Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatatu, Februari 24, 2014

Je una mpango au tayari una mahusiano na mkubwa wako wa kazi (bosi)?



Nini kinafuata? 

Ukweli ni kuwa, mahusiano katika eneo la kazi si jambo geni. Mahusiano yanaathiri (zaidi kwa wasichana, na hasa warembo), walioelimika na wasioelimika, matajiri kwa maskini, kwenye makampuni madogo na makubwa sehemu zote. Kama umeingia au una mpango wa kuingia katika mahusiano hayo, fahamu kuwa unayafanya maisha yako ya kazini kuwa magumu na tata. 

Ni kweli pia kuwa si mara zote watu hutoka na kudhamiria kuwa na mahusiano kazini ila hujikuta tayari wamo.

Kabla hujaanza mahusiano na bosi wako, au katika hali yoyote ambayo umejikuta tayari una mahusiano hayo, tafiti na jiulize haya yafuatayo:-

1. Je, Kampuni unayofanya kazi ina sheria inayohusu mahusiano kazini? Kama ni ndiyo, jua kuwa unajiwekea mazingira magumu na kuhatarisha kazi yako. Hata kama mtu unayeingia naye kwenye mahusiano ni bosi wako, wewe ndiye utakayeondoka . Mtu mwenye cheo mara zote anabaki kwenye kampuni, kampuni haiwezi kuingia gharama ya kumpoteza bosi kwaajili ya mahusiano yako, ila wewe itabidi uondolewe kwakuwa gharama ya kumpata bosi ni kubwa kuliko kupata mtu kama wewe.

2. Je, Uliajiriwa kwa ujuzi wako na si vinginevyo, baada ya kuanza mahusiano mambo yanaanza kuwa tata kikazi. Bosi wako ni bosi wako tu, yeye ndiye anayeamua nani apandishwe cheo, kupata nyongeza za mishahara na mengine mengi. Hivyo mambo yataanza moto moto ila siku za usomi huanza kufifia na kinachobakia ni kutojisikia vizuri unapokuwa kazini. Hivyo uwe makini na maamuzi unayoyafanya hasa kuhusu mahusiano kazini.
3. Jua kuwa mahusiano hayo yatafika mwisho. Je, utajisikiaje kwenda ofisini ukiwa umeshaachana na bosi? Utendaji na ufanisi wa kazi utakuwaje? Hakuna ubishi kuwa utakuwa na maumivu makubwa, ingawaje wengi hujifanya hawajaumia.

Kama Bosi wako ameoa au kuolewa

1. Fahamu kuwa ni 10% tu ya mahusiano kazini ndiyo humea kwa muda mrefu; Mengi huvunjika.
2. Je, haya ni mahusiano yako ya kwanza? Fahamu kuwa watu wana vitu vingi vinavyoendelea kwenye maisha yao, tabia, hulka na mahusiano huwa tofauti. Kuwa makini kujua mtu anapitia nyakati gani.
Kama unaamua kuingia kwenye mahusiano

1. Kuwa makini, na tumia akili nyingi kutambua unamwambia nani hapo kazini. Hii inaweza kuhatarisha kazi na vyeo vyako unavyostahili kupandishwa kihalali uwapo kazini.
2. Kama umeoa au kuolewa, jua kuwa wewe ni mdanganyifu kwenye ndoa yako. Kuwa na mahusiano nje ya ndoa si suluhisho ya tatizo, bali kuwa jasiri kwa kujadili na mwenzi wako kutafuta njia ya kutatua kile kinachopungua kwenye ndoa yenu. Hiyo ndiyo namna ya kuonyesha upendo kwa mtu uliyeamua kuishi naye kwenye ndoa.
3. Tafuta ushauri kwa washauri wa masuala ya ndoa na mahusiano. 
Fikiria kwa makini na tafakari kabla maji hayajamwagika ukajutia. Bado unao uamuzi!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni