Kule Japani, treni inayosafiri mwendo wa kilomita 300
kwa saa ndiyo yenye mwendo wa kasi zaidi ulimwenguni. Kwa kiasi fulani,
mdiria ambaye ni ndege mdogo sana, amechangia sana kufanikiwa kwa treni
hiyo. Jinsi gani?
Fikiria hili:
Mdiria anaweza kuzama ndani ya maji bila kuyafanya yaruke sana
anapotafuta chakula. Jambo hilo lilimvutia sana Eiji Nakatsu, injinia
aliyesimamia majaribio ya treni hiyo. Alijiuliza jinsi mdiria anavyoweza
kustahimili badiliko hilo kutoka hewani kuingia majini. Jibu la swali
hilo lingetatua tatizo kubwa lililokuwa likiikumba treni hiyo
inayosafiri kwa kasi. Nakatsu anaeleza hivi: “Treni inapoingia chini ya
ardhi kwa kasi sana inatokeza mawimbi ya shinikizo la hewa ambayo
huongezeka zaidi na zaidi. Mawimbi hayo hufika mwisho wa barabara hiyo
ya chini ya ardhi kwa kasi ya mwendo wa sauti na hivyo kutokeza sauti
kama ya mlipuko na tetemeko kubwa hivi kwamba wakazi wanaoishi umbali wa
mita 400 walilalamika.”
Uamuzi ulifanywa ili kuunda treni hiyo kwa umbo la
mdomo wa mdiria. Kulikuwa na matokeo gani? Sasa treni hiyo inasonga kasi
zaidi kwa asilimia 10 na kutumia nguvu kidogo zaidi kwa asilimia 15.
Zaidi ya hilo, shinikizo la hewa linalotokezwa na treni hiyo limepungua
kwa asilimia 30. Kwa sababu hiyo, hakuna sauti ya mlipuko treni hiyo
inapopita katika barabara hiyo ya chini ya ardhi.
Una maoni gani? Je, mdomo wa mdiria ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni