Mtayarishaji

Morning Star Radio

Ijumaa, Julai 27, 2012

HIVI MUZIKI NI NINI HASA?


Muziki ni sanaa kama zilivyo sanaa zingine, hivyo hatuna budi kuelewa sanaa ni nini hasa. Imeelezwa kuwa ni ufundi wa kuwasilisha mawazo yaliyomo katika fikra za binadamu ili yadhihirike na kufikisha ujumbe uliokusudiwa kwa walengwa-sanaa hiyoo.

**************************************************** 

 

Hivyo sanaa inabaki kuwa na malengo makuu ambayo ni kuelimisha, kuonya, kuburudisha na hata kuelekeza jamii. Sanaa pia ni utambulisho wa jamii husika. Kupitia sanaa unaweza kuifahamu jamii kuwa huu ni fulani hata kama hujawahi kuishi na jamii hiyo.

Sanaa inayo matawi mengi mno, lakini kwa leo naomba tujikite zaidi katika tawi la muziki.

Muziki ni nini hasa?
Kwa mujibu wa kamusi sanifu ya Kiswahili, muziki umeelezwa kuwa ni “mpangilio wa ala na uimbaji unaoleta athari fulani kwa kiumbe”. Hii ina maana kuwa kama msanii wa muziki hapangilii ala zake na kuimba kwa ustadi basi, anachokifanya msanii huyo si muziki bali ni kelele za kawaida.

Si nia yangu kufundisha muziki kupitia makala haya, isipokuwa ninataka tutafakari ni kwa namna gani wasanii wetu wa muziki wanavyoshiriki katika jitihada za kuleta maendeleo katika taifa letu na pia kuipotosha jamii.

Tutafanya makosa endapo tutaisahau sekta hii ya sanaa ya muziki katika ujenzi wa jamii yoyote.

Muziki una historia ndefu tena usioyumba katika ustawi wa jamii ya binadamu. Katika Biblia tunaambiwa kuwa Mfalme Sauli alipochoka na kujisikia hovyo asijue la kufanya, alipata burudani ya muziki kutoka kwa msanii chipukizi na mchunga kondoo, Daudi.

Kwa kuwa muziki wa kijana huyu ulipangiliwa vilivyo, uliweza kumliwaza Mfalme Sauli na kujisikia aliyepona na kurudia hali yake ya awali. Muziki huponya.

Ukuta mkubwa, mnene na uliojengwa kwa uimara wa hali ya juu, Yeriko, ulisambaratishwa kwa muziki pale wana wa Israeli walipopuliza tarumbeta zao kuuzunguka mji ule kwa siku saba. Ukuta ulianguka kwa kishindo kwa kusukumwa na mawimbi tu ya sauti za tarumbeta. Tukio hili linatufanya tuamini kuwa muziki una nguvu pengine hata kushinda mabomu ya B 52 NA MENGINEYO UNAYOYAFAHAMU.

Muziki umeziunganisha ndoa zilizovunjika. Muziki pia umezisambaratisha ndoa na familia nyingi. Muziki umewatoa watu machozi ya furaha ama huzuni. Muziki umevuruga na kuharibu jamii pia 

Wanasayansi bado wanakesha katika maabara kubwa duniani kutafiti ni kwa nini muziki una athari kubwa katika ubongo wa binadamu. Muziki umetumiwa kama dawa kwa wagonjwa wa akili na walio na msongo wa mawazo.Utafiti uliofanywa miaka ya hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Lomalinda nchini Marekani, ulionesha nguvu ya muziki pale wagonjwa 100 walipowekwa katika chumba maalumu bila kupewa dawa isipokuwa muziki na wengine 100 chumba kingine wakipewa dawa na huduma zote za tiba. Wagonjwa walioliwazwa tu kwa muziki walipona upesi kuliko waliopewa dawa.

Tafiti zote ni msukumo kwetu kuwa muziki ni sanaa yenye nguvu kubwa inayopaswa kuangaliwa kwa umakini.

Na hii inamfanya mtu yeyote anayetaka kujiingiza kwenye sanaa ya muziki sharti kujisahili na kujiridhisha kama kweli amefaulu kuwa mwanamuziki. Kujisahili ni pamoja na kusomea muziki ili kujua miiko ya sanaa hiyo. Kipaji cha muziki huwa na maana zaidi kinaposaidiwa na elimu stahiki.

Muziki ukitumiwa vizuri huwa ni baraka, na matunda yake huwa matamu kwa jamii pana. Lakini pia muziki ukitumiwa vibaya yaweza kuwa laana na kuongoza anguko la jamii inayosikiliza na kuona muziki huo.

Muziki ni uwanja huru wa kutoa mawazo na maoni chanya kwa manufaa ya jamii. Hii inamfanya mwanamuziki kujihoji anataka kuongea nini kupitia tuni ya muziki wake? Mbali na malengo yake binafsi, msanii pia anapaswa kuwa na malengo kwa jamii yake.

Hebu tuone mifano ya wasanii wa muziki waliolenga mambo fulani kwa jamii zao.

Mariam Makeba wa Afrika Kusini, alitumia muziki wake kutetea utamaduni wa Mwafrika hasa wa jamii yake ya Wazulu. Imewahi andikwa kuwa jamii yoyote ile itakayothubutu kuzipa kisogo tamaduni zake na kushadadia tamaduni pepe za watu wengine ni lazima ianguke na huenda isisimame tena.

Sote tunamkumbuka Hayati Bob Nesta Marley wa The Wailers alivyotumia muziki wake wa Reggae wenye asili ya Caribean kupinga ukandamizaji kote duniani. Nyimbo zake zililenga ukombozi kwa wanyonge hasa Waafrika. Nyimbo kama “Liberation” ulikuna hadi ndani ya masikio ya Rais wa Zimbabwe, Komredi Robert Gabriel Mugabe.

Manu Dibango wa Nigeria alitumia muziki kuhamasisha utamaduni wao wa mavazi ambao leo tunauonea gele.

Wanamuziki wenzie wakamuunga mkono. Akina Fela Anikulapo Kuti aliimba nyimbo zenye ujumbe mzito ukiwaasa Waafrika kujitambua na si kukubali kila jambo bila kuhoji. Alieleza fikra zake kwa wimbo kama “I like this gentleman”.

Hatuwezi kuwasahau akina Luambo Luanzo Makiadi, mwasisi wa rhumba ya Kizaire alivyotumia muziki kutangaza nchi yake ya Zaire kwa mataifa makubwa duniani. Alitumia muziki kutangaza utalii wa nchi yake.

Leo pombe aina ya Chibuku inauzwa hadi kwenye maduka makubwa (super markets) Ulaya. Yote ni jitihada za mwanamuziki Yvonne Chaka Chaka wa Afrika Kusini wakati sisi bado tunawafukuza mama zetu kama swala eti wanauza pombe “haramu” gongo. Wenzetu Uganda wanasindika gongo hiyo na sasa inauzwa kwenye soko moja na konyagi.

Hayati Lucky Dube; alipigania ubaguzi wa rangi na hata kutumia muziki ili mfungwa Nelson Mandela aachiwe huru. Hata mwenzie Chico Twala na kibao chake “We miss you Manelo” alipinga ubaguzi wa rangi. Neno “Manelo” ni Mandela, lakini kutokana utawala wa chuma wa Kikaburu, hakuruhusiwa kutaja jina hilo.

Hata baada ya kazi za suluba, hasa kwenye mashamba ya wazungu wa Amerika, watumwa Waafrika walikusanyika jioni kujiliwaza kwa muziki wa soul.

Maandamano makubwa yaliyoitishwa na mpigania haki za Waafrika nambari wani duniani, Martin Luther King yalitawaliwa na sauti za muziki zilizolalamika kudai haki. Kwa kuwa hawakuwa na muda wa kupangilia ala na uimbaji, ndipo walipoamua kuimba kwa kufoka-foka (Hip hop).

Hapa ndipo tunapoweza kuyakumbuka makundi kama Naught by Nature. Na pia hapa ndipo unapogundua kwa nini majina ya wanamuziki wa Kimarekani wenye asili ya Afrika yanatoa taswira ya ukorofi - Bad Boys, Gangstars Unit, Above the Law, Bad Killer na mengine unayoyajua.

Majina haya yalitoa ujumbe wa kutanua misuli kutaka kujikomboa kutoka kwenye makucha ya chuma ya ubaguzi wa rangi.

Hata wakati wa vita vya kumpiga na hatimaye kumng’oa Nduli Idd Amini, tulitumia muziki kuwahamasisha wapiganaji wetu ili waweze kusonga mbele. Kulikuwa na nyimbo kama “Yuko wapi joka huyo, fyeka pori tumkamate”.

Ndugu msomaji, natumai umegundua kuwa muziki wa kila msanii ulilenga kitu fulani mbali na kuburudisha. Wasanii walitumia sanaa yao kukomboa jamii zao. Wapo waliopoteza maisha yao kwa kutetea wanyonge kupitia sanaa ya muziki. Kifo cha Bob Marley bado kimebaki kitendawili hadi leo na Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) ikitajwa kuhusika.

Sasa tuna kitu kinaitwa Tanzania Music Award, eti inatoa tuzo kwa wasanii bora wa muziki ambao wanapoenda kwenye vipimo vya kimataifa hurudi kwa aibu kubwa.

Haijulikani wanatumia vigezo gani kumtambua msanii bora wa Kitanzania.

Hapa tunajiuliza ni yapi malengo ya wasanii wetu wa muziki? Wanalenga ukombozi gani?

Sasa taifa liko kwenye hatari ya kuangamia kutokana na ufisadi unaoendeshwa na tuliowapa mamlaka. Hadi watoto wadogo wanapiga kelele japo hawasikiki. Wako wapi wasanii wetu wa muziki nao watumie sauti zao kupinga na kukemea ufisadi huu? Mfano: HASA WA MUZIKI WA INJILI?.

Mbona wasanii wetu nao wanazidi kujitenga na jamii ambayo ndiyo nguzo yao kuu? Nani aliyewabadilisha wasanii wetu na kuwaambia kuwa taifa lina tatizo la mapenzi tu, nao kila wimbo ni kuimba juu ya mapenzi?. Naona sasa umeanza kupata picha namna muziki unavyobadilisha na kuharibu maadili hata uwezo wa mtu wa kiutashi.

Nani aliyewapiga upofu wasanii wetu wasione hata haja ya kuwakemea si viongozi fisadi pekee kupitia muziki bali hata wasiojali familia zao? Watanzania wanazidi kuogelea kwenye bahari ya umasikini bila kuwa na watetezi wao dhidi ya ugandamizwaji na utawala wa kidhalimu wa kujuana na viunganishi vya hapa na pale. Kwa nini hili lisiwaguse wasanii wetu nao wakapaza sauti angani kwa MUNGU ili afute hali ya ulafi na uporaji wa rasilimali za umma?Kama lengo la sanaa ni pamoja na kuonya na kuelimisha, kwa nini wasanii wetu wasiwaelimishe na wao pia waoneshe njia sahihi ya kuenenda? Kwanini wanazidi kujikita kwenye burudani tu ilhali taifa linaangamia kwa rushwa, tena nzito nzito?

Wako wapi wasanii walio tayari kusema potelea mbali hata kama nitafungwa jela ama iwe ni kwa ajili ya MUNGU lakini nitatumia sanaa yangu kuonya watawala ambao hata hivyo historia imeonesha mara zote wamekufa kwa aibu?

Yuko wapi msanii wa aina hiyo asimame tumtambue na kumbatiza jina la mtetezi wa wanyonge?
Nani aliyewakataza kuimba nyimbo za ukombozi zisizoweza kuisha ladha? Mfano kuna wimbo wa injili unaoimbwa; NIMEKOMBOLEWA NA YESU NA SASA NIMEFURAHI KWA BEI YA MAUTI YAKE MIMI NI MTOTO WAKE.

Kwa nini wasanii wetu wanazidi tu kutekwa nyara na tamaduni za magharibi? Kwa nini wasanii wetu wanazidi kutopea kwenye utumiaji wa dawa za kulevya badala ya kuwa mabalozi wa kuupiga vita?

Wasanii wetu wanatuambia wao ni kioo cha jamii kwa mantiki kwamba tuwatizame ili tujikosoe na kisha tuenende kama wao.

Kwa maneno mengine tuvae suruali za kushuka kama wao, wanaume watoge masikio wawe kama wanawake kama wao, wanawake watembee nusu uchi kama wao, tuweke hereni hadi ulimini kama wao, hata mama zetu watembee vitovu nje kama wao, tuongee Kiingereza cha “yah”, “yu no”, “ze” na “zati” kama wao, tunywe pombe hadi kulala baa kama wao, tufikirie mapenzi muda wote kama wao, tuzisuse tamaduni zetu kama wao. Kwa kifupi tuwe makasuku na chiriku wanaopokea kila kitu kinachotoka Ulaya na Marekani kama wao.

Tuzichukie ngozi zetu kama wao, hata nywele zetu tuzichukie na badala yake tubandike za wazungu waliokufa Ulaya. Tupake midomo yetu damu tuonekane wauaji kama wao.

Eti wanataka tuamini kuwa sisi hatuna utamaduni wowote unaoweza kuigwa na wazungu isipokuwa ni sisi kuiga kila kitu chao! Huu ni utumwa wa kujitakia tena usiohitaji mijeledi.

Kwa nini wasanii wetu wasitambue vita kuu ya utamaduni inayoendelea duniani kote na msingii wake wa kihistoria?

Waarabu wana hamu ya kuona jamii yote ya binadamu inafuata tamaduni zao, Wazungu nao wanatamani watu wote wangekuwa kama wao, Wachina nao hivyo hivyo, Wanaigeria nao hawako nyuma kusambaza utamaduni wao. Kufanya dunia kuwa kijiji kimoja ni matokeo ya kila taifa kuyashawishi mataifa mengine kuwa kama wao. Nani aliyewafunga macho wasanii wetu hasa wa muziki wasiyaone haya? HII INAWAHUSU NA WA INJILI PIA.

Mbona sasa hatuna faida ya kuwa na wasanii kama hawasaidii katika ujenzi wa taifa?

Wanadai eti sanaa ni ajira hivyo maslahi yao mbele, utamaduni nyuma. Sina ugomvi juu ya hilo lakini, kinachowafurahisha ni nini hadi wacheke na kupasuka mbavu pale watakapotumia muziki huo kujinufaisha huku kundi kubwa la vijana wakipotea njia sahihi ya kuenenda kimaadili?

Kwa nini wanunuzi wa kazi zao wasigome kununua tepu zao hadi pale watakapojirekebisha kutanguliza MAADILI mbele, maslahi nyuma?


Umefika wakati wa kuwahukumu wasanii wetu kwa matendo yao. Nao pia imefika wakati wa kusimama na kuitetea jamii yetu kwa kukemea maadili yote yasiyo na asili ya Ki-MUNGU kuanzia ufisadi, uvaaji usio na heshima, ubadhirifu na mengine mengi yasiyotoa picha halisi ya JAMII BORA YENYE MAADILI Tanzania. 
 
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni