Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumapili, Aprili 27, 2014

Ubora wa Sauti

 
Unahitaji kufanya nini?

Unahitaji kuboresha sauti yako kwa kupumua vizuri na kutuliza misuli yako badala ya kuiga mtu mwingine.

Kwa Nini Ni Muhimu?

Sauti nzuri hufanya wengine watulie na kufurahia kusikiliza. Sauti mbaya huharibu mawasiliano, na inaweza kumfadhaisha msemaji na wasikilizaji.

KWA KAWAIDA watu hawavutiwi tu na mambo yanayosemwa, bali wanavutiwa pia na jinsi yanavyosemwa. Ikiwa mtu anayezungumza nawe ana sauti nzuri, changamfu, ya kirafiki, na yenye fadhili, utafurahia kumsikiliza kuliko kama ana sauti kali isiyo ya kirafiki, sivyo?

Kukuza sifa hizo nzuri hakutegemei tu kuboresha sauti. Kunaweza kuhusu utu wa mtu pia. Mtu anapoendelea kujifunza kweli ya Biblia na kuifuata, kwa wazi njia yake ya kuzungumza inabadilika. Sauti yake huonyesha sifa kama vile upendo, shangwe, na fadhili. (Gal. 5:22, 23) Anapojali wengine sana, sauti yake inaonyesha. Anapokuwa mwenye shukrani badala ya kulalamika daima, maneno anayosema na sauti yake inaonyesha hivyo. (Wim. 3:39-42; 1 Tim. 1:12; Yuda 16) Hata kama huelewi lugha fulani, ni rahisi kujua ikiwa mtu anazungumza kwa njia ya ufidhuli, hana uvumilivu, anachambua, ni mkali, na pia ni rahisi kujua kama mwingine anazungumza kwa unyenyekevu, subira, fadhili, na upendo.

Nyakati nyingine sauti isiyofaa inaweza kusababishwa na kasoro fulani ambayo mtu amezaliwa nayo au ugonjwa uliodhuru zoloto. Huenda kasoro hizo zisiweze kurekebishwa katika mfumo huu wa mambo. Lakini, unaweza kuboresha sauti yako ukijifunza kutumia vizuri viungo vya usemi.

Kwanza, tufahamu kwamba sauti za watu hutofautiana. Kwa hiyo, usijaribu kuiga sauti ya mtu mwingine. Badala yake, boresha sauti yako mwenyewe pamoja na hali zake. Unawezaje kufaulu? Kuna mambo mawili makuu.

Pumua Vizuri. Ili sauti yako iwe nzuri, unahitaji hewa ya kutosha na unahitaji kupumua vizuri. Bila kufanya hivyo, sauti yako inaweza kuwa dhaifu mno na unaweza kukata-kata maneno katika hotuba yako.
Sehemu kubwa za mapafu haziko juu kifuani; sehemu hizo huonekana kubwa kwa sababu tu ya mifupa ya mabega. Lakini, sehemu za mapafu zilizo pana zaidi ziko chini, juu tu ya kiwambo. Kiwambo kinashikana na mbavu za chini na kinatenganisha kifua na tumbo.

Ukivuta pumzi na kujaza tu sehemu za juu za mapafu, utakosa pumzi haraka. Sauti yako itakosa nguvu na utachoka haraka. Ili uvute pumzi vizuri, unahitaji kuketi au kusimama vizuri na kurejesha mabega nyuma. Jaribu sana usipanue sehemu ya juu pekee ya kifua unapovuta pumzi. Kwanza vuta pumzi kabisa. Sehemu za chini za mapafu zikijaa hewa, mbavu zako za chini zitapanuka. Kwa wakati huohuo, kiwambo kitasonga chini, kikisukuma chini kwa utaratibu sehemu za tumbo hivi kwamba utasikia mkazo kwenye mshipi wako au kwenye vazi katika eneo la tumbo. Lakini mapafu hayako kwenye eneo la tumbo; yamefunikwa na mbavu. Unaweza kuthibitisha jambo hilo kwa kuweka mkono mmoja kila upande wa mbavu za chini. Kisha vuta pumzi kabisa. Kama unavuta pumzi vizuri, utaona kwamba huingizi hewa tumboni na kuinua mabega. La, badala yake, utasikia mbavu zikisonga juu kidogo na kupanuka.

Kisha, jaribu kushusha pumzi. Usishushe pumzi kwa ghafula. Ishushe polepole. Usijaribu kuzuia pumzi kwa kukaza koo kwa sababu sauti itajikaza au itakuwa nyembamba sana. Mkazo wa misuli ya tumbo na mkazo wa misuli iliyo kati ya mbavu huondosha pumzi, lakini kiwambo hudhibiti mwendo wa pumzi hiyo.
Msemaji anaweza kudhibiti jinsi anavyopumua kwa kujizoeza kama vile tu mwanariadha anavyofanya mazoezi ya mbio. Simama vizuri kama umerejesha nyuma mabega, vuta pumzi kabisa ili sehemu za chini za mapafu zijae hewa, kisha shusha pumzi polepole na kwa utaratibu ukihesabu kwa kadiri uwezavyo kabla ya kuvuta tena pumzi. Kisha jizoeze kusoma kwa sauti ukipumua kwa njia hiyo.

Tuliza Mkazo wa Misuli. Jambo jingine muhimu linalotokeza sauti nzuri ni utulivu! Unaweza kuboresha sana sauti yako ukijifunza kutulia unapozungumza. Ni lazima akili na mwili zitulie, kwa kuwa mkazo wa akili husababisha mkazo wa misuli.

Ondoa mkazo wa akili kwa kuwa na maoni mazuri juu ya watu unaozungumza nao. Ikiwa unakutana nao katika huduma ya shambani, kumbuka kwamba hata kama umejifunza Biblia kwa miezi michache tu, unajua mambo mazuri sana kuhusu kusudi la Yehova ambayo unaweza kuwaeleza. Na unawatembelea kwa sababu wanahitaji msaada, iwe wanatambua jambo hilo au la. Na kama unatoa hotuba katika Jumba la Ufalme, wengi wa wasikilizaji ni watu wa Yehova. Wao ni rafiki zako na wanataka ufaulu. Hakuna wasemaji wengine duniani ambao huhutubia wasikilizaji wenye urafiki na wenye upendo kama sisi.

Ifikirie misuli ya koo na kujaribu kuituliza. Kumbuka kwamba nyuzi zako za sauti hutikisika zinapopitisha hewa. Sauti hubadilika misuli hiyo ikikazika au ikitulia kama tu vile uzi wa gitaa hubadili sauti ukikazwa au ukilegezwa. Sauti hurudi chini nyuzi za sauti zinapotulia. Kutuliza misuli ya koo pia hufanya mianzi ya pua ibaki wazi, na hiyo huboresha sauti.

Tuliza mwili wako mzima—magoti, mikono, mabega, na shingo. Ukifanya hivyo, utaweza kuvumisha sauti vizuri ili isikike wazi. Sauti huvumishwa wakati mwili wote unapohusika kuitokeza, lakini mkazo huizuia. Sauti hutokezwa kwenye zoloto nayo huvumishwa katika mianzi ya pua, kwenye mifupa ya kifua, meno, na kaakaa ya mdomo na mianya iliyo katika mifupa ya pua. Sehemu hizo zote zinaweza kuchangia ubora wa sauti. Ukiweka kitu kwenye kibao cha gitaa cha kupaazia sauti, sauti itafifia; ni lazima kibao hicho kisiwe na kitu ili kitikisike na kutoa sauti vizuri. Ndivyo ilivyo pia na mifupa ya mwili wetu ambayo imeshikiliwa na misuli. Uvumishaji mzuri wa sauti unakuwezesha kuwa na ubadilifu wa sauti na kuweza kuonyesha hisia mbalimbali unapozungumza. Pia utaweza kuhutubia watu wengi zaidi bila kukaza sauti.

JINSI YA KUFAULU

Kuza sifa za utu wa Kikristo.
Fanya mazoezi ya kuvuta pumzi, ukijaza sehemu za chini za mapafu kwa hewa.
Unapozungumza, tuliza misuli yako ya koo, shingo, mabega, na mwili wote mzima.

MAZOEZI: 

 (1) Kwa dakika chache kila siku katika juma, fanya mazoezi ya kuvuta pumzi kabisa mpaka uzijaze sehemu za chini za mapafu yako. 

(2) Jaribu kutuliza misuli ya koo unapoongea, angalau mara moja kwa siku.

SAUTI HUTOKEZWAJE?

  Sauti zote hutokezwa na hewa inayotoka mapafuni. Mapafu hupiga hewa kama pampu kupitia koo na kuingia ndani ya zoloto ambayo iko katikati ya koo. Ndani ya zoloto mna misuli miwili midogo inayoitwa nyuzi za sauti, msuli mmoja uko upande mmoja na msuli mwingine upande mwingine. Nyuzi hizo za sauti ndizo vitokezaji vikuu vya sauti. Misuli hiyo hufungua na kufunga njia ya hewa katika zoloto ili kuingiza hewa na kuitoa na vilevile kuzuia vitu visivyotakikana visiingie kwenye mapafu. Tunapopumua kwa njia ya kawaida nyuzi za sauti hazitokezi sauti wakati hewa inapopita. Lakini mtu akitaka kuzungumza, misuli hufinya nyuzi za sauti, na nyuzi hizo hutikisika wakati hewa inayotoka mapafuni inaposukumwa kuzipitia. Utaratibu huo hutokeza sauti.

  Kadiri nyuzi za sauti zinavyokazika, ndivyo zinavyotikisika kwa kasi zaidi na ndivyo sauti inavyoinuka. Na kadiri nyuzi hizo zinavyolegea, ndivyo sauti inavyopungua. Mawimbi ya sauti yanayotoka kwenye zoloto huingia sehemu ya juu ya koo inayoitwa koromeo. Kisha mawimbi hayo hupitia mdomo na pua. Hapo sauti nyinginezo huongezwa ili kurekebisha, kukuza, na kuimarisha sauti ya awali. Kaakaa la mdomo, ulimi, meno, utaya, na midomo huungana pamoja ili kutawanya mawimbi ya sauti, na kutokeza usemi unaoeleweka.
  Sauti ya mwanadamu ni ajabu sana, na haina kifani ikilinganishwa na chombo chochote kile ambacho binadamu ametengeneza. Ina uwezo wa kuonyesha hisia mbalimbali kama vile upendo na chuki kali. Sauti ikikuzwa na kuzoezwa vizuri, inaweza kubadilikana sana na kutokeza nyimbo tamutamu na semi zinazogusa mioyo.


KUSHINDA MATATIZO FULANI HUSUSA

  Sauti dhaifu. Sauti ndogo huenda isiwe dhaifu. Ikiwa nzuri na yenye kuvutia, wengine wanaweza kufurahi kuisikiliza. Lakini ni lazima sauti iwe yenye kiasi kinachofaa ili iweze kufaidi wengine.

  Ili uboreshe ukubwa wa sauti yako, unahitaji kuivumisha zaidi. Unahitaji kutuliza mwili wote mzima, kama ilivyoonyeshwa katika somo hili. Pamoja na kutuliza mwili, fanya mazoezi ya kuimba hali umefunga midomo. Midomo inapaswa kugusana kidogo, isishikane sana. Unapoimba kwa njia hiyo, sikia mitikisiko ya wimbo huo akilini na kifuani.

  Nyakati nyingine sauti husikika kuwa dhaifu au kukazika kwa sababu ya ugonjwa au kukosa usingizi. Bila shaka, hali hiyo ikiboreka, sauti itaboreka.

  Sauti inayoinuka juu sana. Mkazo kwenye nyuzi za sauti hufanya sauti iinuke. Sauti yenye mkazo hufanya wasikilizaji wawe na mkazo. Unaweza kupunguza sauti nyembamba kwa kutuliza misuli ya koo ili kupunguza mkazo kwenye nyuzi za sauti. Jaribu kufanya hivyo, ukifanya mazoezi kila siku unapozungumza. Pia ni vizuri kuvuta pumzi kabisa.

  Sauti ya kubana pua. Nyakati nyingine pua iliyofungika hutokeza tatizo hilo, lakini mara nyingi hali hiyo husababishwa na jambo jingine. Nyakati nyingine kwa kukaza misuli ya koo na mdomo, mtu hufunga mianya ya pua na kuzuia hewa isipite vizuri. Jambo hilo hutokeza sauti inayobana pua. Unahitaji kutulia ili kuepuka jambo hilo.

  Sauti nzito na kali. Sauti kama hiyo haitokezi mazungumzo ya kirafiki. Inaweza kutisha wengine.
  Katika hali fulani, jambo muhimu ni kuendelea kujitahidi kubadili utu wako. (Kol. 3:8, 12) Ikiwa tayari umefanya hivyo, kujaribu kutumia kanuni za kurekebisha sauti kunaweza kusaidia. Tuliza koo na taya. Kufanya hivyo kutafanya sauti yako ipendeze zaidi na kufanya maneno mengine yasitokee vibaya kwa kuyalazimisha kupitia meno.

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Viungo vya Matamshi
 Kaakaa
Ulimi
Meno
Midomo
Taya

Mkondo wa Hewa Mwilini
 Tundu la pua
Kinywa
Koo
Nyuzi za sauti
Njia ya chakula
Mapafu
Kiwambo

Nyuzi za Sauti (zikitazamwa kutoka juu)
Unapozungumza
Unapovuta pumzi
Unapovuta pumzi kabisa

Jumatatu, Aprili 14, 2014

FAIDA ZA TENDE MWILINI



Katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, tende ndiyo tunda linaloliwa kwa wingi, pengine kuliko tunda lingine. Pamoja na kuwa ni tunda lenye ladha tamu na nzuri mdomoni, lakini kisayansi pia limethibitika kusheheni madini na vitamini lukuki, hivyo kuwa na faida nyingi kiafya. Katika makala ya leo, nimekuorodhoshea faida zake 10:

1. Ukila tende mara kwa mara, mwili wako utapata aina mbalimbali za madini na vitamin za kutosha, ambazo zinapatikana kwenye tunda hili maarufu duniani. Katika tende kuna kiasi kidogo tu cha mafuta (fat) na haina lehemu (kolestrol).

2. Ukila tende, utajipatia kiasi cha kutosha cha protini na vitamin B1, B2, B3, B5, A1, na C, virutubisho ambavyo ni muhimu kwa ustawi wa afya ya mwili wako kwa ujumla.

3. Ulaji wa tende huimarisha na kuboresha mfumo wa usagaji chakula tumboni, hivyo utaondokana na matatizo ya ukosefu wa choo, au matatizo ya kupata choo kigumu kinachosababisha maumivu wakati wa kujisaidia. Pia ndani ya tende kuna virutubisho vya ‘amino acids’ ambavyo ni muhimu mwilini.

4. Ukila tende, mwili utapata nguvu na kukuondolea uchovu ndani ya nusu saa tu, kwa sababu tende ina virutubisho vya sukari asilia kama vile ‘glucose’, ‘sucrose’ na ‘fructose’. Ili kupata faida zaidi za tende,
changanya na maziwa fresh kisha kula. Unapojisikia mchovu, badala ya kunywa vinywaji baridi vinavyodai kuongeza nguvu, kula tende, hata kiasi cha punje tatu kinatosha. Kwa wafunga saumu, ndiyo maana inashauriwa kuanza kufungua kwa kula tende ili kuurejeshea mwili wako nguvu iliyopotea siku nzima.

5. Tende ina madini pia aina ya ‘potassium’ na kiasi kidogo cha chumvi (sodium). Madini haya husaidia uimarishaji wa mishipa ya fahamu. Watafiti wamegundua kwamba ulaji kiasi wa ‘potassium’ huweza kumuepusha mtu na kupatwa na kiharusi (stroke). Pia tende husaidia kupunguza lehemu (cholesterol) mwilini (LDL Cholesterol).

6. Kwa wale wenye matatizo ya ugonjwa wa kukauka damu mwilini (anemia), wanaweza kupata ahueni kwa kula tende kwa wingi ambayo ina kiwango cha kutosha cha madini ya chuma ambayo huhitajika katika utengenezaji wa damu mwilini. Wakati vitu vitamu vingine huozesha meno, utamu wa tende huzuia uozaji wa meno.

7. Kwa tatizo sugu na la muda mrefu la ukosefu wa choo, loweka tende za kutosha kwenye maji kiasi cha lita moja usiku kucha, kisha asubuhi changanya maji hayo pamoja na hizo tende ili upate juisi nzito, kunywa na choo kitafunguka na kuwa laini.

8. Kwa matatizo ya ukosefu wa nguvu za kiume, mchanganyiko maalum wa tende, maziwa, asali na unga wa hiriki vinaweza kuondoa tatizo lako. Chukua kiasi cha kiganja kimoja cha tende, loweka kwenye maziwa ya mbuzi kiasi cha lita moja na yakae usiku kucha.

Asubuhi, zisage tende hizo kwenye maziwa hayo hadi zichangayike, kisha weka asali kiasi cha vijiko vitatu au vinne vikubwa pamoja na unga wa hiriki, kiasi cha nusu kijiko kidogo. Kisha kunywa mchangayiko huo kila siku hadi utakapoona mabadiliko ya kuridhisha.

9. Tende ni dawa ya unene, kwa wale wenye matatizo ya wembamba wa kupindukia na wanataka kuongeza uzito, ulaji wa tende kila siku unaweza kuwasaidia. Lakini hii ina maana kwamba, wale wanaohitaji kupunguza uzito, ulaji wa tende kwa wingi hauwezi kuwafaa. Pia tende husaidia uondoaji wa kilevi mwilini.

10. Tende inatibu saratani ya tumbo. Habari njema kuhusu tende kama tiba ni kwamba, haina madhara yoyote kwa sababu ni dawa asilia na inafanyakazi vizuri kuliko dawa za ‘kizungu’. Tende vile vile ina imarisha nuru ya macho na tatizo la kutokuona usiku (night blindness).

Kwa ujumla faida za tende ni nyingi na unaweza kuila tende kwa namna mbalimbali, kama vile kuchanganya na maziwa, kuchanganya na mkate au vitafunwa vingine. Ifanye tende kuwa sehemu ya mlo wako wa kila siku ili ujipatie faida hizi 10 na nyingine.


Chanzo: http://jiko-langu.blogspot.com

FAIDA ZA NDIZI KATIKA MWILI WA BINADAMU.



TOFAUTI na vyakula vingine, ndizi zinafaida kubwa sana katika mwili wa binadamu. Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, ndizi zina virutubisho vya aina mbalimbali kama vile, protini, mafuta, kalishiamu, wanga, fosiforas, madini ya chuma, vitamin A,B,C na maji.

Ndizi zina faida zipi katika urembo? Chanzo cha nishati Ndizi zina uwezo wa kumeng’enywa kwa urahisi zaidi, tena zina nishati kubwa, sukari iliyomo katika ndizi ni chanzo kizuri sana cha nishati.

Hivyo naweza kusema kuwa ndizi ikiliwa ipasavyo itakusaidia kujenga mwili na misuli yako kwa ujumla. Husaidia kuondoa chunusi Chunusi ni miongoni mwa matatizo ambayo huwasumbua warembo wengi hususan wanawake.

Je, unafahamu kuwa ndizi mbivu zinaweza kukuondolea tatizo hilo? Kwa kuchanganya ndizi mbivu na maziwa na asali na kisha kuzisaga ili kupata urojo ambao utatumia kupaka kwenye maeneo yaliyoathirika, unaweza kuondokana kabisa na tatizo hilo.

Fanya hivyo kila siku na hakikisha unakaa na mchanganyiko huo kwa muda usiopungua dakika 30 hadi 40, kisha osha na maji ya baridi ikiwezekana yaliyopozwa na jokofu.

Ndizi katika ‘diet’ Ndizi zina nafasi kubwa sana kati kuongeza au kupunguza uzito, hivyo unaweza kutumia ikiwa unahitaji kupunguza ama kuongeza uzito wako.

Kwa wajawazito Ndizi ni chakula kizuri kwa wanawake wajawazito, kwani kina kiwango kikubwa cha ‘folic acid’ ambayo inaweza kufyonzwa kwa urahisi sana na kiumbe kilicho tumboni. Ikiwa mama mjamzito atatumia ndizi mara kwa mara ni wazi kuwa atakuwa mwenye muonekano mzuri na wa kuvutia.

Ni kinga dhidi ya magonjwa ya moyo, presha, vidonda vya tumbo, saratani ya figo, kukosa choo

Ndizi mbivu ni tunda ambalo linafahamika na kila mtu, lakini sina hakika kama watu wengi wanafahamu umuhimu na faida za tunda hili ambalo linapatikana kirahisi sana nchini. Bei yake ni kati ya shilingi 50 na 150 tu, kiwango cha pesa ambacho kila mtu anaweza kukimudu.

Iwapo ulikuwa hujui umuhimu wa kula ndizi mbivu, leo utalazimika kubadili mtizamo wako na kuziangalia ndizi kama tunda muhimu katika kuupa nguvu na kuulinda mwili wako dhidi ya maradhi hatari ambayo hayana tiba. Watu wa michezo pia wanapaswa kuliona tunda hili kuwa ni muhimu sana katika kuipa miili yao nguvu.

KINGA DHIDI YA SHINIKIZO LA DAMU NA MARADHI YA MOYO

Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi, ndizi ni chanzo kikubwa cha Potassium, madini ambayo ni muhimu sana katika kuweka shinikizo la damu mwilini katika hali yake ya kawaida (Normal Blood Pressure), na ufanyaji kazi mzuri wa moyo. Kwa kuwa ndizi moja ina wastani wa 467mg za madini aina ya Potasiamu na 1mg ya sodiamu (chumvi), ndizi moja tu kwa siku inaweza kukupa kinga ya maradhi ya shinikizo la damu na matatizo ya moyo.

Ukweli kuhusu vyakula vyenye kiwango kikubwa cha madini ya Potasiamu katika kushusha shinikizo la damu mwilini, umethibitishwa na tafiti nyingi za kisayansi. Kwa mujibu wa jarida moja la masuala ya afya nchini Marekani, zaidi ya Wamarekani 40,000 wa kike na kiume, walifanyiwa utafiti kwa muda wa miaka minne na ikagundulika kwamba watu wanaokula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha madini ya Potasiamu na kirutubisho cha Fiber (Ufumwele), wako katika hatari ndogo ya kupatwa na kiharusi.

Aidha, utafiti mwingine uliofanywa na taasisi moja ya masuala ya tiba ijulikanayo kama Archives of Internal Medicine, ya nchini Marekani, pia ilithibitisha kwamba ulaji wa vyakula vyenye kiasi kikubwa cha ufumwele (fiber) kama vile ndizi, husaidia sana kutoa kinga dhidi ya maradhi ya moyo. Na katika suala hili, zaidi ya watu 10,000 walifanyiwa utafiti kwa muda wa miaka 19.

KINGA DHIDI Y VIDONDA VYA TUMBO

Kwa muda mrefu sana imethibitishwa kwamba ndizi ina virutubisho vyenye uwezo wa kupambana na asidi tumboni hivyo kutoa kinga dhidi ya vidonda vya tumbo (stomach Ulsers) na kutoa ahueni kwa mtu ambaye tayari ameathirika. Katika utafiti mmoja, ilkibainika kwamba mtu akila mchangayiko wa ndizi mbivu na maziwa freshi, huzuia utokaji wa asidi tumboni inayosababisha vidonda vya tumbo.

Kwa mujibu wa utafiti wa kisayansi juu ya suala hili, ndizi hutoa kinga na ahueni ya vidonda vya tumbo kwa njia mbili. Mosi: virutubisho vilivyomo kwenye ndizi huzipa uhai seli zenye kazi ya kutengeneza utandu ambao hutoa aina fulani ya urojo (mucus) unaotumika kama kizuizi dhidi ya asidi tumboni.

Pili: kuna virutubisho vingine kwenye ndizi ambavyo kwa kitaalamu vinajulikana kama ‘Protease’ ambavyo husaidia kuondoa bakteria tumboni ambao wanaelezewa kuwa ndiyo chanzo cha vidonda vya tumbo. Hivyo kama wewe hujaptwa na vidonda vya tumbo, kwa kula ndizi mara kwa mara unajipa kinga madhubuti na kama tayari umeathirika na vidonda, kwa kula ndizi utajipa ahueni kubwa.

NDIZI KAMA TIBA KWA WENYE MATATIZO YA CHOO

Ndizi ni muhimu sana katika kulainisha na kusafisha tumbo na kumuwezesha mtu kupata choo. Mbali ya kusaidia upatikanaji wa choo kwa wenye matatizo hayo, lakini pia hutoa ahueni kwa wagonjwa wa kipindupindu. Mtu aliyepatwa na kipindupindu hupoteza kiasi kikubwa cha madini ya Potasiamu, hivyo kwa kula ndizi ataweza kurejesha mwilini maidni yake yaliyopotea na kuupa mwili nguvu yake.

UIMARISHAJI WA NURU YA MACHO

Wakati ulipokuwa mdogo, bila shaka uliwahi kuambiwa na mama kuwa mtu akila karoti, atakuwa akiona vizuri. Bila shaka hakukosea, lakini sasa ukiwa mtu mzima unaambiwa kwamba ulaji wa matunda, ikiwemo ndizi, ndiyo kinga hasa dhidi ya matatizo ya kutokuona vizuri uzeeni. Utafiti wa hivi karibuni unaonesha kwamba ulaji wa matunda kwa wingi kila siku, hupunguza kwa asilimia 36 matatizo ya kutokuona vizuri kutokana na mtu kuwa na umri mkubwa.

KINGA DHIDI YA SARATANI YA FIGO

Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa na Jarida la Kimataifa la masuala ya Saratani (International Journal of Cancer) la nchini Marekani, umeonesha kwamba ulaji wa mara kwa mara wa matunda halisi, hasa ndizi mbivu, ni kinga madhubuti ya mwili. Zaidi ya wawake 50,000 wenye umri kati ya miaka 40 na 76 waliofanyiwa utafiti, ulionesha kuwa wale waliokula wastani wa milo 2.5 ya matunda na mboga kila siku, walipunguza hatari ya kupatwa na saratani ya figo kwa asilimia 40.

Baadhi ya vitamini na madini yaliyomo kwenye ndizi ni pamoja na Vitamini B6, Vitamin C, Potassium, Dietary Fibre na Mnganese. Hivyo utaona kwamba tunda la ndizi ni muhimu kwa sababu limesheheni vitamini na madini muhimu katika mwili wa binadamu. Kuanzia leo itazame ndizi kama tunda muhimu sana katika ustawi wa afya yako na ni kinga dhidi ya maradhi unayoweza kuyaepuka kesho kwa kula tunda hili kwa wingi leo!

 

Chanzo: http://jiko-langu.blogspot.com

Ijumaa, Aprili 04, 2014

Uwezo Wetu Na Nguvu Za Kuvumilia

Kila asubuhi tunapoamka, tunakumbana na siku mpya iliyojaa changamoto za maisha. Changamoto hizi huja kwa aina nyingi: changamoto za kimwili, pingamizi za kifedha, matatizo na mahusiano, majaribio ya kihisia, na hata mapambano na imani ya mtu.


Nyingi za changamoto tunazokabiliana nazo maishani zinaweza kutatuliwa na kushindwa, hata hivyo, nyengine huenda zikawa ngumu kuelewa na kutowezekana kushindwa na zitakuwa nasi mpaka tutakapoaga duniani. Tunapovumilia kwa muda changamoto tunazoweza kutatua na tunapoendelea kuvumilia changamoto ambazo hatuwezi kutatua, ni muhimu kukumbuka kwamba nguvu ya kiroho tunayokuza zitatusaidia kuvumilia vyema changamoto zote tunazokabiliana nazo maishani.


Ndugu na dada, tunaye Baba wa Mbinguni, anayetupenda, ambaye amesanifu kuwepo kwetu duniani ili tuweze kibinafsi kujifunza masomo tunayohitaji kujifunza ili kufuzu kwa ajili ya uzima wa milele katika uwepo wake.


Kipindi katika maisha ya Nabii Joseph Smith kinaeleza kanuni hii. Nabii na wenzi kadhaa walikuwa wamekuwa wafungwa kule Liberty, Missouri, kwa miezi. Wakiteseka gerazani, Nabii Joseph alimsihi Bwana katika maombi ya unyenyekevu kwamba Watakatifu wangeweza kufarijiwa kutokana na mateso yao ya sasa. Bwana alijibu kwa kumfundisha Nabii Joseph, na sisi sote, kwamba changamoto tunazokumbana nazo, zikivumiliwa vyema, zitatusaidia mwishowe. Hili ndilo jibu la Bwana kwa dua ya Joseph:

“Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako, taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi;

“Na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu.”


Baba wa Mbinguni amepanga safari yetu maishani kuwa mtihani wa silka zetu. Tunaachwa tushawishiwe na mema na mabaya na kisha kupewa wakala wa kimaadili kujichagulia wenyewe njia tutakayochukua. Kama vile nabii Samweli wa Kitabu cha Mormoni wa kale alivyofundisha, “Mko huru, mmekubaliwa kujichagulia, kwani tazama, Mungu amewapatia elimu na amewafanya huru.”


Baba wa Mbinguni pia alielewa kwamba kutokana na hali yetu ya kidunia hatungefanya chaguo sahihi au la haki kila wakati. Kwa sababu sisi si wakamilifu na kwa sababu sisi hufanya makosa, tunahitaji usaidizi ili kurudi kwa uwepo Wake. Msaada unaohitajika hutolewa kupitia mafundisho, mfano, na dhabihu ya upatanisho wa Yesu Kristo. Dhabihu ya upatanisho wa Mwokozi huwezesha wokovu wetu wa baadaye na utukufu kupitia kanuni ya toba. Tukitubu kwa uaminifu na dhati, Upatanisho unaweza kutusaidia kuwa wasafi, kubadilisha asili yetu, na kuvumilia vyema changamoto zetu.


Uvumilivu ni kanuni muhimu inayopatikana katika mafundisho ya Yesu Kristo. Ni muhimu kwa sababu uzuri wa maisha yetu ya baadaye ya milele unalingana na uwezo wetu wa kuvumilia katika wema.

Katika 2 Nefi 31 nabii Nefi anatufundisha kwamba baada ya kupokea agizo lile lile la wokovu la ubatizo ambalo Yesu Kristo alipokea na kisha tupokee karama ya Roho Mtakatifu, lazima “tusonge mbele tukila na kusheherekea neno la Kristo, na tuvumilie hadi mwisho, tazama, [na basi] hivyo ndivyo asema Baba: [Sisi] tutapokea uzima wa milele.”


Hivyo basi, ili kupokea baraka kuu ya zote za Baba yetu wa Mbinguni, ambayo ni uzima wa milele, lazima tukamilishe kazi ya agano inayostahili na kisha tuendelee kutii maagano yanayohusika. Yaani, lazima tuvumilie vyema.


Uwezo wetu wa kuvumilia hadi mwisho katika wema utakuwa unalingana moja kwa moja na nguvu ya ushuhuda wetu na kina cha uongofu wetu. Wakati shuhuda zetu ziko imara na tumeongoka kwa kweli kwa injili ya Yesu Kristo, chaguo zetu zitasawishiwa na Roho Mtakatifu, zitakuwa na msingi katika Kristo, na zitahimili hamu yetu ya kuvumilia katika wema. Ikiwa shuhuda zetu ni dhaifu na uongofu wetu ovyo, hatari ni zaidi kwamba tutashawishiwa na tamaduni za uongo za dunia ili kufanya chaguo mbaya.


Ningependa kushiriki tukio linaloonyesha juhudi inayohitajika kuvumilia kimwili na kisha kulilinganisha kwa juhudi inayohitajika kuvumilia kiroho. Baada ya kurudi kutoka misheni yangu, nilikuwa na nafasi ya kucheza mpira wa vikapu na kocha mwenye ushawishi mkubwa na mwandishi katika chuo kule California. Kocha huyu alikuwa makini sana kuhusu wachezaji wake kuwa katika hali nzuri ya kimwili kabla ya kuanza kwa msimu wa mpira wa vikapu. Moja ya mahitaji yake ya zoezi kabla ya yeyote kati yetu kuweza kugusa mpira wa kikapa kwenye kiwanja cha mazoezi ilikuwa ni kukimbia mzunguko wa mbio za nyika katika milima karibu na shule kwa wakati maalum na ngumu sana. Ninakumbuka jaribio langu la kwanza kabisa katika kukimbia kozi hii ya mbio za nyika punde baada ya kurejea kwangu kutoka misheni: Nilifikiria ningekufa.
Ilichukua wiki nyingi za mafunzo makali ili hatimaye kuvunja rekodi ya wakati ambao kocha alikuwa ameweka kama lengo. Ilikuwa ni hisia nzuri si ​​tu kuweza kukimbia mzunguko lakini pia kuharakisha hadi kwenye uhondo wa mwisho hadi kwenye laini ya kumaliza.


Ili kucheza mpira wa vikapu vyema, unahitaji kuwa katika hali nzuri ya kimwili. Kuwa katika hali nzuri ya kimwili huja kwa gharama, na gharama hiyo ni kujitolea, uvumilivu, na nidhamu ya kibinafsi. Uvumilivu wa kiroho pia huja kwa gharama. Ni gharama ile ile: kujitolea, uvumilivu, na nidhamu ya kibinafsi.


Ushuhuda, kama mwili wako, unahitaji kuwa katika hali nzuri kama unautaka hudumu. Hivyo basi ni jinsi gani tunaweka ushuhuda wetu katika hali nzuri? Hatuwezi kufanya miili yetu kuwa katika hali nzuri ya kucheza mpira wa vikapu kwa kutazama tu mpira wa vikapu kwenye televisheni. Vile vile, hatutaweza kuweka shuhuda zetu katika hali nzuri kwa kutazama tu mkutano mkuu kwenye televisheni. Tunahitaji kusoma na kujifunza kanuni za msingi za injili ya Yesu Kristo, na kisha ni lazima tufanye tuwezavyo kuizitumia maishani. Hivyo ndivyo tunavyokuwa wafuasi wa Yesu Kristo, na hivyo ndivyo tunavyojenga ushuhuda wa kudumu.

Tunapokabiliwa na shida maishani na hamu yetu ni kuiga sifa za Yesu Kristo, ni muhimu kuwa tayari kiroho. Kuwa tayari kiroho kunamaanisha tumekuza sulubu na nguvu ya kiroho---tutakuwa katika hali nzuri ya kiroho. Tutakuwa katika hali nzuri kiroho hata kwamba tutachagua wema kila mara. Tutakuwa hatuhamashiki katika hamu na uwezo wetu wa kuishi injili. Kama vile mwandishi mmoja asiyejulikana aliwahi kusema, “Ni lazima uwe mwamba ambao mto hauwezi kuondoa.”


Kwa sababu sisi tunakabiliwa na changamoto kila siku, ni muhimu kwamba tufanye kazi juu ya ushupavu wetu wa kiroho kila siku. Sisi  tunapokuza ushupavu wa kiroho, tamaduni za uongo za dunia, pamoja na changamoto zetu za kibinafsi za kila siku, zitakuwa na athari ndogo kwa uwezo wetu wa kuvumilia katika wema.


Mifano mizuri ya ushupavu wa kiroho huja kutoka historia za familia zetu wenyewe. Miongoni mwa hadithi nyingi kutoka kwa mababu zetu, tutaweza kupata mifano ambayo inaonyesha tabia chanya ya uvumilivu.

Hadithi kutoka kwa historia ya familia yangu mwenyewe inaeleza kanuni hii. Baba ya babu yangu mkuu Joseph Maynes Watson alizaliwa mnamo 1856 kule Hull, Yorkshire, Uingereza. Familia yake ilijiunga na Kanisa kule Uingereza na kisha kwenda Jijini Salt Lake. Alimuoa Emily Keep mnamo 1883, na wakawa wazazi wa watoto wanane. Joseph aliitwa kuhudumu misheni ya muda mnamo Juni 1910, alipokuwa na umri wa miaka 53. Na kwa usaidizi wa mke wake na watoto wanane, alirudi nchi yake ya asili Uingereza kuhudumu misheni yake.

Baada ya kuhudumu kwa uaminifu kwa takriban miaka miwili, alikuwa akiendesha baiskeli yake pamoja na mwenziwe kwenda misa ya Shule ya Jumapili kule Gloucester, Uingereza, ambapo tairi yake ikapasuka. Alishuka kutoka wa baiskeli yake ili kutathmini uharibifu. Alipoona ya kuwa ilikuwa imeharibika sana na ingechukua muda kurekebisha, alimwaambia mwenziwe amtangulie na kuanza ibada ya Jumapili na angefika pale baada ya muda mfupi. Punde tu alipomaliza kusema hayo, alianguka chini. Alikufa ghafula kutokana na mshtuko wa moyo.

Joseph Watson Maynes kamwe hakumwona mke wake na watoto wanane tena katika maisha haya. Waliweza kusafirisha mwili wake kurudi katika Jiji la Salt Lake na kuwa na huduma ya mazishi yake katika ukumbi mzee wa Waterloo Assembly Hall. Kauli iliyotolewa katika mazishi yake na Mzee Anthony W. Ivins wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili inatufundisha somo muhimu kuhusu maisha, kifo, na uvumilivu: “Hii ndiyo injili inatupa---si kinga kutokana na kifo, lakini ushindi juu yake kupitia matumaini ambayo tunayo katika ufufuo mtukufu. … Unamgusia [Joseph Maynes] . …Ni furaha, na jambo la kuridhisha na shangwe kujua kwamba wanadamu hujitolea maisha yao kwa haki, kwa imani, wakiwa wakweli kwa imani.”


Hadithi hii ya familia yangu inanishawishi kujaribu niwezavyo kufuata mfano wa uvumilivu na sulubu ya kiroho iliyoonyeshwa na baba ya babu yangu. Ninavutiwa pia na imani ya mke wake, Emily, ambaye maisha yake baada ya kifo cha Joseph hakika yalikuwa mzigo mzito kubeba. Ushuhuda wake ulikuwa imara na uongofu wake kamili akiishi maisha yake yote baadaye akiwa mwaminifu kwa imani akiwasaidia watoto wake wanane pekee yake.


Mtume Paulo alisema, “Na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi, na tupige mbio kwa subira katika yale mashinidano yaliyowekwa mbele yetu.” Mashindano yaliyowekwa mbele yetu katika dunia hii ni mbio ya uvumilivu, iliyojaa vizuwizi. Vizuwizi katika mashindano haya ni changamoto tunazoamka nazo kila asubuhi. Tuko hapa duniani ili kukimbia mbio, kutumia wakala wetu wa kimaadili, na kuchagua kati ya mema na mabaya. Ili kukamilisha mbio kwa heshima na mafanikio na kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni, tutalazimika kulipa gharama ya kujitolea, uvumilivu na nidhamu ya kibinafsi. Tunahitaji kuwa katika hali nzuri ya kiroho. Tunahitaji kukuza sulubu ya kiroho. Tunahitaji shuhuda imara zitakazoelekeza kwa uongofu wa kweli, na kwa matokeo tupate ndani yetu amani ya ndani na nguvu inayohitajika kuvumilia changamoto zozote huenda tukakabilina nazo.


Hivyo basi bila kujali changamoto unazoamkia kila asubuhi, kumbuka---na nguvu ya kiroho unayokuza, pamoja na msaada wa Bwana, mwishoni mwa mashindano utaweza kufurahia hakikisho ambalo Mtume Paulo alionyesha aliposema:


“Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.

“Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda:

“Baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile.”

Nawatolea ushuhuda na ushahidi wangu wa uhalisi wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo na mpango wake wa furaha mkuu na wa milele, ambao umetuleta kwenye dunia hii wakati huu. Roho wa Bwana awavutie kukuza ndani yenu nguvu ya kuvumilia. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chanzo:   INGIA HAPA