Unahitaji kufanya nini?
Unahitaji kuboresha sauti yako kwa kupumua vizuri na kutuliza misuli yako badala ya kuiga mtu mwingine.
Kwa Nini Ni Muhimu?
Sauti nzuri hufanya wengine
watulie na kufurahia kusikiliza. Sauti mbaya huharibu mawasiliano, na
inaweza kumfadhaisha msemaji na wasikilizaji.
KWA KAWAIDA watu hawavutiwi tu na mambo yanayosemwa, bali
wanavutiwa pia na jinsi yanavyosemwa. Ikiwa mtu anayezungumza nawe ana
sauti nzuri, changamfu, ya kirafiki, na yenye fadhili, utafurahia
kumsikiliza kuliko kama ana sauti kali isiyo ya kirafiki, sivyo?
Kukuza sifa hizo nzuri
hakutegemei tu kuboresha sauti. Kunaweza kuhusu utu wa mtu pia. Mtu
anapoendelea kujifunza kweli ya Biblia na kuifuata, kwa wazi njia yake
ya kuzungumza inabadilika. Sauti yake huonyesha sifa kama vile upendo,
shangwe, na fadhili. (Gal. 5:22, 23)
Anapojali wengine sana, sauti yake inaonyesha. Anapokuwa mwenye
shukrani badala ya kulalamika daima, maneno anayosema na sauti yake
inaonyesha hivyo. (Wim. 3:39-42; 1 Tim. 1:12; Yuda 16)
Hata kama huelewi lugha fulani, ni rahisi kujua ikiwa mtu anazungumza
kwa njia ya ufidhuli, hana uvumilivu, anachambua, ni mkali, na pia ni
rahisi kujua kama mwingine anazungumza kwa unyenyekevu, subira, fadhili,
na upendo.
Nyakati nyingine sauti isiyofaa
inaweza kusababishwa na kasoro fulani ambayo mtu amezaliwa nayo au
ugonjwa uliodhuru zoloto. Huenda kasoro hizo zisiweze kurekebishwa
katika mfumo huu wa mambo. Lakini, unaweza kuboresha sauti yako
ukijifunza kutumia vizuri viungo vya usemi.
Kwanza, tufahamu kwamba sauti za
watu hutofautiana. Kwa hiyo, usijaribu kuiga sauti ya mtu mwingine.
Badala yake, boresha sauti yako mwenyewe pamoja na hali zake. Unawezaje
kufaulu? Kuna mambo mawili makuu.
Pumua Vizuri.
Ili sauti yako iwe nzuri, unahitaji hewa ya kutosha na unahitaji
kupumua vizuri. Bila kufanya hivyo, sauti yako inaweza kuwa dhaifu mno
na unaweza kukata-kata maneno katika hotuba yako.
Sehemu kubwa za mapafu haziko
juu kifuani; sehemu hizo huonekana kubwa kwa sababu tu ya mifupa ya
mabega. Lakini, sehemu za mapafu zilizo pana zaidi ziko chini, juu tu ya kiwambo. Kiwambo kinashikana na mbavu za chini na kinatenganisha kifua na tumbo.
Ukivuta pumzi na kujaza tu
sehemu za juu za mapafu, utakosa pumzi haraka. Sauti yako itakosa nguvu
na utachoka haraka. Ili uvute pumzi vizuri, unahitaji kuketi au kusimama
vizuri na kurejesha mabega nyuma. Jaribu sana usipanue sehemu ya juu
pekee ya kifua unapovuta pumzi. Kwanza vuta pumzi kabisa. Sehemu za
chini za mapafu zikijaa hewa, mbavu zako za chini zitapanuka. Kwa wakati
huohuo, kiwambo kitasonga chini, kikisukuma chini kwa utaratibu sehemu
za tumbo hivi kwamba utasikia mkazo kwenye mshipi wako au kwenye vazi
katika eneo la tumbo. Lakini mapafu hayako kwenye eneo la tumbo;
yamefunikwa na mbavu. Unaweza kuthibitisha jambo
hilo kwa kuweka mkono mmoja kila upande wa mbavu za chini. Kisha vuta
pumzi kabisa. Kama unavuta pumzi vizuri, utaona kwamba huingizi hewa
tumboni na kuinua mabega. La, badala yake, utasikia mbavu zikisonga juu
kidogo na kupanuka.
Kisha, jaribu kushusha pumzi.
Usishushe pumzi kwa ghafula. Ishushe polepole. Usijaribu kuzuia pumzi
kwa kukaza koo kwa sababu sauti itajikaza au itakuwa nyembamba sana.
Mkazo wa misuli ya tumbo na mkazo wa misuli iliyo kati ya mbavu
huondosha pumzi, lakini kiwambo hudhibiti mwendo wa pumzi hiyo.
Msemaji anaweza kudhibiti jinsi
anavyopumua kwa kujizoeza kama vile tu mwanariadha anavyofanya mazoezi
ya mbio. Simama vizuri kama umerejesha nyuma mabega, vuta pumzi kabisa
ili sehemu za chini za mapafu zijae hewa, kisha shusha pumzi polepole na
kwa utaratibu ukihesabu kwa kadiri uwezavyo kabla ya kuvuta tena pumzi.
Kisha jizoeze kusoma kwa sauti ukipumua kwa njia hiyo.
Tuliza Mkazo wa Misuli.
Jambo jingine muhimu linalotokeza sauti nzuri ni utulivu! Unaweza
kuboresha sana sauti yako ukijifunza kutulia unapozungumza. Ni lazima
akili na mwili zitulie, kwa kuwa mkazo wa akili husababisha mkazo wa
misuli.
Ondoa mkazo wa akili kwa kuwa na maoni mazuri juu ya watu
unaozungumza nao. Ikiwa unakutana nao katika huduma ya shambani, kumbuka
kwamba hata kama umejifunza Biblia kwa miezi michache tu, unajua mambo
mazuri sana kuhusu kusudi la Yehova ambayo unaweza kuwaeleza. Na
unawatembelea kwa sababu wanahitaji msaada, iwe wanatambua jambo hilo au
la. Na kama unatoa hotuba katika Jumba la Ufalme, wengi wa wasikilizaji
ni watu wa Yehova. Wao ni rafiki zako na wanataka ufaulu. Hakuna
wasemaji wengine duniani ambao huhutubia wasikilizaji wenye urafiki na
wenye upendo kama sisi.
Ifikirie misuli ya koo na
kujaribu kuituliza. Kumbuka kwamba nyuzi zako za sauti hutikisika
zinapopitisha hewa. Sauti hubadilika misuli hiyo ikikazika au ikitulia
kama tu vile uzi wa gitaa hubadili sauti ukikazwa au ukilegezwa. Sauti
hurudi chini nyuzi za sauti zinapotulia. Kutuliza misuli ya koo pia
hufanya mianzi ya pua ibaki wazi, na hiyo huboresha sauti.
Tuliza mwili wako mzima—magoti,
mikono, mabega, na shingo. Ukifanya hivyo, utaweza kuvumisha sauti
vizuri ili isikike wazi. Sauti huvumishwa wakati mwili wote unapohusika
kuitokeza, lakini mkazo huizuia. Sauti hutokezwa kwenye zoloto nayo
huvumishwa katika mianzi ya pua, kwenye mifupa ya kifua, meno, na kaakaa
ya mdomo na mianya iliyo katika mifupa ya pua. Sehemu hizo zote
zinaweza kuchangia ubora wa sauti. Ukiweka kitu kwenye kibao cha gitaa
cha kupaazia sauti, sauti itafifia; ni lazima kibao hicho kisiwe na kitu
ili kitikisike na kutoa sauti vizuri. Ndivyo ilivyo pia na mifupa ya
mwili wetu ambayo imeshikiliwa na misuli. Uvumishaji mzuri wa sauti
unakuwezesha kuwa na ubadilifu wa sauti na kuweza kuonyesha hisia
mbalimbali unapozungumza. Pia utaweza kuhutubia watu wengi zaidi bila
kukaza sauti.
JINSI YA KUFAULU
Kuza sifa za utu wa Kikristo.
Fanya mazoezi ya kuvuta pumzi, ukijaza sehemu za chini za mapafu kwa hewa.
Unapozungumza, tuliza misuli yako ya koo, shingo, mabega, na mwili wote mzima.
MAZOEZI:
(1) Kwa dakika chache kila siku katika juma, fanya mazoezi ya kuvuta
pumzi kabisa mpaka uzijaze sehemu za chini za mapafu yako.
(2) Jaribu
kutuliza misuli ya koo unapoongea, angalau mara moja kwa siku.
SAUTI HUTOKEZWAJE?
Sauti zote hutokezwa na hewa
inayotoka mapafuni. Mapafu hupiga hewa kama pampu kupitia koo na kuingia
ndani ya zoloto ambayo iko katikati ya koo. Ndani ya zoloto mna misuli
miwili midogo inayoitwa nyuzi za sauti, msuli mmoja uko upande mmoja na
msuli mwingine upande mwingine. Nyuzi hizo za sauti ndizo vitokezaji
vikuu vya sauti. Misuli hiyo hufungua na kufunga njia ya hewa katika
zoloto ili kuingiza hewa na kuitoa na vilevile kuzuia vitu
visivyotakikana visiingie kwenye mapafu. Tunapopumua kwa njia ya kawaida
nyuzi za sauti hazitokezi sauti wakati hewa inapopita. Lakini mtu
akitaka kuzungumza, misuli hufinya nyuzi za sauti, na nyuzi hizo
hutikisika wakati hewa inayotoka mapafuni inaposukumwa kuzipitia.
Utaratibu huo hutokeza sauti.
Kadiri nyuzi za sauti
zinavyokazika, ndivyo zinavyotikisika kwa kasi zaidi na ndivyo sauti
inavyoinuka. Na kadiri nyuzi hizo zinavyolegea, ndivyo sauti
inavyopungua. Mawimbi ya sauti yanayotoka kwenye zoloto huingia sehemu
ya juu ya koo inayoitwa koromeo. Kisha mawimbi hayo hupitia mdomo na
pua. Hapo sauti nyinginezo huongezwa ili kurekebisha, kukuza, na
kuimarisha sauti ya awali. Kaakaa la mdomo, ulimi, meno, utaya, na
midomo huungana pamoja ili kutawanya mawimbi ya sauti, na kutokeza usemi
unaoeleweka.
Sauti ya mwanadamu ni ajabu
sana, na haina kifani ikilinganishwa na chombo chochote kile ambacho
binadamu ametengeneza. Ina uwezo wa kuonyesha hisia mbalimbali kama vile
upendo na chuki kali. Sauti ikikuzwa na kuzoezwa vizuri, inaweza
kubadilikana sana na kutokeza nyimbo tamutamu na semi zinazogusa mioyo.
KUSHINDA MATATIZO FULANI HUSUSA
Sauti dhaifu.
Sauti ndogo huenda isiwe dhaifu. Ikiwa nzuri na yenye kuvutia, wengine
wanaweza kufurahi kuisikiliza. Lakini ni lazima sauti iwe yenye kiasi
kinachofaa ili iweze kufaidi wengine.
Ili uboreshe ukubwa wa sauti
yako, unahitaji kuivumisha zaidi. Unahitaji kutuliza mwili wote mzima,
kama ilivyoonyeshwa katika somo hili. Pamoja na kutuliza mwili, fanya
mazoezi ya kuimba hali umefunga midomo. Midomo inapaswa kugusana kidogo,
isishikane sana. Unapoimba kwa njia hiyo, sikia mitikisiko ya wimbo huo
akilini na kifuani.
Nyakati nyingine sauti
husikika kuwa dhaifu au kukazika kwa sababu ya ugonjwa au kukosa
usingizi. Bila shaka, hali hiyo ikiboreka, sauti itaboreka.
Sauti inayoinuka juu sana.
Mkazo kwenye nyuzi za sauti hufanya sauti iinuke. Sauti yenye mkazo
hufanya wasikilizaji wawe na mkazo. Unaweza kupunguza sauti nyembamba
kwa kutuliza misuli ya koo ili kupunguza mkazo kwenye nyuzi za sauti.
Jaribu kufanya hivyo, ukifanya mazoezi kila siku unapozungumza. Pia ni
vizuri kuvuta pumzi kabisa.
Sauti ya kubana pua.
Nyakati nyingine pua iliyofungika hutokeza tatizo hilo, lakini mara
nyingi hali hiyo husababishwa na jambo jingine. Nyakati nyingine kwa
kukaza misuli ya koo na mdomo, mtu hufunga mianya ya pua na kuzuia hewa
isipite vizuri. Jambo hilo hutokeza sauti inayobana pua. Unahitaji
kutulia ili kuepuka jambo hilo.
Sauti nzito na kali. Sauti kama hiyo haitokezi mazungumzo ya kirafiki. Inaweza kutisha wengine.
Katika hali fulani, jambo muhimu ni kuendelea kujitahidi kubadili utu wako. (Kol. 3:8, 12)
Ikiwa tayari umefanya hivyo, kujaribu kutumia kanuni za kurekebisha
sauti kunaweza kusaidia. Tuliza koo na taya. Kufanya hivyo kutafanya
sauti yako ipendeze zaidi na kufanya maneno mengine yasitokee vibaya kwa
kuyalazimisha kupitia meno.
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Viungo vya Matamshi
Kaakaa
Ulimi
Meno
Midomo
Taya
Mkondo wa Hewa Mwilini
Tundu la pua
Kinywa
Koo
Nyuzi za sauti
Njia ya chakula
Mapafu
Kiwambo
Nyuzi za Sauti (zikitazamwa kutoka juu)
Unapozungumza
Unapovuta pumzi
Unapovuta pumzi kabisa
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni