Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumamosi, Machi 17, 2012

Tufanye Nini Na Mashaka!!!?....Majibu Yafanyayo Kazi. 
WATU wengi, hasa wale walio wachanga katika maisha yao ya Kikristo, siku
nyingine husumbuliwa na mashauri yatolewayo na wale waonao mashaka juu ya mambo
ya dini na kuyakosoa. Kuna mambo mengi ndani ya Biblia wasiyoweza kuyafafanua, au
hata kuyaelewa, na Shetani huyatumia mambo hayo kuitikisa imani yao katika Maandiko
ili wasipate kuyaamini kuwa ni ufunuo utokao kwa Mungu. Wanauliza, wanasema,
“Nawezaje kujua njia ya kweli? Kama kweli Biblia ni Neno la Mungu, nawezaje
kuondolewa mashaka haya moyoni mwangu, nisije nikachanganyikiwa?”
Mungu hatuombi sisi kuamini bila ya kutupa ushahidi wa kutosha ambao juu yake
tunaweza kujenga imani yetu. Kuwako kwake, tabia yake, na ukweli wa Neno lake,
mambo haya yote yamehakikishwa kwetu kwa ushuhuda unaovutia katika akili zetu; na
ushuhuda huo upo tele. Hata hivyo Mungu hajaondoa kabisa uwezekano wa kuwapo
mashaka. Imani yetu ni lazima ijengwe juu ya ushahidi, siyo juu ya ufafanuzi utumiao
sababu zinazoonyesha mifano fulani. Wale wanaotaka kuona mashaka wataipata nafasi
hiyo; ambapo wale wanaotaka kweli kweli kuijua ile kweli watapata ushahidi mwingi
ambao juu yake wanaweza kuitegemeza imani yao.

Haiwezekani kabisa kwa akili za kibinadamu kuelewa kwa ukamilifu tabia au
kazi za Mungu yule wa milele. Kwa yule aliye na akili kali kabisa, kwa yule aliyepata
elimu ya juu kabisa, Mtakatifu huyo hana budi kubaki amefunikwa katika siri. “Je!
wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu? Waweza kuufikilia upeo wa huyo
Mwenyezi? Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe? Ni wenye kina
kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe?” Ayubu 11:7,8.
Mtume Paulo asema, “Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu!
hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani.” Warumi 11:33. Na ingawa
“Mawingu na giza vyamzunguka,” “haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.” Zaburi
97:2. Mpaka hapo tunaweza kufahamu anavyotushughulikia sisi, na kuyafahamu
makusudi yake yanayomsukuma kufanya hivyo, kiasi kwamba tunaweza kutambua
upendo wake usio na kikomo na rehema yake ifungamanayo na uweza wake usio na
mipaka. Tunaweza kufahamu mengi kuhusu makusudi yake kama aonavyo yeye kuwa ni
vyema kwetu kuyajua; na zaidi ya hapo bado yatupasa kuutegemea mkono wake wenye
uwezo wote, na moyo wake uliojaa upendo.

Neno la Mungu, kama ilivyo tabia ya Mwasisi wake wa kimbingu, lina mambo ya
siri yasiyoweza kufahamika kamwe kwa ukamilifu na wanadamu. Jinsi dhambi
ilivyoingia ulimwenguni, jinsi Kristo alivyofanyika mwili halisi wa kibinadamu,
kuzaliwa upya kulivyo, ufufuo, na masomo mengine mengi yaliyoelezwa katika Biblia, ni
mafumbo makubwa mno kushinda akili za kibinadamu kuyaeleza, wala hata kufahamu
maana yake kwa ukamilifu. Lakini hatuna sababu ya kuwa na shaka juu ya Neno la
Mungu kwa ajili ya kutozifahamu siri za maongozi yake. Katika ulimwengu huu wa asili
tunazungukwa daima na mafumbo tusiyoweza kuyafahamu. Vitu duni kabisa vyenye
uhai huwa tatizo kwetu, hata wanafalsafa wenye hekima nyingi sana hawana uwezo
kabisa wa kutupa maelezo yake. Mahali pote pana maajabu tusiyoweza kuyafahamu. Je! hivi tungeweza kushangaa basi, kuona kwamba katika ulimwengu wa kiroho kuna siri pia
tusizoweza kuzifahamu kabisa? Shida hasa inatokana kabisa na udhaifu na ufinyu wa
akili za kibinadamu. Katika Maandiko Mungu ametupa ushahidi wa kutosha kuonyesha
jinsi yalivyo na tabia ya kimbingu, nasi hatupaswi kuwa na mashaka na Neno lake kwa
sababu tu ya kukosa kuyaelewa mafumbo yote ya maongozi yake.

Mtume Petro amesema kwamba katika Maandiko “yamo mambo ambayo ni
vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa
… kwa uvunjifu wao wenyewe.” 2 Pet. 3:16. Ugumu upatikanao katika Maandiko hayo
umesisitizwa na wale wanaoyaonea mashaka mambo ya kidini kuwa ndiyo hoja yao
wanayotoa kuipinga Biblia; lakini mbali sana na ugumu huo, yenyewe yanatoa ushahidi
wenye nguvu kuonyesha kwamba uvuvio wake watoka kwa Mungu. Kama Biblia
ingekuwa haina habari za Mungu, ila tu mambo yale tuwezayo kuyaelewa kwa urahisi;
kama ukuu na utukufu wake ungeweza kufahamika na akili za kibinadamu, basi Biblia
isingekuwa na vitambulisho visivyokosea vionyeshavyo kwamba ina mamlaka ya
Mungu. Utukufu wenyewe hasa na siri ya mafundisho yake makuu yaliyotolewa humo,
mambo hayo yangeitia nguvu imani kuwa hilo ni Neno la Mungu kweli.

Biblia inaifunua kweli kwa maneno yanayoeleweka na yanayofaa kwa mahitaji na
matakwa ya moyo wa kibinadamu kiasi cha kuwashangaza na kuwavutia wale walio na
elimu ya juu kabisa, wakati inawawezesha walio duni kabisa na wasioelimika kuitambua
njia ya wokovu. Na hata hivyo kweli hizi zilizoelezwa kwa njia iliyo rahisi kueleweka
zinagusa masomo yaliyo juu mno, yenye maana pana mno, yapitayo kabisa upeo wa
ufahamu wa kibinadamu, hata twaweza kuyakubali tu kwa sababu Mungu ndiye
aliyeyatangaza. Hivyo mpango wa Mungu juu ya ukombozi wa wanadamu umewekwa
wazi kwetu, ili mtu awaye yote apate kujua hatua zinazompasa kuchukua katika toba
yake kwa Mungu, na kuwa na imani kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ili apate kuokolewa
kwa njia aliyoiweka Mungu. Walakini chini ya kweli hizo zinazoeleweka kwa urahisi
yapo mafumbo ambayo husitiri utukufu wake - mafumbo yanayozishinda akili za mtu
katika utafiti wake, lakini yanayomvutia yule aitafutaye kweli kwa moyo mnyofu na
kicho na imani. Kadiri anavyozidi kuichunguza Biblia, ndivyo imani yake inavyozidi
kuwa na kina kusadiki ya kwamba hilo ni neno la Mungu aliye hai, na hoja za
kibinadamu husalimu amri chini ya mfalme huyo wa mafunuo ya kimbingu.
Kukiri kwamba hatuwezi kuzielewa kweli kuu za Biblia kwa ukamilifu ni
kukubali tu kwamba akili finyu ya mwanadamu haitoshi kumwelewa Mungu wa milele,
kwamba mwanadamu, pamoja na maarifa yake ya kibinadamu yaliyowekewa mipaka,
hawezi kuyaelewa makusudi ya Mungu ajuaye yote.

Wenye kumkana Mungu hulitupilia mbali Neno lake kwa sababu hawawezi
kuyafahamu mafumbo yake yote; tena si wote wanaojidai kuwa wanaisadiki Biblia
ambao wameikwepa hatari hiyo katika suala hilo. Mtume asema, “Angalieni, ndugu
zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na
Mungu aliye hai.” Ebr. 3:12. Ni vizuri kujifunza sana mafundisho ya Biblia, na
kuyachunguza “hata mafumbo ya Mungu” (1 Kor. 2:10), kwa kadiri yanavyofunuliwa
katika Maandiko. Wakati “mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu,” yale
“yaliyofunuliwa ni yetu sisi.” Kum. 29:29. Lakini ni kazi yake Shetani kuipotosha akili
ya kibinadamu inayofanya uchunguzi huo. Kwa kiasi fulani kiburi huchanganyika na
mawazo yao wakati wa kuitafakari kweli ya Biblia, hata watu hao wanajisikia ya kuwa
wamekosa uvumilivu na kushindwa kama hawawezi kuielezea vizuri kila sehemu ya Maandiko hadi wametosheka kabisa. Wanaona wamejidhalilisha mno kukiri kwamba
hawayaelewi maneno hayo yaliyovuviwa. Hawako tayari kungoja kwa uvumilivu mpaka
Mungu atakapoona inafaa kuwafunulia hiyo kweli. Wanaona kwamba hekima yao ya
kibinadamu pasipo msaada wa Mungu inatosha kuwawezesha kuyaelewa Maandiko
hayo, nao wakishindwa kufanya hivyo, wanayakana kabisa kuwa si ya Mungu. Ni kweli
kwamba nadharia nyingi na mafundisho mengi yanayodhaniwa kuwa yametoka katika
Biblia hayana msingi wo wote kama huo katika mafundisho yake, na kwa kweli
yanapingana na mfumo mzima wa uvuvio. Kwa wengi mambo hayo yamekuwa sababu
ya kuingiwa na mashaka na kuchanganyikiwa. Walakini, shutuma hizo haziwezi
kutolewa dhidi ya Neno la Mungu kutokana na hali hiyo; ila zinaweza kutolewa dhidi ya
upotoshaji wa neno hilo unaofanywa na mwanadamu.

Kama wanadamu wangeweza kufahamu kwa ukamilifu jinsi Mungu alivyo hasa,
pamoja na matendo yake yalivyo, basi, wakiisha kufika hapo, wasingeweza kuvumbua
kweli yo yote mpya, wasingeweza kuongeza maarifa yao, wasingeweza kukua zaidi
kiakili au kiroho. Mungu asingekuwa Mwenye enzi tena; na, mwanadamu, baada ya
kufika mwisho wa maarifa na mafanikio yake, angekoma kusonga mbele. Na tumshukuru
Mungu kwamba mambo hayajawa hivyo. Mungu ni wa milele; na ndani yake zimo
“hazina zote za hekima na maarifa.” Kol. 2:3. Na milele hata milele wanadamu
wataweza kuendelea kuchunguza, na kujifunza, lakini hawataweza kamwe kuzimaliza
hazina zote za hekima yake, wema wake, na nguvu zake.

Mungu amekusudia ya kuwa kweli za Neno lake ziendelee kufunuliwa daima kwa
watu wake hata katika maisha haya. Kuna njia moja tu ambayo kwayo maarifa hayo
yanaweza kupatikana. Tunaweza kuufikia ufahamu wa Neno la Mungu kwa njia moja tu
ya kuelimishwa na Roho ambaye kwa njia yake Neno hilo lilitolewa. “Mambo ya Mungu
hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu,” kwa “maana Roho huyachunguza yote, hata
mafumbo ya Mungu.” 1 Kor. 2:11,10. Na ahadi yake Mwokozi kwa wafuasi wake
ilikuwa ni hii, “Yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye
kweli yote;…atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.” Yoh. 16:13,14.

Mungu ataka mwanadamu atumie akili zake; na kule kujifunza Biblia
kutaiimarisha na kuikuza akili yake kwa namna ambayo hakuna njia nyingine yo yote
iwezavyo kufanya. Lakini tujiangalie tusiifanye akili yetu kuwa mungu wetu, akili
inayokabiliwa na udhaifu wa kibinadamu na kupungua nguvu yake. Kama hatutaki
Maandiko hayo yatuletee hali ya kuchanganyikiwa katika mawazo yetu, kiasi cha
kuzifanya kweli zile zinazoeleweka kwa urahisi sana tusiweze kuzielewa, basi, ni lazima
tujishushe na kuwa na imani kama ya mtoto mdogo, tukiwa tayari kujifunza, na kuomba
sana ili tupate msaada wa Roho Mtakatifu. Hisia ya kutambua uwezo na hekima aliyo
nayo Mungu, na kutambua kutoweza kwetu kuufahamu ukuu wake, mambo hayo
yangetuamsha sisi ili tupate kuwa na unyenyekevu, nasi tungelifungua Neno lake kwa
kicho kitakatifu, kana kwamba tuko mbele zake. Tunapoisoma Biblia, ni lazima akili
zetu zikiri kwamba ina mamlaka kuu mno kuliko zilivyo akili zetu zenyewe, na moyo na
akili zetu ni lazima zimpigie magoti huyo MIMI NIKO aliye mkuu.

Kuna mambo mengi ambayo yanaonekana dhahiri kuwa ni magumu au ni
mafumbo, ambayo Mungu atayafanya kuwa wazi na rahisi kwa wale ambao kweli
wanataka kuyafahamu. Lakini bila uongozi wa Roho Mtakatifu tutaendelea daima
kuyapotoa Maandiko hayo au kuyafasiri vibaya. Kuna usomaji mwingi wa Biblia
usioleta faida yo yote, na katika mifano mingi huleta madhara yaliyo dhahiri. Neno la Mungu linapofunuliwa bila heshima na bila maombi; mawazo ya mtu na mapenzi yake
yasipokazwa kwa Mungu, au yasipopatana na mapenzi yake, hapo ndipo mawazo ya mtu
huyo hufunikwa na wingu la mashaka; na katika kujifunza kuko huko kwa Biblia
mashaka ya kutoliamini Neno la Mungu huimarishwa. Adui anayatawala mawazo ya
mtu huyo, tena anamshawishi kutoa tafsiri zisizo sahihi. Kila mara wanadamu
wasipopatana na Mungu katika maneno na matendo yao, hapo ndipo, licha ya wao kuwa
wasomi sana kama walivyo hasa, wanakuwa na mwelekeo wa kukosea katika uelewa
wao wa Maandiko, wala si salama kuyategemea maelezo yao. Wale wanaoyaangalia
Maandiko ili kugundua hitilafu hawana ufahamu wa kiroho. Wakiwa na mtazamo
uliopotoka wataona sababu nyingi za kuwa na mashaka na kutosadiki mambo yale
ambayo ni wazi na rahisi kweli kweli.

Hata ifichwe namna gani, sababu hasa ya kuwa na mashaka na kulishuku Neno
la Mungu, kwa hali nyingi, ni kupenda dhambi. Mafundisho na vizuizi vya Neno la
Mungu havipendezi kwa wenye moyo wa kujisifu na kupenda dhambi, na wale
wasiotaka kuyatii matakwa ya Biblia huwa wepesi kutosadiki ya kuwa hilo ni Neno halisi
la Mungu. Ili kuweza kuipata kweli ni lazima tutamani kuijua hiyo kweli, na kuwa na
moyo ulio tayari kulitii. Na wote wanaokuja kujifunza Biblia wakiwa na roho hiyo
watapata ushahidi mwingi uonyeshao kuwa hilo ndilo Neno la Mungu, nao wataweza
kuzijua kweli zake zitakazowahekimisha hata wapate wokovu.

Kristo amesema, “Mtu akipenda kuyatenda mapenzi Yake, atajua habari ya yale
mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu.” Yoh. 7:17. Badala ya kuona mashaka na
kuyakosoa mambo msiyoweza kuyafahamu, izingatieni nuru ambayo tayari inaangaza juu
yenu, nanyi mtapokea nuru kubwa zaidi. Kwa neema yake Kristo tekelezeni kila wajibu
uliofunuliwa wazi katika ufahamu wenu, ndipo mtawezeshwa kuujua na kuutekeleza ule
ambao mnauonea mashaka sasa.
Uko ushahidi ulio wazi kwa wote - kwa wasomi sana, na kwa wasiojua kabisa
kusoma na kuandika - huo ni ushahidi unaoonekana katika matukio ya maisha ya mtu
mwenyewe. Mungu anatualika tujihakikishie sisi wenyewe ukweli wa Neno lake, na
ukweli wa ahadi zake. Anatuagiza, anasema, “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu
mwema.” Zab. 34:8. Badala ya kulitegemea neno la mtu mwingine, yatupasa kuonja sisi
wenyewe. Anatutangazia, “Ombeni, nanyi mtapata.” Yoh. 16:24. Ahadi zake
zitatimia. Hazijapata kushindwa kamwe; kamwe haziwezi kushindwa. Na wakati
tunapomkaribia Yesu, na kufurahishwa na upendo wake, mashaka yetu na giza
linalotufunika vitatoweka katika nuru ya kuwako kwake.

Mtume Paulo asema ya kwamba Mungu alituokoa “na nguvu za giza,
akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake.” Kol. 1:13. Na
kila mmoja ambaye “amepita kutoka mautini kuingia uzimani” anaweza kutia “muhuri ya
kwamba Mungu ni kweli.” Yoh. 5:24; 3:33. Anaweza kushuhudia hivi, “Nilihitaji
msaada, niliupata ndani yake Yesu. Mahitaji yangu yote nilipewa, njaa ya moyo wangu
ilishibishwa; na sasa Biblia imekuwa kwangu ufunuo wa Yesu Kristo. Waniuliza mbona
namwamini Yesu? - Kwa sababu ni Mwokozi wangu kutoka mbinguni. Kwa nini
naisadiki Biblia? - Kwa sababu nimeiona kuwa ni sauti ya Mungu kwa moyo wangu.”
Twaweza kuwa na ushuhuda ndani yetu wenyewe uonyeshao kwamba Biblia ni ya kweli,
na ya kwamba Kristo ni Mwana wa Mungu. Twajua kwamba hatufuati “hadithi
zilizotungwa kwa werevu.” 2 Petro 1:16. Petro awasihi ndugu zake anasema, “Kueni katika neema, na katika kumjua
Bwana wetu, na Mwokozi wetu Yesu Kristo.” 2 Petro 3:18. Watu wa Mungu
wakiendelea kukua katika neema yake, wataendelea zaidi kulifahamu Neno lake.
Wataitambua nuru na uzuri mpya na kweli zake takatifu. Jambo hili limedhihirika kuwa
ni la kweli katika historia ya kanisa katika vizazi vyote, na litaendelea kuwa hivyo mpaka
mwisho. “Bali njia ya wenye haki ni kama nuru ing’aayo, ikizidi kung’aa hata mchana
mkamilifu.” Mithali 4:18.

Kwa imani twaweza kutazama mbele, na kuishikilia sana ahadi ya Mungu
kwamba akili zetu zitakua, uwezo wetu wa kibinadamu utaunganika na ule wa Mungu, na
kila nguvu ya kiroho itagusana moja kwa moja na yule aliye Chimbuko la nuru.
Twaweza kushangilia kwamba yote yaliyotufanya tuchanganyikiwe kuhusu maongozi ya
Mungu kwetu, wakati ule yataeleweka wazi; mambo yaliyokuwa magumu kwetu
kuyaelewa, wakati ule tutapata maelezo yake; na pale ambapo akili zetu finyu za
kibinadamu ziliona machafuko tu na makusudi yaliyoshindikana kutekelezwa, tutaona
mwafaka mkamilifu kabisa na mzuri ajabu. “Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo
kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa
sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana.” 1 Kor. 13:12.

WIMBO

1st Stanza:
Kumtegemea Mwokozi,
Kwangu tamu kabisa;
Kukubali neno lake
Nina raha moyoni.

Chorus:
Yesu, Yesu namwamini,
Nimemwona thabiti;
Yesu, Yesu yu thamani,
Ahadi zake kweli.

2nd Stanza:
Kumtegemea Mwokozi,
Kwangu tamu kabisa;
Kuamini damu yake
Nimeoshwa kamili.

3rd Stanza:
Kumtegemea Mwokozi,
Kwangu tamu kabisa;
Kwake daima napata,
Uzima na amani.

4th Stanza:
Nafurahi kwa sababu
Nimekutegemea;
Yesu, M-pendwa, Rafiki,
Uwe nami dawamu.

(Nyimbo za Kristo, 129.. 'Tis so sweet to trust in Jesus’)


********************************

Ngoja nikwambie msomaji wangu jambo hili, kwamba:
MAJIBU YAFANYAYO KAZI ni kipengele kinachoongelea masuala ya kiroho zaidi.

Kwa sababu ya upekee na unyeti wa siku, Sio vibaya tukibadilishana mawazo na kuambizana yaliyomuhimu katika maisha hasa ya kiroho.
Na huu utakuwa ni mfululizo kwa kila siku kama hii ya leo...
(Namaanisha JumaMosi)

Pamoja na kwamba weeengi wanaamini hii ni kweli, lakini kweli halisi jionee mwenyewe ambapo

Cheryl Fortune

Anapoimba Nyimbo kwa mfululiza wa kwanza tafsiri yake ipo hapo juu unaoitwa

'Tis so sweet to trust in Jesus’

na wa pili unaitwa ‘Oh how I love Jesus’

MARA BAADA YA HIZO NYIMBO

Doug Batchelor  

a t a t w a m b i a    k u h u s u:

The Great Judgment Day

Pata nyimbo KWANZA.

 

                                                               ...sasa tufuatilie Ujumbe unaohusu SIKU YA HUKUMU KUU.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni