Mtayarishaji

Morning Star Radio

Alhamisi, Machi 03, 2011

KIPOFU ALIYEPEWA TOCHI AITUMIE WAKATI WA GIZA...TANZANIA YANGU.

Ni hivi:
Nimekusudia kuendeleza kile alichokizungumzia kaka katika blog yake ya www.changamotoyetu.blogspot.com kwamba: TANZANIA YANGU...."Inayokazana" kuona ilihali imefumba macho."Nataka mwache kutazama, ninataka muone...sizuii msifanye mfanyayo, tunafikiri kwa ubongo sio kwa nyayo." Mafanikio hutegemea mazoezi. BINADAMU huwa tunatofautiana sana katika utendaji wetu. Mafanikio yetu katika utendaji hutegemea sana uzoefu katika jambo hilo tunalolitenda. Ili tuweze kuwa na uzoefu katika utendaji wa jambo lolote lile tunapaswa kufanya mazoezi mengi na ya muda mrefu.Kinyume chake lakini, wengi wetu hatuna uzoefu katika mambo yale tunayotenda na hivyo hakuna mafanikio mazuri. Kuna mambo mengi yanayohitaji mazoezi. Tukitaka kuimba kwa ufanisi na kwa ufundi tunahitaji kufanya mazoezi. Mambo ndivyo yalivyo katika taaluma zote na hata michezo mbali mbali.Kwa mfano Watanzania tumekuwa tukishindwa sana katika mashindano ya michezo. Sababu kubwa ni ile ya kutokuwa na uzoefu katika michezo. Uzoefu huo unakosekana kwa sababu hatuna mazoezi ya kutosha na ya muda mrefu. Mazoezi kama mazoezi yanapaswa kuwa ya muda mrefu. Wenzetu walioendelea husema kuwa "mazoezi hufanya kitu kiwe kikamilifu". Mwenye kufanya mazoezi baadaye huwa na mazoea katika jambo hilo alilolifanyia mazoezi. Hapo huitenda hata bila kufikiri kwa kuwa vionjo, akili na mwili mzima vimekwishazoea vina uzoefu. Kwa kawaida mazoezi ni matendo yanayofanyika kwa kurudiarudia na mpaka huwa ni sehemu ya mwili. Hapo tunasema kuwa tendo fulani limo damuni. Mambo ndivyo yalivyo hata huko mashuleni. Watoto wanaojifunza kusoma na kuandika hufanya mazoezi ya kusoma na kuandika siyo kwa siku moja tu, bali kwa siku nyingi na hata miaka mingi. Kila mwalimu kwa kawaida huwa makini sana katika kuwapa wanafunzi wake mazoezi mbalimbali ili wapate uzoefu katika somo hilo.

Ufanisi katika masomo na taaluma mbali mbali hutegemea sana jinsi wanafunzi wanavyozingatia mazoezi ili kujipatia uzoefu. Wakufunzi mara kwa mara hutoa mazoezi yanayojulikana kama
"Home work" yaani kazi za kufanya nyumbani muda baada ya masomo. Yule anayetaka kufahamu lugha ya kigeni hana budi pia kufanya mazoezi ya kusoma, kuandika na hasa kuzungumza lugha hiyo. Wataalamu hutuambia kuwa haitoshi kufahamu kanuni na mbinu za kuogelea. Ili kufahamu namna ya kuogelea, licha ya kuzifahamu kanuni hizo, mwanafunzi anapaswa kuingia ndani ya maji na kufanya zoezi la kuogelea. Ndivyo pia tunavyoshuhudia kwa wanaotaka kujifunza kuendesha magari. Licha ya kujifunza sheria za barabarani pamoja na kanuni za kuendesha ni sherti mwanafunzi akae mbele ya usukani na kuuzungusha huku gari likienda mbele au nyuma.

Kwa kadiri mwanafunzi anavyofanya mazoezi mengi, ndivyo anavyoweza kufahamu kendesha gari. Vinginevyo itachukua muda mrefu kufahamu. Kuna shughuli nyingi baada ya kufanya mazoezi ya muda mrefu huweza kufanyika hata bila kufikiri. Baada ya uzoefu tunaweza kufanya mambo kwa ufanisi zaidi na pengine bila kutambua.
Mazoezi siyo tu katika mambo ya mwili na kiakili bali pia hata katika mambo ya kiroho na kitabia. Mtume Paulo analithibitisha jambo hilo pale anapowaandikia ndugu Wakorintho akisema: "Wanariadha hujipa mazoezi na nidhamu kali; hufanya hivyo ili wajipatie taji iharibikayo! Lakini sisi twafanya hivyo tupate taji ya kudumu daima" (1 Wakorintho 9:25)

Mazoezi huenda pamoja na nidhamu. Wanamichezo wetu wengi na hata wanafunzi hujidai kufanya mazoezi lakini pengine hawana nidhamu. Kumbe licha ya kufanya mazoezi, nidhamu ni ya muhimu sana. Kama hakuna nidhamu au utaratibu huwa ni vigumu sana kufanikiwa katika mashindano yawayo yote yale. Miongoni mwa semi zilizonigusa sana mimi kutoka kwa mzee wa changamoto kaka Bandio Mbelwa ni pamoja na TANZANIA ILIYO MAARUFU KWA KUENDEKEZA WINGI WA VINGI HATA KAMA VINGI HIVYO HAVINA UFANISI WALA TIJA KWA WENGI. Tunaposema kuwa tunajiandaa kuingia katika karne mpya ya Sayansi na Tekinolojia ama kwa namna na jinsi yoyote ile ni kwamba: imetupasa tuwe na uzoefu katika mambo mbali mbali ya kisanyansi. Ili tuweze kufanikiwa yatupasa tujikanie mambo yasiyo ya lazima na tutumie muda wetu mwingi katika kujizoeza katika mambo hayo.Tunapaswa kujijengea mazoea ya kusoma sana. Tunaambiwa kuwa ili tujipatie elimu na maarifa kuna njia tatu:

01. Kusoma mambo yale yaliyokwishaandikwa na wataalamu.
02. Kuwasikiliza wale wenye utaalamu na 03. Ni kufungua macho na kuona mambo yale yaliyokwishatendwa au yanayotendwa si tu na wataalamu. Tuwe na uzoefu wa mambo hayo ili tuweze kufanikiwa. Daima tuzoee kusoma, kuwasilikiza wengine na pia kuangalia yale yaliyofanywa na wengine. Tujifunze kutoka kwa yoyote, wakati wowote na kwa chochote kile kizuri.
IPO SIKU TUTAKAZANA ILIHALI TUMEFUMBUA MACHO!!

Maoni 3 :

 1. Hoja makini mkuu, nashukuru kwa muendelezo wake, nami naogopa kutia doa, kwani nakumbuka sana mwalimu wangu wa ecomics, ambaye licha ya kulifundisha hilo somo kwa ufasaha lakini pia alikwa akilitumia katika maisha yake, Ipo siku alituambia;
  'Niwaulize wanafunzi hivi ukiwa gizani unafumba macho au unayafumbua?' Tukajibu kuwa tunafumbua utaonaje ...'
  'Giazani unaona?' akatuuliza
  'Hata kama huoani, lakini macho yatazoea giza' akajibu mtaalamu wa mambo
  'Kweli nyie hamaiva ki-uchumi, ukiwa kwenye giza totoro, ufumbe macho usifumbe, hutaona, sasa kwanini upoteze `carlos'...nguvu za akili na mwili, kwa kuangalia wakati hutaona. Inabidi ufumbe macho yako, ili nguvu nyingi zisitumike, utakuwa uma`save' some energy'
  Sijui mkuu umenielewa nini ninataka kusema?
  Huenda sisi kwa kile tukionacho kama`ujanja' wetu tumeamua kufumba macho, kwasababu tuyafumbe au tuyafumbue `hatujui na hatuoni tofauti' ....masikini wee...wenzetu wanafikiria kuishi sayari nyingine, sisi tupo katika `kukariri na kuiga, matapishi ya wenzetu!

  JibuFuta
 2. Duh!!! Kaka unasema umeiendeleza hii lakini naamini ulichofanya ni zaidi ya kuiendeleza. UMEFAFANUA KUTOKA PEMBE AMBAYO SIKUWAHI KUIONA NA NIMEELIMIKA MNO.
  Nashukuru kwa kushirikiana kwenye kuelimisha jamii, nami naenda waarifu WAUNGWANA kupita na kuchota maarifa.
  Lakini tatizo linabaki palepale kuwa TUMEKUWA WAJINGA NA WAVIVU WA KUSOMA. Ndio maana naandika makala mengine kuhusu ndugu zangu "waandishi wa habari" ambao wamekuwa wavivu wa kusoma na wanataka kuandika, hawasikilizi lakini wanataka kutangaza. Hawa (WAANDISHI WA HABARI) NDIO CHACHU YA UJINGA NCHINI MWETU.
  Naamini tutazidi kushrikiana kuweka mambo sawa kwa manufaa ya jamii nzima
  BARAKA KWAKO KAKA na kama hutajali, wacha nikaiweke kwenye wall yangu ya Facebook ili wengi waione na kuirejea

  JibuFuta
 3. KWA UJUMLA WAKE:
  Inatia hofu ingawa hili halionekani kuwa tatizo la kitaifa kama tunapoangalia jamii yetu itamezwa na mila na desturi bomu zinazoletwa na ama vyombo vya habari bila uthibiti yakinifu.

  Nakushukuru sana Emu-Three kwa mbinu hii iliyosafarini, japo kuwa kuna hisia zisizokuwa na umbo miongoni wenye fikra mgando Huenda sisi kwa kile tukionacho kama`ujanja' wetu tumeamua kufumba macho pasipo kujielewa. Ni sawa na KUFA KWA KIU HUKU UNAOGA ZIWANI. Nitakuja na kitu hicho hivi karibuni, natayarisha mswada.

  Mzee wa changamoto, kwa changamoto unazozidi kuleta, vyovyote vile utakavyo ama unavyowiwa kufanya kwa lengo la kuijenga jamii fanya, ikiwa ni kwa njia ya facebook kuwa huru KAKA kuendeleza, kila wazo lililo katika jambo ni vyema liwe bayana.

  Hatuna budi kujiuliza hivi tunakwenda wapi?

  "HOW MANY MILES TO H E A V E N...!!!!!".

  JibuFuta