Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumapili, Juni 12, 2016

UMUHIMU WA ELIMU YA MUZIKI NA ELIMU YA UENDESHAJI WA MUZIKI

Photo By: www.borgenmagazine.com


Asilimia kubwa ya wanamuziki hapa Tanzania wanapiga muziki bila ya kuwa na elimu yoyote ya awali ya muziki, hili si jambo la ajabu kwani hali hii iko sehemu nyingi duniani, lakini kitu ambacho ni wazi kinakosekana ni elimu kuhusu utendaji wa taasnia ya muziki. 

Pamoja na kauli nyingi nzuri za viongozi wa Nchi kusifu sanaa hii na wasanii wa sanaa hii lakini ni nadra kusikia kiongozi akiongelea matayarisho rasmi katika sanaa hii na kwa kweli hata katika sanaa nyingine.

Kumekuwepo na ombwe la elimu ya uendeshaji wa tasnia ya sanaa. Ombwe la elimu kwa wataalamu ambao huwezesha wasanii kufika walipo, kuwaendeleza kukaa walipo, kulinda haki za kimaslahi za wasanii na hata kuwapa maelekezo ya kujitayarisha kwa wakati ambapo umaarufu utakuwa umekwisha.

Tasnia ya muziki huhiyaji shule za kujifunza muziki, vyuo vya uongozi wa muziki, au kozi fupi ambapo taaluma za umeneja, uproducer, upublisher, usambazaji, ujuzi wa sheria za hakimiliki na watendaji wengine wa aina hiyo hupata elimu, ujuzi wa sheria za hakimiliki na watendaji wengine wa aina hiyo hupata elimu. Kukosekana kwa elimu hii kumefanya watu kujifunza kwa vitendo kwa kujaribu na hata kubahatisha hivyo mara chache kufanikiwa.

Kukosa elimu sahihi kumewafanya wasanii wengine wenye uwezo mkubwa kupotea kwenye taaluma na wengine kujikuta wakishindwa kuingia kwenye ulingo huu japo uwezo wanao. Pia kumetoa nafasi ya wasio na uwezo kujikita katika uongozi wa sanaa na kuleta matatizo makubwa kwenye sanaa, aidha kwa kuaminika kuwa wanatoa ushauri sahii na hivyo maamuzi yenye hasara kubwa kufanyika. 

Pamoja na mafanikio yaliyoonekana taifa linakwenda kihobela hobela katika tasnia ya sanaa ya muziki. Ushahidi wa wazi upo kwa kupata elimu ya muziki kuanzia umri mdogo kuna faida nyingi sana. Kwanza humuwezesha motto kukuza sehemu ya ubongo ambayo huhusika na hesabu na pia kukuza uwezo wake wa kutafakari. 

Inaeleweka kuwa ubongo huendelea kupata maendeleo miaka mingi baada ya kuzaliwa, hivyo muziki huendelea kuboresha upande wa kushoto wa ubongo ambao ndio huhusika na ujuzi wa lugha na tafakari na hesabu. Muziki husaidia sana watoto kukumbuka mambo mbalimbali, ndio maana hata matangazo ya biashara ya kawaida husindikizwa na muziki ili kukaa katika kumbukumbu kwa urahisi. Kwa watoto muziki husaidia sana katika kazi zao za elimu ya kila siku.

Wasanii waliopata elimu sahihi huwa na uwezo wa kubuni majibu mbalimbali kwa tatizo moja, hii unaweza kuiona kwa mfano ukiwapa wanamuziki kumi semina kuhusu jambo. Kwa mfano: Ukimwi kasha ukawaambia watunge wimbo kuhusu elimu waliyopewa, utashangaa watakuja na tungo tofauti za mtizamo mpya kabisa wa kuelezea elimu hiyo waliyoipata.

Elimu ya muziki hufungua ubongo kuruhusu kuachana na mawazo mengi yaliyopita na kujaribu mawazo mapya. Wasanii kote duniani huwa waanzilishi wa mambo mengi ikiwemo mitindo ya nguo, uvaaji na mambo mengi katika maisha kutokana na ubongo wao kuwa na uwezo wa kuruhusu kufikiria vitu katika mtazamo mpya.

Elimu ya awali ya muziki imeonesha kuwa wanafunzi wa elimu hii hfanya vizuri zaidi katika masomo mengine tofauti sana na mawazo ya kawaida kuwa muziki huharibu watoto. Katika muziki, kosa huwa ni kosa, ukikosea beat, usipotune chombo chako, ukiimba vibaya ni kosa hakuna mbadala, sauti ikiwa juu mno, au chini mno na kadhalika, na wanamuziki hulazimika kurudia tena na tena mpaka atakapopata kitu sahihi na kabisa.

Elimu hii ikiwa kichani kwa watoto toka umri mdogo humsaidia katika kuboresha mambo yake mengine na kuyafanya vizuri zaidi kila mara. Elimu ya awali ya muziki humjenga motto kujua kufanya kazi na watu wengine kama kundi, kutokana na kuelewa kuwa katika muziki watu wengi hutegemeana ili kuleta ubora katika wimbo mmoja, hii huwasaidia katika maisha kila siku.

Kuna mengi yanayopatikana katika elimu bora ya sanaa, pia kubwa likiwa ni kwenda sambamba kitaaluma na ulimwengu, kuna bahati mbaya sana kwa vijana wetu kutaka kuingia katika soko la muziki duniani lakini bila kuwa na matayarisho yanayostahili kufikia huko, wengi ni ndoto zao hazitatimia kwani elimu ya kufikia huko hawana.

Ni wazi kuna haja ya kuanza kutoa elimu ya sanaa kuanzia ngazi ya shule za awali, kuna haja sasa ya kuwasaidia wanamuziki walioko kwenye taaluma kupata elimu ya haki zao. 

Ni wasanii wangapi wanaojua kuwa katika kila tungo, kuna haki tofauti kumi wanazostahili? 

Watunzi wangapi wanajua wana haki kwa kazi zao kutumika kibiashara? 

Wakati viongozi wakisifia wasanii wan je wakumbuke kuwa kinachowafanya wawe na mafanikio ni kutumia kila njia sahihi kukamua mapato kutoka kwenye haki zao hizo zinazolindwa kisheria.
  
Makala hii ni kwa msaada wa John Kitime

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni