Mtayarishaji

Morning Star Radio

Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Maliasili Zetu.. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Maliasili Zetu.. Onyesha machapisho yote

Jumanne, Julai 29, 2014

JIWE LA THAMANI BAHARINI


Ndani ya bahari samaki-gamba mkubwa sana anasonga polepole kati ya miamba, akila magugu-maji yanayoyumbishwa na mikondo ya bahari. Gamba lake la nje lililofunikwa kwa asidi na viumbe vidogo vya maji, hufanya isiwe rahisi kuona rangi zake nyangavu, yaani, rangi tofauti-tofauti za bluu, kijani, na zambarau zilizochangamana na manjano na waridi, na sehemu ndogo zilizo na rangi ya dhahabu na fedha.


Kiumbe huyo wa kushangaza ni paua, wa jamii ya moluska anayepatikana New Zealand peke yake. Kiumbe huyo na viumbe wengine wa jamii hiyo wanaishi chini ya maji karibu na pwani zenye miamba. Ingawa paua anapendwa kwa sababu ya rangi za kupendeza za gamba lake la ndani linaloweza kutumiwa kutengeneza vito maridadi, watu wengi wanapenda nyama yake tamu. Kwa kuongezea, lulu zenye kung’aa sana zinaweza kukuzwa ndani yake.


Kuna jamii zaidi ya 100 za moluska ulimwenguni pote zinazopatikana Afrika Kusini, California huko Marekani, Japani, Australia, na katika kisiwa cha Guernsey kilicho kwenye Mlango-Bahari wa Uingereza. Hata hivyo, katika eneo la kusini la bahari ya Pasifiki Kusini ndiko tu unaweza kupata moluska mwenye rangi nyangavu wa New Zealand, anayeitwa paua (Haliotis iris).


Muujiza wa Kibiolojia


Ndani ya gamba la paua, matabaka ya protini na kalisi hukusanyika na kutokeza rangi maridadi kama jiwe la thamani linaloitwa opali. Kwa sababu hiyo, paua amejulikana kuwa jiwe hilo la thamani la baharini. Kiwango cha joto baharini kinaposhuka, moluska hulala. Kisha matabaka ya magamba yao huchukua muda mrefu zaidi kukua. Mtaalamu mmoja anaamini kwamba rangi mbalimbali za paua huenda zinatokana na virutubisho katika maji na pia rangi mbalimbali za magugu-maji ambayo moluska hula.


Paua huchagua chakula chao kwa uangalifu na vilevile wao huchagua wataishi karibu na nani. Hawawezi kuishi karibu na mwanamizi mwenye miiba, au kina, kwa sababu wanakula aina zilezile za magugu-maji. Pia, kiti cha pweza ni adui hatari kwani wachache tu kati yao wanaweza kumaliza familia nzima ya paua. Kwa ujanja, kiti cha pweza huwekelea mnyiri kwenye mashimo ya kupumulia ya paua na hivyo kufanya asiweze kupumua. Kisha, paua anapoanguka kutoka kwenye jiwe alilolalia, kiti cha pweza humla kwa urahisi.


Matumizi Mbalimbali ya Paua


Ingawa sehemu nyeusi ya nje ya paua haipendezi sana, kwa karne nyingi wenyeji wa New Zealand wanaoitwa Wamaori wamekula paua. Sehemu inayoweza kuliwa ya paua ni musuli mkubwa, au mguu, ambao kiumbe huyo hutumia kusonga kwenye miamba. Pia Wamaori wametumia gamba lake katika mapambo na kama chambo cha kuvua samaki. Wametengeneza vito kwa kutumia magamba yake na wameyatumia kama macho katika michongo yao.


Sasa paua anapendwa sana kuliko wakati mwingine wowote. Watalii hawakosi kununua vito vya paua wanapotembelea New Zealand.


Leo, watu wanaopiga mbizi bila vifaa vya kupumua, wanawavua paua kwa wingi sana. Hiyo imekuwa biashara inayoletea New Zealand dola milioni nyingi sana kutoka kwa nchi za nje. Ili kuhakikisha kwamba paua hawaangamizwi huko New Zealand, serikali imeweka kiwango cha paua wanaoweza kuvuliwa kwa mwaka. Nyama nyingi hutiwa katika mikebe ili ikauzwe huko Asia, na nyingine hugandishwa na kutumwa Singapore na Hong Kong ambako paua wanapendwa sana ingawa wanauzwa kwa bei ghali sana. Mara nyingi, analiwa akiwa mbichi na kukatwa vipande-vipande. Ingawa kuna paua wengi sana huko New Zealand, wenyeji wengi hawajawahi kuonja nyama yake kwa sababu ya kuuzwa sana katika nchi za nje.


Ili waweze kutosheleza uhitaji wa kimataifa wa paua, wafanyabiashara wanatumia mbinu za kisasa kuwafuga. Wafanyabiashara huko Australia, Japani, na Marekani wamefaulu kutumia mbinu hiyo ili kufuga moluska wengine. Mbinu mpya kama hizo zimesaidia paua wafugwe katika matangi yenye mifumo ya kudumisha kiwango kinachofaa cha joto mbali sana na maeneo wanayopatikana kwa ukawaida.


Paua wa kufugwa wanakula kwa kiasi kilekile kama wale wa kiasili. Kila juma wanaweza kula chakula chenye uzito sawa na nusu ya uzito wao. Kwa kushangaza, paua pia wanaweza kusonga haraka. Wanapopinduliwa, wanaweza kujigeuza upesi sana. Ni kazi rahisi kufuga paua. Mtaalamu mmoja anasema kwamba “inafurahisha kufuga paua kwa sababu ni wapole na wenye adabu, na hawawasumbui wafugaji!”


Lulu za Paua


Zaidi ya kutokeza vito vinavyotengenezwa kutokana na magamba yao na kutumiwa kama chakula, paua wanaweza pia kutokeza lulu zenye kung’aa. Ni vigumu kupata lulu za asili katika paua wanaoishi baharini. Lakini wanaweza kutokezwa kupitia mbinu iliyobuniwa katika miaka ya 1890 na mwanasayansi Mfaransa Louis Boutan. Kito chenye umbo la yai kilicho na rangi za kuvutia kama za gamba la paua hutokezwa. Mbinu hiyo hufanya kazi jinsi gani?


Vipande vya udongo, mbao, mfupa, au chuma, huwekwa ndani ya gamba la paua katika sehemu tatu, yaani, mara mbili kwenye upande na mara moja mgongoni. Pole kwa pole, paua hufunika vipande hivyo vilivyoingizwa ndani ya gamba lake kwa matabaka ya lulumizi, yaliyotengenezwa kwa kalisi kaboni, na conchiolin. Kwa angalau miezi 18, maelfu ya matabaka hutokezwa na kufanyiza lulu ndogo. (Ona sanduku lililo chini.) Inachukua miaka sita ili kufanyiza lulu kubwa. paua 1 hivi kati ya 50 hutokeza lulu ambayo imekaribia kuwa kamili. Hii ni lulu laini, yenye rangi nyangavu, na inayong’aa kwa kustaajabisha.


Bado watafiti hawajafaulu kutokeza lulu yenye umbo la mviringo kutoka kwa paua. Hiyo ni kwa sababu, tofauti na chaza, paua ana musuli katika tumbo ambao hutema kitu chochote kinachowekwa katika mfumo wake wa kumeng’enya. Huenda siku moja mtu akagundua siri ya kutokeza lulu ya mviringo.


Kwa sasa, tunaweza kufurahia vitu tunavyopata kutoka kwa samaki-gamba huyu aliye na matumizi mengi, yaani, vito vyenye kupendeza, nyama tamu, na gamba lenye rangi maridadi. Je, hatumshukuru Mungu kwa kutupa zawadi yenye kupendeza kama hiyo?—Yakobo 1:17.

Jumamosi, Novemba 16, 2013

KUKOMESHA MAUAJI YA TEMBO


Tumekuwa tukisoma na kuangalia habari tofauti kuhusu tembo wanavyouwawa na pembe zao kuchukuliwa. Ujangili dhidi ya tembo umeshamiri licha ya kauli mbalimbali kutoka katika vyombo tofauti vya kitaifa na kimataifa za kusimamisha mauaji hayo zinazotolewa.

Tanzania inaoongoza kwa uuzaji nje wa pembe za ndovu.
Inakadiriwa kuwa wastani wa tembo 10,000 huuwawa kila mwaka nchini Tanzania.

Je, nini ni chanzo cha kuuwawa kwa tembo hao?

Huku tukipambana na jinsi ya kumaliza mauwaji ya tembo wetu,soko la pembe za ndovu limekuwa likishamiri huko Asia(China).Pembe za ndovu ambazo si halali zikifanikiwa kuingia nchini China basi hugeuka kuwa halali.

Kwa mtazamo wangu nadhani vitaa hii inabidi ipiganiwe pande zote yaani ni jinsi gani tutakomesha uwindaji huu haramu nchini mwetu na pili ni jinsi gani tutashughulika na wanunuzi wa pembe haramu.
Nadhani hapa ndipo penye changamoto zaidi kwani kunapokuwa na mwanya katika sheria ndipo watu hufanya yao.Kama wanunuzi wangebanwa na sheria za manunuzi ya pembe za ndovu sidhani kama ujangili huu ungekuwepo kwa kiasi hiki tunachoona sasa. Ni vizuri kukawa na sheria za kitaifa na kimataifa zisizokinzana katika kutekeleza hili. Kwa kufanya hivi tunasuru si tembo tu bali maliasili yote kwa ujumla.


Kukamatwa kwa vipande saizi ya 700 za pembe za ndovu inaonyesha jinsi gani uzao wa mnyama huyo asiye na hatia unavoelekea kumalizwa nchini.Inasikitisha na kutia hasira.Hivi tutavieleza nini vizazi vijavyo?

Tumeona wachina waliokamatwa na pembe za ndovu walivyojiamini na kuja kukusanya pembe nchini kwetu kama vile hakuna sheria.Wameonyesha jinsi gani walivyojihalalishia ukusanyaji wa nyara hizo.Watu wetu wakimatwa na madawa ya kulevya kwao wanawanyonga au kuwafunga kifungo cha muda mrefu,sisi tutawafanya nini hawa tuliowakamata?Sheria zetu zinasemaje?

NINI KIFANYIKE KUTOKOMEZA BIASHARA YA MENO YA TEMBO?

Hili ni swala la kuingizwa katika katiba mpya (kama halipo) kuwa atakayeshikwa na nyara za serikali ,au kujihusisha na uwindaji haramu ahukumiwe kama mhaini iwe ni raia au siyo na tusikubali kubadilishana wafungwa(extradiction) wa aina hii.

Sijui sheria yetu inasemaje kuhusu kukamatwa na nyara ila hawa Wachina inabidi wawe somo kwa wawindaji na wanunuzi haramu wengine wote kwani wamekutwa na kielelezo mikononi mwao.Kikubwa wautaje mtandao wao ili sheria ichukuwe mkondo wake.

Watanzania tuisaidie serikali yetu katika kutokomeza tatizo hili.Nina imani kuwa wapo wanaowajua watu wanaojishughulisha na biashara hii haramu.Tuwe na moyo wa uzalendo katika kulinda maliasili zetu.

Kingine "tugomee kununua bidhaa zote zilizotengenezwa kwa pembe za ndovu!Tukigoma kununua bidhaa mauwaji ya tembo yatakwisha.

Maelezo kwa hisani ya Rainbo-tz