Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Julai 29, 2014

JIWE LA THAMANI BAHARINI


Ndani ya bahari samaki-gamba mkubwa sana anasonga polepole kati ya miamba, akila magugu-maji yanayoyumbishwa na mikondo ya bahari. Gamba lake la nje lililofunikwa kwa asidi na viumbe vidogo vya maji, hufanya isiwe rahisi kuona rangi zake nyangavu, yaani, rangi tofauti-tofauti za bluu, kijani, na zambarau zilizochangamana na manjano na waridi, na sehemu ndogo zilizo na rangi ya dhahabu na fedha.


Kiumbe huyo wa kushangaza ni paua, wa jamii ya moluska anayepatikana New Zealand peke yake. Kiumbe huyo na viumbe wengine wa jamii hiyo wanaishi chini ya maji karibu na pwani zenye miamba. Ingawa paua anapendwa kwa sababu ya rangi za kupendeza za gamba lake la ndani linaloweza kutumiwa kutengeneza vito maridadi, watu wengi wanapenda nyama yake tamu. Kwa kuongezea, lulu zenye kung’aa sana zinaweza kukuzwa ndani yake.


Kuna jamii zaidi ya 100 za moluska ulimwenguni pote zinazopatikana Afrika Kusini, California huko Marekani, Japani, Australia, na katika kisiwa cha Guernsey kilicho kwenye Mlango-Bahari wa Uingereza. Hata hivyo, katika eneo la kusini la bahari ya Pasifiki Kusini ndiko tu unaweza kupata moluska mwenye rangi nyangavu wa New Zealand, anayeitwa paua (Haliotis iris).


Muujiza wa Kibiolojia


Ndani ya gamba la paua, matabaka ya protini na kalisi hukusanyika na kutokeza rangi maridadi kama jiwe la thamani linaloitwa opali. Kwa sababu hiyo, paua amejulikana kuwa jiwe hilo la thamani la baharini. Kiwango cha joto baharini kinaposhuka, moluska hulala. Kisha matabaka ya magamba yao huchukua muda mrefu zaidi kukua. Mtaalamu mmoja anaamini kwamba rangi mbalimbali za paua huenda zinatokana na virutubisho katika maji na pia rangi mbalimbali za magugu-maji ambayo moluska hula.


Paua huchagua chakula chao kwa uangalifu na vilevile wao huchagua wataishi karibu na nani. Hawawezi kuishi karibu na mwanamizi mwenye miiba, au kina, kwa sababu wanakula aina zilezile za magugu-maji. Pia, kiti cha pweza ni adui hatari kwani wachache tu kati yao wanaweza kumaliza familia nzima ya paua. Kwa ujanja, kiti cha pweza huwekelea mnyiri kwenye mashimo ya kupumulia ya paua na hivyo kufanya asiweze kupumua. Kisha, paua anapoanguka kutoka kwenye jiwe alilolalia, kiti cha pweza humla kwa urahisi.


Matumizi Mbalimbali ya Paua


Ingawa sehemu nyeusi ya nje ya paua haipendezi sana, kwa karne nyingi wenyeji wa New Zealand wanaoitwa Wamaori wamekula paua. Sehemu inayoweza kuliwa ya paua ni musuli mkubwa, au mguu, ambao kiumbe huyo hutumia kusonga kwenye miamba. Pia Wamaori wametumia gamba lake katika mapambo na kama chambo cha kuvua samaki. Wametengeneza vito kwa kutumia magamba yake na wameyatumia kama macho katika michongo yao.


Sasa paua anapendwa sana kuliko wakati mwingine wowote. Watalii hawakosi kununua vito vya paua wanapotembelea New Zealand.


Leo, watu wanaopiga mbizi bila vifaa vya kupumua, wanawavua paua kwa wingi sana. Hiyo imekuwa biashara inayoletea New Zealand dola milioni nyingi sana kutoka kwa nchi za nje. Ili kuhakikisha kwamba paua hawaangamizwi huko New Zealand, serikali imeweka kiwango cha paua wanaoweza kuvuliwa kwa mwaka. Nyama nyingi hutiwa katika mikebe ili ikauzwe huko Asia, na nyingine hugandishwa na kutumwa Singapore na Hong Kong ambako paua wanapendwa sana ingawa wanauzwa kwa bei ghali sana. Mara nyingi, analiwa akiwa mbichi na kukatwa vipande-vipande. Ingawa kuna paua wengi sana huko New Zealand, wenyeji wengi hawajawahi kuonja nyama yake kwa sababu ya kuuzwa sana katika nchi za nje.


Ili waweze kutosheleza uhitaji wa kimataifa wa paua, wafanyabiashara wanatumia mbinu za kisasa kuwafuga. Wafanyabiashara huko Australia, Japani, na Marekani wamefaulu kutumia mbinu hiyo ili kufuga moluska wengine. Mbinu mpya kama hizo zimesaidia paua wafugwe katika matangi yenye mifumo ya kudumisha kiwango kinachofaa cha joto mbali sana na maeneo wanayopatikana kwa ukawaida.


Paua wa kufugwa wanakula kwa kiasi kilekile kama wale wa kiasili. Kila juma wanaweza kula chakula chenye uzito sawa na nusu ya uzito wao. Kwa kushangaza, paua pia wanaweza kusonga haraka. Wanapopinduliwa, wanaweza kujigeuza upesi sana. Ni kazi rahisi kufuga paua. Mtaalamu mmoja anasema kwamba “inafurahisha kufuga paua kwa sababu ni wapole na wenye adabu, na hawawasumbui wafugaji!”


Lulu za Paua


Zaidi ya kutokeza vito vinavyotengenezwa kutokana na magamba yao na kutumiwa kama chakula, paua wanaweza pia kutokeza lulu zenye kung’aa. Ni vigumu kupata lulu za asili katika paua wanaoishi baharini. Lakini wanaweza kutokezwa kupitia mbinu iliyobuniwa katika miaka ya 1890 na mwanasayansi Mfaransa Louis Boutan. Kito chenye umbo la yai kilicho na rangi za kuvutia kama za gamba la paua hutokezwa. Mbinu hiyo hufanya kazi jinsi gani?


Vipande vya udongo, mbao, mfupa, au chuma, huwekwa ndani ya gamba la paua katika sehemu tatu, yaani, mara mbili kwenye upande na mara moja mgongoni. Pole kwa pole, paua hufunika vipande hivyo vilivyoingizwa ndani ya gamba lake kwa matabaka ya lulumizi, yaliyotengenezwa kwa kalisi kaboni, na conchiolin. Kwa angalau miezi 18, maelfu ya matabaka hutokezwa na kufanyiza lulu ndogo. (Ona sanduku lililo chini.) Inachukua miaka sita ili kufanyiza lulu kubwa. paua 1 hivi kati ya 50 hutokeza lulu ambayo imekaribia kuwa kamili. Hii ni lulu laini, yenye rangi nyangavu, na inayong’aa kwa kustaajabisha.


Bado watafiti hawajafaulu kutokeza lulu yenye umbo la mviringo kutoka kwa paua. Hiyo ni kwa sababu, tofauti na chaza, paua ana musuli katika tumbo ambao hutema kitu chochote kinachowekwa katika mfumo wake wa kumeng’enya. Huenda siku moja mtu akagundua siri ya kutokeza lulu ya mviringo.


Kwa sasa, tunaweza kufurahia vitu tunavyopata kutoka kwa samaki-gamba huyu aliye na matumizi mengi, yaani, vito vyenye kupendeza, nyama tamu, na gamba lenye rangi maridadi. Je, hatumshukuru Mungu kwa kutupa zawadi yenye kupendeza kama hiyo?—Yakobo 1:17.