Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumapili, Februari 17, 2013

TEKNOHAMA -KOMPYUTA HUTUMIA UMEME ILI IWEZE KUFANYA KAZI


Kwa kawaida vyombo vingi vinavyorahisisha kazi hutumia kazi hutumia umeme ili viweze kuleta ufanisi katika shughuli mbalimbali. Kompyuta nayo hutumia umeme katika kutekeleza majukumu yake. Umeme huu huingizwa kwa kutumia nyanya (cable) ambazo hutoa umeme kutoka katika soketi zilizopo mahali husika. Umeme huu hupitia chombo maalum kifahamikacho kama power supply

Chombo hiki huwa kimeunganishwa kuelekea motherboard na sehemu nyingine muhimu. Kwa kawaida umeme huu hubadilishwa kutoka mfumo wa kubadilika badilika (alternating current a.c) kwenda mfumo wa moja kwa moja (direct current d.c) ambao kompyuta inaweza kuutumia. Umeme huu hugawanywa katika kiwango kinachotakiwa kulingana na matumizi ya sakiti husika.

Ijumaa, Februari 15, 2013

TEKNOHAMA - KOMPYUTA IMEGAWANYIKA KATIKA SEHEMU INAYOSHIKIKA NA SEHEMU ISIYOSHIKIKA!


Photo Credity By: http://metrology.zeiss.com

 Hakika kompyuta ni kifaa kilichoundwa katika utaalam wa hali ya juu. Unapokuwa unaitazama kompyuta, yaani unapokuwa unaiona monitor, keyboard, case na vinginevyo unakuwa unaona sehemu ya ‘nje’ ya kompyuta. Unakuwa unaiona sehemu ijulikanayo kama hardware part. Hardware part ni sehemu ambayo unaweza kuishika na kuiona kwa macho. Ni sehemu ambayo ni hard au ‘ngumu’ kwa maana ya kwamba inaonekana na kuweza kubebwa na kufanyiwa marekebisho. Sehemu hii ya kompyuta haiko peke yake katika ufanyaji kazi wa kompyuta.

Yenyewe kama ilivyo haiwezi kufanya lolote; ni kopo lisilo na maana! Ni kama unaponunua baiskeli na kuiweka ndani. Itakuwa na manufaa kwako endapo tu utaiendesha. Ni kama unapokuwa na gari ambalo bado halina mafuta. Ili liweze kujongea utahitaji kuliwekea mafuta. Vivyo hivyo kompyuta haitaweza ‘kujiendesha’ yenyewe bila kuwa na muendeshaji (ambaye ni wewe). Kompyuta haitaweza kufanya kazi kama itakuwa na hardware part peke yake. Ni lazima kuwe na muendeshaji wa hardware part hiyo.

Sehemu ya kompyuta ambayo ni muhimu sana katika kuifanya ifanye kazi iliyokusudiwa ni ile ‘isiyoonekana’. Ni sehemu ambayo huwezi kuiona na inajulikana kama software part. Tazama jinsi maneno yalivyotumika: hardware na software ambayo yanatia msisitizo katika ‘ugumu’ na ‘ulaini’. Sofware ni mkusanyiko wa maelekezo maalum ambayo kompyuta hupewa ili kuiwezesha kufanya kazi kulingana na maelekezo hayo. Kwa jina jingine software inafahamika kama computer

Ni namna gani software na hardware hufanya kazi kwa ushirikiano?

Kama nilivyosema hapo awali hardware part ya kompyuta ni mkusanyiko wa sakiti mbalimbali ambazo zimeunganishwa katika mfumo maalum unaoiwezesha kompyuta kufanya kazi. Lakini ni lazima sakiti ya kompyuta ipewe maelekezo maalum ili iweze kufanya kazi. Ni kama kuiamuru runinga yako ioneshe kituo Fulani cha matangazo ambacho unataka kutazama. Kwa kutumia dhana hii wataalam wa mambo ya kompyuta waliamua kutumia mkusanyiko wa maelekezo uitwao software ili kufanikisha hili. Software ni mkusanyiko wa maelekezo mbalimbali yaliyogawanyika kulingana na kazi yanayotakiwa kufanya. Kuna maelekezo ya kuwasha kompyuta, kuna maelekezo ya kuizima kompyuta, kuna maelekezo ya kutoa ishara za hatari, maelekezo ya kutoa mlio na kuacha kutoa mlio, maelekezo ya kuandaa picha za video na za kawaida, maelekezo ya kuhifadhi habari zinazoandaliwa na mengine chungu nzima. Hii inamaansiha kuwa kuna software tofauti tofauti kulingana na kazi zinazotakiwa kufanya. Kuna software ya kuandikia, software ya kupigia mziki, software ya kuendeshea mitambo, software ya kutengeneza sauti, softwares za kuendesha mitambo mbalimbali kama robots, ndege, camera za ulinzi nk.

Mkusanyiko wa software mbalimbali hufanya vipi kazi katika hardware?

Software zote huunganishwa na kupangiliwa kufanya kazi kwa kutumia software kuu ijulikanayo kama system software au operating system kwa kifupi OS. OS ni maelekezo mama ambayo huingizwa katika kompyuta mara tu kompyuta inapokuwa imetengenezwa. Ni maelekezo ambayo huiendesha kompyuta katika kupokea na kutoa maelekezo mengine ambayo binadamu hutaka ifanye. OS ndiyo huiwasha kompyuta na kuiweka katika hali tayarifu kwa ajili ya kufanya kazi. Kifuatacho ni sehemu ndogo ya kile ambacho OS hufanya unapotaka kuitumia kompyuta: Unawasha kompyuta kwa kubonyeza kitufe cha kupokea umeme Umeme hutiririka katika sakiti nzima ya kompyuta OS hufahamu kuwa umeme umeingia hivyo huiwasha kompyuta OS hutizama kama kila sehemu muhimu ya kompyuta ipo kwa mfano keyboard, mouse, monitor n.k

Baada ya muda kompyuta inakuwa tayari imewashwa na iko tayari kufanya kazi ikimsubiri mtumiaji ailekeze nini cha kufanya. Mtumiaji wa kompyuta hutumia peripheral devices kama keyboard na mouse katika kuilekeza kompyuta ifanye kile anachokihitaji. Na hao ndipo panakuwa na maelekezo mengine ambayo niliyazungumzia hapo mwanzo. Kwa mfano kama mtumiaji anataka kuandika barua basi itambidi aanzishe maelekezo yatakayomwezesha kuandika barua hiyo. Maelekezo haya madogodogo hutekelezwa na programu ndogo inayfanya kazi pamoja na programu mama ikijulikana kama application software. Kwa maana hii tunaweza kusema kuwa software part ya kompyuta imegewanyika katika sehemu kuu mbili; system software na application software.

Je, maelekezo haya yajulikanavyo Kama application software na system
software hueleweka vipi ndani ya kompyuta?

Kwa hakika unaweza kujiuliza ni vipi maelekezo haya hutambulika na sakiti ndogondogo za kompyuta. Lakini ni dhana rahisi tu kuilewa. Ni kama wewe unapozungumza na mtu ambaye hatumii lugha unayoizungumza. Itakubidi uzungumze na mtu huyo kwa kutumia mfasiri (mkalimani). Vivyo hivyo maelekezo ya kompyuta inabidi yatafsiriwe na kuwekwa katika mfumo ambao hardware ya kompyuta itayaelewa. Lakini jambo moja la kufahamu ni kwamba maelekezo haya huandaliwa au kuandikwa kwa utaalamu maalum ili yaweze kueleweka katika kompyuta.

Utaalam huu hutumiwa na wanasayansi wa kompyuta. Utaalam huu hufahamika kama programming. Utaalamu huu hutumia lugha maalum ammbazo si kama zile tuzitumiazo katika maisha ya kawaida katika kuwasiliana. Lugha hizi zina herufi na namba ambazo tunazifahamu (A mpaka Z na 0 mpaka 9) ukijumuisha na alama kadhaa kama mkato, nukta, mabano na nyingine nyingi ambazo ni nadra kutumika katika maandishi ya kawaida ya lugha. Mkusanyiko wa herufi na namba hujulikana kama codes na uandikaji wake hufahamika kama coding. Kwa lugha ya kawaida ya kimombo neno codes humaanisha maneno ya siri yasiyoweza kufahamika kwa urahisi na watu wengine isipokuwa wale wachache wenye utaalam maalum waliousomea. Kwa hiyo lugha hizi za kuandikia maelekezo ya kompyuta hufahamika kama programmming languages. Hivyo ni lugha hizi ambazo huifanya kompyuta kujengewa maelekezo ambayo itayatambua na hatimaye kuweza kufanya kazi. Kwa hapa nchini utaalam wa lugha hizi hujifunza katika vyuo mbalimbali nchini kama kile chuo kuku cha Dar es Salaam. Mfano wa lugha hizi za kompyuta ni kama Java, Visual Basic, PHP na C.

Je Kompyuta inayaelewa vipi Maelekezo Haya?

Maelekezo yanayowekwa ndani ya kompyuta hayawezi kuelewekwa moja kwa moja ndani ya sakiti za kompyuta. Yanapaswa kutafsiriwa katika mfumo ambao kompyuta inaweza kuyaelewa. Katikati ya hardware part na software ya kompyuta kuna maelekezo maalum yajulikanayo kama assembler ambayo hufanya kazi ya kutafsiri software part kwenda katika sakiti ya kompyuta. Sakiti ya kompyuta haiwezi kutambua maelekezo yanayokuwa na herufi au namba (ambayo software huundwa) bali hutambua mtiririko wa namba mbili maalum ziandikwazo kama 0 na 1. Kwa hiyo assembler hubadilisha herufi na namba kwenda namba mbili 0 na 1. Kwa mfano neno ‘do’ linaweza kutafsiriwa na assember katika tarakimu 01100 ambazo sakiti ya kompyuta huielewa. Kwa namna hii kompyuta huweza kufanya kazi na kuleta matokeo yanayotarajiwa.

Je Maelekezo au software hutunzwa wapi ndani ya Kompyuta?

Tuliona kuwa kompyuta hutunza kumbukumbu. Na ni uwezo wa kompyuta kutunza kumbukumbu ndiyo unaifanya kuwa chombo cha kipekee katika ulimwengu huu ambacho kinaweza kufananishwa na ubongo wa binadamu na hata kufanya kazi kwa ufanisi. Kumbukumbu za kompyuta hutunzwa katika mfumo wa ki-elektroniki katika kifaa maalum kilicho ndani ya system unit kifahamikacho kama hard disk. Kifaa hiki kina uwezo wa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu na kimeundwa katika mfumo ambao unaruhusu kufuta, kurekebisha na kuandika tena kumbukumbu; kuongeza na kupunguza kumbukumbu. Ni kifaa muhimu katika kompyuta. Huwa kimeunganishwa na motherboard kwa kutumia waya maalum. Kifaa kifahamikacho kama hard disk

Alhamisi, Februari 14, 2013

LICHA YA KUWAPO AINA KUU NNE; KOMPYUTA ZIMEUNDWA KATIKA MSINGI MMOJA!


Licha ya kuwa na aina za kompyuta lakini bado kuna msingi ambao zote huutegemea. Msingi huo ni kuwa na sehemu kuu mbili; sehemu kuu ya kutengeneza habari kutokana na data zilizoingizwa ijulikanayo kama Central Processing Unit au CPU kwa kifupi na sehemu ya kuingizia data na kutolea habari iliyokwisha tengenezwa kwa ajili ya faida ya mtumiaji ijulikanayo kama peripheral devices. Kwa hiyo data huingizwa kupitia sehemu zinazofahamika Kama peripheral devices na kupelekwa ndani ya CPU ambako hunyumbulishwa na kufafanunuliwa na hatimaye kutoa kile kilichokusudiwa kupitia tena peripheral devices hizohizo. CPU hufanya kazi ya kufafanua data (processing) kulingana na maelekezo ya mtumiaji. Tuone sehemu mbalimbali za kompyuta ambazo huifanya kazi ya kompyuta kutekelezeka kwa ufanisi.



Ubongo wa Kompyuta (Central Processing Unit)



Hii ni sehemu maalum kabisa katika kompyuta. Ndiko ambako maamuzi yote kuhusu data na habari hufanywa ili kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda vyema. Ni kama ubongo wa binadamu ambao huamua mambo yote yanayohusiana na shughuli zote za mwili ili kumfanya aishi katika afya njema. Sehemu hii ya kompyuta huwa ndani ya kifaa kiitwacho computer case ambacho kinafunika ‘ubongo’ huu wa kompyuta. 

Computer Case inaweza kuwa bapa na yenye umbo la msitatili au mraba (kwa aina ya personal computers) ambayo huwekwa katika meza ili iweze kutumika vyema. Aina hii ya computer case inajulikana kama desktop case na ndiyo maana kompyuta huitwa desktop computer. Pia computer case inaweza kuwa na umbo lililosimama, kama umbo la mche msitatili na lijulikanalo kama Tower case – na ndiyo huzaa jina la Tower computer. Lakini kwa notebook computer na palmtop computers computer case huwa imunganishwa na sehemu ya peripheral kiasi kwamba ni vigumu kuweza kuifafanua vyema.



Ubongo wa kompyuta huwa ni muunganiko wa sehemu mbalimbali ambazo kwa pamoja huwekwa katika mfumo mmoja ujulikanao kama motherboard. Muundo wa motherboard hutofautiana kutegemeana na aina ya kompyuta (mtengenezaji) na ukubwa wa kompyuta yenyewe na hata toleo (version) la kompyuta husika. Kompyuta aina ya desktop ina motherboard tofauti na kompyuta aina ya notebook. Pia kompyuta toleo la mwaka 1995 ina muundo wa motherboard ulio tofauti na lile la toleo la mwaka 2005.



Ubongo wa kompyuta (CPU) huwa na vifaa muhimu vifuatavyo:



Kifaa ambacho ni mkusanyiko wa mamilioni ya sakiti ndogondogo zijulikanazo kama transistors. Sakiti hizi zinakwa na ukubwa wa chini ya unywele mmoja wa nywele za binadamu! Kifaa hiki ndicho ambacho kinachukuliwa kama moyo au ‘roho’ ya kompyuta. Bila kifaa hiki kompyuta haiwezi kufanya lolote. Kifaa hiki kinajulikana kwa jina la microprocessor. Ni kifaa hiki ambacho hupokea mamilioni ya maelekezo kutoka kwa mtumiaji na kuyafanyia kazi ili kutoa majibu yanayotakiwa. Kina uwezo wa kufafanua na kunyumbulisha data kwa uwezo wa hata kufikia maelekezo trilioni moja kwa sekunde! (hii ni kulingana na ukubwa na uwezo wa microprocessor hiyo kutegemeana na aina ya kompyuta).



Kifaa kingine muhimu ni kitunza kumbukumbu kijulikanacho kama random access memory chip ambacho hutunza kumbukumbu zinazofanyiwa kazi na kompyuta. Kumbukumbu hizi huhifadhiwa katika mfumo ambao ni wa muda tu; ikiwa na maana kwamba mfumo huu hupoteza kumbukumbu hizo mara tu umeme ambao unaozunguka katika sakiti nzima ya kompyuta unapotoweka. Kifaa kijulikanacho kama random acess memory



Kifaa kingine ni mkusanyiko wa nyanya ndondogo sana ambazo huunganishwa pamoja na kufungwa vyema ndani ya material aina ya plastiki. Kifaa hiki hupitisha data ndani na nje ya motherboard. Ni kama barabara ambayo inaunganisha mji mkubwa ili kufanya mawasiliano kuwapo baina ya watu. Kifaa hiki kinafahamika kama system bus.


System bus (utepe manjano)



Pia kuna vifaa mbalimbali ambavyo vinahusika na utoaji wa sauti, picha na kadhalika. Pia matundu ya aina mbalimbali ambayo huwezesha uunganishwaji wa sehemu za nje ya motherboard yaani peripheral devices.



Sehemu Za Nje ya Motherboard (Peripheral Devices)



Hizi ni sehemu ambazo zinakamilisha ufanyaji kazi wa kompyuta. Sehemu hizi ziko nje ya system case na zinakuwepo katika kompyuta kulingana na matumizi ya mtu husika ingawa kuna sehemu ambazo lazima ziwepo (basic peripheral devices). Sehemu hizi za kompyuta hujulikana pia kama sehemu za kutoa na kuingizia habari na data au kwa jina la kitaalam kama input and output devices. Sehemu hizi ni kama zifuatazo:



Sehemu ya kuingizia maneno na maelekezo maalum ijulikanayo kama keyboard. Hiki ni kifaa ambaco kina mkusanyiko wa herufi (A mpaka Z) na namba 0 mpaka 9. Kifaa hiki kina mkusanyiko wa vitufe au buttons ambazo herufi au namba hizo huandikwa. Mtumiaji wa keyboard anapaswa kubonyeza (press) vitufe hivyo ili kuweza kuingiza malekezo haya (herufi na namba) katika kompyuta. Pia keyboard huwa na buttons maalum ambazo huingiza malekezo maalum kea ajili ya ufanisi wa kazi wa kompyuta. Tutazungumzia zaidi sehemu hii.



Sehemu ya kukuwezesha kuona nini unakifanya katika kompyuta. Huwezi kwenda kwa mfano sokoni ilihali hauoni. Unahitaji kuona barabara na kufahamu soko lipo wapi ili uweze kufika kwa urahisi. Vivyo hivyo unapokuwa unatumia kompyuta au unafanya kazi na kompyuta unahitaji kuona kile unachokifanya. Unahitaji kusikia kile unachokitarajia. Sehemu hii ya kompyuta hujulikana kama monitor. Monitor ina umbo kama la runinga ambayo umezoea kuiona na kwa uhalisia teknolojia ya uundwaji wake ipo sawa na ya runinga isipokuwa marekebisho kidogo. Monitor ndipo mahala pekee pa kuweza kufahamu nini kinaendelea ndani ya kompyuta kwani shughuli zote za utengenezwaji na utoji habari huonekana katika kifaa hiki.



Sehemu ya kuweza kuingiliana na monitor na kufanya kile unachikihitaji na ambayo hufanya kazi kwa kushirikiana na keyboard ni sehemu ya tatu katika hili kundi la peripheral devices. Sehemu hii inajulikana sana kama mouse. Mouse ni kifaa ambacho mtumiaji hukitumia kuwasiliana na kompyuta (CPU) ili kuzaa au kutoa kile kinachotarajiwa. Kifaa hiki huwa na mahali ambapo unabonyeza kwa kutumia kidole na ubonyezawji wa kidole hiki husafirisha habari katika kompyuta na kuilekeza ifanye nini. Mouse huonekana katika kompyuta kama mshale na mshale huu hutembea katika monitor kumuwezesha mtumiaji kuamua nini cha kufanya. Mshale huu hujulikana kama cursor kwa kimombo.



Sehemu hizi tatu za kwanza katika kundi la peripheral devices zinategemeana na hujulikana kama basic input & output devices. Hii ina maana kwamba sehemu hizi ni lazima ziwepo ili kuifanya kompyuta ifanye kazi zilizo za muhimu. Sehemu nyingine muhimu ni zile zinazotoa na kuingiza sauti. Sehemu hizi hufahamika kama input

and output sound devices. Mfano wa sehemu hizi ni kama speakers, microphones, webcam, cameras na nyingine nyingi. Pia sehemu za kuingizia picha na kutolea picha kama cameras. Aina mbalimbali za Microphones



Sehemu nyingine muhimu ambayo ni ya muhimu sana inajulikana kama printer. Ni kifaa ambacho hutumika katika kuchapa matokeo ya ufafanuzi wa kompyuta ulio katika mfumo wa maandishi (text) kwa shughuli mbalimbali anazozihitaji mtumiaji. Kifaa hiki kina uwezo wa kutoa maandishi na picha zilizo na zisizo na rangi. Kifaa hiki kinatofautiana katika utengenezwaji kulingana na mahitaji ya watumiaji.



Sehumu tulizozizungumzia hapo juu ndizo sehemu zinazojumuisha peripheral devices. Kwa hakika sehemu hizi ni muhimu katika kuifanya kompyuta iitwe kompyuta kwani ndizo zinazowezesha kupata matokeo ambayo binadamu anayahitaji katika maisha yake.

Jumanne, Februari 12, 2013

TEKNOHAMA - KOMPYUTA INAFANYAJE KAZI?


Picha kwa hisani ya: http://www.macwallpapers.eu



Unaweza ukawa unajiuliza, ni vipi sasa kompyuta inafanya kazi kama ina sakiti ambazo zinaweza kufikia milioni kumi? Je si kifaa kilicho tata sana?

Kwa ujumla kompyuta haifanyi kazi vigumu kiasi hicho kama unavyoweza kudhani. Sakiti hizo zinaisaidia kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja na kwa haraka sana na ndiyo matarajio ya binadamu; kwamba ifanye kazi kwa haraka sana ili kufanya uzalishaji mali kuwa mkubwa. Maelekezo ambayo kompyuta inatoa na kufanya (baada ya kupewa na binadamu) ni rahisi kabisa: jumlisha namba moja na nyingine, toa data kutoka sehemu moja kupeleka sehemu nyingine, peleka habari kutoka kifaa kimoja kwenda kifaa kingine, punguza jotoridi la kifaa fulani endapo jotoridi hilo litazidi kiwango kilichowekwa na kadhalika. Maelekezo haya hufanyika Kwa haraka Sana kiasi kwamba unapata majibu unayoyataka papo kea papo!

Ni jambo moja tu ambalo linaifanya kompyuta kuwa tofauti Na mashine nyingine katika dunia hii: jambo hili Ni kwamba kompyuta inaweza kupangiliwa kufanya mambo kutokana na matakwa ya mtumiaji (can be programmed). Hii inamaanisha kuwa mpangilio wa maelekezo (a list of instructions) ambayo ndiyo huitwa programu ya kompyuta (computer program) huweza kuingizwa katika kompyuta na kuhifadhiwa na kuyatumia baadaye kulingana na matakwa ya mtumiaji. Ndiyo maana ukitaka kuandika barua katika kompyuta unafungua program inayohusika na kuanza kuandika barua hiyo. Ukimaliza unaifunga program hiyo na siku nyingine au mtu mwingine anaweza kuitumia.

Kuna aina kuu NNE za Kompyuta

Kompyuta hutofautiana Sana kulingana na kazi inayopaswa kufanya. Kompyuta inayotumika katika lift za majengo si sawa na kompyuta inayotumika katika mahospitali kusaidia kutibu wagonjwa. Kulingana na matumizi husika, kompyuta hutofautiana ukubwa, bei, uwezo wa kufanya kazi na hata uendeshwaji wake.

Aina ya kwanza ya Kompyuta

Kompyuta aina ya kwanza ni zile ambazo mara nyingi watu wa kawaida huzimiliki majumbani na maofisini na ndizo zilizo za bei ya chini, uwezo mdogo na umbo dogo zaidi kuliko aina nyingine ya kompyuta. Kompyuta hizi hujulikana kama personal computers au PC kwa kifupi. Ukitazama Kwa undani zaidi utagundua kuwa kompyuta hizi ni maalum kwa ajili ya matumizi binafsi ya mtu au kwa ajili ya kuendeshea mitambo midogo midogo kwa faida ya maisha ya kila siku ya binadamu. Kompyuta hizi hupatikana katika maumbo mbalimbali. Zipo desktop Na tower computers ambazo hupatikana mara nyingi maofisini katika meza; notebook computers ambayo hujulikana Sana Kama laptops; zipo palm tops (kompyuta za viganjani ambazo hujulikana Sana Kama PDA-Personal Digita Assistant). Hizi ndizo kompyuta ambazo mara nyingi tunaziona katika maduka na supermarkets zinazouza kompyuta. Tutakuwa Na sehemu kubwa ya kutazama juu ya kompyuta aina hii huko mbele Kwa sababu ndizo zinazotumika Na kuonekana zaidi Kwa sasa mionogni mwa watu wa kawaida.

Aina ya pili ya Kompyuta

ina ya pili ya kompyuta inajulikana kama miniframe computers. Aina hii ya kompyuta ina uwezo, na ukubwa zaidi ya aina ya kwanza na ni ghali zaidi. Ni kompyuta ambazo zimetengenezwa maalum Kwa ajili ya kufanyia kazi zinazohitaji nguvu kubwa na za haraka zaidi. Mitambo mingi ya kuendeshea mawasiliano ya habari katika majengo makubwa huendeshwa Kwa kutumia kompyuta hizi.

Aina ya tatu ya Kompyuta

Aina ya tatu ya kompyuta ni zile zijulikanazo kama Mainframe computers. Hizi ni kompyuta zenye uwezo mkubwa na zinazogharimu fedha nyingi. Hutumika katika utafiti katika maabara za kisayansi katika sehemu maalum hasa katika taasisi za utaiti na katika vyuo vikuu. Pia katika kuendesha mitambo ya kutafiti maswala ya hali ya hewa (weather forecast). Kwa mfano, pale mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) makao makuu unaweza kukuta kompyuta ya namna hii.

Aina ya NNE ya Kompyuta

ina ya nne na ya mwisho ya kompyuta ni ile iitwayo super-computers. Hizi ni kompyuta ambazo ni kubwa na zenye nguvu sana na ambazo huweza kugharimu mamilion ya dolla. Ni kompyuta hizi ambazo hutumika katika kuendesha mitambo ya kinyukilia (nuclear control) na urushaji wa maroket katika kufanya utafiti katika sayari za mbali (space exploration). Hizi kompyuta zinahitaji watu wenye utaalam wa juu katika kuziendesha na kuzifanyia marekebisho.
Kompyuta aina ya Supercomputer

Kompyuta aina ya Notebook ama Laptop

Kompyuta aina ya notebook ni kama gari dogo la kuendeshea mambo nyumbani. Kila kitu kuanzia muonekano wa nje yaani hardware, mpaka katika matumizi ya nishati ya umeme kuendeshea programs ni madogo. Kwa namna hii wataalam wa masuala ya umeme katika kompyuta ya aina hii wamefanya kazi kubwa ya kupunguza matumizi ya umeme na mahitaji ya ukubwa katika sehemu zote za kompyuta hii. Ukubwa wa kompyuta hii pamoja na matumizi ya umeme yanapunguzwa kadiri inavyowezekana. Kwa mfano hard disks za notebook computer ni ndogo kuliko hard disks za desktop computers na zinaweza kupachikwa katika upande mmoja wa system unit au kuwekwa katika sehemu ya chini ya system unit.


Katika nyakati hizi CPUs za notebook computer zijulikanazo Kama Mobile CPUs zina muundo maalum unaozitofautisha na zile za zamani. Mobile CPU Ni aina maalum ya CPU kwa kompyuta aina ya Notebook ama Laptop ambayo hubadilisha mwendokasi (wa kufafanua maelekezo) na hivyo matumizi ya umeme kwa kadiri ya kupungua au kuongezeka kwa mahitaji ya kufafanua (exection of instructions) maelekezo hayo. Kwa mfano CPU ya desktop kompyuta yenye uwezo wa kufafanua maelekezo katika mwendokasi wa 1 GH (CPU speed) inatumia kati ya wati (watts) 75 mpaka 100 za umeme ilihali CPU aina ya Mobile ya Notebook kompyuta kwa mfano SpeedStep
CPU ambayo hutumia kiwango cha wati 34 za umeme wakati notebook kompyuta hii imechomekwa katika waya ya kuingizia umeme. Hii husababisha kupunguka Kwa umeme ambao CPU huhitaji na hivyo kusababisha kuzalishwa kwa kiwango kidogo cha joto ambalo husababisha feni ya kupoza joto hilo kutumia umeme mdogo.

Feni ya CPU ya notebook kompyuta huwa haifanyi kazi muda wote Kama ilivyo Kwa feni za kompyuta za aina nyingine. Feni hufanya kazi pale tu joto linapokuwa limezidi kiwango Fulani. Kumbuka kwamba Notebook kompyuta huwa Na Betri inayoweza kutunza umeme Na hivyo kukuwezesha wewe kuitumia bila kuichomeka kwenye soketi ya umeme. Ni Kama unavyoweza kuingiza umeme kwenye simu ya mkononi Na inapokuwa umejaa unaenda zako ukitumia Na unapokuwa umekwisha unarudi Na kujaza tena.