Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatano, Mei 25, 2016

MCHUCHUMIO (HIGH HEELS)


Wengi hawafahamu kuwa ni Viatu hatari kwa afya ya miguu ya wanawake japo pia wapo wanaofahamu hilo ila wanakaidi tu. ‘Mchuchumio’ ama viatu vyenye visigino virefu, ni mojawapo ya vitu vinavyopendwa na baadhi ya wanawake mbalimbali, si katika Tanzania bali dunia nzima.

Wataalamu wanaeleza kuwa viatu hivi huharibu pingili za uti wa mgongo na huvunjavunja mifupa ya visigino. Wanawake wenye maumbo ya kati, ambao si wanene wala wembamba wamekuwa wakipendelea viatu virefu. Kwa kiasi kikubwa wasichana wafupi, wamekuwa wakipendelea kuvaa viatu virefu ili angalau na wao waonekane warefu ingawa vinawatesa.

Kuna maelezo yanayosema kuwa viatu virefu vinaharibu visigino na misuli ya miguu na kutengeneza vigimbi ambavyo baadaye husababisha maumivu makali. Wasichana wengi wanafahamu ‘mchuchumio’ husababisha maumivu makali lakini je, ndiyo kutimiza usemi wa ukitaka uzuri shurti udhurike? Kwa kawaida, urembo hauwezi kusababisha maumivu, lakini kuvaa viatu virefu kuna athari kubwa.

Utafiti mbalimbali unaonesha kuwa viatu virefu havifai hata kidogo. Kimsingi, uvaaji wa viatu virefu husababisha maumivu makali ya misuli ya miguu pamoja na nyama za nyuma kwenye maungio ya magoti na enka. Uharibifu ni mkubwa pia huweza kutokea ndani ya magoti kwa kuhamisha maungio (dislocate). Kwa jinsi mhusika anapovaa viatu virefu kwa muda mrefu, ndipo inaposababisha madhara ya muda mrefu.



Mbali na hayo, vilevile, husababisha mwili kukosa usawa wakati wa kutembea, misuli ya miguu kubana, kupoteza mwelekeo wa mwendo halisi na wakati mwingine husababisha mhusika kuanguka na kumsababishia maumivu makali. Katika uchunguzi uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Applied Physiology, Dk Cronin anasema wanawake wengi waliofanyiwa utafiti wamebainika kutokuwa imara katika miguu yao, kupatwa na maumivu makali na kuharibiwa misuli na enka ya mguu.

Naye Dk Orly Avitzur, Mganga Mshauri kwenye kitongoji cha Tarrytown, New York, Marekani anasema kuwa alifanya utafiti kwa wanawake wa zaidi ya miaka 40 kuwa hawawezi kuvaa viatu virefu kwa kuwa miguu yao tayari imeharibiwa. Katika uchunguzi uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Applied Physiology, Dk Cronin anasema wanawake wengi waliofanyiwa utafiti wamebainika kutokuwa imara katika miguu yao, kupatwa na maumivu makali na kuharibiwa misuli na enka ya mguu.

Mtaalamu wa Mifupa katika Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam, Dk Edemeza Machange alieleza kuwa matatizo ni makubwa kwa mtumiaji wa viatu virefu na athari zaidi huwakumba wanawake wanene. “Ni mbaya sana…kwa wanawake wanene haishauriwi watumie viatu virefu kwa kuwa vitawaletea matatizo mengi katika miili yao,” anasema.

“Kwa kawaida mtu anapoteza mwendo halisi, sasa kutotembea kwa mpangilio, huharibu mfumo wa pingili za mgongo, hata kiuno na kusababisha maumivu makali”. Anawashauri kinamama hasa wasichana, wafahamu kuwa pamoja na kutaka urembo, lazima wajali afya zao kwa kuvaa viatu virefu katika kipindi kifupi na zaidi ni kuangalia madhara kwa baadaye kuliko kukimbilia kuvaa viatu virefu kwa ajili ya urembo.

Chanzo: Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni