KATIKA miongo kadhaa iliyopita
sinema nyingi zenye mafanikio zimetokezwa huko Hollywood. Hilo limekuwa
na uvutano mkubwa ulimwenguni pote kwani sinema nyingi za Marekani
hutazamwa katika nchi nyingine majuma machache au hata siku chache tu
baada ya kuonyeshwa kwa mara ya kwanza nchini Marekani. Sinema fulani
hata zimeonyeshwa kwa mara ya kwanza tarehe ileile duniani kote. Dan
Fellman, rais wa usambazaji wa filamu nchini Marekani wa shirika la
Warner Brothers anasema hivi: “Soko la ulimwenguni kote la uuzaji wa
sinema linazidi kukua nalo linasisimua sana, kwa hiyo tunapotengeneza
sinema, huwa tunaitengeneza kwa ajili ya soko la ulimwenguni kote.” Sasa
kuliko wakati mwingine wowote, kile kinachotendeka huko Hollywood
huathiri biashara ya sinema ulimwenguni.
Lakini kupata faida kutokana na
sinema si rahisi kama unavyowazia. Sinema nyingi zinahitaji zaidi ya
dola milioni 100 ili kulipia gharama ya kuzitengeneza na kuziuza. Na
kufanikiwa kwake kunategemea watazamaji ambao mtu hawezi kutabiri
watapendezwa na nini. David Cook, profesa wa masomo ya sinema katika
Chuo Kikuu cha Emory anasema hivi: “Huwezi kujua ni lini jambo fulani
litawavutia au kuwasisimua watazamaji.” Kwa hiyo watengenezaji wa sinema
huongezaje uwezekano wa sinema yao kufanikiwa? Ili kupata jibu,
tunahitaji kuelewa mambo machache ya msingi yanayohusika katika
utengenezaji wa sinema.
Matayarisho Yanayofanywa Kabla ya Kutengeneza Sinema
Mara nyingi, matayarisho
yanayofanywa kabla ya upigaji picha ndiyo sehemu muhimu zaidi ambayo
huchukua muda mrefu katika utengenezaji wa sinema. Kama tu ilivyo na
mradi wowote mkubwa, mafanikio yake hutegemea sana matayarisho.
Inatumainiwa kwamba pesa zozote zinazotumiwa wakati wa matayarisho
zitapunguza sana gharama za kutengeneza sinema yenyewe.
Kutengenezwa kwa sinema huanza na
hadithi fulani ambayo huenda ikabuniwa au ikategemea matukio halisi.
Mwandikaji huandika hadithi hiyo kwenye hati. Hati hiyo inaweza
kufanyiwa marekebisho mengi kabla ya hati ya mwisho kutokezwa. Hati hiyo
ya mwisho huwa na wahusika pamoja na maelezo mafupi kuhusu kitendo
kitakachofanywa. Pia hati hiyo hutoa maagizo mengine kama vile mahali
ambapo kamera zitakuwa na mabadiliko yatakayofanywa katika kila onyesho.
Hata hivyo, hati hiyo inapokuwa katika hatua za kwanza, mtayarishaji atakayeinunua huanza kutafutwa.
Mtayarishaji anaweza kupendezwa na hati ya aina gani? Kwa kawaida
sinema ambayo hutolewa msimu wa kiangazi hukusudiwa iwavutie vijana wa
kati ya miaka 13 hadi 25 hivi. Kwa hiyo mtayarishaji atapendezwa hasa na
sinema ambayo itawavutia vijana.
Hati inayofaa hata zaidi ni ile
itakayowavutia watu wa umri mbalimbali. Kwa mfano, bila shaka sinema
inayotegemea shujaa anayetajwa katika vitabu vya vibonzo itawavutia
watoto wadogo ambao wanamfahamu shujaa huyo. Na bila shaka wazazi wao
wataambatana nao kuitazama sinema hiyo. Lakini watengenezaji wa sinema
huwavutiaje vijana walio na umri wa kati ya miaka 13 na 25 hivi? Katika
gazeti The Washington Post Magazine, Liza Mundy anasema kwamba
“habari inayosisimua” ndiyo jambo muhimu. Ili sinema “ilete faida kubwa
na kuwavutia watu wa umri mbalimbali bila kupuuza yeyote,” lugha chafu,
jeuri nyingi, na picha nyingi za ngono hutiwa ndani.
Mtayarishaji akiona kwamba hati
inaweza kuwa sinema nzuri, huenda akainunua na kumpa kandarasi mwelekezi
na mwigizaji maarufu. Kuwa na mwelekezi na mwigizaji maarufu kutafanya
sinema hiyo ivutie sana wakati itakapotolewa. Hata katika hatua hii ya
kwanza, waelekezi na waigizaji maarufu wanaweza kuwavutia wawekezaji
wanaohitajika ili kugharimia utayarishaji wa sinema hiyo.
Hatua nyingine ya matayarisho ni
kuchora vibonzo mbalimbali vya filamu hiyo hasa vile vinavyohusisha
mapigano. Michoro hiyo humwongoza mpiga-picha za sinema nayo husaidia
kupunguza wakati unaotumiwa kupiga picha. Mwelekezi aliye pia mwandikaji
wa hati, Frank Darabont, anasema: “Hakuna jambo baya zaidi kama
kupoteza wakati wa kupiga picha kwa sababu tu ya kutojua mahali ambapo
kamera inapaswa kuwa.”
Kuna mambo mengine mengi muhimu
yanayopaswa kushughulikiwa wakati wa matayarisho. Kwa mfano, picha
zitapigiwa wapi? Je, itakuwa lazima kusafiri? Je, kuna picha
zitakazopigwa ndani ya nyumba, nayo itapambwaje? Je, mavazi maalumu
yatahitajika? Ni nani atakayeshughulikia mwangaza, kupamba na
kutengeneza nywele za waigizaji? Na vipi kuhusu sauti, madoido, na yule
atakayeigiza sehemu hatari badala ya mwigizaji mkuu? Hayo ni baadhi ya
mambo yanayohitaji kufikiriwa hata kabla ya kupiga picha za filamu.
Ukitazama majina yanayoonyeshwa mwishoni mwa sinema inayotazamiwa kuleta
faida kubwa, huenda ukaona kwamba mamia ya watu walihusika
kuitayarisha! Fundi mmoja wa mitambo ambaye amehusika katika kutengeneza
sinema nyingi anasema kwamba “watu wengi sana huhusika katika
kutengeneza filamu nzuri.”
Kutengeneza Sinema Yenyewe
Kupiga picha za sinema kunaweza
kuchukua wakati mwingi, kunaweza kuchosha, na pia kunaweza kugharimu
pesa nyingi. Kwa kweli, kupoteza dakika moja tu kunaweza kugharimu
maelfu ya dola. Nyakati nyingine inabidi waigizaji, wafanyakazi, na
vifaa visafirishwe hadi sehemu ya mbali. Hata hivyo, haidhuru picha hizo
zitapigiwa wapi, lazima pesa nyingi sana zitatumika kila siku.
Watu wanaoshughulikia mwangaza,
wale watakaowapamba na kuwatengeneza nywele waigizaji huwa kati ya watu
wa kwanza kufika mahali ambapo picha zitapigiwa. Kila siku ya kupiga
picha, waigizaji wakuu hupambwa kwa saa kadhaa. Kisha picha hupigwa kwa
siku nzima.
Mwelekezi husimamia kwa
uangalifu kupigwa picha kwa kila onyesho. Inaweza kuchukua siku nzima
kupiga picha za onyesho fupi sana. Picha za maonyesho mengi katika
sinema hupigwa kwa kutumia kamera moja, kwa hiyo, onyesho moja linaweza
kupigwa picha kadhaa kutoka pembe tofauti-tofauti. Isitoshe, huenda
onyesho lilelile likapigwa picha mara kadhaa ili kupata picha bora zaidi
au kurekebisha tatizo la kiufundi. Ikiwa onyesho ni refu, huenda
picha 50 au zaidi zikapigwa! Kwa kawaida, mwishoni mwa kila siku,
mwelekezi huchunguza picha zote na kuamua ni zipi zitakazotumiwa. Kazi
ya kupiga picha inaweza kuchukua majuma au hata miezi kadhaa.
Hatua ya Kuunganisha Sinema Iliyotengenezwa
Katika hatua hii, picha zilizopigwa huboreshwa na kupangwa zinavyopaswa kufuatana. Kwanza, muziki utakaotumiwa huambatanishwa na sinema hiyo. Kisha, mhariri huunganisha sehemu za sinema hiyo na kufanyiza nakala ya kwanza isiyo kamili.
Madoido ya sauti na picha pia
huongezwa katika hatua hiyo. Nyakati nyingine kompyuta hutumiwa kutia
madoido hayo katika hatua hii ambayo ni mojawapo ya sehemu ngumu zaidi
za utengenezaji wa filamu. Kazi inayofanywa katika hatua hii inaweza
kuifanya sinema ivutie na ionekane kuwa halisi.
Muziki uliotungwa hasa kwa ajili
ya sinema hiyo huongezwa katika hatua hiyo, na jambo hilo ni muhimu
katika filamu za leo. Edwin Black anaandika hivi katika gazeti Film Score Monthly:
“Sasa watengenezaji wa sinema hutaka muziki uliotungwa hasa kwa ajili
ya sinema, nao hawataki muziki wa dakika ishirini tu au vipindi vifupi
vya muziki, bali wao hutaka muziki utakaochezwa kwa muda unaozidi saa
nzima.”
Nyakati nyingine filamu
iliyoboreshwa huonyeshwa watu wachache ambao wanaweza kutia ndani rafiki
za mwelekezi au wafanyakazi wenzake ambao hawakuhusika katika
kutengeneza filamu hiyo. Ikitegemea jinsi watakavyoitikia, mwelekezi
anaweza kupiga picha upya maonyesho fulani au kuyaondoa kabisa. Katika
visa fulani, umalizio wote wa filamu ulibadilishwa kwa sababu watu
walioitazama kwanza hawakuupenda.
Hatimaye, filamu iliyokamilika
huonyeshwa kwenye majumba ya sinema. Ni wakati huo tu ndipo inaweza
kujulikana ikiwa sinema hiyo itafanikiwa au haitafanikiwa, au itakuwa ya
wastani. Lakini mambo mengi yanahusika kuliko kupata faida. Sinema
kadhaa zikikosa kufanikiwa zinaweza kuharibu sifa ya mwelekezi na
matarajio ya mwigizaji kupata kazi. Anapofikiria miaka yake ya mapema ya
kutengeneza filamu, mwelekezi John Boorman anasema hivi: “Niliwaona
waelekezi wenzangu wakikosa kandarasi baada ya sinema kadhaa
walizoelekeza kukosa kufanikiwa. Ukweli wenye kusikitisha ni kwamba
katika biashara ya kutengeneza sinema, usipowaletea faida mabwana zako,
unapoteza kazi yako.”
Bila shaka, watu wanapotazama
ubao wa kutangazia sinema, kwa ujumla hawafikirii ikiwa watengenezaji wa
sinema hiyo watapoteza kazi zao au la. Yaelekea wao huhangaikia mambo
kama: ‘Je, nitafurahia sinema hii? Je, inafaa nitumie pesa zangu ili
kuitazama? Je, sinema hii itanivutia au itanichukiza? Je, inawafaa
watoto wangu?’ Unaweza kujibuje maswali hayo unapoamua sinema
utakazotazama?
[Maelezo ya Chini]
Anita Elberse,
ambaye ni profesa wa Chuo cha Biashara cha Harvard, anasema kwamba
“ingawa mara nyingi pesa zinazopatikana kutokana na mauzo ya sinema
katika nchi za ng’ambo ni nyingi kuliko zile za mauzo nchini Marekani,
jinsi watu wanavyoipokea sinema nchini Marekani huamua jinsi
itakavyopokelewa katika nchi nyingine.”
Ingawa huenda njia
ambazo hutumiwa kutengeneza sinema zikatofautiana, mambo yanayoelezwa
hapa yanaonyesha njia moja inayoweza kutumiwa.
Nyakati nyingine
mtayarishaji hupewa muhtasari wa hadithi badala ya hati yenyewe. Ikiwa
atavutiwa na hadithi hiyo, anaweza kununua haki za kuimiliki na
kuitengeneza kuwa hati.
“Huwezi kujua ni lini jambo fulani litawavutia au kuwasisimua watazamaji.”—David Cook, profesa wa masomo ya sinema
JINSI YA KUFANYA SINEMA IVUTIE NA ILETE FAIDA KUBWA
Sinema imekamilishwa. Iko
tayari kutazamwa na mamilioni ya watu. Je, itafanikiwa? Fikiria njia
mbalimbali ambazo watengenezaji wa sinema hutumia ili sinema yao ivutie
na ilete faida kubwa.
▪ UVUMI: Mojawapo ya njia
zenye mafanikio za kuwafanya watu wawe na hamu ya kutazama sinema
fulani ni kupitia uvumi. Nyakati nyingine uvumi kuhusu sinema fulani
huanza miezi kadhaa kabla ya sinema hiyo kuonyeshwa kwa umma. Huenda
ikatangazwa kwamba kutakuwa na sinema itakayokuwa mwendelezo wa sinema
fulani iliyofanikiwa hapo awali. Je, itakuwa na waigizaji walewale
maarufu wa sinema ya awali? Je, itakuwa nzuri (au mbaya) kama ile ya
kwanza?
Katika visa fulani, uvumi
huanzishwa kuhusu jambo fulani katika sinema, labda kuonyesha picha za
ngono waziwazi katika sinema itakayotazamwa na watu wote. Je, sinema
hiyo ni mbaya sana? Je, sinema hiyo imepita mipaka kabisa? Watengenezaji
wa sinema hunufaika watu wanapotoa maoni mbalimbali yanayopingana
kuihusu, kwa kuwa hiyo ni njia moja ya kuitangaza bila malipo. Nyakati
nyingine mijadala hiyo huwafanya watu wengi waitazame sinema hiyo
inapoonyeshwa kwa mara ya kwanza.
▪ VYOMBO VYA HABARI: Njia
za kawaida za kutangaza sinema zinatia ndani mabango, matangazo ya
magazeti, matangazo ya biashara ya televisheni, kuonyeshwa kwa sehemu
ndogo ya sinema hizo katika majumba ya sinema kabla ya sinema nyingine,
na kasheshe. Sasa Intaneti imekuwa njia kuu ya kutangaza sinema.
▪ KUUZA BIDHAA: Kuuza
bidhaa zinazotangaza sinema fulani kunaweza kuifanya ivutie inapotolewa.
Kwa mfano, sinema moja iliyotegemea shujaa anayetajwa katika kitabu
fulani cha kibonzo ilitangazwa katika vifaa vya kubebea vyakula,
vikombe, vito, mavazi, minyororo ya funguo, saa, taa, na michezo ya
dama, na kadhalika. Joe Sisto anaandika hivi katika jarida la vitumbuizo
la Shirika la Mawakili la Marekani: “Kwa kawaida, asilimia 40 ya bidhaa
za kutangaza sinema huwa zimeuzwa hata kabla ya sinema hiyo kutolewa.”
▪ KANDA ZA VIDEO: Sinema
ambayo haileti faida kubwa inapoonyeshwa katika majumba ya sinema
inaweza kuleta faida inaporekodiwa katika kanda za video. Bruce Nash,
ambaye huchunguza faida zinazotokana na sinema anasema kwamba “kanda za
video huchangia asilimia 40 hadi 50 ya mapato ya sinema.”
▪ VIWANGO VYA SINEMA:
Watengenezaji wa sinema wamejifunza kutumia viwango vinavyowekwa vya
sinema ili kujifaidi. Kwa mfano, huenda mambo fulani yakaingizwa
kimakusudi katika sinema ili kuifanya iwekewe kiwango cha juu zaidi
kinachowafaa watu wazima pekee. Kwa upande mwingine, sehemu chache
zinaweza kuondolewa ili sinema isipewe kiwango cha watu wazima na
kuifanya iwavutie vijana. Liza Mundy anaandika katika gazeti The Washington Post Magazine
kwamba kuwekea sinema kiwango cha vijana “kumekuwa njia ya kutangaza
sinema: Majumba ya kurekodia sinema hutumia kiwango hicho kupitisha
ujumbe kwa vijana na watoto wanaotamani sana kuwa vijana kwamba sinema
hiyo itakuwa yenye kuvutia sana.” Mundy anasema kwamba kiwango hicho
“hutokeza uvutano kati ya mzazi na mtoto kwani humwonya mzazi na
kumvutia mtoto.”
JINSI SINEMA ZINAVYOTENGENEZWA
HATI
MICHORO
MAVAZI
KUPAMBWA
UPIGAJI PICHA
KUTIA MADOIDO
KUREKODI MUZIKI
KUINGIZA SAUTI
KUTENGENEZA VIBONZO KWA KUTUMIA KOMPYUTA
KUBORESHA NA KUPANGA PICHA