LAZIMA nimshukuru Mungu sana kuwa mimi
ni msanii wa hapa Tanzania na bado sijapotea sana kwenye masikio na
macho ya watu. Lakini kuna wenzangu wengi waliokuwa maarufu kuliko mimi
waliokuwa na mafanikio ya kisanii na kiuchumi kuliko mimi kwa sasa hali
zao za maisha ni mbaya sana. Kuna sababu kadhaa za matokeo haya, lakini
kuna moja kubwa nalo ni kukosa ufahamu wa haki zao.
Wakati msanii anapoanza kutafuta
umaarufu huwa mtu wa kutaka kupata ushauri, lakini pindi anapojulikana
hataki tena ushauri hasa kuhusu haki anazostahili kuzipata kutokana na
kazi yake. Hali hii hutokana na sababu mbili kubwa, moja ni kiburi
kinachojengeka kutokana na umaarufu hivyo kumfanya muhusika kuona kuwa
haiwezekani kamwe akashuka na kuwa mtu wa kawaida. Pili ni mtego ambao
wasanii wengi huingia na kujikuta chini ya wafanya biashara wahuni ambao
ili waendelee kuwamiliki wasanii huwa wanawakataza kujihusisha na
harakati zozote ambazo zitaweza kuwaamsha akili zao kudai haki yao.
Na
wafanyabiashara wengine huweza hata kuwafundisha mambo yasiyo ya ukweli
katika biashara na kuwafanya wasanii waamini kuwa hawataweza kufanya
kazi bila ya kuwa na wafanya biashara hawa. Lakini ubora wa wanamuziki
hawa unaposhuka wafanyabiashara hawa hawa huwatema kama kaa la moto na
wasanii kujikuta wakihangaika maisha ya tabu bila msaada wowote.
HAKIMILIKI
Ni haki zaidi ya kumi
anazopata msanii katika kila kazi yake, wasanii wengi hawajui haya na
wengi wala hawataki kujua, mmoja aliwahi kunijibu, ‘Hakimiliki ni Ulaya
tu”, japo alikuwa hajui hata hiyo hakimiliki ina beba nini. Namjua
mfanya biashara mmoja ambaye moja ya kampeni zake kuu ni kuhakikisha
wasanii walio chini yake hawajui Hakimiliki, wala hawahudhurii semina au
warsha yoyote ya Hakimiliki. Lakini Hakimiliki ni mali ya mtunzi maisha
yake yote na miaka 50 baada ya kifo chake kadri ya Sheria ya Hakimiliki
ya Tanzania. Kwa kipindi hicho Hakimiliki inakulindia haki za
kiuchumi, ‘Economic Rights’ ambazo ndizo zinazokupa uwezo wa kupata
halali yako kiuchumi kutokana na kazi zako. Katika kila kazi, kwa mfano
wimbo, kuna haki zifuatazo;
i. Kurudufu,
ii.Kusambaza,
iii. Kukodisha,
iv. Kuonyesha hadharani (exhibition),
v. Kutafsiri,
vi.Kutangaza hadharani (Public Performance),
vii. Kurusha katika vyombo vya utangazaji (Broadcasting),
viii Kubadili matumizi,
ix. Njia zozote zile nyingine za utangazaji hadharani (ikiwemo Cable network),
x. kuingiza nakala nchini
Hali ilivyo mbaya hapa Tanzania,
wanamuziki wetu siku hizi hawasambazi, wengi hawana album rasmi, japo
wanaweza kuwa na nyimbo zinazotosha album, baada ya kurekodi hutumia
kipengele cha vi, na kuweka nyimbo zao kwenye mtandao kama youtube ili
kila anaeutaka anaweza kuutumia bure, hiyo ikidhaniwa kuwa ndio njia
bora ya promosheni ya wimbo mpya, wajanja hutumia kipengele cha i. na
ii, wanarudufu na kusambaza na kutengeneza pesa bila kuwashirikisha
wasanii, kisha wasanii huruhusu kazi zao zitumiwe kwa haki na vii, redio
na tv huingiza mabilioni ya fedha kutokana na matangazo, kwa kupiga
nyimbo hizo bila kulipa hata senti tano.
Zikiwemo radio za wale
wanaotambulika kuwa ni watu wasafi na wakombozi wa vijana na wanyonge,
na hata radio ya Taifa nayo imo katika ufisadi huu. Hatimae tunaona
nakala za DVD na CD za wasanii wa Kitanzania zikiingizwa nchini kutoka
Uchina na kuuzwa mitaani zikiwa zinavunja kipengele x.
Wasanii wengi wakiona kazi zao
zimesambaa hujisifu kuwa ‘Kazi yangu inafanya vizuri’. Umbumbumbu huu
wa hakimiliki unawafanya wasione umuhimu wa mikataba itakayoelekeza
matumizi yatakayoleta tija kwenye maisha yao, hivyo baada ya muda msanii
anajikuta hata fedha ya nauli kwenda kudai chake hana. Na wengine huona
njia ni kuendelea kurekodi, bila kujali kilichokwisha rekodiwa
kiliingiza na nini na kusababisha hasara gani.
Masikitiko zaidi ni pale unapokuta
msanii yuko katika hali mbaya kimaisha wakati kazi zake bado zinaendelea
kuingiza mamilioni kutokana na matangazo katika vyombo vya utangazaji
na muhusika wala hajui kuwa anastahili mgao wa pesa inayotokana na jasho
lake.
Umoja ni nguvu na kila mtu anajua
hivyo, hata wale wanyonyaji wa wasanii wanalijua hilo hivyo kati ya vitu
vinavyopigwa vita na wanyonyaji ni umoja wowote wa wasanii. Ukionekana
unafanikiwa patapenyezwa rupia ili kuchafua jitihada zozote za kuunda
umoja wenye nguvu. Japo wanyonyaji hao wao wamejitengenezea umoja wenye
nguvu sana kulinda maslahi yao ya kuwanyonya wasanii.
Katika wizi wa kazi za sanaa kadri
unavyokuwa maarufu zaidi ndivyo unavyoibiwa zaidi, ungetegemea kuwa
wasanii maarufu ndio wangekuwa wakihakikisha kunakuweko na umoja na pia
kuhamasisha ulinzi wa haki zao, hilo ndilo kinyume, nadra sana watu
maarufu kuhuduhuria mikutano ya wasanii, labda kama huo mkutano
umehamasishwa na wafanyabiashara wanaonyonya wasanii hapo utakuta
mkutano una wasanii wote muhimu na mara nyingi mada hapa huwa hazina
umakini wa kutoa elimu kwa wahusika.
NI jambo la kusikitisha kusikia mama
huyu Bi Cheka ambaye miaka miwili tu iliyopita alikuwa kwenye masikio ya
kila mtu anaishi kwenye nyumba ya udongo. Tuombee iwe ni hadithi tu na
si kweli kuwa hali ni hiyo, japo haitashangaza kamwe kwa nchi hii
iliyojaa ufisadi kila kona.
Stori zaidi: Gladness Mallya na Mayasa Mariwata
DAH MASIKINI!
Hivi ndivyo unavyoweza kusema wakati unapomuona msanii wa muziki wa
kizazi kipya, Cheka Hija, maarufu kama Bi. Cheka kutoka Kundi la Mkubwa
na Wanawe, linaloongozwa na Said Fella ‘Mkubwa’ lenye maskani yake,
Temeke jijini Dar es Salaam.
Bi Cheka akiwa nje ya nyumba anayoishi.
Mtoa habari wetu aliwasiliana na gazeti hili na kulieleza kuwa msanii
huyo mwenye umri wa miaka 55, hivi karibuni alianguka ghafla nyumbani
kwake na kukata kauli, wakati alipokuwa akienda chooni kujisaidia.
Wikiendi iliyopita, Amani lilifika nyumbani kwa msanii huyo mzee,
anayeishi Bunju B, nje kidogo ya jiji la Dar na kumkuta akiwa na wajukuu
zake huku hali yake ikiwa tete tokea alipoanguka Oktoba mwaka huu.
Akiwa anaishi katika kijumba chake kilichojengwa kwa miti na kukandikwa
udongo, mtu anayemuona katika luninga akifanya vitu vyake, asingeweza
kuamini kama hapo ndipo anapoishi.
Upande wa nyumba yake.
“Ukweli nilikuwa na hali mbaya, afadhali sasa, naongea na kusimama
kwani nilikuwa siwezi kutembea, wiki iliyopita alikuja meneja wetu,
Yusuf Chambuso na akina Dogo Aslay.
“Jamani maisha yangu kwa sasa ni magumu kwani siwezi kufanya kazi
yoyote na sina msaada na kwenye muziki sijaona faida yoyote labda ya
nguo tu, kwamba nilizoea kuvaa madela na kanzu sasa nina suruali,”
alisema Bi Cheka kwa machungu.
Bi Cheka akiwa na wajukuu zake.
Alisema anasikitishwa na maisha yake kwani kutokana na umaarufu wake,
mtaani kwao anaonekana kama mtu mwenye uwezo, wakati siyo kweli kwani
anaishi kwenye nyumba ya tembe katikati ya nyumba nzuri.
“Kuhusu malipo makubwa kuwahi kupata ni shilingi laki tatu
nilizolipwa kwenye shoo ya Fiesta mwaka juzi, hizo ndizo hela kubwa
niliyowahi kupata katika muziki.”Gazeti hili lilimtafuta Fella ambaye
alikiri Bi. Cheka kuumwa, akisema anasumbuliwa na magonjwa ya uzee na
kwamba ahadi yake ya kumsaidia kujenga nyumba imeishia kwenye mchango
wake wa matofari.
...Bi Cheka akiimba na Chege.
“Mimi kama Fella nimesaidia ninapoweza, nimemchangia matofari kidogo,
kwa hiyo watanzania wenzangu nao tuungane tumchangie ili aweze
kurekebisha kibanda chake,” alisema.
Global Publishers inaanzisha kampeni maalum ya kumsaidia na hivyo
inawaomba watanzania kumchangia msanii huyu ili apate nyumba nzuri na
matibabu yake. Ili kumsaidia tuma fedha kwenye namba 0654-880707 ambayo
itasimamiwa na kampuni.
Chanzo: INGIA HAPA