1. Biblia yasemaje juu ya Amerika ya Kiprotestanti itakavyoisujudu Mamlaka ile ya Kikatoliki ya Roma? Ufu.13:11-17.
Photo Credit By: temcat.com
2. Je, unabii huo utatimizwa lini?
a. "Unabii wa Ufunuo 13 unatangaza kwamba mamlaka ile iliyowakilishwa na mnyama aliye na pembe kama za mwana-kondoo ita"ifanya dunia na wote wakaao ndani yake wausujudu upapa -----ulioonyeshwa hapo kama mnyama "mfano wa chui."... Unabii huo utatimizwa wakati ule Marekani itakapotunga amri ya kuitunza Jumapili, tendo ambalo Roma inadai kuwa ni kuutambua ukuu wake kwa namna ya pekee." GC 578,579.
b. "Kulazimisha utunzaji wa Jumapili kwa upande wa Uprotestanti ni sawa na kulazimisha ibada ya upapa." GC 448.
3. Shinikizo la kuitungia amri [sheria] Jumapili litatoka wapi?
a. "Viongozi wakuu wa kanisa na serikali wataungana ili kuwahonga, kuwashawishi, au kuwalazimisha watu wa tabaka zote wapate kuiheshimu Jumapili. Kule kukosekana kwa mamlaka ya Mungu [katika Biblia] kutafanya zipate kutungwa amri kali za ukandamizaji. Rushwa katika ngazi za kisiasa inaharibu moyo ule wa kupenda haki na kuijali kweli; hata katika Amerika iliyo huru, watawala na watunga sheria, ili kupata upendeleo wa umma, watakubali madai ya wengi wanaopendelea iwepo amri [sheria] ya kulazimisha utunzaji wa Jumapili." GC 592 (Angalia pia 4SP 410).
b. "Ili kujipatia hali ile ya kupendwa na watu wengi na haki ya kuweza kuteuliwa, watunga sheria watakubaliana na madai ya kuwapo kwa amri ya Jumapili." 5T 451.
c. "Watunga sheria watakubaliana na madai ya kuwapo kwa amri za Jumapili." PK 606.
d. "Waprotestanti wa Marekani watakuwa mstari wa mbele katika kuinyosha mikono yao juu ya ghuba ili kuushika mkono wa Imani ya Mizimu; tena, watainyosha juu ya shimo kubwa lenye kilindi kirefu kushikana mikono na Mamlaka ile ya Roma; hapo ndipo, chini ya uongozi wa muungano huo wa utatu, nchi hii itafuata katika nyayo za Roma kwa kuikanyaga chini ya miguu yake haki ya mtu kuamini kama dhamiri yake inavyotaka." GC 588.
e. "Iwapo watu wanaweza kushawishika kupendelea iwepo amri ya Jumapili, basi, wachungaji na mapadre wanakusudia kutumia nguvu ya mvuto wao wa pamoja katika kujipatia marekebisho ya dini katika Katiba ya nchi, na kulilazimisha Taifa zima [la Marekani] kuitunza Jumapili." RH, Extra 12-24-1889, uk.2.
4. Je! hao wanaoitetea Amri ya Jumapili wanatambua wanalolitenda?
a. "Pana watu wengi, hata miongoni mwa wale walio katika shughuli hiyo ya kutaka itungwe Amri ya Jumapili, ambao wamepofushwa macho yao wasiweze kuona matokeo yatakayofuata baada ya kitendo hicho kutekelezwa. Hawaoni ya kwamba wanaupiga rungu uhuru wa dini moja kwa moja. Wako wengi ambao hawajapata kuyaelewa kamwe madai ya Sabato ya Biblia na msingi wa uongo ambao Amri ya Jumapili inaukalia." 5T 711. b. "Wanafanya kazi hiyo wakiwa vipofu. Hawaoni ya kwamba kama Serikali yao ya Kiprotestanti inaziachilia mbali kanuni zilizowafanya kuwa Taifa huru, linalojitegemea, na kwa njia ya kutunga sheria wanaingiza katika Katiba ya Nchi, kanuni ambazo zitatangaza uongo wa upapa na madanganyo ya upapa, watakuwa wanajitumbukiza katika utawala wa hofu wa Roma wa Zama zile za Giza." RH, Extra 12-11-1888, uk.4.
c. "Kuna nguvu ya Kishetani inayoliendesha tapo [kundi] hilo la Jumapili, ila imejificha. Hata watu wale waliojiingiza katika kazi hiyo, wamepofushwa macho yao wasiweze kuona matokeo yatakayofuata baada ya kazi ya tapo lao kukamilika." RH 1-1-1889, uk.1; 7BC 975.
5. Ni nani hasa aliye mwanzilishi mwamba mkuu wa kuitungia amri Jumapili?
a. "Hakuna hatua yo yote iliyochukuliwa katika kuitukuza Sabato hiyo ya sanamu, na kuileta Jumapili ipate kutunzwa kwa kuitungia amri [sheria], isipokuwa ni yule Shetani aliye nyuma yake, na ndiye amekuwa mtendaji mkuu." 7BC 977.
b. "Bunge litakapotunga sheria ambazo zinaitukuza siku ya kwanza ya juma, na kuiweka mahali pa siku ile ya saba, hapo ndipo hila ya Shetani itakuwa imekamilika." 7BC 976.
c. "Sabato hiyo ya uongo [Jumapili] italazimishwa kwa njia ya kuitungia sheria [amri] ya ukandamizaji. Shetani na malaika zake wako macho sana, nao wanashughulika vibaya sana, wakifanya kazi kwa nguvu na ustahimilivu kupitia kwa wakala wao wa kibinadamu ili kulitimiza kusudi lake la kufutilia mbali katika mioyo ya watu maarifa ya kumjua Mungu." 7BC 985; RH 12- 13-1892.
6. Je, Amri hiyo ya Jumapili inaonyesha dharau juu ya nani?
"Juhudi zaidi ya wazi itafanyika kuitukuza sabato hiyo ya uongo, na kumwonyesha dharau Mungu Mwenyewe kwa kuibadili siku ile aliyoibariki na kuitakasa. Sabato hiyo ya uongo [Jumapili] italazimishwa kwa sheria ya ukandamizaji." 7BC 985.
7. Je, tutazamie kuziona sheria za Jumapili katika majimbo yanayojitawala (states) fulani fulani tu au Bunge la Marekani litachukua hatua ya kuitunga sheria hiyo[kwa Taifa zima]?
a. "Nchi yetu [ya Marekani] imeingia hatarini. Wakati unakaribia ambapo watunga sheria [Wabunge] wake watakapozikataa kabisa kanuni zile za Uprotestanti na kuunga mkono uasi wa Kanisa Katoliki. Watu hao ambao Mungu amewatendea maajabu makubwa sana, akiwatia nguvu kulitupilia mbali lile kongwa linaloumiza sana la upapa, kwa njia ya sheria ya taifa zima wataitia nguvu nyingi imani potofu ya Roma, na kwa njia hiyo kuuamsha utawala ule wa mabavu ambao unangojea tu uguswe ili uanze tena ukatili wake na udikteta." 4SP 410 (1884); ST, 7-17-1907, uk.1907, uk.7.
b. "Tunaona ya kwamba juhudi zinafanywa ili kutuwekea vizuizi katika uhuru wetu wa dini. Hoja ya Jumapili sasa inafikia viwango vikubwa. Marekebisho ya Katiba yetu ya nchi yanasisitizwa katika Bunge la Marekani, na mara yatakapopatikana, basi, ni lazima ukandamizaji utafuata." RH, 12-18-1888, uk.786 (Angalia pia 5T 711).
c. "Hivi karibuni kitatokea kipindi cha kusisimua sana kwa wote walio hai. Malumbano ya zamani yataanza tena; malumbano mapya yatazuka. Mandhari [picha] ya mambo yale yatakayotendwa kama maigizo katika dunia yetu bado hata hayajapata kuingia katika mawazo yetu. Shetani yuko kazini kupitia kwa mawakala wake wa kibinadamu. Wale wanaofanya juhudi ya kuibadilisha Katiba ya Nchi na kujipatia nafasi ya kutunga sheria inayolazimisha utunzaji wa Jumapili hawatambui hata kidogo matokeo yake yatakavyokuwa. Hatari kubwa imetukabili hivi sasa." 5T 753.
d. "Taifa letu litakapozikataa kabisa kanuni za Serikali yake hata kutunga sheria ya Jumapili, katika kitendo hicho Uprotestanti utakuwa umeshikana mikono na upapa." 5T 712.
e. "Hatari kubwa inawangojea watu wa Mungu. Karibu sana Taifa letu litajaribu kuwalazimisha wote kuitunza siku ya kwanza ya juma kama siku takatifu. Kwa kufanya hivyo, hawatakuwa na haya [aibu] kuwalazimisha wanadamu kinyume cha sauti ya dhamiri zao wenyewe ili kuitunza siku ambayo Taifa linaitangaza kuwa ndiyo Sabato." RH, Extra 12-ll-1888, uk. 4.
e. "Sheria ya Mungu itakapobatilishwa, na uasi kuwa dhambi ya Taifa hili, hapo ndipo Bwana atakapotenda kazi kwa ajili ya watu wake." RH, Extra 12-11-1888, uk.3.
g. "Kwa agizo lile linalolazimisha [utunzaji wa] siku ile iliyowekwa na upapa kwa kukiuka sheria ya Mungu, Taifa letu litajitenga kabisa mbali na haki." 5T 451.
Photo Credit By: Yusuph Mcharia
8. Je, Marekani litaendelea kuwa Taifa lililopata upendeleo wa Mungu baada ya kuchukua hatua ya kisheria na kuiweka kando Sheria ya Mungu?
a. "Watu wa Marekani ni watu waliopata upendeleo; lakini watakapouwekea vizuizi uhuru wa dini, kuachilia mbali Uprotestanti, na kuunga mkono upapa, hapo ndipo kikombe chao cha maovu kitakuwa kimejaa, na 'uasi wa Taifa' hili utaandikwa katika vitabu vile vya mbinguni." RH, 5-2- 1893, uk.274.
b. "...Kwa hiyo, uasi huo na uwe ishara kwetu sisi ya kwamba kikomo cha uvumilivu wa Mungu kimefikiwa, ya kwamba kikombe cha maovu ya Taifa letu kimejaa...." 5T 451.
9. Je, matokeo ya uasi wa Taifa letu hili yatakuwaje?
a. "Wakati unakuja ambapo sheria ya Mungu, kwa maana ya pekee, itabatilishwa katika nchi yetu. Watawala wa Taifa letu, kwa njia ya kutunga sheria Bungeni, wataitia nguvu sheria hiyo ya Jumapili, na kwa njia hiyo watu wa Mungu wataingia katika hatari kubwa sana. Taifa letu, katika vikao vyake vya Bunge, litakapotunga sheria za kuzibana dhamiri za watu kuhusu haki zao za kidini, likilazimisha utunzaji wa Jumapili, na kutumia nguvu ya ukandamizaji dhidi ya wale wanaoitunza Sabato ya Siku ya Saba, hapo ndipo sheria ya Mungu, kwa makusudi na nia kamili, itakuwa imebatilishwa katika nchi yetu; na uasi wa Taifa hili utafuatiwa na maangamizi yaTaifa hili." RH, 12-18-1888, uk. 785; 7BC 977.
b. "Ni katika wakati ule wa uasi wa Taifa hili, wakiwa wanazitekeleza sera za Shetani, watawala wa nchi hii watakapojipanga wenyewe upande wa mtu yule wa dhambi, ----- hapo ndipo, kikombe chao cha maovu kitakuwa kimejaa; uasi wa taifa hili ni ishara ya maangamizi ya Taifa hili." GCB 1891, uk.259.
c. "Matokeo ya uasi huu yatakuwa ni maangamizi ya Taifa hili." RH, 5-2-1893, uk. 274.
d. "Waprotestanti watashughulika sana na watawala wa nchi hii kutunga sheria zitakazourejesha ukuu alioupoteza mtu yule wa dhambi, anayeketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu. Kanuni za Ukatoliki wa Roma zitahifadhiwa na kulindwa na Serikali hii. Uasi huo wa Taifa hili utafuatiwa kwa haraka sana na maangamizi ya Taifa hili.... Serikali za Kiprotestanti zitaifikia njia ngeni, nyembamba ipitayo katikati ya milima. Wataongolewa na dunia. Pia, katika kujitenga kwao na Mungu, watafanya kazi kuufanya uongo na uasi wao kwa Mungu viwe ndiyo sheria ya Taifa." RH, 6-15-1897, uk.370.
e. "Makanisa ya Kiprotestanti yatakapoungana na mamlaka za kidunia kuiimarisha dini hiyo ya uongo, ambayo kwa kuipinga mababu zao walistahimili mateso makali sana, hapo ndipo sabato ya papa itakapolazimishwa kwa mamlaka iliyoungana ya kanisa na serikali [dola]. Patakuwa na uasi wa Taifa, ambao utaishia tu katika maangamizi ya Taifa hili. Ev 235 (1899).
f. "Makanisa ya Kiprotestanti yatakapotafuta msaada kutoka kwa mamlaka za kidunia, hivyo kuiga mfano wa kanisa lile asi, ambalo kwa kulipinga babu zao walistahimili mateso makali sana, hapo ndipo patakuwa na uasi wa Taifa ambao utaishia tu katika maangamizi ya Taifa hili." 4SP 410 (1884); ST 7-17-1907, uk. 7.
g. "Makanisa ya Kiprotestanti yatakapoungana na mamlaka za kidunia kuiimarisha dini hiyo ya uongo,... dola hii itakapotumia mamlaka yake kulazimisha amri hizo na kutoa ruzuku kwa taasisi za kanisa ----- hapo ndipo Amerika ya Kiprotestanti itakuwa imeunda sanamu ya upapa, na kutakuwa na uasi wa Taifa ambao utaishia tu katika maangamizi ya Taifa hili." ST, 3-22-1910; 7BC 976.
10. Je, Amerika ya Kiprotestanti itaiundaje sanamu ya mnyama?
a. "Makanisa makuu ya Marekani yatakapoungana katika mafundisho yale wanayoshirikiana pamoja, watakapoishawishi serikali kuyatia nguvu maagizo yao kisheria na kuzipa ruzuku taasisi zao, hapo ndipo Amerika ya Kiprotestanti itakuwa imeunda sanamu ya utawala [wa kidini] wa Roma, na adhabu ya serikali haitaweza kuepukwa kutolewa juu ya wale wasioafiki." GC 445 (Angalia pia 4SP 278).
b. "Katika tendo lile lile la kulazimisha wajibu wa kidini kwa kutumia mamlaka ya kidunia, makanisa yenyewe yangeunda sanamu ya mnyama; kwa hiyo, kulazimisha utunzaji wa Jumapili kule Marekani kungekuwa ndiko kulazimisha ibada ya mnyama na sanamu yake." GC 449.
11. Je, kulazimisha utunzaji wa Jumapili (kuunda sanamu ya mnyama) kule Marekani kutakuja baada au kabla ya kufungwa kwa mlango wa rehema?
a. "Bwana amenionyesha waziwazi ya kwamba sanamu ya mnyama itaundwa kabla ya mlango wa rehema kufungwa; maana hiyo ndiyo itakuwa jaribio kubwa kwa watu wake Mungu.... Hilo ndilo jaribio ambalo watu wa Mungu hawana budi kuwa nalo kabla hawajatiwa muhuri." 7BC 976.
b. "Kwa agizo lile linalolazimisha siku iliyowekwa na upapa, Taifa letu litajitenga kabisa mbali na haki. Uprotestanti utakapounyosha mkono wake ng'ambo ya ghuba kuushika mkono wa Mamlaka ya Roma, utakapounyosha juu ya shimo kubwa lenye kilindi kirefu kushikana mikono na Imani ya Mizimu, nchi yetu, chini ya uongozi wa muungano huo wa utatu, itakapokuwa imeikataa kila kanuni ya Katiba yake kama Serikali ya Kiprotestanti na ya Jamhuri, na kutunga sheria inayotangaza uongo na madanganyo ya upapa, hapo ndipo tunaweza kujua kwamba wakati umewadia kwa utendaji wa miujiza ya ajabu ya Shetani na ya kwamba mwisho u karibu.
Kama vile kukaribia kwa majeshi yale ya Kirumi kulivyokuwa ishara ya maangamizi ya Yerusalemu yaliyokuwa karibu sana kwa wanafunzi wake wale, hivyo ndivyo uasi huo unavyoweza kuwa ishara kwetu kwamba kikomo cha uvumilivu wa Mungu kimefikiwa, na ya kwamba kikombe cha maovu ya Taifa letu kimejaa, na ya kwamba malaika yule wa rehema karibu ataruka kwenda zake, asirudi tena kamwe." 5T 451.
c. "Njozi za Anna zinaweka kuundwa kwa sanamu ya mnyama baada ya kufungwa kwa mlango wa rehema. Hivyo sivyo mambo yalivyo. Unajidai kuziamini shuhuda; hebu na zikuweke sawa katika suala hili. Bwana amenionyesha mimi waziwazi kwamba sanamu ya mnyama itaundwa kabla ya mlango wa rehema kufungwa; maana hiyo ndiyo itakuwa jaribio kuu kwa watu wa Mungu, ambalo kwalo umilele wao utaamuliwa." 2SM 81.
12. Kwa kuzingatia matarajio ya kutungwa kwa Amri ya Jumapili, Waadventista wanaokaa katika miji mikubwa wanasihiwa kufanya nini upesi iwezekanavyo?
a. "Anataka sisi tuishi mahali palipo na nafasi ya kutosha. Watu wake hawapaswi kusongamana katika miji mikubwa. Anawataka kwenda na familia zao nje ya miji mikubwa, ili wapate kujiandaa vizuri kwa uzima ule wa milele. Kitambo kidogo tu watatakiwa kuiacha miji mikubwa.... Tokeni katika miji mikubwa upesi iwezekanavyo...." 2SM 356.
b. "Hatari kubwa inakuja haraka kuhusiana na utunzaji wa Jumapili.... Kama kwa mpango wa Mungu tunaweza kujipatia mahali palipo mbali kutoka katika miji mikubwa, basi, Bwana atatutaka sisi kufanya hivyo. Kuna nyakati za taabu mbele yetu.... Nauona umuhimu upo wa kuharakisha kuyaweka mambo yote tayari kwa hatari hiyo." 2SM 359.
Photo Credit By: Morning Star Radio 105.3 fm
13. Sheria za Jumapili zitatoa onyo gani kwa Waadventista ambao bado wanaendelea kukaa katika miji mikubwa?
"Kama kuzingirwa kwa Yerusalemu na majeshi ya Warumi kulivyokuwa ishara ya kukimbia kwa Wakristo wale wa Yudea, ndivyo kutwaa madaraka kwa upande wa Taifa letu katika kutoa amri iie inayolazimisha sabato ya papa kutakavyokuwa onyo kwetu. Basi huo utakuwa ndio wakati wa kuondoka kwenye miji midogo kwenda kwenye makazi ya upweke mahali pa faragha miongoni mwa milima." 5T 464,465.
14. Je, tutazitumiaje siku za Jumapili baada ya Amri za Jumapili kupitishwa?
a. "Waadventista Wasabato walitakiwa kuonyesha hekima yao kwa kujizuia kufanya kazi zao za kawaida katika siku ile, wakiitumia kwa shughuli za kimishonari. "Kuzipinga Amri za Jumapili kutawaimarisha tu washupavu wa dini wanaojaribu kuzilazimisha kwao ili kuongeza mateso yao. Msiwape nafasi yo yote kuwaita ninyi kuwa wavunjaji wa sheria hizo.... Mtu hapokei alama ya mnyama kwa sababu anaonyesha kwamba anatambua hekima ya kutunza amani kwa kujizuia kufanya kazi inayoleta uvunjaji wa sheria hizo.... "Wakati wo wote inapowezekana, endesheni huduma za kidini katika siku hiyo ya Jumapili.... Waalimu wetu katika shule zetu waitumie Jumapili kwa shughuli za kimishonari." 9T 232,233.
b. "Msifanye maandamano yo yote siku ya Jumapili kupinga sheria hiyo." 9T 235.
c. "Wakati mmoja wale waliokuwa wasimamizi wa shule yetu ya Avondale waliniuliza mimi wakisema: 'Tufanye nini? Mapolisi wanaoilinda sheria hiyo wameagizwa kuwakamata wale wanaofanya kazi siku ya Jumapili.' Mimi niliwajibu hivi: 'Litakuwa ni jambo rahisi sana kuliepuka tatizo hilo. Itoeni siku ya Jumapili kwa Bwana kama siku ya kufanya kazi ya kimishonari. Nendeni nje na wanafunzi wenu kuendesha mikutano mahali mbalimbali, na kufanya kazi ya uganga. Watawakuta watu majumbani mwao, nao watakuwa na wakati mzuri sana wa kuifundisha ile kweli. Njia hii ya kuitumia Jumapili sikuzote inakubaliwa na Bwana." 9T 238.
d. "Tulipokuwa tunaishi mahali paitwapo Cooranbong, ambapo shule yetu ya Avondale imejengwa,... Hoja ya kufanya kazi Jumapili ilikuja kwetu kwa ajili ya kuitafakari. Ilionekana kana kwamba punde kamba zingetufunga sana kila upande hata tusiweze kufanya kazi yo yote siku ya Jumapili. Shule yetu ilikuwa katikati ya misitu, mbali na kijiji cho chote au kituo cha reli.
Hakuna ye yote aliyekuwa anaishi karibu kiasi cha kutosha kutufanya tuingiwe na wasiwasi kwa njia iwayo yote kwa jambo lo lote ambalo tungeweza kulifanya. Hata hivyo, tulikuwa tunachunguzwa. Maofisa wa polisi walishurutishwa kuja kuangalia tulichokuwa tukifanya katika eneo lile la shule; nao walikuja hakika, lakini hawakuweza kuwaona wale waliokuwa wanafanya kazi. Imani yao na heshima yao kwa watu wetu ilikuwa imepatikana kutokana na kazi ile tuliyokuwa tumeifanya kwa wagonjwa katika jumuia ile kiasi kwamba awakutaka kuingilia kati kazi yetu isiyokuwa na madhara yo yote ambayo sisi tuliifanya katika siku ya Jumapili.
"Wakati mwingine ndugu zetu walipotishiwa kuteswa, tena wakawa wanauliza kile ambacho wangeweza kufanya, niliwapa ushauri uo huo niliokuwa nimeutoa kujibu hoja ya kuitumia Jumapili kwa michezo. Niliwaambia, "Itumieni Jumapili kwa kufanya kazi ya kimishonari kwa ajili yake Mungu. Waalimu, nendeni pamoja na wanafunzi wenu.'... "Waalimu katika shule zetu na waitumie Jumapili kwa shughuli za kimishionari." CT 459-551.
15. Je, mtazamo wetu leo uweje? Twawezaje kufanya kazi na kuomba?
a. "Hatufanyi mapenzi ya Mungu tunapokaa kimya tu, bila kufanya kitu cho chote kuuhifadhi uhuru wa dhamiri zetu. Maombi ya bidii, yenye kuleta matokeo yangekuwa yakipanda mbinguni ili janga hilo lipate kuahirishwa mpaka hapo tutakapoweza kuimaliza kazi ambayo imeachwa kwa muda mrefu sana. Hebu na pawe na maombi yanayotolewa kwa bidii sana, kisha na tufanye kazi kulingana na maombi yetu. Yaweza kuonekana kwamba Shetani anashinda na ya kwamba kweli imeshindwa na makosa [mafundisho potofu] na uongo;... Lakini Mungu angetutaka sisi kukumbuka alivyowatendea watu wake wa zamani kuwaokoa kutoka kwa maadui wao. Sikuzote amechagua upeo wa matatizo ili kuonyesha uweza wake, yaani, wakati ule ilipoonekana ya kuwa hakuna uwezekano wo wote wa kuokoka kutoka katika utendaji wa Shetani. Shida ya mwanadamu ni nafasi ya Mungu ya kutenda kazi yake." 5T 714.
b. "Tungejifunza kwa bidii Neno la Mungu, na kuomba kwa imani ili Mungu apate kuzizuia nguvu za giza; maana mpaka sasa ujumbe umekwenda karibu kwa watu wachache mno, na ulimwengu huu unapaswa kuangazwa kwa utukufu wake. Ukweli wa leo ----- amri za Mungu [kumi] na Imani ya Yesu ----- bado haujatangazwa kama unavyopaswa kutangazwa.... Yatupasa kuwa na msimamo thabiti ya kwamba sisi hatutaiheshimu siku ya kwanza ya juma kama sabato...." RH, Extra 12-24-1889, uk.2.
c. "Kwa miaka mingi tumekuwa tukiitazamia Amri ya Jumapili kutungwa katika nchi yetu; na sasa kwa vile tapo hilo liko juu yetu, tunauliza hivi, Watu wetu watafanya nini katika suala hili?...
Tungemtafuta Mungu hasa ili watu wake wapewe neema na nguvu sasa. Mungu wetu yu hai; wala hatuamini kwamba wakati umefika kabisa ambao angeruhusu uhuru wetu uwekewe vizuizi. Nabii aliwaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za nchi, wakizizuia pepo nne za nchi, upepo usivume juu ya nchi, wala juu ya bahari, wala juu ya mti wo wote. Malaika mwingine akipanda kutoka maawio ya jua, akawapigia kelele, akisema, 'Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao.' Hii inaonyesha kazi tunayopaswa kuifanya sasa, ambayo ni kumlilia Mungu wetu ili malaika wale waendelee kuzizuia pepo zile nne mpaka Wamishonari wapate kutumwa sehemu zote za dunia, na mpaka watakapokuwa wamelitangaza lile onyo juu ya wale wanaoivunja Sheria ya Yehova." RH, Extra 12-11-1888, uk.4,5.
d. "Jukumu zito limekabidhiwa kwa wanaume na wanawake wenye maombi katika nchi nzima, kupeleka dua ili Mungu alifagilie nyuma wingu hili la maovu, na kutupatia miaka michache zaidi ya kufanya kazi kwa ajili ya Bwana." RH, Extra 12-11-1888, uk.4.
e. "Twaona ya kwamba wale ambao sasa wanazishika amri zake Mungu wanahitaji kujishughulisha ili waweze kupata msaada maalum ambao ni Mungu peke yake awezaye kuwapa. Wangefanya kazi kwa bidii zaidi ili kuchelewesha kwa muda mrefu iwezekanavyo janga hilo linalotishia. RH 12-18-1888, uk. 785.
f. "Iwapo hawafanyi lo lote kuielimisha mioyo ya watu, na kwa njia ya ujinga wa kutoijua kweli Mabunge yetu yangeweza kuzikataa kanuni za Uprotestanti, na kuunga mkono na kulitia nguvu kosa la Roma, yaani, sabato ya bandia [Jumapili], basi, Mungu atawashikilia watu wake waliopokea nuru kubwa kuwa wanawajibika kwa utovu wao wa juhudi na uaminifu. Lakini kama suala hili la kutunga sheria ya dini linawekwa mbele ya watu kwa busara na kwa akili, nao wanaona ya kwamba kwa njia hiyo ya kuilazimisha Jumapili uasi wa Roma ulitokea, ya kwamba ulimwengu wa Kikristo ungeweza kuigiza tena kitendo kama hicho, na ya kwamba utawala wa mabavu wa vizazi vile vilivyopita ungerudiwa tena, basi, lo lote lijalo na lije, sisi tutakuwa tumefanya wajibu wetu." RH Extra 12-24-1889, uk.3.
g. "Hebu watu wa Mungu wanaozishika amri zake [kumi] wasinyamaze wakati kama huu, kana kwamba tulikuwa tunaikubali hali hii na kuipenda. Kuna matarajio mbele yetu ya kupigana vita ya kudumu, kwa hasara ya kufungwa, kupoteza mali zetu na hata maisha yenyewe katika kuitetea Sheria ya Mungu [Amri Kumi], ambayo inabatilishwa kwa sheria za wanadamu." RH 1-1-1889, uk.1; 7BC 975.
h. "Ni matumaini yangu kuwa tarumbeta itatoa sauti ya hakika kuhusu tapo [kundi] hili linalotaka kuiweka Amri ya Jumapili. Nadhani kwamba ingekuwa bora sana kama katika magazeti yetu somo la umilele wa Sheria ya Mungu [Amri Kumi] lingetolewa kama somo maalum.... Hivi sasa tungekuwa tunafanya kila tuwezalo kuishinda sheria hiyo ya Jumapili." CW 97,98 (1906).
j. "Wale waliokwisha kuonywa juu ya matukio yaliyo mbele yao hawapaswi kukaa wakiwa wanaingojea kimya kimya dhoruba ile inayokuja, wakijifariji wenyewe kwamba Bwana atawalinda wale walio waaminifu katika siku ile ya taabu. Yatupasa sisi kuwa kama watu wanaomngojea Bwana wao, si kwa kukaa bila kazi, bali kwa kufanya kazi kwa juhudi nyingi, kwa imani isiyotikisika. Huu sasa sio wakati wa kuiacha mioyo yetu kujazwa na mambo yale yasiyo na maana...
Tapo hilo la Jumapili hivi sasa linasonga mbele gizani. Viongozi wake wanaficha hoja halisi, na wengi wanaojiunga na tapo hilo wao wenyewe hawaoni ni wapi mkondo wake wa chini unakokwenda. Itikadi zake ni laini, na mwonekano wake ni wa Kikristo; lakini litakaponena, litaifunua roho ile ya joka. Ni jukumu letu kufanya yote yaliyo katika uwezo wetu kuiepusha hatari hii inayotishia. Tungejitahidi kuzizima hisia za chuki kwa kujiweka wenyewe katika nuru ile inayofaa mbele ya watu. Tungeweka mbele yao hoja halisi ya jambo hilo, hivyo kuingilia kati kwa kupinga kunakofaa dhidi ya hatua za kuuwekea kizuizi uhuru wa dhamiri zetu. Yatupasa kuyachunguza Maandiko, na kuweza kutoa sababu kwa imani yetu." RH Extra 12-11-1888, uk. 4.
k. "Vitabu vya 'Patriarchs and Prophets, Daniel and Revelation, na The Great Controversy' vinahitajika sana sasa kuliko vilivyopata kuhitajika huko nyuma. Vingetawanywa kwa wingi sana kwa sababu kweli zile vinazozisisitizia zitayafungua macho mengi yaliyopofuka.... Wengi miongoni mwa watu wetu wamekuwa vipofu kwa umuhimu wa vitabu vile vile hasa vinavyohitajika sana. Kama busara na ustadi vingekuwa vimeonyeshwa kwa wakati ule katika kuviuza vitabu hivyo, basi, tapo hilo la Sheria ya Jumapili lisingefika hapo lilipo leo." CM 123; RH 12-16-1905.
l. "Hatuwezi kufanya kazi ili kuwafurahisha watu wale watakaoutumia mvuto wao kuukandamiza uhuru wa dini, na kuanzisha hatua za ukandamizaji ili kuwaongoza au kuwalazimisha wanadamu wenzao kuitunza Jumapili kama Sabato. Siku ya kwanza ya juma sio siku ya kuiheshimu. Ni sabato ya bandia, na washiriki wa familia yake Bwana hawawezi kushirikiana na watu hao wanaoitukuza siku hiyo, na kuivunja Sheria ya Mungu [Amri Kumi] kwa kuikanyaga chini ya miguu yao Sabato yake. Watu wa Mungu hawapaswi kupiga kura ili kuwaweka watu kama hao katika ofisi; maana wanapofanya hivyo, wanashiriki pamoja nao dhambi zile watakazozitenda wakiwa ofisini." FE 475; GW 39l,392.
********************
UNA MAONI AU USHAURI WOWOTE?
USISITE KUACHA KTK KIBOSKI CHA MAONI MTAA FLANI HAPO CHINI.
********************
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni