Mtayarishaji

Morning Star Radio

Ijumaa, Juni 03, 2016

UGONJWA WA MKAZO (STRESS)

Photo Credit By:  http://luxuryspablog.com/


Ni ukweli usiopingika kwamba mwanadamu anakabiliwa na changamoto mbalimbali za kiuchumi, kiafya, kijamii na kadhalika. 

Changamoto zote hizo huongezeka zaidi pindi mwadamu anapofikia umri wa utu uzima, kwa maana ya umri wa kubebeshwa majukumu ya kimaisha, kama vile kusaidia wanafamilia, wanaukoo na jamii kiujumla. Hata hivyo, changamoto kubwa za kiafya zinazomkabili mwanadamu huyu, karibu kote ulimwenguni ni ugonjwa wa Mkazo, ambao kitaalamu wanaita Stress pamoja na kupanda kwa Shinikizo la Damu, kitaalamu Hypertension. 

Baadhi ya vitu vinavyosababisha ugonjwa huu wa Mkazo kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ni pamoja na hofu au wasiwasi kuhusiana na jambo lolote linaloweza kumkumba mwanadamu, hasa ukosefu wa fedha mfukoni au kutamani utajiri ambao hajui ataupataje. 

 Lakini pia, ratiba za shughuli za kiuchumi na huduma zenye mambo mengi yasiyokuwa na mpangilio huweza kumsababisha ugonjwa huo binadamu, pamoja na ugomvi usiokwisha ndani ya familia, kukumbana na matukio ya kutisha kama vile ya ugaidi na kadhalika.  

Watu wengi ulimwenguni wamezoea kutumia kilevi, kama vile pombe, tumbaku na vileo vingine ili kukabiliana na maradhi hayo ya Mkazo na kupanda kwa Shinikizo la Damu. Hali hiyo, inatokana na wengi wao hao kushidwa hata kula vizuri, huku baadhi yao wakilazimika kutumia muda mwingi kuangalia matukio katika televisheni au kutumia vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta na simu za mkononi kwa muda mrefu ili tu kujisahaulisha na msongo wa mawazo kichwani. 

Mkazo na Kupanda kwa Shinikizo la Damu, ni vitu vinavyoendana sana katika maisha ya mwanadamu, ndiyo maana ili kudhibiti magonjwa hayo, mhusika hushauriwa kudhibiti kwanza hali yake ya Mkazo.

Kituo kimoja cha Matibabu ya Akili kilichoko nchini Uingereza, zinabainisha kwamba katika kila kundi la watu watano ulimwenguni, basi mtu mmoja hukumbwa na maradhi ya Mkazo unaotokana na mazingira ya mahali pake pa kazi. Kwa mujibu wa taarifa hizo, kushindwa kukabiliana na hali hiyo ya Mkazo mwingi, mtu mmoja kati ya watu wanne, hujikuta akilia peke yake bila kupigwa wala kukasirishwa na yeyote, akiwa kazini kwake. 

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba mwanadamu ameumbwa kwa njia ya kipekee kabisa, kwa kuwekewa mifumo mbalimbali mwilini inayofanya kazi mbalimbali usiku na mchana ili tu kumweka vizuri na salama katika maisha yake. 

Kwa mfano, mwanadamu amewekewa mfumo wa hisia za dharura, ambao ni kichochea kikuu cha mwili pindi mwanadamu huyu anapopatwa na Mkazo mwingi. Vichocheo hivyo, ndivyo vinavyomfanya binadamu huyo anapopatwa na hali hiyo aweze kupumua haraka, moyo wake uende mbio na kadhalika hali inayochangia kuongezeka kwa Shinikizo la Damu. 

Aidha, vichocheo hivyo, ndivyo huongeza chembe za damu na sukari kwenye damu. Kwa kawaida, mfumo huo wa hisia za dharura unafanya kazi kubwa ya kumtayarisha mwanadamu kukabiliana na kitu chochote au mtu yeyote anayemsababishia hali hiyo ya Mkazo. 

Hata hivyo, baada ya jambo hilo linalosababisha Mkazo kupita, mwili hurudi katika hali yake ya kawaida, ingawa baadhi ya wataalamu wanaweka wazi kuwa endapo hali hiyo ya hisia za dharura inajirudia mara kwa mara, mtu anaweza akakumbwa na ugonjwa mwingine wa hofu au wasiwasi, ambao kitaalamu unajulikana kama 'Anxiety Disorder'. 

 Kwa hiyo, kwa kila binadamu awaye yeyote yule, ni muhimu kujifunza mbinu za kukabiliana na maradhi hayo Mkazo na kupanda kwa Shinikizo la Damu. Kwa sasa zipo njia kuu rahisi 10 za kukabiliana na hali hiyo. 

mediaphotos/Getty Images


Mosi, ni kuhakikisha unapata muda wa kutosha wa kulala usingizi, Kutopata usingizi wa kutosha kunaathiri hisia, akili, kiwango cha nishati mwilini pamoja na afya kiujumla. Wataalamu wa afya wanashauri mtu mzima apate usingizi wa walau saa nane (8) katika kila saa 24 za siku. 

 Pili, katika kujipangia mipango ya maisha, unashauriwa kutanguliza mambo muhimu yanayokuwezesha kuishi maisha yenye kiasi. Kwa maneno mengine, binadamu anatakiwa kufikiri jinsi ya kurahisisha maisha yake, pengine kwa kupunguza gharama za maisha pamoja na kupunguza muda anaotumia kufanya kazi kazini kwake. 

Tatu, jifunze mbinu za kupumzisha mwili. Kutafakari kwa kina (Meditation), mazoezi ya kuvuta pumzi na yoga ni njia imara za kuondoa Mkazo. 

 Nne, mtu inampasa kuimarisha mtandao wake wa kijamii. Kujiunga na vikundi mbalimbali kama vile vya masomo, kutoa misaada kama vile kwa watoto, yatima na wajane au vikundi vya wajasiriamali. Mwaka 2008, baadhi ya watafiti raia wa Uingereza waligundua njia moja ya kubaki imara pindi mtu anapopatwa na Mkazo. Katika utafiti wao, wanasema moja ya njia ya kubakia imara, ni kujitolea kuwasaidia wengine kwa njia fulani fulani. 

Tano, mtu inampasa kujitahidi kuelewa vizuri hisia za wengine, kitu kitakachomsaidia kupunguza hasira, na wakati huo huo awe mwepesi kusamehe kwa kuwa ni jambo jema pia kimaisha. Utafiti uliofanywa mwaka 2001 nchini Uingereza, ulionyesha kwamba mtu anapokuwa na kinyongo fulani kwa mtu, humsababishia kupanda kwa Shinikizo la Damu pamoja na kuongezeka kwa mapigo ya moyo. Hali hiyo, kwa mujibu wa utafiti huo, inaweza kuondolewa kwa mtu kuwa mwepesi wa kusamehe haraka. 

Sita, kwa gharama yoyote, mtu anatakiwa kujiepusha na ugomvi wa aina yoyote ile. Kugombana na wengine kunaweza kumletea au kumsababishia mtu Mkazo mwingi. Mtu anapokuchokoza jitahidi kutulia, usimwage ugali kwa kuwa yeye kamwaga mboga. Inashauriwa kujitenga naye kwa kukaa faragha, hivyo kusuluhisha mambo kwa hekima na busara nyingi. 

Saba, jipangie ratiba ya matumizi ya muda kwa kuandaa muda wa kutatua matatizo ya familia na ya kazini, kwa kutumia mbinu bora za makubaliano. Aidha, mtu anaweza akatunza muda wake wa kazi na familia kwa ufanisi hivyo kupunguza kiwango cha Mkazo kwake. 

Nane, inampasa mtu ajitahidi kupunguza hali zitakazomwongezea Mkazo kadri awezavyo, kwa kutoruhusu hali zenye kuongeza Mkazo. Kwa mfano, kujiepusha kuwaza mambo mabaya yanayoweza kutokea na kuchota hisia zake. 

Tisa ni kuhakikisha mwili mzima unatunzwa. Baada ya kazi nzito, jitahidi kuukanda mwili kwa maji ya uvuguvugu, kabla ya kula chakula. Mazoezi ya kutembea na kusikiliza muziki unaoifurahisha nafsi yako ni muhimu pia. 10, ni kuondokana na woga wa kuomba msaada kwa jamaa na marafiki au majirani. 

Baadhi ya tafiti zinaonyesha kwamba kuzungumza na marafiki au watu wa familia kuhusu hali inayokupata, husaidia kuondoa ugonjwa wa Mkazo. Hata hivyo, pamoja na njia zote hizo 10 rahisi, inashauriwa na wataalamu wa akili na mifumo ya miili kwamba endapo Mkazo na hali ya wasiwasi itaendelea, ni muhimu kutafuta msaada zaidi kwa Daktari, ikiwezekana upatiwe dawa za kutibu hali hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni