Wengi hawafahamu kuwa ni Viatu hatari
kwa afya ya miguu ya wanawake japo pia wapo wanaofahamu hilo ila
wanakaidi tu. ‘Mchuchumio’ ama viatu vyenye visigino virefu, ni mojawapo
ya vitu vinavyopendwa na baadhi ya wanawake mbalimbali, si katika
Tanzania bali dunia nzima.
Wataalamu wanaeleza kuwa viatu hivi
huharibu pingili za uti wa mgongo na huvunjavunja mifupa ya visigino.
Wanawake wenye maumbo ya kati, ambao si wanene wala wembamba wamekuwa
wakipendelea viatu virefu. Kwa kiasi kikubwa wasichana wafupi, wamekuwa
wakipendelea kuvaa viatu virefu ili angalau na wao waonekane warefu
ingawa vinawatesa.
Kuna maelezo yanayosema kuwa viatu virefu
vinaharibu visigino na misuli ya miguu na kutengeneza vigimbi ambavyo
baadaye husababisha maumivu makali. Wasichana wengi wanafahamu
‘mchuchumio’ husababisha maumivu makali lakini je, ndiyo kutimiza usemi
wa ukitaka uzuri shurti udhurike? Kwa kawaida, urembo hauwezi
kusababisha maumivu, lakini kuvaa viatu virefu kuna athari kubwa.
Utafiti mbalimbali unaonesha kuwa viatu virefu havifai hata kidogo.
Kimsingi, uvaaji wa viatu virefu husababisha maumivu makali ya misuli ya
miguu pamoja na nyama za nyuma kwenye maungio ya magoti na enka.
Uharibifu ni mkubwa pia huweza kutokea ndani ya magoti kwa kuhamisha
maungio (dislocate). Kwa jinsi mhusika anapovaa viatu virefu kwa muda
mrefu, ndipo inaposababisha madhara ya muda mrefu.
Mbali na hayo,
vilevile, husababisha mwili kukosa usawa wakati wa kutembea, misuli ya
miguu kubana, kupoteza mwelekeo wa mwendo halisi na wakati mwingine
husababisha mhusika kuanguka na kumsababishia maumivu makali. Katika
uchunguzi uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Applied Physiology,
Dk Cronin anasema wanawake wengi waliofanyiwa utafiti wamebainika
kutokuwa imara katika miguu yao, kupatwa na maumivu makali na kuharibiwa
misuli na enka ya mguu.
Naye Dk Orly Avitzur, Mganga Mshauri
kwenye kitongoji cha Tarrytown, New York, Marekani anasema kuwa alifanya
utafiti kwa wanawake wa zaidi ya miaka 40 kuwa hawawezi kuvaa viatu
virefu kwa kuwa miguu yao tayari imeharibiwa. Katika uchunguzi
uliochapishwa kwenye jarida la Journal of Applied Physiology, Dk Cronin
anasema wanawake wengi waliofanyiwa utafiti wamebainika kutokuwa imara
katika miguu yao, kupatwa na maumivu makali na kuharibiwa misuli na enka
ya mguu.
Mtaalamu wa Mifupa katika Hospitali ya TMJ, Dar es
Salaam, Dk Edemeza Machange alieleza kuwa matatizo ni makubwa kwa
mtumiaji wa viatu virefu na athari zaidi huwakumba wanawake wanene. “Ni
mbaya sana…kwa wanawake wanene haishauriwi watumie viatu virefu kwa kuwa
vitawaletea matatizo mengi katika miili yao,” anasema.
“Kwa
kawaida mtu anapoteza mwendo halisi, sasa kutotembea kwa mpangilio,
huharibu mfumo wa pingili za mgongo, hata kiuno na kusababisha maumivu
makali”. Anawashauri kinamama hasa wasichana, wafahamu kuwa pamoja na
kutaka urembo, lazima wajali afya zao kwa kuvaa viatu virefu katika
kipindi kifupi na zaidi ni kuangalia madhara kwa baadaye kuliko
kukimbilia kuvaa viatu virefu kwa ajili ya urembo.
Chanzo: Mwananchi