Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatatu, Julai 30, 2012

ULIWAHI SIKIA MAKAMBI YA MAUTI?

Wafungwa katika kambi la KZ Buchenwald wakati wa ukombozi 1945.

Makambi ya KZ ni jina la kutaja makambi ya wafungwa yaliyotumiwa hasa na Ujerumani wakati wa utawala wa Nazi miaka ya 1933 hadi 1945. "KZ" ni kifupi cha neno la Kijerumani "Konzentrationslager". Maana yake ni "Kambi la kukusanya wafungwa".

Wanazi walianzisha hayo makambi ya KZ baada ya kuteka utawala wa Ujerumani mwaka 1933. Walikamata wapinzani wao wengi, kiasi kwamba magereza hayakutosha tena. Makambi hayo hayakuwa tena chini ya wizara ya sheria bali chini ya polisi ya kisiasa na vitengo vya chama cha Nazi. Tangu mwaka 1934 yalikuwa yote chini ya kikosi cha SS.

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia yalitumiwa kukusanya mamilioni ya watu waliokamatwa na Wanazi kote Ulaya, hasa vikundi viwili:

  • Wayahudi pamoja na vikundi vingine vilivyobaguliwa upande mmoja na
  • wapinzani wa utawala wa Nazi kwa upande mwingine.

    Makambi ya KZ ya kawaida

    Makambi hayo yalikuwa hasa na kusudi la kuadhibu wapinzani na kutumia wafungwa kwa ajili ya kazi za kulazimishwa. Hasa wakati wa vita Wajerumani wengi walikuwa wanajeshi na nchi ikaona uhaba wa wafanyakazi. Hivyo makambi haya yalijengwa mara nyingi karibu na viwanda.
    Idadi ya vifo ilikuwa kubwa hasa katika miaka ya mwisho ya vita kutokana na unyama wa walinzi na uhaba wa chakula pamoja na ukosefu wa matibabu. Njaa ilisababisha magonjwa na vifo vingi.

     

    Makambi ya KZ chini ya Ujerumani wa Nazi 1933-1945;
    makambi ya mauti yamepewa alama nyekundu

    Makambi ya mauti

    Baada ya azimio la Maangamizi makuu dhidi ya Wayahudi wa Ulaya makambi ya mauti yalijengwa. Makambi ya mauti ni lugha ya kutaja hasa makambi saba yafuatayo:
  • Chelmno – Kulmhof
  • Auschwitz-Birkenau
  • Belzec
  • Sobibor
  • Treblinka
  • Majdanek
  • Maly Trostinez
Yote yalijengwa nje ya eneo la Ujerumani wenyewe, sita katika Poland na moja katika Belarusi.
Mwisho wa mwaka 1941 Adolf Hitler na viongozi wengine wa Ujerumani waliamua kuwaua Wayahudi wote waliopatikana Ulaya. Majaribio ya kwanza ya kuua Wayahudi katika Ulaya ya Mashariki yalionyesha matatizo mbalimbali: uchovu kwa upande wa wanajeshi wa vikosi maalumu waliopaswa kutekeleza mauaji haya ya watu maelfu na sauti za masikitiko upande wa wanajeshi wa kawaida waliobahatika kuona mauaji haya. Azimio lilifanywa la kutumia mbinu za kisasa katika makambi maalumu ambako tendo lenyewe liliweza kufichwa vizuri zaidi.
Wayahudi na wengine waliotakiwa kuuawa walipelekwa kwa treni hadi makambi haya maalumu. Hapa wafungwa waligawiwa:
  • watu wenye afya nzuri walipelekwa kando na kupewa kazi katika viwanda vilivyojengwa pamoja na makambi haya kwa kusudi la kufanya kazi ya uzalishaji kwa ajili ya mahitaji ya uchumi wa vita. Wafanyakazi hawa walitakiwa kufanya kazi ngumu wakipewa chakula kidogo hadi kuchoka. Mara walipokuwa hawaleti tena faida walipelekwa kuuawa kwenye chumba cha gesi.
  • watoto, wazee na wagonjwa walipelekwa kando mara moja hadi vyumba vilivyoitwa "bafu". Hapo milango ilifungwa, na gesi ya sumu kuingizwa. Maiti zilichomwa katika majiko makubwa.
Kwa jumla watu milioni sita waliuawa katika makambi ya KZ hadi 1945.

Jina la "KZ"

Wanazi walitumia jina la KZ = "Konzentrationslager" kama tafsiri ya neno la Kiingereza "concentration camp". Waingereza waliwahi kutumia mbinu ya kusimamia wafungwa wengi katika kambi maalumu zilizofungwa kwa seng'enge tangu vita yao dhidi ya Makaburu katika Afrika Kusini mwaka 1899-1902; Waingereza walianzisha makambi haya kwa sababu walitaka kutenganisha familia za Makaburu na wanaume wao walioendesha vita ya porini ili kuzuia wasipate chakula na usaidizi kutoka kwa wasio wanajeshi. Makambi haya yalisababisha vifo vya makumi elfu wanawake, watoto na wazee kutokana na njaa na magonjwa ingawa hayakujengwa kwa kusudi hiyo.

Tangu kuanzishwa na Waingereza huko Afrika Kusini imeonekana ya kwamba makambi ya aina hii husababisha mara nyingi vifo hata kama wale wanaoanzisha makambi hawana nia ya kuua watu kwa njia hiyo. Matatizo ya kulisha watu wengi mahali pamoja, ya kuhakikisha usafi na matibabu ama shambani tu au katika mahema au kwenye majengo yasiyo imara, kuwalinda wafungwa dhidi ya baridi na joto na juu ya haya yote kuzuia kuambukizana kwa magonjwa ni magumu ya kushinda uwezo wa walinzi wa kambi. Hasa kama wafungwa wanatazamiwa kama maadui ambao hawapaswi kupewa uangalizi mwingi.  Kama Vipi Jihakikishie  H  A P A.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni