anaongea kwa simu na bwana wa
kizigua". Hii ni moja ya athari za teknolojia. Kuna wakati unatamani
hata upigane, maana unaenda hospitalini huku kuna foleni kubwa inasubiri
kumuona daktari, lakini yeye yupo
bize kwenye simu akicheka
kuhusu matokeo ya mpira wa jana. Hapo sizungumzii muda wanaotumia
kuangalia picha na maoni kwenye Facebook au kuchat kwenye Yahoo na
rafiki yake aliye Wuhan. Idara husika lazima iweke mipaka na maadili ya
kazi yatakayomuongoza muhusika katika matumizi ya teknolojia. Tukumbuke
kuwa teknolojia sasa imekuwa ni kazi na maisha hivyo haiepukiki.
Wakati namalizia haya maneno ya mwisho chaji nayo ikawa imeisha
kwenye iPad yangu, ni bahati mbaya kwamba jana sikuichaji kutokana
kukatika kwa umeme. Sasa basi inanibidi kusubiri umeme urudi ili niweze
kuichaji na kumalizia makala hii ambayo nitaituma kwenye jarida lijalo,
makala ambayo itazungumzia mambo ambayo ningependa kuishauri
jamii/serikali ifanye ili kujenga na kudumisha afya bora kwenye karne
hii ya teknolojia
Chanzo:
INGIA HAPA