Mtayarishaji

Morning Star Radio

Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Viumbe. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo Viumbe. Onyesha machapisho yote

Ijumaa, Desemba 05, 2014

Nyigu na Mrija Utoboao Miti






 Nyigu wa kike ambaye hutoboa miti na kutaga mayai ndani ya misonabari, amewashangaza sana wanasayansi kwa mbinu yake ya kutoboa miti na kuwachochea kubuni vifaa bora zaidi vya kufanya upasuaji kwa njia salama zaidi.

Fikiria hili: 

Nyigu huyo hutoboa msonobari kwa kutumia mrija ulio kama sindano na wenye mitaimbo miwili, au “valvu” zilizoingiana, ambapo kila moja imefunikwa kwa meno yanayoangalia nyuma. Meno ya valvu moja hushikilia mti na hivyo kumfanya asisonge, na valvu ile nyingine husonga hatua moja mbele. 

Kisha meno ya valvu hiyo ya pili hushikilia mti tena na hivyo ile valvu ya kwanza inasonga mbele. Katika mwendo huu wa kasi unaofanyika kwa kurudia-rudia—ambapo valvu hizo hubadilishana kushikilia mti na kusonga mbele—mrija huo huchimba milimita 20 hivi bila kutumia nguvu nyingi kwenye sehemu laini ya nje ya mti bila kujipinda wala kuvunjika.


Wanasayansi wamechochewa na mrija huo hivi kwamba wanabuni kifaa cha kufanya upasuaji katika ubongo ambacho kitachimba kwa kutumia mbinu hiyo. Sindano yake ya silikoni ina valvu mbili ambazo husonga mbele na nyuma, kila moja ikiwa na meno madogo ambayo yanaweza kuingia katika sehemu za ndani zaidi za ubongo bila kusababisha madhara makubwa. Hata hivyo, kifaa hicho kitaweza kufanya jambo lingine. 

Gazeti New Scientist linaeleza, “Tofauti na vifaa vingine vya upasuaji visivyoweza kujipinda, kifaa hiki kitaweza kujipinda kwa kiasi kikubwa hivi kwamba kitapitishwa katika sehemu salama zaidi za ubongo, bila kugusa sehemu nyeti wakati wa upasuaji.” Kifaa hicho pia kitafanya iwe rahisi kufikia sehemu ambazo huwa ni vigumu kufikia bila kukata viungo ambavyo havina tatizo.

Zaidi INGIA HAPA

Alhamisi, Desemba 04, 2014

Bawa la Kipepeo




● Rangi maridadi inayong’aa juu ya mabawa ya vipepeo fulani hubadilika ikitegemea upande ambao unatazama. Rangi ya bawa la vipepeo wa aina fulani ni laini na inang’aa sana hivi kwamba inaweza kuonekana umbali wa mita 805. Ni nini kinachofanya bawa la kipepeo liwe la kipekee hivyo?


Fikiria hili: Mistari midogo iliyobonyea kwenye sehemu ya juu ya mabawa ya kipepeo anayeitwa green swallowtail (Papilio blumei) hurudisha nuru kwa njia kadhaa. Kwa mfano, sehemu ya katikati ya eneo lililobonyea hurudisha nuru yenye rangi ya manjano na kijani, huku sehemu za nje zikirudisha nuru yenye rangi ya bluu. 

Pia, sehemu ya katikati ya eneo lililobonyea hurudisha nuru moja kwa moja, lakini nuru inapopiga sehemu za kando inalazimika kupitia kwenye matabaka kadhaa, ambayo huongeza na kuzungusha mawimbi ya nuru. Mchanganyiko wa mwisho unaotokea huwa tata sana.



Watafiti walitumia miaka kumi kutokeza kitu kinachofanana na sehemu ya juu ya bawa la kipepeo. Wanatumaini kwamba teknolojia hiyo itawasaidia kutokeza noti za benki na kadi za mkopo zisizoweza kuigwa kwa urahisi na mabamba yanayoweza kunasa nguvu za jua kwa njia nzuri zaidi. 

Hata hivyo, ni vigumu sana kuiga sehemu ya juu ya bawa la kipepeo. “Ingawa wanasayansi wanaelewa mambo mengi sana kuhusu elimu ya nuru,” anaandika Profesa Ullrich Steiner wa Chuo Kikuu cha Cambridge, “unamna-namna wa rangi wenye kushangaza unaopatikana katika bawa hilo unazidi mambo yanayoweza kutokezwa kwa kutumia teknolojia.”

Una maoni gani? 

Je, sehemu ya juu ya bawa la kipepeo ilijitokeza yenyewe? 

Au ilibuniwa?

Jumatano, Novemba 26, 2014

Mdomo wa Ndege aitwaye Mdiria

Kule Japani, treni inayosafiri mwendo wa kilomita 300 kwa saa ndiyo yenye mwendo wa kasi zaidi ulimwenguni. Kwa kiasi fulani, mdiria ambaye ni ndege mdogo sana, amechangia sana kufanikiwa kwa treni hiyo. Jinsi gani?

 

Fikiria hili: Mdiria anaweza kuzama ndani ya maji bila kuyafanya yaruke sana anapotafuta chakula. Jambo hilo lilimvutia sana Eiji Nakatsu, injinia aliyesimamia majaribio ya treni hiyo. Alijiuliza jinsi mdiria anavyoweza kustahimili badiliko hilo kutoka hewani kuingia majini. Jibu la swali hilo lingetatua tatizo kubwa lililokuwa likiikumba treni hiyo inayosafiri kwa kasi. Nakatsu anaeleza hivi: “Treni inapoingia chini ya ardhi kwa kasi sana inatokeza mawimbi ya shinikizo la hewa ambayo huongezeka zaidi na zaidi. Mawimbi hayo hufika mwisho wa barabara hiyo ya chini ya ardhi kwa kasi ya mwendo wa sauti na hivyo kutokeza sauti kama ya mlipuko na tetemeko kubwa hivi kwamba wakazi wanaoishi umbali wa mita 400 walilalamika.”

  
Uamuzi ulifanywa ili kuunda treni hiyo kwa umbo la mdomo wa mdiria. Kulikuwa na matokeo gani? Sasa treni hiyo inasonga kasi zaidi kwa asilimia 10 na kutumia nguvu kidogo zaidi kwa asilimia 15. Zaidi ya hilo, shinikizo la hewa linalotokezwa na treni hiyo limepungua kwa asilimia 30. Kwa sababu hiyo, hakuna sauti ya mlipuko treni hiyo inapopita katika barabara hiyo ya chini ya ardhi.


Una maoni gani? Je, mdomo wa mdiria ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?

Samaki Anayetumia Nishati Yake Vizuri

Ili watokezeshe gari lenye nguvu, lisilotumia nishati nyingi, na lisiloharibu mazingira, wanasayansi walichunguza eneo ambalo wengi hawakutarajia, chini ya bahari! Samaki anayeitwa boxfish anayepatikana kwenye matumbawe yaliyo kwenye bahari za tropiki ana muundo unaofaa kutengeneza gari jepesi, linaloenda kwa kasi na kutumia nishati kidogo.


Fikiria hili: Samaki huyo anaweza kuogelea kwa kasi akisonga umbali unaolingana na mara sita ya urefu wa mwili wake kwa sekunde. Lakini hatumii nguvu ili asonge kasi hivyo. Umbo lake humwezesha kusonga kwa kasi bila kutumia nishati nyingi. Wahandisi walitengeneza gari lenye muundo wa samaki huyo na kulijaribu kwenye barabara yenye upepo mkali iliyo chini ya ardhi na wakagundua kwamba gari hilo hukata upepo kwa njia bora zaidi kuliko magari mengine.

 
Samaki huyo ana ngozi ya nje yenye mifupa ambayo humfanya asonge kwa nguvu lakini bado awe mwepesi. Maji yanayozunguka kwa kasi kando ya samaki huyo humfanya asiyumbeyumbe bahari inapochafuka. Kwa hiyo, samaki huyo ana uwezo mkubwa wa kudhibiti mwili wake hata anaposonga kwa kasi na anakingwa asiumie.



Wahandisi wanaamini kwamba samaki huyo atawasaidia kutokeza gari salama, jepesi, na lisilotumia mafuta mengi. Dakt. Thomas Weber, mtafiti na mbuni anasema hivi: “Kusema kweli tulishangazwa kwamba kati ya viumbe wote, samaki huyo anayeonekana mzembe ndiye angechaguliwa kutokeza muundo wa gari linaloenda kwa kasi na kutumia nishati kidogo.”

Una maoni gani? Je, samaki huyo anayetumia nishati yake vizuri alijitokeza mwenyewe? Au alibuniwa?