Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Novemba 19, 2013

Namna Sinema Zinavyotengenezwa



KATIKA miongo kadhaa iliyopita sinema nyingi zenye mafanikio zimetokezwa huko Hollywood. Hilo limekuwa na uvutano mkubwa ulimwenguni pote kwani sinema nyingi za Marekani hutazamwa katika nchi nyingine majuma machache au hata siku chache tu baada ya kuonyeshwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani. Sinema fulani hata zimeonyeshwa kwa mara ya kwanza tarehe ileile duniani kote. Dan Fellman, rais wa usambazaji wa filamu nchini Marekani wa shirika la Warner Brothers anasema hivi: “Soko la ulimwenguni kote la uuzaji wa sinema linazidi kukua nalo linasisimua sana, kwa hiyo tunapotengeneza sinema, huwa tunaitengeneza kwa ajili ya soko la ulimwenguni kote.” Sasa kuliko wakati mwingine wowote, kile kinachotendeka huko Hollywood huathiri biashara ya sinema ulimwenguni. 

Lakini kupata faida kutokana na sinema si rahisi kama unavyowazia. Sinema nyingi zinahitaji zaidi ya dola milioni 100 ili kulipia gharama ya kuzitengeneza na kuziuza. Na kufanikiwa kwake kunategemea watazamaji ambao mtu hawezi kutabiri watapendezwa na nini. David Cook, profesa wa masomo ya sinema katika Chuo Kikuu cha Emory anasema hivi: “Huwezi kujua ni lini jambo fulani litawavutia au kuwasisimua watazamaji.” Kwa hiyo watengenezaji wa sinema huongezaje uwezekano wa sinema yao kufanikiwa? Ili kupata jibu, tunahitaji kuelewa mambo machache ya msingi yanayohusika katika utengenezaji wa sinema.

Matayarisho Yanayofanywa Kabla ya Kutengeneza Sinema

Mara nyingi, matayarisho yanayofanywa kabla ya upigaji picha ndiyo sehemu muhimu zaidi ambayo huchukua muda mrefu katika utengenezaji wa sinema. Kama tu ilivyo na mradi wowote mkubwa, mafanikio yake hutegemea sana matayarisho. Inatumainiwa kwamba pesa zozote zinazotumiwa wakati wa matayarisho zitapunguza sana gharama za kutengeneza sinema yenyewe.

Kutengenezwa kwa sinema huanza na hadithi fulani ambayo huenda ikabuniwa au ikategemea matukio halisi. Mwandikaji huandika hadithi hiyo kwenye hati. Hati hiyo inaweza kufanyiwa marekebisho mengi kabla ya hati ya mwisho kutokezwa. Hati hiyo ya mwisho huwa na wahusika pamoja na maelezo mafupi kuhusu kitendo kitakachofanywa. Pia hati hiyo hutoa maagizo mengine kama vile mahali ambapo kamera zitakuwa na mabadiliko yatakayofanywa katika kila onyesho.

Hata hivyo, hati hiyo inapokuwa katika hatua za kwanza, mtayarishaji atakayeinunua huanza kutafutwa. Mtayarishaji anaweza kupendezwa na hati ya aina gani? Kwa kawaida sinema ambayo hutolewa msimu wa kiangazi hukusudiwa iwavutie vijana wa kati ya miaka 13 hadi 25 hivi. Kwa hiyo mtayarishaji atapendezwa hasa na sinema ambayo itawavutia vijana.

Hati inayofaa hata zaidi ni ile itakayowavutia watu wa umri mbalimbali. Kwa mfano, bila shaka sinema inayotegemea shujaa anayetajwa katika vitabu vya vibonzo itawavutia watoto wadogo ambao wanamfahamu shujaa huyo. Na bila shaka wazazi wao wataambatana nao kuitazama sinema hiyo. Lakini watengenezaji wa sinema huwavutiaje vijana walio na umri wa kati ya miaka 13 na 25 hivi? Katika gazeti The Washington Post Magazine, Liza Mundy anasema kwamba “habari inayosisimua” ndiyo jambo muhimu. Ili sinema “ilete faida kubwa na kuwavutia watu wa umri mbalimbali bila kupuuza yeyote,” lugha chafu, jeuri nyingi, na picha nyingi za ngono hutiwa ndani.

Mtayarishaji akiona kwamba hati inaweza kuwa sinema nzuri, huenda akainunua na kumpa kandarasi mwelekezi na mwigizaji maarufu. Kuwa na mwelekezi na mwigizaji maarufu kutafanya sinema hiyo ivutie sana wakati itakapotolewa. Hata katika hatua hii ya kwanza, waelekezi na waigizaji maarufu wanaweza kuwavutia wawekezaji wanaohitajika ili kugharimia utayarishaji wa sinema hiyo.

Hatua nyingine ya matayarisho ni kuchora vibonzo mbalimbali vya filamu hiyo hasa vile vinavyohusisha mapigano. Michoro hiyo humwongoza mpiga-picha za sinema nayo husaidia kupunguza wakati unaotumiwa kupiga picha. Mwelekezi aliye pia mwandikaji wa hati, Frank Darabont, anasema: “Hakuna jambo baya zaidi kama kupoteza wakati wa kupiga picha kwa sababu tu ya kutojua mahali ambapo kamera inapaswa kuwa.”

Kuna mambo mengine mengi muhimu yanayopaswa kushughulikiwa wakati wa matayarisho. Kwa mfano, picha zitapigiwa wapi? Je, itakuwa lazima kusafiri? Je, kuna picha zitakazopigwa ndani ya nyumba, nayo itapambwaje? Je, mavazi maalumu yatahitajika? Ni nani atakayeshughulikia mwangaza, kupamba na kutengeneza nywele za waigizaji? Na vipi kuhusu sauti, madoido, na yule atakayeigiza sehemu hatari badala ya mwigizaji mkuu? Hayo ni baadhi ya mambo yanayohitaji kufikiriwa hata kabla ya kupiga picha za filamu. Ukitazama majina yanayoonyeshwa mwishoni mwa sinema inayotazamiwa kuleta faida kubwa, huenda ukaona kwamba mamia ya watu walihusika kuitayarisha! Fundi mmoja wa mitambo ambaye amehusika katika kutengeneza sinema nyingi anasema kwamba “watu wengi sana huhusika katika kutengeneza filamu nzuri.”

Kutengeneza Sinema Yenyewe

Kupiga picha za sinema kunaweza kuchukua wakati mwingi, kunaweza kuchosha, na pia kunaweza kugharimu pesa nyingi. Kwa kweli, kupoteza dakika moja tu kunaweza kugharimu maelfu ya dola. Nyakati nyingine inabidi waigizaji, wafanyakazi, na vifaa visafirishwe hadi sehemu ya mbali. Hata hivyo, haidhuru picha hizo zitapigiwa wapi, lazima pesa nyingi sana zitatumika kila siku.

Watu wanaoshughulikia mwangaza, wale watakaowapamba na kuwatengeneza nywele waigizaji huwa kati ya watu wa kwanza kufika mahali ambapo picha zitapigiwa. Kila siku ya kupiga picha, waigizaji wakuu hupambwa kwa saa kadhaa. Kisha picha hupigwa kwa siku nzima.

Mwelekezi husimamia kwa uangalifu kupigwa picha kwa kila onyesho. Inaweza kuchukua siku nzima kupiga picha za onyesho fupi sana. Picha za maonyesho mengi katika sinema hupigwa kwa kutumia kamera moja, kwa hiyo, onyesho moja linaweza kupigwa picha kadhaa kutoka pembe tofauti-tofauti. Isitoshe, huenda onyesho lilelile likapigwa picha mara kadhaa ili kupata picha bora zaidi au kurekebisha tatizo la kiufundi. Ikiwa onyesho ni refu, huenda picha 50 au zaidi zikapigwa! Kwa kawaida, mwishoni mwa kila siku, mwelekezi huchunguza picha zote na kuamua ni zipi zitakazotumiwa. Kazi ya kupiga picha inaweza kuchukua majuma au hata miezi kadhaa.

Hatua ya Kuunganisha Sinema Iliyotengenezwa

Katika hatua hii, picha zilizopigwa huboreshwa na kupangwa zinavyopaswa kufuatana. Kwanza, muziki utakaotumiwa huambatanishwa na sinema hiyo. Kisha, mhariri huunganisha sehemu za sinema hiyo na kufanyiza nakala ya kwanza isiyo kamili.

Madoido ya sauti na picha pia huongezwa katika hatua hiyo. Nyakati nyingine kompyuta hutumiwa kutia madoido hayo katika hatua hii ambayo ni mojawapo ya sehemu ngumu zaidi za utengenezaji wa filamu. Kazi inayofanywa katika hatua hii inaweza kuifanya sinema ivutie na ionekane kuwa halisi.

Muziki uliotungwa hasa kwa ajili ya sinema hiyo huongezwa katika hatua hiyo, na jambo hilo ni muhimu katika filamu za leo. Edwin Black anaandika hivi katika gazeti Film Score Monthly: “Sasa watengenezaji wa sinema hutaka muziki uliotungwa hasa kwa ajili ya sinema, nao hawataki muziki wa dakika ishirini tu au vipindi vifupi vya muziki, bali wao hutaka muziki utakaochezwa kwa muda unaozidi saa nzima.”

Nyakati nyingine filamu iliyoboreshwa huonyeshwa watu wachache ambao wanaweza kutia ndani rafiki za mwelekezi au wafanyakazi wenzake ambao hawakuhusika katika kutengeneza filamu hiyo. Ikitegemea jinsi watakavyoitikia, mwelekezi anaweza kupiga picha upya maonyesho fulani au kuyaondoa kabisa. Katika visa fulani, umalizio wote wa filamu ulibadilishwa kwa sababu watu walioitazama kwanza hawakuupenda.

Hatimaye, filamu iliyokamilika huonyeshwa kwenye majumba ya sinema. Ni wakati huo tu ndipo inaweza kujulikana ikiwa sinema hiyo itafanikiwa au haitafanikiwa, au itakuwa ya wastani. Lakini mambo mengi yanahusika kuliko kupata faida. Sinema kadhaa zikikosa kufanikiwa zinaweza kuharibu sifa ya mwelekezi na matarajio ya mwigizaji kupata kazi. Anapofikiria miaka yake ya mapema ya kutengeneza filamu, mwelekezi John Boorman anasema hivi: “Niliwaona waelekezi wenzangu wakikosa kandarasi baada ya sinema kadhaa walizoelekeza kukosa kufanikiwa. Ukweli wenye kusikitisha ni kwamba katika biashara ya kutengeneza sinema, usipowaletea faida mabwana zako, unapoteza kazi yako.”

Bila shaka, watu wanapotazama ubao wa kutangazia sinema, kwa ujumla hawafikirii ikiwa watengenezaji wa sinema hiyo watapoteza kazi zao au la. Yaelekea wao huhangaikia mambo kama: ‘Je, nitafurahia sinema hii? Je, inafaa nitumie pesa zangu ili kuitazama? Je, sinema hii itanivutia au itanichukiza? Je, inawafaa watoto wangu?’ Unaweza kujibuje maswali hayo unapoamua sinema utakazotazama?

[Maelezo ya Chini]

Anita Elberse, ambaye ni profesa wa Chuo cha Biashara cha Harvard, anasema kwamba “ingawa mara nyingi pesa zinazopatikana kutokana na mauzo ya sinema katika nchi za ng’ambo ni nyingi kuliko zile za mauzo nchini Marekani, jinsi watu wanavyoipokea sinema nchini Marekani huamua jinsi itakavyopokelewa katika nchi nyingine.”

Ingawa huenda njia ambazo hutumiwa kutengeneza sinema zikatofautiana, mambo yanayoelezwa hapa yanaonyesha njia moja inayoweza kutumiwa.

Nyakati nyingine mtayarishaji hupewa muhtasari wa hadithi badala ya hati yenyewe. Ikiwa atavutiwa na hadithi hiyo, anaweza kununua haki za kuimiliki na kuitengeneza kuwa hati.

“Huwezi kujua ni lini jambo fulani litawavutia au kuwasisimua watazamaji.”—David Cook, profesa wa masomo ya sinema

JINSI YA KUFANYA SINEMA IVUTIE NA ILETE FAIDA KUBWA

  Sinema imekamilishwa. Iko tayari kutazamwa na mamilioni ya watu. Je, itafanikiwa? Fikiria njia mbalimbali ambazo watengenezaji wa sinema hutumia ili sinema yao ivutie na ilete faida kubwa.

UVUMI: Mojawapo ya njia zenye mafanikio za kuwafanya watu wawe na hamu ya kutazama sinema fulani ni kupitia uvumi. Nyakati nyingine uvumi kuhusu sinema fulani huanza miezi kadhaa kabla ya sinema hiyo kuonyeshwa kwa umma. Huenda ikatangazwa kwamba kutakuwa na sinema itakayokuwa mwendelezo wa sinema fulani iliyofanikiwa hapo awali. Je, itakuwa na waigizaji walewale maarufu wa sinema ya awali? Je, itakuwa nzuri (au mbaya) kama ile ya kwanza?

  Katika visa fulani, uvumi huanzishwa kuhusu jambo fulani katika sinema, labda kuonyesha picha za ngono waziwazi katika sinema itakayotazamwa na watu wote. Je, sinema hiyo ni mbaya sana? Je, sinema hiyo imepita mipaka kabisa? Watengenezaji wa sinema hunufaika watu wanapotoa maoni mbalimbali yanayopingana kuihusu, kwa kuwa hiyo ni njia moja ya kuitangaza bila malipo. Nyakati nyingine mijadala hiyo huwafanya watu wengi waitazame sinema hiyo inapoonyeshwa kwa mara ya kwanza.

VYOMBO VYA HABARI: Njia za kawaida za kutangaza sinema zinatia ndani mabango, matangazo ya magazeti, matangazo ya biashara ya televisheni, kuonyeshwa kwa sehemu ndogo ya sinema hizo katika majumba ya sinema kabla ya sinema nyingine, na kasheshe. Sasa Intaneti imekuwa njia kuu ya kutangaza sinema.

KUUZA BIDHAA: Kuuza bidhaa zinazotangaza sinema fulani kunaweza kuifanya ivutie inapotolewa. Kwa mfano, sinema moja iliyotegemea shujaa anayetajwa katika kitabu fulani cha kibonzo ilitangazwa katika vifaa vya kubebea vyakula, vikombe, vito, mavazi, minyororo ya funguo, saa, taa, na michezo ya dama, na kadhalika. Joe Sisto anaandika hivi katika jarida la vitumbuizo la Shirika la Mawakili la Marekani: “Kwa kawaida, asilimia 40 ya bidhaa za kutangaza sinema huwa zimeuzwa hata kabla ya sinema hiyo kutolewa.”

KANDA ZA VIDEO: Sinema ambayo haileti faida kubwa inapoonyeshwa katika majumba ya sinema inaweza kuleta faida inaporekodiwa katika kanda za video. Bruce Nash, ambaye huchunguza faida zinazotokana na sinema anasema kwamba “kanda za video huchangia asilimia 40 hadi 50 ya mapato ya sinema.”

VIWANGO VYA SINEMA: Watengenezaji wa sinema wamejifunza kutumia viwango vinavyowekwa vya sinema ili kujifaidi. Kwa mfano, huenda mambo fulani yakaingizwa kimakusudi katika sinema ili kuifanya iwekewe kiwango cha juu zaidi kinachowafaa watu wazima pekee. Kwa upande mwingine, sehemu chache zinaweza kuondolewa ili sinema isipewe kiwango cha watu wazima na kuifanya iwavutie vijana. Liza Mundy anaandika katika gazeti The Washington Post Magazine kwamba kuwekea sinema kiwango cha vijana “kumekuwa njia ya kutangaza sinema: Majumba ya kurekodia sinema hutumia kiwango hicho kupitisha ujumbe kwa vijana na watoto wanaotamani sana kuwa vijana kwamba sinema hiyo itakuwa yenye kuvutia sana.” Mundy anasema kwamba kiwango hicho “hutokeza uvutano kati ya mzazi na mtoto kwani humwonya mzazi na kumvutia mtoto.”

JINSI SINEMA ZINAVYOTENGENEZWA

HATI
MICHORO
MAVAZI
KUPAMBWA
UPIGAJI PICHA
KUTIA MADOIDO
KUREKODI MUZIKI
KUINGIZA SAUTI
KUTENGENEZA VIBONZO KWA KUTUMIA KOMPYUTA
KUBORESHA NA KUPANGA PICHA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni