Kila
asubuhi tunapoamka, tunakumbana na siku mpya iliyojaa changamoto za
maisha. Changamoto hizi huja kwa aina nyingi: changamoto za kimwili,
pingamizi za kifedha, matatizo na mahusiano, majaribio ya kihisia, na
hata mapambano na imani ya mtu.
Nyingi
za changamoto tunazokabiliana nazo maishani zinaweza kutatuliwa na
kushindwa, hata hivyo, nyengine huenda zikawa ngumu kuelewa na
kutowezekana kushindwa na zitakuwa nasi mpaka tutakapoaga duniani.
Tunapovumilia kwa muda changamoto tunazoweza kutatua na tunapoendelea
kuvumilia changamoto ambazo hatuwezi kutatua, ni muhimu kukumbuka kwamba
nguvu ya kiroho tunayokuza zitatusaidia kuvumilia vyema changamoto zote
tunazokabiliana nazo maishani.
Ndugu
na dada, tunaye Baba wa Mbinguni, anayetupenda, ambaye amesanifu kuwepo
kwetu duniani ili tuweze kibinafsi kujifunza masomo tunayohitaji
kujifunza ili kufuzu kwa ajili ya uzima wa milele katika uwepo wake.
Kipindi
katika maisha ya Nabii Joseph Smith kinaeleza kanuni hii. Nabii na
wenzi kadhaa walikuwa wamekuwa wafungwa kule Liberty, Missouri, kwa
miezi. Wakiteseka gerazani, Nabii Joseph alimsihi Bwana katika maombi ya
unyenyekevu kwamba Watakatifu wangeweza kufarijiwa kutokana na mateso
yao ya sasa. Bwana alijibu kwa kumfundisha Nabii Joseph, na sisi sote,
kwamba changamoto tunazokumbana nazo, zikivumiliwa vyema, zitatusaidia
mwishowe. Hili ndilo jibu la Bwana kwa dua ya Joseph:
“Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako, taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi;
“Na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu.”
Baba
wa Mbinguni amepanga safari yetu maishani kuwa mtihani wa silka zetu.
Tunaachwa tushawishiwe na mema na mabaya na kisha kupewa wakala wa
kimaadili kujichagulia wenyewe njia tutakayochukua. Kama vile nabii
Samweli wa Kitabu cha Mormoni wa kale alivyofundisha, “Mko huru,
mmekubaliwa kujichagulia, kwani tazama, Mungu amewapatia elimu na
amewafanya huru.”
Baba
wa Mbinguni pia alielewa kwamba kutokana na hali yetu ya kidunia
hatungefanya chaguo sahihi au la haki kila wakati. Kwa sababu sisi si
wakamilifu na kwa sababu sisi hufanya makosa, tunahitaji usaidizi ili
kurudi kwa uwepo Wake. Msaada unaohitajika hutolewa kupitia mafundisho,
mfano, na dhabihu ya upatanisho wa Yesu Kristo. Dhabihu ya upatanisho wa
Mwokozi huwezesha wokovu wetu wa baadaye na utukufu kupitia kanuni ya
toba. Tukitubu kwa uaminifu na dhati, Upatanisho unaweza kutusaidia kuwa
wasafi, kubadilisha asili yetu, na kuvumilia vyema changamoto zetu.
Uvumilivu
ni kanuni muhimu inayopatikana katika mafundisho ya Yesu Kristo. Ni
muhimu kwa sababu uzuri wa maisha yetu ya baadaye ya milele unalingana
na uwezo wetu wa kuvumilia katika wema.
Katika 2 Nefi 31
nabii Nefi anatufundisha kwamba baada ya kupokea agizo lile lile la
wokovu la ubatizo ambalo Yesu Kristo alipokea na kisha tupokee karama ya
Roho Mtakatifu, lazima “tusonge mbele tukila na kusheherekea neno la
Kristo, na tuvumilie hadi mwisho, tazama, [na basi] hivyo ndivyo asema
Baba: [Sisi] tutapokea uzima wa milele.”
Hivyo
basi, ili kupokea baraka kuu ya zote za Baba yetu wa Mbinguni, ambayo
ni uzima wa milele, lazima tukamilishe kazi ya agano inayostahili na
kisha tuendelee kutii maagano yanayohusika. Yaani, lazima tuvumilie
vyema.
Uwezo
wetu wa kuvumilia hadi mwisho katika wema utakuwa unalingana moja kwa
moja na nguvu ya ushuhuda wetu na kina cha uongofu wetu. Wakati shuhuda
zetu ziko imara na tumeongoka kwa kweli kwa injili ya Yesu Kristo,
chaguo zetu zitasawishiwa na Roho Mtakatifu, zitakuwa na msingi katika
Kristo, na zitahimili hamu yetu ya kuvumilia katika wema. Ikiwa shuhuda
zetu ni dhaifu na uongofu wetu ovyo, hatari ni zaidi kwamba
tutashawishiwa na tamaduni za uongo za dunia ili kufanya chaguo mbaya.
Ningependa
kushiriki tukio linaloonyesha juhudi inayohitajika kuvumilia kimwili na
kisha kulilinganisha kwa juhudi inayohitajika kuvumilia kiroho. Baada
ya kurudi kutoka misheni yangu, nilikuwa na nafasi ya kucheza mpira wa
vikapu na kocha mwenye ushawishi mkubwa na mwandishi katika chuo kule
California. Kocha huyu alikuwa makini sana kuhusu wachezaji wake kuwa
katika hali nzuri ya kimwili kabla ya kuanza kwa msimu wa mpira wa
vikapu. Moja ya mahitaji yake ya zoezi kabla ya yeyote kati yetu kuweza
kugusa mpira wa kikapa kwenye kiwanja cha mazoezi ilikuwa ni kukimbia
mzunguko wa mbio za nyika katika milima karibu na shule kwa wakati
maalum na ngumu sana. Ninakumbuka jaribio langu la kwanza kabisa katika
kukimbia kozi hii ya mbio za nyika punde baada ya kurejea kwangu kutoka
misheni: Nilifikiria ningekufa.
Ilichukua
wiki nyingi za mafunzo makali ili hatimaye kuvunja rekodi ya wakati
ambao kocha alikuwa ameweka kama lengo. Ilikuwa ni hisia nzuri si tu
kuweza kukimbia mzunguko lakini pia kuharakisha hadi kwenye uhondo wa
mwisho hadi kwenye laini ya kumaliza.
Ili
kucheza mpira wa vikapu vyema, unahitaji kuwa katika hali nzuri ya
kimwili. Kuwa katika hali nzuri ya kimwili huja kwa gharama, na gharama
hiyo ni kujitolea, uvumilivu, na nidhamu ya kibinafsi. Uvumilivu wa
kiroho pia huja kwa gharama. Ni gharama ile ile: kujitolea, uvumilivu,
na nidhamu ya kibinafsi.
Ushuhuda,
kama mwili wako, unahitaji kuwa katika hali nzuri kama unautaka hudumu.
Hivyo basi ni jinsi gani tunaweka ushuhuda wetu katika hali nzuri?
Hatuwezi kufanya miili yetu kuwa katika hali nzuri ya kucheza mpira wa
vikapu kwa kutazama tu mpira wa vikapu kwenye televisheni. Vile vile,
hatutaweza kuweka shuhuda zetu katika hali nzuri kwa kutazama tu mkutano
mkuu kwenye televisheni. Tunahitaji kusoma na kujifunza kanuni za
msingi za injili ya Yesu Kristo, na kisha ni lazima tufanye tuwezavyo
kuizitumia maishani. Hivyo ndivyo tunavyokuwa wafuasi wa Yesu Kristo, na
hivyo ndivyo tunavyojenga ushuhuda wa kudumu.
Tunapokabiliwa
na shida maishani na hamu yetu ni kuiga sifa za Yesu Kristo, ni muhimu
kuwa tayari kiroho. Kuwa tayari kiroho kunamaanisha tumekuza sulubu na
nguvu ya kiroho---tutakuwa katika hali nzuri ya kiroho. Tutakuwa katika
hali nzuri kiroho hata kwamba tutachagua wema kila mara. Tutakuwa
hatuhamashiki katika hamu na uwezo wetu wa kuishi injili. Kama vile
mwandishi mmoja asiyejulikana aliwahi kusema, “Ni lazima uwe mwamba
ambao mto hauwezi kuondoa.”
Kwa
sababu sisi tunakabiliwa na changamoto kila siku, ni muhimu kwamba
tufanye kazi juu ya ushupavu wetu wa kiroho kila siku. Sisi tunapokuza
ushupavu wa kiroho, tamaduni za uongo za dunia, pamoja na changamoto
zetu za kibinafsi za kila siku, zitakuwa na athari ndogo kwa uwezo wetu
wa kuvumilia katika wema.
Mifano
mizuri ya ushupavu wa kiroho huja kutoka historia za familia zetu
wenyewe. Miongoni mwa hadithi nyingi kutoka kwa mababu zetu, tutaweza
kupata mifano ambayo inaonyesha tabia chanya ya uvumilivu.
Hadithi
kutoka kwa historia ya familia yangu mwenyewe inaeleza kanuni hii. Baba
ya babu yangu mkuu Joseph Maynes Watson alizaliwa mnamo 1856 kule Hull,
Yorkshire, Uingereza. Familia yake ilijiunga na Kanisa kule Uingereza
na kisha kwenda Jijini Salt Lake. Alimuoa Emily Keep mnamo 1883, na
wakawa wazazi wa watoto wanane. Joseph aliitwa kuhudumu misheni ya muda
mnamo Juni 1910, alipokuwa na umri wa miaka 53. Na kwa usaidizi wa mke
wake na watoto wanane, alirudi nchi yake ya asili Uingereza kuhudumu
misheni yake.
Baada
ya kuhudumu kwa uaminifu kwa takriban miaka miwili, alikuwa akiendesha
baiskeli yake pamoja na mwenziwe kwenda misa ya Shule ya Jumapili kule
Gloucester, Uingereza, ambapo tairi yake ikapasuka. Alishuka kutoka wa
baiskeli yake ili kutathmini uharibifu. Alipoona ya kuwa ilikuwa
imeharibika sana na ingechukua muda kurekebisha, alimwaambia mwenziwe
amtangulie na kuanza ibada ya Jumapili na angefika pale baada ya muda
mfupi. Punde tu alipomaliza kusema hayo, alianguka chini. Alikufa
ghafula kutokana na mshtuko wa moyo.
Joseph
Watson Maynes kamwe hakumwona mke wake na watoto wanane tena katika
maisha haya. Waliweza kusafirisha mwili wake kurudi katika Jiji la Salt
Lake na kuwa na huduma ya mazishi yake katika ukumbi mzee wa Waterloo
Assembly Hall. Kauli iliyotolewa katika mazishi yake na Mzee Anthony W.
Ivins wa Jamii ya Mitume Kumi na Wawili inatufundisha somo muhimu kuhusu
maisha, kifo, na uvumilivu: “Hii ndiyo injili inatupa---si kinga
kutokana na kifo, lakini ushindi juu yake kupitia matumaini ambayo
tunayo katika ufufuo mtukufu. … Unamgusia [Joseph Maynes] . …Ni furaha,
na jambo la kuridhisha na shangwe kujua kwamba wanadamu hujitolea maisha
yao kwa haki, kwa imani, wakiwa wakweli kwa imani.”
Hadithi
hii ya familia yangu inanishawishi kujaribu niwezavyo kufuata mfano wa
uvumilivu na sulubu ya kiroho iliyoonyeshwa na baba ya babu yangu.
Ninavutiwa pia na imani ya mke wake, Emily, ambaye maisha yake baada ya
kifo cha Joseph hakika yalikuwa mzigo mzito kubeba. Ushuhuda wake
ulikuwa imara na uongofu wake kamili akiishi maisha yake yote baadaye
akiwa mwaminifu kwa imani akiwasaidia watoto wake wanane pekee yake.
Mtume
Paulo alisema, “Na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile
ituzingayo kwa upesi, na tupige mbio kwa subira katika yale mashinidano
yaliyowekwa mbele yetu.”
Mashindano yaliyowekwa mbele yetu katika dunia hii ni mbio ya
uvumilivu, iliyojaa vizuwizi. Vizuwizi katika mashindano haya ni
changamoto tunazoamka nazo kila asubuhi. Tuko hapa duniani ili kukimbia
mbio, kutumia wakala wetu wa kimaadili, na kuchagua kati ya mema na
mabaya. Ili kukamilisha mbio kwa heshima na mafanikio na kurudi kwa Baba
yetu wa Mbinguni, tutalazimika kulipa gharama ya kujitolea, uvumilivu
na nidhamu ya kibinafsi. Tunahitaji kuwa katika hali nzuri ya kiroho.
Tunahitaji kukuza sulubu ya kiroho. Tunahitaji shuhuda imara
zitakazoelekeza kwa uongofu wa kweli, na kwa matokeo tupate ndani yetu
amani ya ndani na nguvu inayohitajika kuvumilia changamoto zozote huenda
tukakabilina nazo.
Hivyo
basi bila kujali changamoto unazoamkia kila asubuhi, kumbuka---na nguvu
ya kiroho unayokuza, pamoja na msaada wa Bwana, mwishoni mwa mashindano
utaweza kufurahia hakikisho ambalo Mtume Paulo alionyesha aliposema:
“Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.
“Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda:
“Baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile.”
Nawatolea
ushuhuda na ushahidi wangu wa uhalisi wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo
na mpango wake wa furaha mkuu na wa milele, ambao umetuleta kwenye
dunia hii wakati huu. Roho wa Bwana awavutie kukuza ndani yenu nguvu ya
kuvumilia. Katika jina la Yesu Kristo, amina.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni