Mtayarishaji

Morning Star Radio

Ijumaa, Agosti 31, 2012

UNAOMBWA KUFANIKISHA KONGAMANO LA HIGH PROFILESALAAM KATIKA KRISTO MDAU..

USHINDI SDA CHURCH WAMEANDAA KONGAMANO LINALOLENGA KUWAFIKIA KIROHO WATU MAARUFU NA VIONGOZI MBALIMBALI (High Profile).

ILI KUFANIKISHA JAMBO HILI
SABATO YA TAREHE 1st, 09, 2012 NI YA CHANGIZO KWA WASHIRIKI NA WOTE WANAOWIWA NA KONGAMANO HILI. UKIWA MMOJA WA WATU HAO UNAKARIBISHWA KANISANI USHINDI SABATO HII ILI USHIRIKIANE NASI KUBARIKI KAZI YA MUNGU.

KAMA HAUTAWEZA KUFIKA, TUNAOMBA MCHANGO/AHADI YAKO.
 KWA MAELEZO ZAIDI WASILIANA NA MCHUNGAJI ROBSON NKONKO KWA NAMBA HIZI +255 784 432 283 AU MHAZINI WA KANISA KWA NAMBA +255 754 562 984.
 
PIA WAWEZA WEKA KUPITIA ACOUNT NAMBA YA NBC BANK:

USHINDI SDA CHURCH - 011201011534.

Jumapili, Agosti 05, 2012

NADHARIA YA MUZIKI


MUZIKI NI NINI?!.
Hili ndilo swali la kwanza la kujiuliza kwa yeyote anayetaka kuigusa nyanja hii japo kwa kusoma kama historia na si kuingia katika mazoezi ya vitendo na hatimaye kuonesha kipaji chake mbele ya kadamnasi.

Hapa kila mtu anaweza kulijibu swali hili kulingana na utashi wake na uelewa alionao katika fani hii, kutokana na aliyoyaona na kuyasikia kuhusu muziki.Ikumbukwe kwamba,"sikio" ni kiungo muhimu katika mwili kinachoupokea mdundo wa ngoma kwa namna ya kipekee, na kumfanya mlengwa aanze kutikisa viungo vya mwili wake wakati mwingine pasipo mwenyewe kujijua.

Lakini kwangu mimi, kwa kutumia neno moja, nitasema.... muziki ni "SOUND"(MLIO). SOUND ndiyo inayotengeneza muziki,endapo sound hizo zitapangwa katika ufundi na umaridadi unaovutia masikioni mwa m/(wa)-lengwa. SOUND hiyo hiyo,inaweza kuwa mbaya au "kelele" masikioni endapo mtumiaji hakufanya kazi ya ziada kuzioanisha sauti ili ziwe burudani masikioni.

SOUND inaweza kutumika pia kama kiashirio cha tukio linalotegemea kutokea au lililokwisha tokea.Mfano ni kama kengele zinazoashiria tukio la Ibada makanisani, matumizi ya ngoma vijijini tangu karne nyingi zilizopita,kama njia ya mawasiliano katika matukio muhimu yanayowajumuisha wanakijiji wote.SOUND imekuwa ikitumika katika mataifa mbalimbali tangu enzi na enzi kama kiashirio.

TUNAPATAJE SOUND:)-
Tunapata sound-"mlio" kwa kugonga/kupiga kitu chochote,au kutoka kwenye milio ya ndege,maji ya bahari,magari na vyombo vingine vya usafiri. Mashine za viwandani hutoa pia milio ambayo ni milio tu hatuwezi kuiita muziki.Tunaweza kupata sound pia kutoka kwenye vyombo vya muziki vilivyotengenezwa maalum  kwa ajili ya kuutengeneza/kupiga muziki. 

Ni pale tu chombo kinapopigwa na mtaalamu anayekijua,ndipo tunaweza kusema....muziki umesikika kwakuwa,sauti ya kupendeza imeingia masikioni mwetu na kugusa hisia zetu.

TUNAWEZAJE KUTENGENEZA MUZIKI?.
Kwanza ielewekee kwamba si kila mtu anaweza kujiingiza kwenye tasnia hii, kwani "kipaji" ni kitu cha kwanza katika kujiendeleza ki-muziki.Muziki ni sanaa inayohusiana na kuufanya mlio ugeuke burudani,ni sanaa ambayo inaweza kugeuza sauti zisizo katika mpangilio kama mvumo wa maji ya bahari, kuchanganywa katika muziki uliopangwa na zikasikika kwa namna ambayo walengwa wataliwazwa.
Mwenye kipaji katika sanaa hii anaweza kukiendeleza kipaji chake kwa kuingia shule ya muziki na kujifunza namna ya kusoma lugha ya wanamuziki ambayo kwa kitaalamu inaitwa "STAFF-NOTATION". Staff-notation ni mchanganyiko wa alama mbalimbali za ki-muziki ambazo zinajenga lugha ambayo kuisoma kwake ni kuimba kwa kutumia sauti au kwa kutumia sauti ya chombo cha muziki.

Alama hizo ni kama kitambulisho cha sauti za juu ndani ya chombo cha
muziki,kwa kitaalamu tunakiita "TREBLE CLEF",au "G clef" kwani kitambulisho hiki kinaanzia kwenye noti ya G.Ukiangalia vyema kielelezo cha hapo chini utaona, mduara wa treble clef unajizungushia kwenye mstari mwekundu ambayo ni sehemu tunayopata noti ya G au cha sauti za chini kijulikanacho kwa jina la "BASS CLEF" au "F clef" kwani kinaanzia kwenye noti ya F kama duara la Fclef linavyoonesha.
Hivi ni vitambulisho muhimu sana kwani vinaziunganisha sauti za juu na za chini za muimbaji au za vyombo vya muziki, kwa kuitumia noti iitwayo C ya kati (MIDDLE C). Noti za muziki husomwa ki-alfabeti kama C,D,E,F,G,A,B,C ambayo ni sawa na kusema,DO,RE,MI,FA,SO,LA, TI,DO.Kwa kifupi hii ni ngazi (scale)  ndani yake tunapata ghani ya nyimbo.
Kisha ngazi inapovunjwa vunjwa katika vipande vipande,hapo tunapata kodi zilizo vunjwa (broken chords)ambazo husaidia kutengeneza ridhimu ya wimbo. Kutoka kwenye DO hadi DO ya juu,tunaita oktava moja(ONE OCTAVE). Vyombo vya muziki kama Piano huwa na urefu wa octave 5 hadi 6. Octave ni sauti zinazorudiana kwa kwenda juu au chini.
Musical staff
Kuna alama nyingine kama vile STAVE ni mistari mitano yenye nafasi nne,ndani ya mistari na nafasi hizi kuna noti(NOTES) ambazo zinapangwa kwenye mistari na nafasi za stave


Noti hizi zinapanda na kushuka kwa viwango vya nusu hatua (SEMI TONE) na hatua nzima (TONE). Kuna alama za noti nyingi tu,lakini nitumie noti nne ambazo ni za msingi.Kwanza ni "noti nzima" yenye umbo la yai( WHOLE NOTE)ambayo ina idadi ya mapigo manne. 
Hicho kitofali cheusi ni pigo la kimya (REST) ambalo lina thamani sawa na noti nzima. Noti ya pili ni nusu noti(MINIM ) yenye idadi ya mapigo mawili, noti hii ina umbo la yai tupu lenye mkia upande wake wa kulia. Noti ya tatu ni robo noti(CROTCHET ) yenye umbo kama la nusu noti ila tofauti yake ni kwamba robo noti tumbo lake lina giza na mkia kama wa nusu noti upande wa kulia Thamani yake ni pigo moja.
File:Music-eighthnote.png
 
Noti ya nne ni kinane(QUAVER )inafanana kabisa na robo noti ila mkia wake una alama ya "kibendera kinachopepea,ikiwa na thamani ya nusu pigo.Pigo lake la kimya linaonekana na alama kama unavyoiona kwenye chati hapo chini.

Kuna noti nyingi tu lakini katika mada hii nitaishia kuitambulisha noti yenye idadi ya robo pigo,ambayo kwa kitaalamu tunaiita SEMIQUAVER. Noti hii ni sawa kabisa na  kinane lakini ina bendera mbili zinazopepea katika mlingoti wake. Tuiangalie umbo lake.
Bado kuna utitiri wa alama zinazojenga staff-notation ziweze kuimbika kikamilifu, kama Vipandisho"SHARPS", kama unavyoiona(). Sharp, hutumika kuipandisha noti na viteremsho "FLATS " kama unavyokiona (♭), hutumika kuishusha noti. Sharp huipandisha noti kwa kiwango cha nusu hatua(SEMITONE)  au hatua nzima(TONE) kwenda juu au chini. Vilevile Flat huishusha noti katika kiwango cha nusu hatua au hatua nzima.
Naturals
Pia kuna alama inayoitwa (NATURAL )inayofuta alama ya flat au sharp iliyotumika mbeleni inapotakiwa i-lie kama noti ya awaida(natural). Utitiri wa alama ni mwingi lakini kwa mada ya leo, hizi nilizotaja zinatosha.

Hapa nazipanga noti zote zikionekana kwa sura, idadi ya mapigo yake pamoja na alama zake za mapigo yake ya kimya(Rests) kwenye chati ifuatayo. Mapigo ya kimya ni muhimu sana katika muziki kwani huufanya wimbo uwe na mlingano uliowiana.
Kila pigo la noti lina pigo lake la kimya kama ninavyoorodhesha kwenye chati hii.

Ndani ya STAVE, vyumba mblimbali hugawanywa kulingana na mwendo(Tempo) wa wimbo na mapigo yake ili yasizidiane na kuufanya wimbo au muziki uwe katika uwiano uliolingana sambamba na mapigo. Mlingano huu kwa kitaalamu tunauita Time signature kama mfano huu unavyoonesha.
Ukijua kusoma na kuandika muziki,inasaidia kutengeneza muziki kwa kuandika kwa kutumia alama hizi, ambazo zinasomwa katika somo la nadharia ya muziki (Theory of music). Kujua kusoma na kuandika muziki kunamfanya mwanamuziki awe na upeo mkubwa katika uelewa wa miziki ya namna mbalimbali duniani.

Mwanamuziki asiyejua kusoma na kuandika muziki, anaweza kutunga wimbo kwa kutumia hisia na kipaji Mungu alichompandikizia kwenye damu yake lakini...., upeo wake utakuwa finyu katika kuielewa aina nyingine ya miziki duniani.
Hata wakati wa kukopi nyimbo, kuna baadhi ya nyimbo ambazo zimetungwa kwa kutumia utaalamu wa juu kwa mfano miziki ya classic ambayo watunzi wake hutumia ufundi na utaalamu wa kisomi kuitengeneza.

Miziki ya aina hii haiwezekani kuikopi kwa kutumia masikio pekee,ina utaalamu mwingi wa kisomi katika tasnia ya uandishi wa muziki.Kujua kusoma muziki ni nyongeza itakayomuwezesha mwanamuziki "kuelea" ndani ya anga ya muziki popote duniani,ingawa pengine anaweza kuikosa "feeling" halisi.

Mfano mzungu ajuaye kusoma na kuandika muziki,anapewe noti zilizoandikwa muziki wa kiutamaduni wa Wagogo. Haiyumkini, ataweza kuupiga lakini hawezi kuupiga kama mgogo mwenyewe kutokana na kukosa "feeling". Cha muhimu hapa ni kwamba "angalau atajitahidi. Lakini kwa asiyejua kabisa kusoma na kuandika muziki, atanawa mikono na kushindwa kabisa kuusoma muziki ulioandikwa.

Wanamuziki waliokosa elimu ya muziki, huweza kupiga miziki iliyo katika mahadhi ya maeneo ya nchi  walizokulia. Kusikia miziki ya aina fulani tangu utotoni, kunamjengea mwanamuziki mazingira ya uwepo wa milio ya miziki hiyo katika nafsi yake. Kitu ulichozoea kukisikia tangu utotoni, ni rahisi kukifuatisha kama kipaji kipo hata kama husomi na kuandika muziki.

FUNGUO (KEYS ) NA CHORD (KODI) ZA MUZIKI.
Funguo zinafanya wanamuzuki waweze kupiga muziki wakipita kwenye mstari mmoja. Funguo ni kama barabara inayowawezesha wanamuziki kuendesha gari lao (muziki) juu yake. Funguo ni kipimo cha kiwango cha sauti iliyo chini na iliyo juu.
Kwa mfano waimbaji wenye kuimba sauti za juu, hupendelea key za juu kulingana na uwezo wa sauti zao. Waimbaji wenye sauti nzito, huchagua key za chini ili wasikwame wakati wanapoimba sehemu iliyo juu katika wimbo.

Chord hutumiwa zaidi na wapiga vyombo ili kuufanya wimbo usikike na uzito. Chord moja inaweza kuwa na idadi ya noti tatu hadi nne zinazopigwa kwa pamoja ili kumjengea muimbaji mazingira mazuri katika uimbaji wake. Chord huonekana kama hivi.

Kuna Chord za namna nyingi kutegemeana na uamuzi wa mtunzi, Chord zinaweza kuubadilisha wimbo mbaya ukasikika vizuri masikioni. Chord zinaweza kuufanya wimbo uwe wa huzuni au wa furaha. Ili kuufanya wimbo uwe wa huzuni, tunatumia kodi zinazoitwa "minor chords" au kodi ndogo. Kuna aina nyingi ya kodi zinazotumika kulingana na melody (ghani) ya mtunzi.

Kuna kodi zilizoongezwa (augmented chords), kodi zilizopunguzwa (diminished chords), kodi ndogo za seventh  zilizoongezwa flat katika noti ya 5 (minor seventh flat 5), au kodi kuu ambazo noti ya tano inawekewa alama ya flat (major seventh flat 5). Kuna kodi kuu na ndogo za kawaida. Hili ni somo pana sana ambalo linamchukua mwanafunzi wa muziki miaka kadhaa kabla ya kujua kodi zote na namna ya kuzitumia katika chombo chake.

VYOMBO VYA MUZIKI NA MAKUNDI YAKE.
Vyombo vya muziki vimetengenezwa na kugawanywa katika makundi manne makubwa,makundi haya yanagawanywa kulingana na nini kinachokiwezesha chombo kutoa mlio wake. Kundi la kwanza ni STRINGS INSTRUMENTS-vyombo hivi vinategemea NYUZI ili tupate sauti zake,kama vile gitaa na violin kama unavyoona picha. 

violin
Kundi la pili linaitwa "MEMBRANOPHONES"-hivi ni vyombo vinavyotegemea sana "mtetemo wa NGOZI ili viweze kutoa sauti zake,Wengine huita "Percussion". Ngoma za namna zote au hata drums inayotumika sana kwenye muziki wa dansi inapatikana kwenye kundi hili.
                       
Kundi la tatu linaitwa "IDIOPHONES" au kwa kiswahili chepesi ni vyombo vya kugongwa kama kengele, marimba nk. Kundi la mwisho linaitwa "AEROPHONES"-hivi ni vyombo vinavyotumia hewa ili vitoe sauti yake. Saxaphoni, filimbi, tarumbeta na vinginevyo vinaangukia kwenye kundi hili.
Kila chombo kimetengenezwa tofauti na namna ya kujifunza ni tofauti,ingawa vyote vinatoa sound na vinaweza kupigwa kwa pamoja katika bendi kubwa yenye wanamuziki wengi yaani "ORCHESTRA". Mpigaji wa chombo hiki si lazima awe anajua na kile kwani mazingira ya kujifunza ni tofauti kabisa. 
 

Kwa leo nimeona haya machache yanaweza kuwa msaada kwa yeyote anayependa kujifunza japo mawili matatu kuhusiana na tasnia hii. Siku zijazo nitaendelea na sehemu ya pili ya mada hii, ambapo tutaingia ndani zaidi, kujifunza mwendo wa mapigo na alama nyingine za muziki.