Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Januari 28, 2014

RAIA WALAANI JARIBIO LA AL-SHABAAB KUHUSU INTERNET

Wasomali wanaperuzi intaneti katika mkahawa mjini Mogadishu. [Na Majid Ahmed/Sabahi]

Jaribio la al-Shabaab kupiga marufuku mkonga wa mawasiliano na huduma za mtandao wa intaneti limekumbana na hasira kali kutoka kwa raia wa Somalia na kuchochea onyo kali kutoka kwa serikali.
Katika taarifa iliyochapishwa siku ya tarehe 8 Januari kwenye mtandao wa Somalimemo, al-Shabaab ilitangaza kupiga marufuku intaneti wakiamuru kampuni za simu kuacha kutoa huduma ya intaneti ndani ya siku 15.

Taarifa hiyp pia ilionya kwamba kampuni na watu wasiofuata amri hiyo watachukuliwa kama maadui na kuadhibiwa chini ya sharia.
Al-Shabaab ilihalalisha tangazo lake la marufuku kwa kusema kwamba mashirika ya kijasusi wa Kimagharibi, hasa mashirika ya Marekani na Uingereza, yanatumia intaneti kukusanya taarifa dhidi ya mujahidina.

"Intaneti ya kwenye simu ni hatari kwa kila Muislamu kutumia huduma hiyo [kwani] inamruhusu adui kujua harakati za watu na kukusanya taarifa," lilisema tamko hilo.

"Intaneti ya kwenye simu ni hatari zaidi kwa usalama wa Waislamu wanaopigana na maadui waliokuja, kwa sababu inaongeza fursa ya majasusi [wao] kusambaza taarifa za kijasusi kuhusiana na mujahidina kwa mashirika ya kijasusi yaliyopo nchini," ilisema.

Taarifa hiyo ya al-Shabaab ilisema pia intaneti kwenye simu ya mkononi ilikuwa hatari kwa watoto na vijana ambao wanapata na kusambaza mambo yanayokwenda kinyume na misingi ya Uislamu. Kuendelea kutumia intaneti kwa vijana kutapelekea wawe na "tabia mbaya, ukosefu wa elimu na kupoteza wakati," ilisema taarifa hiyo.

Al-Shabaab iko kwenye shinikizo inayoongezeka

Al-Shabaab ina hofu kubwa na inayoongezeka juu ya huduma za kisasa, ambazo zimelipelekea kundi hilo kufanya uamuzi wa kiholela sana, alisema Abdi Aynte, mkurugenzi wa taasisi ya sera ya Heritage Institute for Policy Studies mjini Mogadishu.

"Wanaogopa kwamba simu zenye huduma ya intaneti zitatumika kuwasiliana na mashirika ya kijasusi ya kimataifa ambayo yanawawinda wapiganaji wa al-Shabaab, hasa ndege zisizo na rubani, ambazo zimepunguza kwa kiasi kikubwa pirika za viongozi wa al-Shabaab," aliiambia Sabahi.

Aynte alisema sababu nyengine ya uamuzi huo wa al-Shabaab ilikuwa ni kampeni yake ya kuwazuia wananchi kupata habari za kilimwengu.

Katika siku za karibuni, al-Shabaab imepiga marufuku upatikanaji wa taarifa muhimu kwenye maeneo inayoyadhibiti, kama vile marufuku yake dhidi ya kuangalia televisheni na unyanyasaji wake dhidi ya raia wanaotumia simu za kisasa.

"Wanataka kuwazuia watu kuishi kwenye ardhi wanazozikalia kuzungumzia ugumu wanaokabiliana nao na kuuwambia ulimwengu juu ya dhila ambayo [al-Shabaab] wanawasabishia," alisema Aynte. "Intaneti inawapa watu uhuru wa kupata habari na al-Shabaab iko dhidi ya uhuru."

Alisema inawezekana pia kwamba al-Shabaab inataka kuchopoa fedha kutoka kwenye kampuni za simu kwa mabadilishano ya kuondosha marufuku ya intaneti.

Aynte alisema hafikirii kuwa marufuku hiyo itatekelezwa kwenye maeneo yasiyo chini ya udhibiti wa al-Shabaab.

Mwezi Novemba, kampuni ya simu ya Liquid Telecommunications ilitangaza mkonga wake wa kwanza wa mawasiliano ndani ya Somalia. Mkonga huo unavuka mpaka wa Kenya na Somalia, na kisha kuunganisha na mtandao wa Hormuud Telekom, unaoongeza kasi ya intaneti katika eneo lote la kusini na kati ya Somalia.

Abdirahman Yusuf al-Adala, mkurugenzi wa idara ya vyombo vya habari katika Wizara ya Habari, Posta na Mawasiliano ya Simu, alisema kwamba jaribio la al-Shabaab kuzuia upatikanaji wa intaneti ya njia ya mkonga litashindwa kwa sababu serikali ilileta huduma hii nchini Somalia na itailinda. 

Hata hivyo, alisema kuwa vitisho vya al-Shabaab vingeweza kuathiri maisha ya watu wanaotumia intaneti jongevu na wanaoishi katika udhibiti wa wanamgambo. 

"Watu wanatumia intaneti kwa ajili ya biashara, elimu, kupata habari, na watayakosa hayo. Tatizo jengine ambalo litasababishwa na suala hili ukosefu wa ajira ambao watu wanaofanyakazi kama watoaji hduma za intaneti," al-Adala aliiambia Sabahi. "Makampuni yana chaguo la kupoteza biashara zao na kwa hivyo kukabiliana na kufilisika, au kudharau amri ya al-Shabaab na kugeuka kuwa lengo la mashambulizi holela ya al-Shabaab." 

Katika kujibu jaribio la al-Shabaab la kupiga marufuku intaneti, Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa alisema itachukua hatua za kupambana na mbinu mpya za al-Shabaab. 

"Wasomali, kama walivyo watu wengine popote pale, wanatuia intaneti kwa ajili ya elimu na kuifikia jamii ya kimataifa ili kupata habari za dunia. Hatutaruhusu wananchi wetu kunyimwa kupata intaneti na kutumia smartphones," Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Taifa Abdikarim Hussein Guled alisema hapo tarehe 11 Januari.

"Serikali ya Somalia itafanya kazi na makampuni yote ya simu ili kuhakikisha uhuru wa kutoa intaneti kwa wananchi wetu, na serikali litafanya kila juhudi katika kulinda maslahi ya umma," alisema. 

Guled aliyaonya makampuni ya mawasiliano ya simu dhidi ya kufanya kazi na magaidi na alisema kwamba serikali ina dhamana ya kuwalinda wananchi wake. 

Makampuni ya mawasliano ya simu ambayo yanatoa huduma jongevu za intaneti hayajatoa kauli yoyote juu ya marufuku ya al-Shabaab na hayakujibu maombi ya Sabahi ya kutoa maoni.

Wananchi wapinga vikali marufuku ya intaneti ya al-Shabaab

Ahmed Mohamud, mwandishi wa habari mwenye umri wa miaka 27 anayefanya kazi na kituo cha redio chenye makao mjini Mogadishu, alisema kuwa alikuwa na matumaini kwamba upatikanaji wa intaneti nchini Somalia utaboreshwa kwa kuunganishwa na mkonga.

"Inanichukua muda mrefu kila mara ninapotaka kupata kitu kidogo chochote kile kutoka intaneti, lakini mkonga ni intaneti ya kasi kubwa sana ambayo inakuwezesha kupata kiasi kikubwa [cha data] kwa muda mdogo sana," aliiambia Sabahi.

Mohamud alisema kwamba njia pekee kwa watu wanaoishi katika maeneo yanayodhbitiwa na al-Shabaab kuwasiliana na dunia na kuwapa taarifa wengine ni kupitia intaneti jongevu. Lakini sasa, alisema, "watakuwa viziwi na vipofu." 

Abdi Ahmed Maalin, mkazi wa kitongoji cha Taleh cha Mogadishu mwenye umri wa miaka 27, alisema kuwa marufuku ya intaneti ya al-Shabaab itakuwa ni ushahidi zaidi kwamba kikundi hiki kiko kinyume na maendeleo na kuboresha maisha ya watu. 

Maalin anayo digirii ya kwanza katika sayansi ya siasa kutoka Chuo Kikuu cha Mogadishu na alikuwa akijitayarisha kujiandikisha na programu ya diplomasia ya kimataifa mtandaoni katika Chuo Kikuu cha Kampala.

"Uamuzi wa al-Shabaab inamaanisha kuwa hakuna elimu kwa ajili yangu," alisema. "Wanasema wanapambana dhidi ya adui, lakini ukweli ni kwamba wao ndio maadui." 

Maalin alisema kwamba matendo yanayoongezeka kwa matendo makali ya al-Shabaab yanatoa wito kwa umma kupambana kukishinda kikundi hiki. 

"Hapo awali tulijua kuwa waliwagawa watu katika makundi mawili: kikundi kinachoishi chini yao ambacho wanakinyanyasa na kikundi ambacho wamekipa jina la makafiri na wanakiuwa," alisema. "Kile wanachofanya sasa kuyafanya watu walio hai wawe wamekufa." 

"Je, tunawasubiri waidai kioa familia itoe mtu mmoja wamle? Hiki ni kikundi kidogo, kwa hivyo tukivamie mara ili tuweze kujikomboa wenyewe dhidi yao," Maalin alisema. "Hatuwezi kusubiri kwa hatua za kijeshi." 

CHANZO: http://sabahionline.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni