Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatano, Machi 02, 2011

NDANI YA DALADALA

JE UNAJUA YATOKEAYO NI KWA SABABU YA CHANZO?? NIANZE KWA KUSEMA: JAPOKUWA HUWA KUNA UGUMU KTK KUANZA KILA JAPO JAMBO, ILA MWISHOWE URAHISI HUONEKANA ULIJIFICHA WAKATI MAWAZO YA KUANZA YALIPOKUJITOKEZA...NIMEJIPA WAKATI ILA http://changamotoyetu.blogspot.com INANIFIKIRISHA ZAIDI NA KUNIJENGA.

Kila siku ni siku ya heka heka katika jiji la Dar es salaam.

Ni rahisi kufikiri kwamba wale wanaowatumikisha vijana na watoto wanawasaidia, lakini kama ni hivyo wengine wasingeishia kuchoma mishikaki na vitumbua na kuhifadhi pesa peke yao, mtangazaji katika redio iliyokuwa imeifunguliwa katika gari alisikika akiongea, akaendelea...

…kuna mtoto amelazimika kukimbilia Dar es salaam akitokea kwao huko alipokuwa anaishi na wazazi wake baada ya kushindwa kwenda shule licha ya kuwa alifaulu mtihani wa darasa la saba na wazazi wake kufariki.

Nduguze hawana uwezo wa kumgharamia masomo???

Tukiwa ndani ya daladala dereva alibadilisha stesheni redio ilisikika ikipiga muziki kwa sauti ya juu kiasi kwamba baadhi ya abiria wakalalamika na kumtaka dereva apunguze sauti. Dereva alitii lakini akabadilisha stesheni ya redio na kuweka nyingine.

kulionekana kuna watangazaji wawili katika stesheni ya redioni aliyoiweka dereva. Mara sauti ikakata ghafla, dereva akaichapa kofi redio ikaanza kuongea tena, abiria walicheka.

Mtangazaji mwingine akadakia; hotuba iliyotolewa kwa taifa na raisi wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kuuaga mwaka elfu mbili na tisa na kuukaribisha mwaka wa elfu mbili na kumi, aligusia mkakati wa kilimo.

Wapo wanao hofu kwamba mkakati huu unaweza kuibua migogoro ya ardhi hasa ikizingatiwa kwamba unalenga katika kilimo kikubwa cha biashara na chenye kutumia zana za kisasa na si jembe la mkono kama ilivyozoeleka.

Wakati mtangazaji akiendelea kuongea, muziki ulikuwa ukisikika kwa mbaali na kumfanya awe kama anaongea kwa kufuata mapigo ya muziki kwa haraka haraka,

ilivutia kwa kweli na

Watu wote katika gari tulifurahia mazungumzo ya watangazaji waliokuwa wanaendesha kipindi ila mimi waliniudhi kitu kimoja, hawakuwa wakimalizia hadi mwisho. Huyu akiongea jambo kidogo mwingine anaingilia kati na hoja nyingine tofauti.

Nadhani hayo yameeleweka, haswaa kabisa ingawa inabidi ufafanuzi zaidi. Mtangazaji wa kwanza alimalizia na wa pili akaitikia.

Konda shusha, shusha bwana mmenipitilizisha kituo. Mtu mmoja alipaza sauti na kuufanya utulivu uliokuwa ndani kuisha. Kuna mama Jirani na siti niliyokuwa nimekaa alishituka!.

Katika redio mtangazaji akaendelea…

Na sasa tuelekee katika hoja ambayo ndio msingi mkuu wa kipindi hiki, pamoja na yote hayo niliyoyaeleza, kuna baadhi ya vijana bado wanawaza namna ya kujikomboa kutoka katika lindi la umasikini kama nilivyosema mwanzo.

…mtangazaji wa kwanza alimaliza kuongea na wa pili akadakia.

Katika kundi hilo kuna kila aina ya vijana; kuna waliosoma na kutunukiwa vyeti, stashahada, shahada na shahada za juu, huku wengine wakiwa ni mbumbumbu kabisa kwa maana hawakwenda shule na kuna walioishia darasa la tatu, tano na la saba.
Kimsingi, wako tofauti lakini linapokuja suala la kuukimbia umasikini fikra zao zina fanana kwa kiwango kikubwa kwani mawazo yao makuu yanawiana kwa namna moja ama nyingine.

Kwa nini unasema hivyo?? Mtangazaji wa pili alisikika akiuliza…

Kwa mfano, kuna kijana anayehitaji mtaji wa Shilingi milioni mbili ili aweze kufanya biashara zitakazomsaidia kupunguza hali ngumu ya maisha aliyonayo, na wakati huyo akiwa hivyo kuna kijana mwingine anahitaji Shilingi elfu tano tu, ili aende Tandale kununua mahindi mabichi ambayo atakuja nayo mtaani tayari kwa kuyachoma kisha ayauze.

Kwa kweli ndugu msomaji hoja zilizokuwa zinatolewa na watangazaji zilikuwa za maana sana. Lakini, ah. Maisha yangu tangu nimezaliwa yalikuwa ya taabu sana,

hata hivyo maisha ya kijijini ni tofauti na hapa mjini hata utakuwa na elimu na huku upo kijijini.

kwanza yawezekana hawa watangazaji wamezaliwa hapa hapa mjini na kusomea hapa hapa kwa hiyo sehemu kubwa ya maisha yao hawana picha ya kijijini kukoje, hakuna umeme, tunapikia kuni na mafiga, usafiri mkubwa ni miguu.

Mawazo yaliendelea kupita kichwani huku redio ikiendelea kutoa habari.

…kama nilivyosema mwanzo kwamba fikra zao zinafanana ila michakato na michanganuo yao ndio inatofautiana, kwani mmoja anahitaji mtaji mkubwa ili aweze kuendesha shughuli zake wakati mwingine anahitaji mtaji mdogo ili naye aendeshe shughuli zake.

Hata hivyo, mtangazaji akaendelea tena. katika kundi lolote lile la vijana iwe wasichana au wavulana kuna ambao hawataki kusubiri, wenyewe kila wakati wana haraka, wanataka wafanikiwe na wafikie kilele kama ilivyo kwa matajiri wengine.

Wakati hoja zikiendelea kumwagwa na watangazaji mtu mmoja ndani ya daladala nililokuwa nimepanda pasipo kutambua kuwa yupo ndani ya gari tena daladala akapaza sauti na kuitikia;

…ni kweli ndugu mtangazaji! ni kweli kabisa unayosema ni kweli mnaakili sana nyie. Watu wote wakageuka kumwangalia huku wengine wakiangua vicheko, ni kama vile alikuwa mgeni mjini Dar es salaam. Redio ikaendelea.

Hawataki kudunduliza, na hawaiamini ile falsafa kwamba kabla ya mafanikio binadamu yeyote yule huwa anapitia katika tanuri lenye shida na vikwazo chungu nzima, ambavyo wakati mwingine vinakatisha tama.

Kikubwa kinachowafanya watumbukie huko ni tamaa za nafsi zao, na msukumo huo wanakuwa nao kwa kuwa wanataka utajiri wa haraka haraka kama nilivyosema mwanzo.

Moja kati ya tamaa hizo ambazo karibia vijana wengi wanayo ni ile ya kutaka kushika na kumiliki usukani wa motokari, wakati hawana uwezo hata wa kumiliki mkweche wa baiskeli.Na kwa kuwa hawana nyenzo na vyanzo vya kujipatia utajiri wanaoutaka, hatimaye wanajikuta wanakuwa wezi, majambazi, matapeli, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya, machangudoa na makahaba walioshindikana.

Hakuna ubishi katika hilo, kwani kwa sasa kuna vijana wengi wapo magerezani ndani na nje ya nchi kwa sababu ya tamaa za kutaka utajiri wa njia ya mkato, na wengi wapo katika Magereza yanayopatikana nchi nzima.

Kila kijana katika kundi hilo anatumikia muda wake wa kifungo baada ya kuhukumiwa, na wengine bado ni mahabusu na kesi zao zinaendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali.

Mbali na hao, kuna wanaotumikia vifungo katika magereza yaliyopo nje ya nchi baada ya kubainika kuwa ni wasambazaji wa dawa za kulevya na wengine baada ya kuwa matapeli, hakika idadi yao ni kubwa.

Kuna wasichana ambao leo hii wanateseka vitandani baada ya kuathirika na Ukimwi, na wengine bado wanaendelea kudunda kutokana na kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi.

Katika kundi hilo, kuna baadhi ya wasichana waliopata virusi hivyo kutokana tamaa za kutaka kuishi maisha ya gharama na fahari kubwa, kwa hiyo wakalazimika kufanya ngono na wanaume wenye fedha ambao ni waathirika.

Wapo walioathirika baada ya kufanya ngono na watu ambao hawana fedha za kutisha, bali walijiingiza katika mahusiano na watu hao pengine kwa bahati mbaya au kwa sababu ya vishawishi vidogo vidogo, huku wengine wakiwa wameathirika na Ukimwi baada ya kufanya biashara ya uchangudoa katika maeneo mbalimbali.

Baada ya kusadifu yote hayo, nahitimisha kwa kuwaomba vijana wenzagu, na watanzania wenzangu kwamba pamoja na haraka waliyonayo kuna haja ya kusubiri na waitazame Serikali kama kweli itatekeleza na kutimiza maazimio yake hata kama itatugharimu miaka mingi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni