Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe
(Mb.) atafanya ziara ya kikazi ya siku tano katika Jamhuri ya Watu wa
China kuanzia tarehe 24 hadi 28 Februari, 2014. Ziara ya Mhe. Membe
inakuja kufuatia mwaliko kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya
Watu wa China, Mhe. Wang Yi.
Mhe.
Membe anafanya ziara hiyo nchini China kwa lengo la kuimarisha uhusiano
wa kirafiki uliopo kati ya Tanzania na China. Wakati wa ziara hiyo,
Mhe. Membe atafuatana na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Ziara
hii pia ni muendelezo wa maeneo ya utekelezaji baada ya ziara ya Rais
wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping aliyoifanya hapa nchini
tarehe 24 na 25 Machi, 2013 na baadaye ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda nchini China mwezi
Oktoba, 2013.
Akiwa
nchini China, Mhe. Membe atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake
Mhe. Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa China tarehe 25 Februari 2014.
Siku hiyo hiyo Mhe. Membe atamtembelea Makamu wa Rais wa China, Mhe. Li
Yuanchao kwa lengo la kumsalimia na baadaye atafanya mazungumzo rasmi na
Waziri wa Biashara wa China, Mhe. Gao Hucheng.
Aidha,
tarehe 26 Februari, 2014 Mhe. Membe atatembelea Makao Makuu ya Kampuni
ya Poly Technologies yaliyopo katika mji wa Shenzhen na kujionea
shughuli mbalimbali zinazofanywa na Kampuni hiyo kabla ya kutembelea
Makao Makuu ya Kampuni ya China Merchant Holdings International ambako
atapokea taarifa ya maandalizi ya kuanza kwa mradi wa Ujenzi wa Bandari
katika eneo la Mbegani huko Bagamoyo.
Mhe.
Membe pia atapata fursa ya kutembelea Kampuni ya HUAWEI ili kujionea
shughuli mbalimbali. Kampuni ya HUAWEI ina Mkataba na Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi ya hapa nchini kuhusu Elimu kwa Njia ya Mtandao
(e-Education) kwa Shule za Sekondari.
Vile
vile tarehe 27 Februari, 2014, Mhe. Membe atautembelea Mji maarufu wa
biashara wa Guangzhou na kukutana na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi
mjini hapo. Mhe. Membe atatoa taarifa kuhusu hali ya uchumi, siasa na
masuala ya jamii yalivyo hapa nchini kwa sasa pamoja na kutoa taarifa ya
maendeleo ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba.
Waziri Membe pia atatembelea Eneo la Viwanda la Huadu tarehe 28 Februari, 2014 kabla ya kurejea nchini tarehe 1 Machi, 2014.
IMETOLEWA NA: KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI, WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA, DAR ES SALAAM.
24 FEBRUARI, 2014
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni