Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Mei 24, 2016

Kichwa cha Kigogota Kinachohimili Mshtuko

Photo Credit By: www.popsci.com
 

Msukumo unaozidi nguvu za uvutano kwa mara 80 hadi 100 unaweza kukufanya upoteze fahamu. Hata hivyo, kigogota anaweza kuhimili msukumo unaozidi nguvu za uvutano kwa mara 1,200 hivi anapopigapiga mti kwa mdomo wake. Ndege huyo anafanyaje kazi hiyo, bila kupoteza fahamu au hata kupata maumivu ya kichwa? 

Fikiria hili:  

Watafiti wamegundua sehemu nne za kichwa cha kigogota zinazofanya kichwa chake kiweze kuhimili mshtuko huo:

1. Ana mdomo wenye nguvu lakini unaonyumbulika
2. Ana kitu kinachoitwa hyoid kilichofanyizwa kwa mfupa na tishu inayoweza kutanuka kinachofunika fuvu la kichwa
3. Ana eneo fulani la mfupa ulio kama sifongo ndani ya fuvu
4. Ana nafasi ndogo kati ya fuvu na ubongo iliyo na umajimaji unaofanana na ule unaopatikana kwenye uti wa mgongo

Kila moja ya sehemu hizo huhimili mshtuko, na kumwezesha kigogota kuugonga mti mara 22 hivi kwa sekunde bila kuumiza ubongo wake.

Wakichochewa na muundo wa kichwa cha kigogota, watafiti wametokeza kifaa fulani kinachoweza kuhimili msukumo unaozidi nguvu za uvutano kwa mara 60,000. Huenda hilo likawawezesha kutokeza vifaa bora zaidi kutia ndani, vile vinavyolinda vifaa vya kurekodia jinsi ndege inavyoruka, ambavyo kwa sasa vinaweza kuhimili msukumo unaozidi nguvu za uvutano kwa mara 1,000 tu. 

Kim Blackburn, injinia katika Chuo Kikuu cha Cranfield huko Uingereza, anasema kwamba mambo ambayo yamegunduliwa kuhusu kichwa cha kigogota yanatoa “mfano mzuri wa jinsi vitu vya asili vinavyoweza kutusaidia kutokeza miundo tata na pia kutatua mambo ambayo hapo awali yalionekana kuwa hayawezi kutatuliwa.”

Una maoni gani?  

Kichwa cha kigogota kinachoweza kuhimili mshtuko kilijitokeza chenyewe? 

Au kilibuniwa?

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni