Mtayarishaji

Morning Star Radio

Ijumaa, Desemba 12, 2014

HATMA YA WASANII TANZANIA NI MBAYA WASIPOBADILIKA

BI CHEKAAA


LAZIMA nimshukuru Mungu sana kuwa mimi ni msanii wa hapa Tanzania na bado sijapotea sana kwenye masikio na macho ya watu. Lakini kuna wenzangu wengi waliokuwa maarufu kuliko mimi waliokuwa na mafanikio ya kisanii na kiuchumi kuliko mimi kwa sasa hali zao za maisha ni mbaya sana. Kuna sababu kadhaa za matokeo haya, lakini kuna moja kubwa nalo ni kukosa ufahamu wa haki zao. 
 
Wakati msanii anapoanza kutafuta umaarufu huwa mtu wa kutaka kupata ushauri, lakini pindi anapojulikana hataki tena ushauri hasa kuhusu haki anazostahili kuzipata kutokana na kazi yake. Hali hii hutokana na sababu mbili kubwa, moja ni kiburi kinachojengeka kutokana na umaarufu hivyo kumfanya muhusika kuona kuwa haiwezekani kamwe akashuka na kuwa mtu wa kawaida. Pili ni mtego ambao wasanii wengi huingia na kujikuta chini ya wafanya biashara wahuni ambao ili waendelee kuwamiliki wasanii huwa wanawakataza kujihusisha na harakati zozote ambazo zitaweza kuwaamsha akili zao kudai haki yao. 

Na wafanyabiashara wengine huweza hata kuwafundisha mambo yasiyo ya ukweli katika biashara na kuwafanya wasanii waamini kuwa hawataweza kufanya kazi bila ya kuwa na wafanya biashara hawa. Lakini ubora wa wanamuziki hawa unaposhuka wafanyabiashara hawa hawa huwatema kama kaa la moto na wasanii kujikuta wakihangaika maisha ya tabu bila msaada wowote.

HAKIMILIKI 

Ni haki zaidi ya kumi anazopata msanii katika kila kazi yake, wasanii wengi hawajui haya na wengi wala hawataki kujua, mmoja aliwahi kunijibu, ‘Hakimiliki ni Ulaya tu”, japo alikuwa hajui hata hiyo hakimiliki ina beba nini. Namjua mfanya biashara mmoja ambaye moja ya kampeni zake kuu ni kuhakikisha wasanii walio chini yake hawajui Hakimiliki, wala hawahudhurii semina au warsha yoyote ya Hakimiliki. Lakini Hakimiliki ni mali ya mtunzi maisha yake yote na miaka 50 baada ya kifo chake kadri ya Sheria ya Hakimiliki ya Tanzania. Kwa kipindi hicho  Hakimiliki inakulindia haki za kiuchumi, ‘Economic Rights’ ambazo ndizo zinazokupa uwezo wa kupata halali yako kiuchumi kutokana na kazi zako. Katika kila kazi, kwa mfano wimbo, kuna haki zifuatazo; 

i. Kurudufu,
ii.Kusambaza,
iii. Kukodisha,
iv. Kuonyesha hadharani (exhibition),
v. Kutafsiri,
vi.Kutangaza hadharani (Public Performance),
vii. Kurusha katika vyombo vya utangazaji (Broadcasting),
viii Kubadili matumizi,
ix. Njia zozote zile nyingine za utangazaji hadharani (ikiwemo Cable network),
x. kuingiza nakala nchini 

Hali ilivyo mbaya hapa Tanzania, wanamuziki wetu siku hizi hawasambazi, wengi hawana album rasmi, japo wanaweza kuwa na nyimbo zinazotosha album, baada ya kurekodi hutumia kipengele cha vi, na kuweka nyimbo zao kwenye mtandao kama youtube  ili kila anaeutaka anaweza kuutumia bure, hiyo ikidhaniwa kuwa ndio njia bora ya promosheni ya wimbo mpya, wajanja hutumia kipengele cha i. na ii, wanarudufu na kusambaza na kutengeneza pesa bila kuwashirikisha wasanii, kisha wasanii huruhusu kazi zao zitumiwe kwa haki na vii, redio na tv huingiza mabilioni ya fedha kutokana na matangazo, kwa kupiga nyimbo hizo bila kulipa hata senti tano.

 Zikiwemo radio za wale wanaotambulika kuwa ni watu wasafi na wakombozi wa vijana na wanyonge, na hata radio ya Taifa nayo imo katika ufisadi huu. Hatimae tunaona nakala za DVD na CD za wasanii wa Kitanzania zikiingizwa nchini kutoka Uchina na kuuzwa mitaani zikiwa zinavunja kipengele x.

Wasanii wengi wakiona kazi zao zimesambaa hujisifu kuwa ‘Kazi yangu inafanya vizuri’.  Umbumbumbu huu wa hakimiliki unawafanya wasione umuhimu wa mikataba itakayoelekeza matumizi yatakayoleta tija kwenye maisha yao, hivyo baada ya muda msanii anajikuta hata fedha ya nauli kwenda kudai chake hana. Na wengine huona njia ni kuendelea kurekodi, bila kujali kilichokwisha rekodiwa kiliingiza na nini na kusababisha hasara gani.

Masikitiko zaidi ni pale unapokuta msanii yuko katika hali mbaya kimaisha wakati kazi zake bado zinaendelea kuingiza mamilioni kutokana na matangazo katika vyombo vya utangazaji na muhusika wala hajui kuwa anastahili mgao wa pesa inayotokana na jasho lake.

Umoja ni nguvu na kila mtu anajua hivyo, hata wale wanyonyaji wa wasanii wanalijua hilo hivyo kati ya vitu vinavyopigwa vita na wanyonyaji ni umoja wowote wa wasanii. Ukionekana unafanikiwa patapenyezwa rupia ili kuchafua jitihada zozote za kuunda umoja wenye nguvu. Japo wanyonyaji hao wao wamejitengenezea umoja wenye nguvu sana kulinda maslahi yao ya kuwanyonya wasanii.

Katika wizi wa kazi za sanaa kadri unavyokuwa maarufu zaidi ndivyo unavyoibiwa zaidi, ungetegemea kuwa wasanii maarufu ndio wangekuwa wakihakikisha kunakuweko na umoja na pia kuhamasisha ulinzi wa haki zao, hilo ndilo kinyume, nadra sana watu maarufu kuhuduhuria mikutano ya wasanii, labda kama huo mkutano umehamasishwa na wafanyabiashara wanaonyonya wasanii hapo utakuta mkutano una wasanii wote muhimu na mara nyingi mada hapa huwa hazina umakini wa kutoa elimu kwa wahusika.


NI jambo la kusikitisha kusikia mama huyu Bi Cheka ambaye miaka miwili tu iliyopita alikuwa kwenye masikio ya kila mtu anaishi kwenye nyumba ya udongo. Tuombee iwe ni hadithi tu na si kweli kuwa hali ni hiyo, japo haitashangaza kamwe kwa nchi hii iliyojaa ufisadi kila kona.


Stori zaidi: Gladness Mallya na Mayasa Mariwata

DAH MASIKINI! Hivi ndivyo unavyoweza kusema wakati unapomuona msanii wa muziki wa kizazi kipya, Cheka Hija, maarufu kama Bi. Cheka kutoka Kundi la Mkubwa na Wanawe, linaloongozwa na Said Fella ‘Mkubwa’ lenye maskani yake, Temeke jijini Dar es Salaam.

Bi Cheka akiwa nje ya nyumba anayoishi.

Mtoa habari wetu aliwasiliana na gazeti hili na kulieleza kuwa msanii huyo mwenye umri wa miaka 55, hivi karibuni alianguka ghafla nyumbani kwake na kukata kauli, wakati alipokuwa akienda chooni kujisaidia.

Wikiendi iliyopita, Amani lilifika nyumbani kwa msanii huyo mzee, anayeishi Bunju B, nje kidogo ya jiji la Dar na kumkuta akiwa na wajukuu zake huku hali yake ikiwa tete tokea alipoanguka Oktoba mwaka huu.

Akiwa anaishi katika kijumba chake kilichojengwa kwa miti na kukandikwa udongo, mtu anayemuona katika luninga akifanya vitu vyake, asingeweza kuamini kama hapo ndipo anapoishi.Upande wa nyumba yake.

“Ukweli nilikuwa na hali mbaya, afadhali sasa, naongea na kusimama kwani nilikuwa siwezi kutembea, wiki iliyopita alikuja meneja wetu, Yusuf Chambuso na akina Dogo Aslay.

“Jamani maisha yangu kwa sasa ni magumu kwani siwezi kufanya kazi yoyote na sina msaada na kwenye muziki sijaona faida yoyote labda ya nguo tu, kwamba nilizoea kuvaa madela na kanzu sasa nina suruali,” alisema Bi Cheka kwa machungu.


Bi Cheka akiwa na wajukuu zake.

Alisema anasikitishwa na maisha yake kwani kutokana na umaarufu wake, mtaani kwao anaonekana kama mtu mwenye uwezo, wakati siyo kweli kwani anaishi kwenye nyumba ya tembe katikati ya nyumba nzuri.

“Kuhusu malipo makubwa kuwahi kupata ni shilingi laki tatu nilizolipwa kwenye shoo ya Fiesta mwaka juzi, hizo ndizo hela kubwa niliyowahi kupata katika muziki.”Gazeti hili lilimtafuta Fella ambaye alikiri Bi. Cheka kuumwa, akisema anasumbuliwa na magonjwa ya uzee na kwamba ahadi yake ya kumsaidia kujenga nyumba imeishia kwenye mchango wake wa matofari.


...Bi Cheka akiimba na Chege.

“Mimi kama Fella nimesaidia ninapoweza, nimemchangia matofari kidogo, kwa hiyo watanzania wenzangu nao tuungane tumchangie ili aweze kurekebisha kibanda chake,” alisema.

Global Publishers inaanzisha kampeni maalum ya kumsaidia na hivyo inawaomba watanzania kumchangia msanii huyu ili apate nyumba nzuri na matibabu yake. Ili kumsaidia tuma fedha kwenye namba 0654-880707 ambayo itasimamiwa na kampuni.

 Chanzo: INGIA HAPA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni