Mtayarishaji

Morning Star Radio

Alhamisi, Februari 07, 2013

TEKNOHAMA - UTANGULIZI



Kompyuta ama Tarakilishi katika lugha ya Kiswahili ni kifaa ambacho kimebadilisha
kabisa mfumo wa maisha ya binadamu katika miongo takribani sita iliyopita. Kutokana na kuwapo kifaa hiki dunia imejikuta katika maendeleo makubwa kabisa kuliko kipindi chochote kile katika historia ya kuwapo kwake. Kifaa hiki kimeleta mabadiliko makubwa Sana katika maisha ya kawaida ya binadamu. Kifaa hiki kimesababisha mambo mengi kufanyika katika hali ambayo hakika isingewezekana au ambayo awali ingeonekana kama ya kufikirika!.

Kompyuta imeyafanya maisha kuwa rahisi zaidi. Kompyuta imeifanya dunia kuwa Kama
kijiji kidogo ambacho unaweza kukizunguka katika muda mfupi Sana wa sekunde chache! Lakini je unaifahamu kompyuta? Je wajua kuwa ni kifaa kidogo sana lakini chenye uwezo wa kufanya mambo mengi? Je wajua kuwa ndicho kifaa kinachoiendesha dunia katika Nyanja za kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni?

Bila shaka umekwisha sikia na kukiona kifaa kinachoitwa kompyuta. Umekwisha sikia habari nyingi tu juu ya kifaa hiki ambacho hakika kimeifanya dunia nzima kukitegemea katika shughuli zote za kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na hata kisiasa. Bila shaka umekwisha sikia kuwa unaweza kununua bidhaa kwa kutumia kompyuta ukiwa nyumbani kwako bila ya hata kwenda huko sokoni au dukani. Bila shaka umekwisha sikia kuwa mabenki, hospitali, taa za kuongozea magari barabarani, kamera za usalama, ndege za abiria na kivita na hata lift unazopanda kila siku unapoingia na kutoka ofisini katika jengo refu huendeshwa kwa msaada wa kompyuta. Bila shaka umekwisha jionea mwenyewe au kusikia habari kama hizi. Umekwisha sikia kuwa mtu anaweza kumchagua mgombea wa urais au ubunge kwa kutumia kompyuta! Haya na mambo chungu nzima hufanyika kwa msaada wa kompyuta.

Katika nchi zilizoendelea matumizi ya kifaa hiki yanaendelea kushika hatamu kiasi kwamba kila
kitu sasa kinafanywa Kwa kutumia mashine zinazoongozwa Na kifaa hiki.

Lakini pia wengi hubaki wakijiuliza maswali mengi juu ya kifaa hiki. Je, ni vipi kifaa hiki kinakuwa na uwezo mkubwa kiasi hiki? Kinaweza vipi kufanya kazi automatically? Je kinaweza kufanya jambo lolote? Je ni nani ambaye alitengeneza kifaa hiki? Je kompyuta ikitengenezwa hujiendesha yenyewe bila msaada wa binadamu? Je kompyuta imetengenezwa Kwa kutumia vifaa gani na viko vingapi? Haya ni maswali ambayo kila mtu ambaye haifahamu vizuri teknolojia hii atapenda kupata majibu yake. Katika mfululizo wa makala haya nitakuletea ufafanuzi wa kina juu ya kifaa hiki ambacho hakika kinasisimua katika ufanyaji kazi na katika uundwaji wake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni