Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Julai 19, 2011

TOKENI MIJINI...SEHEMU YA TANO

Kujiandaa kwa Hatari Kubwa Itakayoletwa na Amri ya JumapiliNyakati za Taabu Ziko Mbele Yetu

Haitupasi sisi kujiweka wenyewe mahali ambapo tutalazimishwa kuwa na uhusiano wa karibu

sana na wale wasiomheshimu Mungu....

Hatari kubwa karibu sana inakuja kuhusiana na utunzaji wa Jumapili....

Kundi la Jumapili linajiimarisha lenyewe katika madai yake ya uongo, na jambo hilo litamaanisha mateso kwa wale wanaokata shauri kuitunza Sabato ya Bwana [Jumamosi].

Yatupasa kujiweka wenyewe mahali pale tutakapoweza kuishika amri hiyo ya Sabato

[Jumamosi] kwa ukamilifu wake. "Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote;

lakini siku ya saba ni Sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote."

Tena yatupasa kuwa waangalifu tusijiweke mahali pale itakapokuwa vigumu kwetu sisi wenyewe na watoto wetu kuitunza Sabato [Jumamosi].

Endapo kwa maongozi yake Mungu tunaweza kujipatia mahali pa kuishi mbali na miji, basi,

Bwana angependa kwamba sisi tufanye hivyo. Nyakati za taabu ziko mbele yetu.

----- Manuscript 99, 1908.

Harakisheni Kujiweka Tayari

Uwezo waliopewa wafalme [Ma-Rais] ukifungamana na wema ni kwa sababu yule aliyeshika

madaraka hayo yuko chini ya uongozi wa Mungu. Uwezo huo unapofungamana na uovu, basi, unafungamana na nguvu za Shetani, nao utafanya kazi ya kuwaangamiza wale walio mali yake Bwana. Ulimwengu wa Kiprotestanti umeisimamisha sanamu ya sabato [Jumapili] mahali pale

ambapo Sabato ya Mungu [Jumamosi] ingepaswa kusimama, nao wanatembea katika nyayo za Upapa.

Kwa sababu hiyo mimi nauona umuhimu kwa watu wa Mungu kuondoka mijini kwenda

kwenye sehemu za upweke huko mashambani [vijijini], ambako wanaweza kulima mashamba yao na kuzalisha wenyewe mazao yao. Kwa njia hiyo wanaweza kuwalea watoto wao kuwa na tabia ya kawaida, inayoleta afya. Nauona umuhimu wa kuharakisha kuyaweka mambo yote tayari ili kuweza kukabiliana na hatari hiyo kubwa. ----- Letter 90, 1897.SURA YA SITA

Tusikae Wengi Mahali Pamoja Katika Vituo Vya Taasisi Zetu

Tusikae Wengi Mahali Pamoja

Katika siku zetu hizi Bwana anataka watu wake watawanyike ulimwenguni kote. Haiwapasi kukaa wengi mahali pamoja. Yesu alisema, "Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe [mtu]." Marko 16:15. Wanafunzi walipofuata mapenzi [matakwa] yao ya kubaki kwa idadi kubwa kule Yerusalemu, mateso yaliruhusiwa kuwapata, nao wakatawanyika kwenda mahali pote katika ulimwengu ule uliokaliwa na watu.

Kwa miaka mingi ujumbe huu wa onyo na wa kuwasihi umekuwa ukija kwa watu wetu,

ukiwashurutisha kusonga mbele na kuingia katika shamba la Bwana la mavuno, na kufanya kazi

bila kujifikiria wenyewe kwa ajili ya roho za watu. ----- Testimonies, Gombo la 8, uk 215. (1904)

Tawanyikeni Na Kwenda Kule Wasikolipata Onyo Hilo

Washiriki wa makanisa yetu makubwa ni wengi ambao karibu hawafanyi kitu cho chote kabisa.

Hao wangeweza kufanikiwa kufanya kazi nzuri kama wangeweza kutawanyika na kwenda mahali ambako kweli hii bado haijaingia badala ya kujikusanya wengi mahali pamoja. Miti iliyopandwa karibu karibu sana haisitawi. Hupandikizwa mahali pengine na mwenye bustani ili ipate nafasi ya kutosha kukua, isizuiwe kukua zaidi wala isiwe dhaifu.

Kanuni iyo hiyo ingefanya kazi yake vizuri kwa makanisa yetu makubwa. Wengi miongoni mwa washiriki wetu wanakufa kiroho kwa kukosa kazi hii hii [ya kwenda mahali kule ambako ujumbe bado haujafika]. Wanakuwa dhaifu, tena wanashindwa kufanya kazi yao vizuri. angepandikizwa [wangehamia] mahali pengine, wangeweza kupata nafasi ya kutosha kuweza kukua [kiroho] na kuwa na nguvu.

Si kusudi lake Mungu kwamba watu wake wakae wengi mahali pamoja, au waishi pamoja katika jumuia kubwa. Wanafunzi wa Yesu ni wawakilishi wake hapa duniani, na Mungu anakusudia kwamba wao watatawanyika kila mahali duniani, katika miji midogo, miji mikubwa, na vijijini, na kuwa kama mianga kati ya giza nene la ulimwengu huu. Wanapaswa kuwa wamishonari wa Mungu, kwa imani yao wakishuhudia ukaribu sana wa marejeo ya Mwokozi wao.
MAHALI PALE ILIPOFUNGUKA NJIA YA KUJIPATIA RIZIKI

Washiriki walei [wa kawaida] wa makanisa yetu wanaweza kufanikiwa kufanya kazi ile ambayo,

hata sasa, hawajaanza kuifanya. Wasiwepo watu wanaohamia mahali papya kwa ajili ya faida ya

kidunia tu; bali mahali pale ilipofunguka njia ya kujipatia riziki ziende familia zile zilizojizatiti

katika kweli, familia moja au mbili hivi ziende mahali pamoja kufanya kazi kama wamishonari.

Wangejisikia kuwa wanayo haja ya kuwapenda watu, kwamba wanao mzigo wa kuwashughulikia watu hao, tena, kama somo lao, wangejifunza namna ya kuwaingiza katika kweli hii. Wanaweza kugawa vitabu vyetu, kufanya mikutano nyumbani mwao, kufahamiana na majirani zao, na kuwaalika waje kwenye mikutano hiyo. Wanaweza kuiacha nuru yao kuangaza kwa matendo yao mema. ----- Testimonies, Gombo la 8, uk. 244,245. (1904)

Vishawishi Vya Taasisi Zetu Visiwavute

Wale wanaojisikia kupenda kuishi karibu na nyumba yetu ya kuchapisha vitabu au hospitali na

shule yetu iliyo kwenye bustani ile kubwa ya Takoma [Takoma Park] hawana budi kupata ushauri kabla hawajahamia huko.

Kwa wale wanaotarajia kwenda kule Mountain View kama ndipo mahali pazuri pa kuishi, ati kwa sababu tu mtambo wetu wa kuchapisha vitabu wa Pasifiki [Pacific Press] utajengwa pale,

ningependa kuwaasa hivi: Zitupieni macho sehemu nyingine za ulimwengu zinazohitaji nuru yenu mliyoipokea kama amana. Kumbukeni kwamba Mungu amempa kila mtu kazi yake. Chagueni mahali fulani mtakapokuwa na nafasi nzuri ya kuiacha nuru yenu kuangaza kati ya giza hilo la kimaadili.

Inatokea sikuzote ya kwamba taasisi yetu inapojengwa mahali fulani, ziko familia nyingi

zinazotaka kwenda huko na kuweka makao yao karibu nayo. Hivyo ndivyo ilivyokwisha kutokea

kule Battle Creek na Oakland, na, kwa kiwango fulani, karibu kila mahali ambapo tunayo shule au hospitali yetu. ----- Fundamentals of Christian Education, uk. 494,495. (1904).

Msianzishe Vituo Vya Yerusalemu

Watu wetu ... hawapaswi kupaangalia ...

kama kituo cha Yerusalemu. Wasifikiri kwamba kwa sababu idadi fulani ya ndugu zetu wameitwa kuja hapa kujiunga na kazi hii ya uchapishaji, basi, hapa ndipo mahali pa kukaa idadi kubwa ya watu wetu na familia zao. Na kila mtu anayehusika na Ofisi hiyo ajiweke tayari kuondoka endapo Mungu atamwita kwenda mahali fulani papya.-----Manuscript 148, 1905.

Msisongamane mahali pamoja, mkifanya kosa lile lile lililokwisha kufanywa kule Battle Creek.

Kuna mamia ya mahali pengine panapohitaji nuru hiyo aliyowapa Mungu. ----- Fundamentals of

Christian Education, uk. 495. (1904).

Bakini Katika Makanisa Madogo - Anzisheni Shule Nyingi Mpya

Familia nyingi ambazo, kwa madhumuni ya kuwapatia elimu watoto wao, huhamia mahali kule

zilikojengwa shule zetu kubwa, wangeweza kufanya kazi bora kwa ajili ya Bwana kwa kuendelea kubaki pale pale walipo. Wangelitia moyo kanisa ambalo wao ndio washiriki wake kujenga shule ya kanisa ambayo watoto walio katika mipaka yake wangeweza kujipatia elimu kamili ya Kikristo itakayowawezesha kufanya kazi yao.

Lingekuwa ni jambo bora sana kwa watoto wao, kwao wenyewe, na kwa kazi ya Mungu, kama wangeendelea kubaki katika makanisa hayo madogo, ambamo msaada wao unahitajika badala ya kwenda kule yaliko makanisa yetu makubwa, ambako, kwa vile wao hawahitajiki [hawatakuwa na kazi kanisani], kuna majaribu daima ya kuanguka katika uzembe [uvivu] wa kiroho.

Po pote pale walipo Wasabato wachache, wazazi wangeungana pamoja na kutenga eneo kwa ajili

ya shule ya kutwa ambamo watoto na vijana wao wanaweza kupata mafunzo yao. Wamwajiri

mwalimu Mkristo, ambaye, kama mmishonari aliyejitoa wakf, ataweza kuwaelimisha watoto wao kwa njia ambayo itawafanya nao wawe wamishionari.

----- Counsels to Teachers, uk. 173,174. (1913)

Hivi Malaika Wanajisikiaje

Nafikiria jinsi malaika wanavyojisikia wanapouona mwisho ule ukikaribia, na kuwaona wale

wanaodai kuwa wanayo maarifa ya kumjua Mungu na Yesu Kristo aliyemtuma, wakisongamana

sana mahali pamoja, wakikaa wengi mahali pamoja, na kuhudhuria mikutano yao, na kuwa na hisia ya kukata tamaa na kutoridhika endapo hakuna mahubiri mengi yanayozinufaisha roho zao na kuliimarisha kanisa, wakati wao hawafanyi kazi yo yote kabisa. ----- Letter 16e, 1892.

Ipanueni Kazi na Kuieneza - Ila Sio Pale Makao Makuu

Watu wanahamasishwa [wanatiwa moyo] kulundikana pale Battle Creek, tena wanalipa zaka yao

na kutoa mvuto wao ili ipate kujengwa Yerusalemu ya leo pale ambayo haifuati mpango wa

Mungu. Kwa kufanya kazi hiyo mahali pengine panakosa msaada ambao wangeweza kuupata.

Panueni kazi, enezeni, naam; lakini sio mahali pamoja. Tokeni na kujenga vituo vyenye mvuto

mahali pale ambapo hakuna kitu au karibu hakuna cho chote kilichofanyika pale. Livunje-vunjeni kundi hilo kubwa sana lililosongamana mahali pamoja; tawanyeni miali ya nuru ile iokoayo, na kuiangaza nuru hiyo katika pembe [kona] za dunia zilizotiwa giza.

----- Testimonies to Ministers, Uk. 254,255. (1895)


------------------------------------------------------

Nimekusudia jambo, hili ndilo fundisho ninalotamani sote tulipate. Nitafanya muendelezo wa machapisho ya kitabu kiitwacho TOKENI MIJINI. Kwa kuzingatia umuhim wa huduma katika jamii…sina budi kukichapisha kitabu chote hapa kwa msaada wa www.swahilitruth.com. FUATANA NAMI.