Mtayarishaji

Morning Star Radio

Ijumaa, Juni 29, 2012

UWEZO WA NENO



“Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.” 2 Timotheo 3:16-17. Katika Neno la Mungu kimo kila kitu cha muhimu kiwezacho kumkamilisha mtu wa Mungu. Ni kama nyumba ya hazina iliyojaa bidhaa bora sana na za thamani.

“Lenye pumzi ya Mungu,” “ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu” (fungu la 15), na kumfanya mtu wa Mungu, “awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema,” Kitabu hiki kipitacho vitabu vyote kina madai ya juu kabisa kwetu ili tupate kukiangalia kwa kicho. Kukisoma kwa juu juu tu hakuwezi kukidhi [kutosheleza] madai ambayo kinayo juu yetu, wala kutupatia sisi manufaa yanayoahidiwa humo.
 
Tungejitahidi kujifunza maana kamili ya lile Neno la kweli, na kuinywa kwa kina roho ile iliyomo ndani ya Mausia hayo Matakatifu. Kusoma kila siku idadi fulani ya sura, au kukariri kiasi fulani cha Maandiko kilichowekwa , bila kutafakari kwa makini maana ya fungu hilo, kutaleta faida ndogo sana. Kujifunza kifungu cha maneno kimoja mpaka maana yake imekuwa wazi mawazoni mwako, na uhusiano wake kwa mpango ule wa wokovu uwe unaonekana wazi, kuna manufaa sana kuliko kusoma sura nyingi bila kuwa na lengo lo lote linaloeleweka, wala kupata mafundisho yo yote yanayokujenga.

Hatuwezi kupata hekima toka katika Neno la Mungu bila kuwa na bidii ya dhati na maombi katika kujifunza kwetu. Ni kweli kwamba sehemu fulani za Maandiko zi wazi mno kuweza kukosewa; lakini ziko nyingine nyingi ambazo maana yake haiwezi kuonekana upesi kwa kuziangalia kwa haraka, maana ile kweli haiwi juu. Ili kuelewa maana ya vifungu vya maneno kama hivyo, ni lazima kulinganisha andiko na andiko; ni lazima pawepo na utafiti wa makini na kutafakari kwa moyo wa maombi. Kujifunza kama huko kutalipwa maridhawa. Kama mchimba machimbo anavyozigundua tabaka za thamani za madini zilizofichwa chini ya uso wa nchi, ndivyo yule anayeendelea kwa bidii kulichunguza Neno la Mungu kama hazina iliyositirika, atakavyoweza kuziona kweli zile za thamani sana, ambazo zimefichwa kwa mtafutaji mzembe.

Lakini mafundisho hayo matakatifu ya Neno la Mungu usipoyafanya kuwa kanuni na mwongozo wa maisha yako, kweli hiyo itakuwa si kitu kwako. Kweli inafaa tu wakati ule inapotekelezwa kwa matendo katika maisha yako. Kama Neno la Mungu linaishutumu tabia yako moja unayoipenda, hisia yako unayoitunza moyoni mwako, roho uliyoidhihirisha, basi, wewe usigeuke na kumpa kisogo mshauri wako huyo mtakatifu [Neno la Mungu], bali uupe kisogo uovu ule unaoufanya na kumruhusu Yesu kukusafisha na kukutakasa moyo wako. Ungama makosa yako, na kuachana nayo kabisa na kwa nia thabiti, ukiziamini ahadi za Mungu, na kuonyesha imani yako kwa matendo yako. 

Kama kweli za Biblia zinafumwa pamoja na matendo ya maisha yako, basi, zitaweza kuyainua mawazo yako toka katika hali yake ya kuipenda dunia pamoja na upotovu wake. Wale wanaoyajua sana Maandiko watakuwa ni wanaume na wanawake ambao mvuto wao una nguvu ya kuwainua watu. Katika kuzichunguza kweli hizo za Mbinguni zilizofunuliwa, Roho wa Mungu huunganishwa na moyo wako kwa karibu sana. Kuyaelewa mapenzi ya Mungu yaliyofunuliwa huukuza ubongo, huupa mawazo bora, na kuupa nguvu mpya, kwa kuuleta uwezo wake mbalimbali katika mgusano na ile kweli kubwa mno ajabu.

Hakuna somo liwezalo kuupa ubongo nguvu yake na kuiimarisha akili kama kulivyo kujifunza Neno la Mungu. Hakuna kitabu kinginecho chote chenye uwezo mkubwa mno katika kuyaadilisha mawazo, kuupa nguvu uwezo wa akili, kama ilivyo Biblia, ambayo inazo kweli bora kabisa. Kama Neno la Mungu lingesomwa linavyopaswa kusomwa, basi, tungeweza kuuona upana wa mawazo, uthabiti wa nia, ubora wa tabia, kama ule unaoonekana kwa nadra sana katika nyakazi hizi.

Walakini, kujifunza Biblia kunapewa nafasi ya pili katika mawazo yetu, na kwa ajilihiyo, hasara kubwa inapatikana. Ufahamu wetu unafuata usawa wa mambo yale unayoyazoea. Kama wote wangeifanya Biblia kuwa somo lao, tungeweza kuwaona watu waliokua vizuri, wenye uwezo wa kufikiri kwa kina zaidi, ambao wangeonekana kuwa na ujuzi mkubwa kuliko wale waliosoma kwa bidii sayansi mbalimbali pamoja na historia za ulimwengu huu, ambao wanaiacha Biblia. 

Biblia humpa mtafutaji wa ile kweli nidhamu ya hali ya juu kiakili, naye anapotoka katika kutafakari mambo hayo ya Mungu, nguvu zake za akili zikiwa zimesitawishwa; nafsi yake inanyenyekezwa, wakati Mungu na kweli yake iliyofunuliwa kwake inapotukuzwa. Ni kwa sababu watu hawazifahamu historia za thamani zilizo katika Biblia, ndiyo maana kuna hali ya kumtukuza mno mwanadamu na heshima ndogo mno hutolewa kwa Mungu.

Biblia inacho kile kiwezacho kumfanya Mkristo kuwa na nguvu ya kiroho na kiakili. Mtunga Zaburi asema hivi, “Kuyafafanusha maneno yako kwatia nuru, na kumfahamisha mjinga.” Zaburi 119:130. Biblia ni kitabu cha ajabu. Ni historia inayotufunulia sisi mambo ya karne zile zilizopita. Pasipo kuwa na Biblia, sisi tungekuwa tumeachwa kufuata dhana mbalimbali na hadithi za uongo kwa habari ya matukio ya vizazi vile vilivyopita. Ni unabii unaolifunua pazia la siku zijazo. 

Ni Neno la Mungu, liufunualo mpango ule wa wokovu, ambalo linatuonyesha njia ile ambayo kwayo sisi tunaweza kuikwepa mauti ile ya milele, na kujipatia wema wa milele na uzima wa milele. Katika vitabu vyote vinavyoigharikisha [vinavyoijaza] dunia hii, haidhuru viwe
vya thamani ilioje, Biblia ni Kitabu kipitacho vitabu vyote, inastahili kabisa kuwa somo letu na kupewa heshima. Haitupatii sisi historia ya ulimwengu huu tu, bali maelezo ya ulimwengu ule ujao. Ina mafundisho yahusuyo maajabu ya malimwengu mbalimbali; inatufunulia katika ufahamu wetu tabia ya Mwasisi yule wa mbingu na nchi. Ndani yake umo ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu.

Kuvichunguza vitabu vya falsafa na sayansi hakuwezi kuiletea akili na maadili kile ambacho kujifunza Biblia kunaweza kutuletea, mradi tu kiwekwe katika matendo yetu. Yule anayejifunza Biblia anaongea na wazee wa zamani pamoja na manabii. Anagusana na ile kweli iliyovikwa mavazi ya lugha ya heshima, ambayo ina mvuto wenye nguvu unaoupendeza moyo, na kuyainua mawazo toka katika mambo ya dunia hii kwenda kwenye utukufu ule wa maisha ya baadaye ya milele. Ni hekima gani ya mwanadamu inayoweza kulinganishwa na ufunuo wa utukufu wa Mungu. Mwanadamu mwenye maisha mafupi, asiyemjua Mungu, anajitahidi kuipunguza thamani ya Maandiko, akidai kwamba, maarifa yake ya sayansi anayodhania kuwa anayo, hayawezi kupatana na Neno la Mungu; lakini Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu.

Wale wanaojigamba kwamba wanayo hekima nyingi kuliko ile ifundishwayo katika Neno la Mungu wanahitaji kunywa kwa kina zaidi katika chemchemi hiyo ya maarifa, ili wapate kuuona ujinga wao ulivyo hasa. Wanadamu hujisifu wenyewe kwa hekima waliyo nayo, wakati hekima hiyo ni upumbavu mtupu. Hebu na asiwepo mtu awaye yote anayejidanganya mwenyewe. “Mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu. 

Kwa maana imeandikwa, Yeye ndiye awanasaye wenye hekima katika hila yao.” 1 Wakorintho 3:18-19. Ujinga mkubwa mno unaowaletea laana wanadamu hivi sasa ni ujinga wa kukosa kuyajua masharti ya Sheria ya Mungu [Amri Kumi – Kut. 20:3-17] ambayo yanawafunga wanadamu wote; na ujinga huo ni matokeo ya kudharau kulichunguza Neno la Mungu. Ni mpango wake Shetani kuyashughulisha mno mawazo kiasi cha kuwafanya wanadamu kukiacha Kitabu hicho Kikuu cha Mwongozo, na hivyo kuwafanya waongozwe katika njia ile ya uasi [uvunjaji wa Amri Kumi – Yak. 2:10-12] na maangamizi.

Biblia haipewi heshima na kuwekwa mahali pake inapostahili miongoni mwa vitabu vya ulimwengu huu, japokuwa kuisoma kuna umuhimu usio na kifani kwa roho za wanadamu. Katika kuzichunguza kurasa zake mawazo yetu huziona mandhari [picha] zile tukufu za milele. Twamwona Yesu, Mwana wa Mungu, akija katika dunia yetu, na kuingia katika pambano la ajabu ambalo limezivunjilia mbali nguvu zile za giza. Lo! ni ajabu jinsi gani, ni jambo ambalo karibu halisadikiki kabisa kwamba Mungu yule wa milele angeweza kukubali Mwana wake apate kudhalilishwa kiasi kile, ili sisi tupate kuinuliwa juu na kuketi pamoja naye katika kiti chake cha enzi!

 Hebu kila mwanafunzi wa Maandiko na atafakari ukweli huo mkuu, ndipo hatatoka katika kujifunza Biblia pasipo kutakaswa, kuinuliwa juu na kuadilishwa. Ile kweli itafunuliwa akilini mwake na kutumiwa na Roho wa Mungu katika moyo wake. Kwa njia ya kuunganishwa na Mungu, Mkristo atakuwa na mawazo safi na mapana zaidi, yasiyopendelea kufuata maoni yake mwenyewe aliyokuwa nayo hapo kwanza. Uwezo wake wa kupambanua mema na mabaya utapenya ndani zaidi, uwezo wake wa akili utakuwa na uwiano mzuri zaidi.

Akili yake, ikitumika katika kuzitafakari zile kweli tukufu, itapanuka, na katika kujipatia maarifa yale ya mbinguni ataweza kuujua vizuri zaidi udhaifu wake alio nao, naye atakua katika imani na katika unyenyekevu wake wa moyo. Usikivu mdogo tu ukitolewa kwa Neno la Mungu, mashauri ya Mungu huwa hayazingatiwi, maonyo yanayotolewa huwa kazi bure, neema na hekima ya mbinguni haitafutwi ili dhambi zile zilizopita zipate kuepukwa na kila waa la ufisadi lipate kusafishwa katika tabia yetu. Daudi aliomba, akasema, “Unifahamishe njia ya mausia yako [yaani, amri zako – KJV].” “Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika Sheria yao [Amri Kumi].” Zaburi 119:27,18.

Ipo kazi kubwa ya kufanywa na mwanafunzi wa Biblia mwenye bidii; kwa sababu vito vya thamani vya ile kweli vinatakiwa kukusanywa na kuletwa juu, kisha vinapaswa kutengwa mbali na urafiki wo wote na makosa [mafundisho potofu]. Ingawa Biblia ni ufunuo utokao mbinguni, hata hivyo, wengi hawayaelewi mafundisho yake ya mbinguni. Tunapaswa kugundua maono mapya ya ile kweli katika Agano la Kale na Agano Jipya, hatuna budi kukiona kina na upana upitao kiasi wa zile kweli tunazofikiri kwamba tunazijua, lakini ambazo sisi tuna ujuzi wake wa juu juu tu. Yule anayeyachunguza Maandiko kwa bidii ataona kwamba mwafaka upo kati ya sehemu mbalimbali za Biblia; atagundua uhusiano wa kifungu kimoja cha maneno na kile kingine, na thawabu ya taabu yake [ya kujitahidi kukichunguza] itakuwa ya thamani kubwa mno.

Katika eneo lote la ufunuo huo zimetawanyika chemchemi za furaha, amani na shangwe za ile kweli ya mbinguni. Chemchemi hizo za furaha zinaweza kufikiwa na kila mmoja atafutaye. Maneno yale ya Uvuvio, yakifikiriwa sana moyoni, yatakuwa kama vijito vinavyotiririka kutoka katika mto ule wa maji ya uzima. Mwokozi wetu aliomba kwamba akili za wafuasi wake zipate kuzinduliwa ili kuyaelewa Maandiko hayo. Kila tunapojifunza Biblia kwa moyo wa maombi, Roho Mtakatifu huwa karibu nasi kutufunulia maana ya maneno yale tusomayo. 

Mtu yule ambaye akili yake imetiwa nuru kwa kulifafanua Neno la Mungu, hatajisikia tu kuwa anapaswa kutafuta kwa bidii ili apate kulielewa Neno lile, bali kwamba anapaswa kuwa na ujuzi bora wa sayansi zile nyingine. Atajisikia kwamba ameitwa kwa mwito ule mkuu katika Kristo Yesu. Kadiri mwanadamu anavyounganishwa kwa karibu sana na lile Chimbulo la maarifa yote na hekima, ndivyo kadiri atakavyojisikia kwamba hana budi kusonga mbele katika kujipatia mambo yale ya kiakili na kiroho. Roho Mtakatifu, kwa njia ya ile kweli ya Mungu, huuhuisha uwezo ule wa kiroho uliokufa na kuuvuta moyo kuelekea mbinguni.

Basi, chukua Biblia yako na kujiweka mbele za Baba yako wa Mbinguni, ukisema, “Unitie nuru; unifundishe kweli ni nini.” Bwana ataifikiria sala yako, na Roho Mtakatifu ataitia kweli hiyo moyoni mwako. Katika kuyachunguza Maandiko wewe mwenyewe, utakuwa umejiimarisha katika imani. Ni jambo la maana sana kwamba uweke moyoni mwako akiba ya kweli hizo za Mungu. Unaweza kujikuta uko mahali ambako hutapata nafasi ya kukutana na watoto wa Mungu. Unahitaji kuzificha hazina za Neno la Mungu
moyoni mwako, ili upinzani utakapokuja dhidi yako, upate kulipima kila jambo kwa Maandiko hayo.

Kweli ni ya milele, na kupambana kwake na uongo [mafundisho potofu] kutaudhihirisha tu uwezo wake. Kamwe tusikatae kuyachunguza Maandiko pamoja na wale ambao tunayo sababu ya kuamini kwamba wanataka kujua kweli hiyo ni nini. Tuseme ndugu mmoja anashikilia maoni yaliyo tofauti na yako, naye anakuja kwako, na kupendekeza kwamba wewe uketi chini pamoja naye na kulichunguza jambo lile katika nuru ya Maandiko; je! ungesimama ukiwa umejazwa na chuki bila sababu na kuyashutumu mawazo yake, na wakati uo huo ukiwa unakataa kumpa usikivu wako usiopendelea upande wo wote? Njia pekee sahihi kwetu sisi kama Wakristo ingekuwa ni ile ya kuchunguza msimamo uliotolewa katika nuru ya Neno la Mungu, ambalo litaifunua kweli na kuufichua uongo. 

Kuyadhihaki mawazo yake kusingeweza kuudhofisha msimamo wake, ingawa [yale usemayo] yangekuwa ni ya kweli. Hebu kilete kila kitu kwenye Biblia; kwa maana hiyo peke yake ndiyo kanuni ya imani na mafundisho ya dini. Hatuna budi kujifunza ile kweli sisi wenyewe; tusimtegemee mtu awaye yote kufikiri kwa niaba yetu, haidhuru awe ni nani au awe na cheo gani. Hatupaswi kumwangalia mwanadamu ye yote kama kiongozi mkamilifu [asiye na dosari] aliyewekwa kwa ajili yetu. Tunapaswa kushauriana pamoja na kunyenyekeana; lakini wakati uo huo hatuna budi kumwangalia Mungu kwa ajili ya kututia sisi nuru ile ya mbinguni, ili kila mmoja wetu apate kukuza tabia ile itakayoweza kushinda katika jaribio la siku ile kuu.

Sisi tunaishi katika siku za mwisho, wakati makosa [mafundisho ya uongo] yaliyojaa udanganyifu wa hali ya juu yanapokelewa na watu na kusadikiwa, wakati ile kweli [Neno la Mungu – Yn. 17:17] inapotupiliwa mbali. Wengi wanachukuliwa na mkondo wa maji na kuingia katika giza [la ujinga] na ukafiri, wanaikosoa Biblia, wanaleta mavumbuzi ya kishirikina [uchawi], wanaleta nadharia zisizoungwa mkono na Maandiko, pamoja na dhana zinazotokana na falsafa ya kipumbavu; lakini ni jukumu la kila mmoja wetu
kujitahidi kupata ujuzi kamili wa Maandiko. Umuhimu na faida ya kujifunza Biblia haviwezi kusifiwa mno. Katika kuyachunguza Maandiko mawazo yetu huongozwa katika kuifikiria sana ile kafara ya Kristo isiyo na kikomo katika kutupatanisha sisi. Tunapouona upendo wake, tunapotafakari juu ya kujidhili kwake na mateso yake, roho ile ile ya kujikana nafsi na kujitoa mhanga kwa faida ya wengine inaamshwa ndani ya mioyo yetu. Tunapomtazama Yesu kwa jicho la imani, tuta“badilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile utukufu utokao kwa Bwana, aliyeRoho.” 2 Wakorintho 3:18.
 
Na Bibi E. G. White, The Power of the Word, 
...au Kichwa cha makala ya awali ni: “Apples of Gold Library No. 10.”
 
ZINGATIA: Maneno na mafungu ya Biblia yaliyofungiwa ndani ya mabano haya [ ] yameongezwa kwa ufafanuzi tu kwa yule anayetaka kusoma kwa kina au anayeona neno lililotumika pale ni gumu. Wakati wa kusoma unatakiwa kuyaruka, isipokuwa kama yanasaidia kuikamilisha sentensi hiyo.

Jumatatu, Juni 25, 2012

USAFI WA MOYO




Hili neno hutumika mara nyingi kuelezea adili ambalo linapingana na uzinifu na kutegemea kiasi. Kwa maana hiyo unawahusu watu wanaojua kutawala maelekeo ya kijinsia yaweze kujenga maisha yao binafsi, familia na hata jamii.

Neno hilo lilivyotumiwa na Yesu katika Hotuba ya mlimani lina maana pana zaidi na kuhusisha unyofu wa dhamiri kwa jumla.

Adili, ni uzoefu wa kutenda kiutu.

Huko Ugiriki katika karne ya 5 K.K. wanafalsafa Plato na hasa Aristotle waliorodhesha maadili mengi yanayotegemea nne za msingi (maadili bawaba): busara, haki, nguvu na kiasi. Zaidi ya hayo, walionyesha kwamba haiwezekani kujipatia adili moja tu, bali uadilifu unadai mtu awe na maadili yote. Kwa mfano, haiwezekani kuwa mtu wa haki pasipo busara.

Katika Ukristo, juu ya maadili ya kiutu, mwamini anatakiwa kupokea maadili ya Kimungu yaliyoorodheshwa na mtume Paulo, yaani imani, tumaini na upendo ambayo yanaendana vilevile.

Maadili bawaba:
Ni maadili manne ya kiutu yaliyojulikana na wanafalsafa wa Ugiriki, hasa Plato na Aristotle, kuwa ndiyo yanayotegemeza maadili mengine yote ya kiutu, kama vile bawaba zinavyotegemeza mlango uweze kufanya kazi yake vizuri. Yanaitwa pia maadili ya kiutu ya msingi au fadhila za msingi, kwa kuwa ndiyo hasa yanayomfanya mtu atende kadiri ya utu wake.

Majina yake ni: busara, haki, nguvu na kiasi.
Katika Ukristo yanatofautishwa na maadili ya Kimungu, yaani imani, tumaini na upendo ambayo yanatokana na Mungu na kumlenga yeye.

Maadili ya kiutu:
Ni yale yanayotakiwa kupatikana katika binadamu yeyote ili aweze kutenda kwa uadilifu kadiri ya utu wake unaomtofautisha na wanyama, yaani hasa akili inayomwezesha kufikiria na kuelewa maana na matokeo ya matendo yake.

Kadiri ya wanafalsafa wa Ugiriki wa kale Plato na Aristotle, maadili hayo ni mengi (si chini ya 40), lakini yanategemea manne (maadili bawaba): busara, haki, nguvu na kiasi.
Katika Ukristo maadili ya Kimungu ni yale yanayotokana na Mungu na kumwezesha binadamu kuhusiana naye inavyotakiwa, yaani kwa:
Kwa maadili hayo, yale ya kiutu yanakuwa hai na bora, kwa mfano wa Yesu Kristo. Kadiri ya Kanisa Katoliki, tofauti na yale ya kiutu, maadili ya Kimungu hayawezi kupatikana kwa juhudi anazofanya mtu, bali kwa neema tu: yanamiminiwa rohoni, yaani katika akili na katika utashi.