Mtayarishaji

Morning Star Radio

Alhamisi, Februari 14, 2013

LICHA YA KUWAPO AINA KUU NNE; KOMPYUTA ZIMEUNDWA KATIKA MSINGI MMOJA!


Licha ya kuwa na aina za kompyuta lakini bado kuna msingi ambao zote huutegemea. Msingi huo ni kuwa na sehemu kuu mbili; sehemu kuu ya kutengeneza habari kutokana na data zilizoingizwa ijulikanayo kama Central Processing Unit au CPU kwa kifupi na sehemu ya kuingizia data na kutolea habari iliyokwisha tengenezwa kwa ajili ya faida ya mtumiaji ijulikanayo kama peripheral devices. Kwa hiyo data huingizwa kupitia sehemu zinazofahamika Kama peripheral devices na kupelekwa ndani ya CPU ambako hunyumbulishwa na kufafanunuliwa na hatimaye kutoa kile kilichokusudiwa kupitia tena peripheral devices hizohizo. CPU hufanya kazi ya kufafanua data (processing) kulingana na maelekezo ya mtumiaji. Tuone sehemu mbalimbali za kompyuta ambazo huifanya kazi ya kompyuta kutekelezeka kwa ufanisi.



Ubongo wa Kompyuta (Central Processing Unit)



Hii ni sehemu maalum kabisa katika kompyuta. Ndiko ambako maamuzi yote kuhusu data na habari hufanywa ili kuhakikisha kuwa mambo yanakwenda vyema. Ni kama ubongo wa binadamu ambao huamua mambo yote yanayohusiana na shughuli zote za mwili ili kumfanya aishi katika afya njema. Sehemu hii ya kompyuta huwa ndani ya kifaa kiitwacho computer case ambacho kinafunika ‘ubongo’ huu wa kompyuta. 

Computer Case inaweza kuwa bapa na yenye umbo la msitatili au mraba (kwa aina ya personal computers) ambayo huwekwa katika meza ili iweze kutumika vyema. Aina hii ya computer case inajulikana kama desktop case na ndiyo maana kompyuta huitwa desktop computer. Pia computer case inaweza kuwa na umbo lililosimama, kama umbo la mche msitatili na lijulikanalo kama Tower case – na ndiyo huzaa jina la Tower computer. Lakini kwa notebook computer na palmtop computers computer case huwa imunganishwa na sehemu ya peripheral kiasi kwamba ni vigumu kuweza kuifafanua vyema.



Ubongo wa kompyuta huwa ni muunganiko wa sehemu mbalimbali ambazo kwa pamoja huwekwa katika mfumo mmoja ujulikanao kama motherboard. Muundo wa motherboard hutofautiana kutegemeana na aina ya kompyuta (mtengenezaji) na ukubwa wa kompyuta yenyewe na hata toleo (version) la kompyuta husika. Kompyuta aina ya desktop ina motherboard tofauti na kompyuta aina ya notebook. Pia kompyuta toleo la mwaka 1995 ina muundo wa motherboard ulio tofauti na lile la toleo la mwaka 2005.



Ubongo wa kompyuta (CPU) huwa na vifaa muhimu vifuatavyo:



Kifaa ambacho ni mkusanyiko wa mamilioni ya sakiti ndogondogo zijulikanazo kama transistors. Sakiti hizi zinakwa na ukubwa wa chini ya unywele mmoja wa nywele za binadamu! Kifaa hiki ndicho ambacho kinachukuliwa kama moyo au ‘roho’ ya kompyuta. Bila kifaa hiki kompyuta haiwezi kufanya lolote. Kifaa hiki kinajulikana kwa jina la microprocessor. Ni kifaa hiki ambacho hupokea mamilioni ya maelekezo kutoka kwa mtumiaji na kuyafanyia kazi ili kutoa majibu yanayotakiwa. Kina uwezo wa kufafanua na kunyumbulisha data kwa uwezo wa hata kufikia maelekezo trilioni moja kwa sekunde! (hii ni kulingana na ukubwa na uwezo wa microprocessor hiyo kutegemeana na aina ya kompyuta).



Kifaa kingine muhimu ni kitunza kumbukumbu kijulikanacho kama random access memory chip ambacho hutunza kumbukumbu zinazofanyiwa kazi na kompyuta. Kumbukumbu hizi huhifadhiwa katika mfumo ambao ni wa muda tu; ikiwa na maana kwamba mfumo huu hupoteza kumbukumbu hizo mara tu umeme ambao unaozunguka katika sakiti nzima ya kompyuta unapotoweka. Kifaa kijulikanacho kama random acess memory



Kifaa kingine ni mkusanyiko wa nyanya ndondogo sana ambazo huunganishwa pamoja na kufungwa vyema ndani ya material aina ya plastiki. Kifaa hiki hupitisha data ndani na nje ya motherboard. Ni kama barabara ambayo inaunganisha mji mkubwa ili kufanya mawasiliano kuwapo baina ya watu. Kifaa hiki kinafahamika kama system bus.


System bus (utepe manjano)



Pia kuna vifaa mbalimbali ambavyo vinahusika na utoaji wa sauti, picha na kadhalika. Pia matundu ya aina mbalimbali ambayo huwezesha uunganishwaji wa sehemu za nje ya motherboard yaani peripheral devices.



Sehemu Za Nje ya Motherboard (Peripheral Devices)



Hizi ni sehemu ambazo zinakamilisha ufanyaji kazi wa kompyuta. Sehemu hizi ziko nje ya system case na zinakuwepo katika kompyuta kulingana na matumizi ya mtu husika ingawa kuna sehemu ambazo lazima ziwepo (basic peripheral devices). Sehemu hizi za kompyuta hujulikana pia kama sehemu za kutoa na kuingizia habari na data au kwa jina la kitaalam kama input and output devices. Sehemu hizi ni kama zifuatazo:



Sehemu ya kuingizia maneno na maelekezo maalum ijulikanayo kama keyboard. Hiki ni kifaa ambaco kina mkusanyiko wa herufi (A mpaka Z) na namba 0 mpaka 9. Kifaa hiki kina mkusanyiko wa vitufe au buttons ambazo herufi au namba hizo huandikwa. Mtumiaji wa keyboard anapaswa kubonyeza (press) vitufe hivyo ili kuweza kuingiza malekezo haya (herufi na namba) katika kompyuta. Pia keyboard huwa na buttons maalum ambazo huingiza malekezo maalum kea ajili ya ufanisi wa kazi wa kompyuta. Tutazungumzia zaidi sehemu hii.



Sehemu ya kukuwezesha kuona nini unakifanya katika kompyuta. Huwezi kwenda kwa mfano sokoni ilihali hauoni. Unahitaji kuona barabara na kufahamu soko lipo wapi ili uweze kufika kwa urahisi. Vivyo hivyo unapokuwa unatumia kompyuta au unafanya kazi na kompyuta unahitaji kuona kile unachokifanya. Unahitaji kusikia kile unachokitarajia. Sehemu hii ya kompyuta hujulikana kama monitor. Monitor ina umbo kama la runinga ambayo umezoea kuiona na kwa uhalisia teknolojia ya uundwaji wake ipo sawa na ya runinga isipokuwa marekebisho kidogo. Monitor ndipo mahala pekee pa kuweza kufahamu nini kinaendelea ndani ya kompyuta kwani shughuli zote za utengenezwaji na utoji habari huonekana katika kifaa hiki.



Sehemu ya kuweza kuingiliana na monitor na kufanya kile unachikihitaji na ambayo hufanya kazi kwa kushirikiana na keyboard ni sehemu ya tatu katika hili kundi la peripheral devices. Sehemu hii inajulikana sana kama mouse. Mouse ni kifaa ambacho mtumiaji hukitumia kuwasiliana na kompyuta (CPU) ili kuzaa au kutoa kile kinachotarajiwa. Kifaa hiki huwa na mahali ambapo unabonyeza kwa kutumia kidole na ubonyezawji wa kidole hiki husafirisha habari katika kompyuta na kuilekeza ifanye nini. Mouse huonekana katika kompyuta kama mshale na mshale huu hutembea katika monitor kumuwezesha mtumiaji kuamua nini cha kufanya. Mshale huu hujulikana kama cursor kwa kimombo.



Sehemu hizi tatu za kwanza katika kundi la peripheral devices zinategemeana na hujulikana kama basic input & output devices. Hii ina maana kwamba sehemu hizi ni lazima ziwepo ili kuifanya kompyuta ifanye kazi zilizo za muhimu. Sehemu nyingine muhimu ni zile zinazotoa na kuingiza sauti. Sehemu hizi hufahamika kama input

and output sound devices. Mfano wa sehemu hizi ni kama speakers, microphones, webcam, cameras na nyingine nyingi. Pia sehemu za kuingizia picha na kutolea picha kama cameras. Aina mbalimbali za Microphones



Sehemu nyingine muhimu ambayo ni ya muhimu sana inajulikana kama printer. Ni kifaa ambacho hutumika katika kuchapa matokeo ya ufafanuzi wa kompyuta ulio katika mfumo wa maandishi (text) kwa shughuli mbalimbali anazozihitaji mtumiaji. Kifaa hiki kina uwezo wa kutoa maandishi na picha zilizo na zisizo na rangi. Kifaa hiki kinatofautiana katika utengenezwaji kulingana na mahitaji ya watumiaji.



Sehumu tulizozizungumzia hapo juu ndizo sehemu zinazojumuisha peripheral devices. Kwa hakika sehemu hizi ni muhimu katika kuifanya kompyuta iitwe kompyuta kwani ndizo zinazowezesha kupata matokeo ambayo binadamu anayahitaji katika maisha yake.

Jumanne, Februari 12, 2013

TEKNOHAMA - KOMPYUTA INAFANYAJE KAZI?


Picha kwa hisani ya: http://www.macwallpapers.eu



Unaweza ukawa unajiuliza, ni vipi sasa kompyuta inafanya kazi kama ina sakiti ambazo zinaweza kufikia milioni kumi? Je si kifaa kilicho tata sana?

Kwa ujumla kompyuta haifanyi kazi vigumu kiasi hicho kama unavyoweza kudhani. Sakiti hizo zinaisaidia kufanya kazi nyingi kwa wakati mmoja na kwa haraka sana na ndiyo matarajio ya binadamu; kwamba ifanye kazi kwa haraka sana ili kufanya uzalishaji mali kuwa mkubwa. Maelekezo ambayo kompyuta inatoa na kufanya (baada ya kupewa na binadamu) ni rahisi kabisa: jumlisha namba moja na nyingine, toa data kutoka sehemu moja kupeleka sehemu nyingine, peleka habari kutoka kifaa kimoja kwenda kifaa kingine, punguza jotoridi la kifaa fulani endapo jotoridi hilo litazidi kiwango kilichowekwa na kadhalika. Maelekezo haya hufanyika Kwa haraka Sana kiasi kwamba unapata majibu unayoyataka papo kea papo!

Ni jambo moja tu ambalo linaifanya kompyuta kuwa tofauti Na mashine nyingine katika dunia hii: jambo hili Ni kwamba kompyuta inaweza kupangiliwa kufanya mambo kutokana na matakwa ya mtumiaji (can be programmed). Hii inamaanisha kuwa mpangilio wa maelekezo (a list of instructions) ambayo ndiyo huitwa programu ya kompyuta (computer program) huweza kuingizwa katika kompyuta na kuhifadhiwa na kuyatumia baadaye kulingana na matakwa ya mtumiaji. Ndiyo maana ukitaka kuandika barua katika kompyuta unafungua program inayohusika na kuanza kuandika barua hiyo. Ukimaliza unaifunga program hiyo na siku nyingine au mtu mwingine anaweza kuitumia.

Kuna aina kuu NNE za Kompyuta

Kompyuta hutofautiana Sana kulingana na kazi inayopaswa kufanya. Kompyuta inayotumika katika lift za majengo si sawa na kompyuta inayotumika katika mahospitali kusaidia kutibu wagonjwa. Kulingana na matumizi husika, kompyuta hutofautiana ukubwa, bei, uwezo wa kufanya kazi na hata uendeshwaji wake.

Aina ya kwanza ya Kompyuta

Kompyuta aina ya kwanza ni zile ambazo mara nyingi watu wa kawaida huzimiliki majumbani na maofisini na ndizo zilizo za bei ya chini, uwezo mdogo na umbo dogo zaidi kuliko aina nyingine ya kompyuta. Kompyuta hizi hujulikana kama personal computers au PC kwa kifupi. Ukitazama Kwa undani zaidi utagundua kuwa kompyuta hizi ni maalum kwa ajili ya matumizi binafsi ya mtu au kwa ajili ya kuendeshea mitambo midogo midogo kwa faida ya maisha ya kila siku ya binadamu. Kompyuta hizi hupatikana katika maumbo mbalimbali. Zipo desktop Na tower computers ambazo hupatikana mara nyingi maofisini katika meza; notebook computers ambayo hujulikana Sana Kama laptops; zipo palm tops (kompyuta za viganjani ambazo hujulikana Sana Kama PDA-Personal Digita Assistant). Hizi ndizo kompyuta ambazo mara nyingi tunaziona katika maduka na supermarkets zinazouza kompyuta. Tutakuwa Na sehemu kubwa ya kutazama juu ya kompyuta aina hii huko mbele Kwa sababu ndizo zinazotumika Na kuonekana zaidi Kwa sasa mionogni mwa watu wa kawaida.

Aina ya pili ya Kompyuta

ina ya pili ya kompyuta inajulikana kama miniframe computers. Aina hii ya kompyuta ina uwezo, na ukubwa zaidi ya aina ya kwanza na ni ghali zaidi. Ni kompyuta ambazo zimetengenezwa maalum Kwa ajili ya kufanyia kazi zinazohitaji nguvu kubwa na za haraka zaidi. Mitambo mingi ya kuendeshea mawasiliano ya habari katika majengo makubwa huendeshwa Kwa kutumia kompyuta hizi.

Aina ya tatu ya Kompyuta

Aina ya tatu ya kompyuta ni zile zijulikanazo kama Mainframe computers. Hizi ni kompyuta zenye uwezo mkubwa na zinazogharimu fedha nyingi. Hutumika katika utafiti katika maabara za kisayansi katika sehemu maalum hasa katika taasisi za utaiti na katika vyuo vikuu. Pia katika kuendesha mitambo ya kutafiti maswala ya hali ya hewa (weather forecast). Kwa mfano, pale mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA) makao makuu unaweza kukuta kompyuta ya namna hii.

Aina ya NNE ya Kompyuta

ina ya nne na ya mwisho ya kompyuta ni ile iitwayo super-computers. Hizi ni kompyuta ambazo ni kubwa na zenye nguvu sana na ambazo huweza kugharimu mamilion ya dolla. Ni kompyuta hizi ambazo hutumika katika kuendesha mitambo ya kinyukilia (nuclear control) na urushaji wa maroket katika kufanya utafiti katika sayari za mbali (space exploration). Hizi kompyuta zinahitaji watu wenye utaalam wa juu katika kuziendesha na kuzifanyia marekebisho.
Kompyuta aina ya Supercomputer

Kompyuta aina ya Notebook ama Laptop

Kompyuta aina ya notebook ni kama gari dogo la kuendeshea mambo nyumbani. Kila kitu kuanzia muonekano wa nje yaani hardware, mpaka katika matumizi ya nishati ya umeme kuendeshea programs ni madogo. Kwa namna hii wataalam wa masuala ya umeme katika kompyuta ya aina hii wamefanya kazi kubwa ya kupunguza matumizi ya umeme na mahitaji ya ukubwa katika sehemu zote za kompyuta hii. Ukubwa wa kompyuta hii pamoja na matumizi ya umeme yanapunguzwa kadiri inavyowezekana. Kwa mfano hard disks za notebook computer ni ndogo kuliko hard disks za desktop computers na zinaweza kupachikwa katika upande mmoja wa system unit au kuwekwa katika sehemu ya chini ya system unit.


Katika nyakati hizi CPUs za notebook computer zijulikanazo Kama Mobile CPUs zina muundo maalum unaozitofautisha na zile za zamani. Mobile CPU Ni aina maalum ya CPU kwa kompyuta aina ya Notebook ama Laptop ambayo hubadilisha mwendokasi (wa kufafanua maelekezo) na hivyo matumizi ya umeme kwa kadiri ya kupungua au kuongezeka kwa mahitaji ya kufafanua (exection of instructions) maelekezo hayo. Kwa mfano CPU ya desktop kompyuta yenye uwezo wa kufafanua maelekezo katika mwendokasi wa 1 GH (CPU speed) inatumia kati ya wati (watts) 75 mpaka 100 za umeme ilihali CPU aina ya Mobile ya Notebook kompyuta kwa mfano SpeedStep
CPU ambayo hutumia kiwango cha wati 34 za umeme wakati notebook kompyuta hii imechomekwa katika waya ya kuingizia umeme. Hii husababisha kupunguka Kwa umeme ambao CPU huhitaji na hivyo kusababisha kuzalishwa kwa kiwango kidogo cha joto ambalo husababisha feni ya kupoza joto hilo kutumia umeme mdogo.

Feni ya CPU ya notebook kompyuta huwa haifanyi kazi muda wote Kama ilivyo Kwa feni za kompyuta za aina nyingine. Feni hufanya kazi pale tu joto linapokuwa limezidi kiwango Fulani. Kumbuka kwamba Notebook kompyuta huwa Na Betri inayoweza kutunza umeme Na hivyo kukuwezesha wewe kuitumia bila kuichomeka kwenye soketi ya umeme. Ni Kama unavyoweza kuingiza umeme kwenye simu ya mkononi Na inapokuwa umejaa unaenda zako ukitumia Na unapokuwa umekwisha unarudi Na kujaza tena.

Jumatatu, Februari 11, 2013

MAANA YA KOMPYUTA


Kompyuta au Kinakilishi katika tafsiri ya Kiswahili ni kifaa au mashine ambayo inafafanua
na kunyumbulisha/kuchakata (process) habari isiyo rasmi (data) kwenda katika habari
rasmi (information) ambayo mtumiaji au mtu anaweza kuielewa na kuifanyia kazi
kutokana na maelekezo kiliyopewa na mtu. Hivyo kompyuta kama kompyuta kwa hakika haifanyi
kazi bila kupewa maelekezo. Bila kupewa maelekezo ifanye jambo gani kompyuta ni kama kopo!
Hii inabadilisha kabisa imani kuwa kompyuta inafanya kazi kuliko binadamu na kwamba ina
uwezo wa juu kuliko hata ubongo wa binadamu! Bila binadamu kompyuta haiwezi kuwapo.
Hiki ni kifaa ambacho hakika kimebadilisha maisha ya binadamu katika karne ya ishirini na
kuweza kuyafanya kuwa rahisi zaidi kwa maana ya kutenda kazi kwa ufanisi wa hali ya juu. Neno
Kompyuta, kwa kimombo ‘Computer’; linataokana na neno ‘computing’ likiwa na maana ya
kukokotoa au kuchanganua hesabu kama kujumlisha, kugawanya, kutoa na kuzidisha. Kompyuta
ina historia ndefu kutoka katika kipindi cha kabla ya kuzaliwa Kristo ambako watu mbalimbali
kama Charles Babbage,

Lakini kifaa cha kwanza kabisa ambacho kinafanana kiutendaji na kompyuta ya leo hii
kiligunduliwa mnamo karne ya 20 (kati ya mwaka 1940 – 1945) ingawa nadharia ya kompyuta na
mashine mbalimbali zinazofanana nayo vilikuwapo kabla kama nilivyosema hapo mwanzo.
Mfululizo wa ugunduzi wa kompyuta ambazo zilikuwa na nguvu ya kutosha kufanya hisabati na
hata kutunza kiasi kidogo cha kumbukumbu ulifanyika kati ya miaka ya 1930 na 1940. Utumiaji
wa vifaa vya ki-eletroniki katika mfumo wa digital ambao uligunduliwa na kuendelezwa kwa kiasi
kikubwa na mtu aliyeitwa Claude Shannon mnamo mwaka 1937 ulifanikisha kwa kiasi kikubwa
kuimarisha ubora wa kompyuta hizo.

Kompyuta inaweza kuelezewa kuwa imepitia hatua kadhaa katika kufikia ubora ilionao sasa. Kati
ya miaka ya 1940 mpaka miaka ya 1950 kompyuta ilikuwa ikitengenezwa kwa teknolojia
iliyojulikana kama vacuum tube. Hii ilikuwa ni teknolojia ambayo ilikuwa ikitumia tubes ndogo
mfano wa vichupa vidogo ambavyo viliondolewa hewa ndani na kuvitengeneza katika mfumo
ambao viliweza kupitisha umeme ambao ndiyo uliunganishwa katika chombo kizima kwa ajili ya
kufanya kazi(kumbuka hata kompyuta ya sasa hufanya kazi kwa kutumia mtiririko wa elektron
ambao umefanywa katika mfumo maalum). Mfano wa kompyuta hizi ni Konrad Zuse's
electromechanical au "Z machines" au Z3 (1941), Atanasoff–Berry Computer (1941), Colossus
computer (1944) ambayo ilitumika kwa ajili ya shughuli za siri katika jeshi la uingereza na
ilitumika katika kupata taarifa za siri za jeshi la ujerumani katika vita ya pili ya dunia, Harvard
Mark I (1944) na kompyuta iliyotumika na jeshi la Wamarekani iliyojulikana kama ENIAC.

Hata hivyo teknolojia hii ya vacuum tubes ilitumika mpaka mwishoni mwa miaka ya 1950 na
mwanzoni mwa miaka ya 1960 kulizinduliwa teknolojia mpya inayofahamika kama transistor
technology. Kompyuta zilizotumia teknolojia hii ziliweza kufanya kazi kwa urahisi zaidi, hazikuwa
aghali sana, zilikuwa ndogo, zilitumia umeme mdogo zaidi na ziliweza kufanya kazi kwa uhakika
zaidi kuliko zile za mwanzo. Kumbuka kuwa kompyuta za mwanzo zilikuwa na ukubwa sawa na
chumba kikubwa cha nyumba! Teknolojia ambayo mpaka sasa inatumika katika utengenezaji wa
kompyuta inaitwa integrated circuit technology. Teknolojia hii ilizinduliwa mnamo miaka ya 1970.
Ni teknolojia hii ambayo imesababisha kuzaliwa kwa kompyuta ambazo ni ndogo zaidi kuweza hata kubebwa katika kiganja cha mkono! Hii ni kea sababu ya kuundwa kwa kifaa kijulikanacho
kama microprocessor ambacho ndicho kama ubongo wa kompyuta. Kifaa hiki kina ukubwa wa
kama saizi ya milimita tano kwa nne. Ingawa kina umbo ndogo sana lakini kina jumla ya zaidi ya
transistor (sakiti ndogondogo zinazofanya kazi kwa ushirikiano) milioni moja!


Alhamisi, Februari 07, 2013

TEKNOHAMA - UTANGULIZI



Kompyuta ama Tarakilishi katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha
kabisa mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita. Kutokana na kuwapo kifaa hiki dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile katika historia ya kuwapo kwake. Kifaa hiki kimeleta mabadiliko makubwa Sana katika maisha ya kawaida ya binadamu. Kifaa hiki kimesababisha mambo mengi kufanyika katika hali ambayo hakika isingewezekana au ambayo awali ingeonekana kama ya kufikirika!.

Kompyuta imeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi. Kompyuta imeifanya dunia kuwa Kama
kijiji kidogo ambacho unaweza kukizunguka katika muda mfupi Sana wa sekunde chache! Lakini je unaifahamu kompyuta? Je wajua kuwa ni kifaa kidogo sana lakini chenye uwezo wa kufanya mambo mengi? Je wajua kuwa ndicho kifaa kinachoiendesha dunia katika Nyanja za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni?

Bila shaka umekwisha sikia na kukiona kifaa kinachoitwa kompyuta. Umekwisha sikia habari nyingi tu juu ya kifaa hiki ambacho hakika kimeifanya dunia nzima kukitegemea katika shughuli zote za kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na hata kisiasa. Bila shaka umekwisha sikia kuwa unaweza kununua bidhaa kwa kutumia kompyuta ukiwa nyumbani kwako bila ya hata kwenda huko sokoni au dukani. Bila shaka umekwisha sikia kuwa mabenki, hospitali, taa za kuongozea magari barabarani, kamera za usalama, ndege za abiria na kivita na hata lift unazopanda kila siku unapoingia na kutoka ofisini katika jengo refu huendeshwa kwa msaada wa kompyuta. Bila shaka umekwisha jionea mwenyewe au kusikia habari kama hizi. Umekwisha sikia kuwa mtu anaweza kumchagua mgombea wa urais au ubunge kwa kutumia kompyuta! Haya na mambo chungu nzima hufanyika kwa msaada wa kompyuta.

Katika nchi zilizoendelea matumizi ya kifaa hiki yanaendelea kushika hatamu kiasi kwamba kila
kitu sasa kinafanywa Kwa kutumia mashine zinazoongozwa Na kifaa hiki.

Lakini pia wengi hubaki wakijiuliza maswali mengi juu ya kifaa hiki. Je, ni vipi kifaa hiki kinakuwa na uwezo mkubwa kiasi hiki? Kinaweza vipi kufanya kazi automatically? Je kinaweza kufanya jambo lolote? Je ni nani ambaye alitengeneza kifaa hiki? Je kompyuta ikitengenezwa hujiendesha yenyewe bila msaada wa binadamu? Je kompyuta imetengenezwa Kwa kutumia vifaa gani na viko vingapi? Haya ni maswali ambayo kila mtu ambaye haifahamu vizuri teknolojia hii atapenda kupata majibu yake. Katika mfululizo wa makala haya nitakuletea ufafanuzi wa kina juu ya kifaa hiki ambacho hakika kinasisimua katika ufanyaji kazi na katika uundwaji wake.