Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatatu, Januari 27, 2014

MASHAMBULIZI NA USALAMA WA KOMPYUTA

Picha kwa hisani ya www.cybersecurepakistan.com


Hebu wazia kundi la wahalifu wenye ustadi wa kutumia kompyuta wakitumia Intaneti kuongoza mitandao ya kompyuta walizoteka nyara. Kompyuta hizo zinazojulikana kama botnets (mitandao ya roboti), zinatoa habari za siri zenye madhara zinazolenga taifa fulani. Baada ya dakika chache, Tovuti za kijeshi, kifedha, na kibiashara za taifa hilo zinaacha kufanya kazi. Mashine za benki za kutolea pesa (ATM) pamoja na mitandao ya simu inashindwa kufanya kazi. Usafiri wa ndege unakatizwa na kompyuta pamoja na mifumo ya usalama katika kituo cha kutokeza nguvu za nyuklia inavurugwa. Watu wangetendaje? Wewe ungefanya nini?
Huenda tukio hilo likaonekana kuwa lisilo halisi. Lakini kulingana na Richard A. Clarke, aliyekuwa Msimamizi wa Kitaifa wa Usalama, Ulinzi wa Miundo-Msingi, na Kupambana na Ugaidi nchini Marekani, jambo kama hilo linaweza kufanyika kihalisi. Isitoshe, tayari kumekuwa na mashambulizi kupitia kompyuta Huenda hata wewe umewahi kushambuliwa.

Kwa nini mtu awashambulie wengine kupitia kompyuta? Mashambulizi hayo hufanywaje? Na kwa kuwa ni kawaida kwa mashambulizi hayo kumlenga mtu mmojammoja, unaweza kujilindaje unapotumia Intaneti?

Uwanja wa Vita Kwenye Kompyuta

Kuna sababu kadhaa zinazowafanya watu wawashambulie wengine kupitia kompyuta. Kwa mfano, magaidi au serikali zinaweza kupenya kwenye mitandao ya kompyuta ya maadui wao ili waibe siri au waharibu vifaa vinavyoongozwa na mitandao hiyo. Katika mwaka wa 2010, Waziri Msaidizi wa Ulinzi wa Marekani William J. Lynn wa Tatu alisema kwamba “maadui” wa kigeni walikuwa wamepenya mara nyingi kwenye mitandao ya kompyuta iliyo na habari za siri za Marekani na kuiba “maelfu ya mafaili . . . kutia ndani maagizo ya kutengenezea silaha, habari kuhusu mipango ya kijeshi, na habari za upelelezi.”—Ona sanduku (LINK HAPO MBELE) “Mashambulizi ya Hivi Karibuni Kupitia Kompyuta.”

Wahalifu wanaotumia kompyuta hutumia njia sawa na hizo kuiba habari za kitaaluma au za kifedha kutoka kwa mitandao ya kompyuta ya makampuni na hata kompyuta za watu binafsi. Wahalifu hupata mabilioni ya dola kila mwaka kupitia biashara za ulaghai zinazofanywa kwenye mitandao.

Pia, wahalifu hao wameunganisha kompyuta nyingi sana walizoteka nyara ili waweze kutekeleza mashambulizi yao. Katika mwaka wa 2009, kampuni moja inayoshughulika na usalama wa intaneti iligundua kwamba kundi moja la “wahalifu” lilikuwa likidhibiti kisiri karibu kompyuta milioni mbili kotekote ulimwenguni, nyingi zikiwa ni za watu binafsi. Ripoti ya karibuni ya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) linakadiria kwamba kompyuta 1 kati ya 3 zilizounganishwa kwenye Intaneti inadhibitiwa kisiri na mhalifu fulani. Namna gani kuhusu kompyuta yako? Je, mtu fulani anaweza kuidhibiti bila wewe kujua?

Maadui Wanaoshambulia Kimyakimya

Wazia tukio hili. Mhalifu fulani anasambaza programu fulani yenye madhara kupitia Intaneti. Programu hiyo inapoingia katika kompyuta yako, inapenya ndani ya programu inayolinda kompyuta yako. Programu hiyo yenye madhara inapopata eneo ambalo halijalindwa vizuri, inapenya ndani hata zaidi na kutafuta-tafuta habari muhimu katika kompyuta yote.

 Kisha programu hiyo inaweza kubadilisha au kufuta mafaili yaliyo kwenye kompyuta yako, na inajituma yenyewe kama barua pepe kwenye kompyuta zingine, au kumtumia mhalifu huyo neno lako la siri la utambulisho, habari za kifedha, au habari nyingine za siri zinazokuhusu.

Wahalifu hao wanaweza kukufanya uingize virusi kwenye kompyuta yako mwenyewe! Jinsi gani? Unaweza kufanya hivyo kwa kufungua barua-pepe inayoonekana kuwa ya kawaida tu, kwa kubonyeza kiunganishi cha Tovuti fulani, kupakua na kuunganisha programu ya bure ya kompyuta, kuingiza kifaa cha kuhifadhi habari kilicho na virusi katika kompyuta yako, au tu kutembelea Tovuti yenye kutiliwa shaka. Mambo yote hayo yanaweza kuingiza programu yenye madhara kwenye kompyuta yako na kuifanya idhibitiwe kisiri na mhalifu.

Unaweza kujuaje ikiwa kompyuta yako imeshambuliwa? Kwa kweli inaweza kuwa vigumu kugundua. Huenda kompyuta au Intaneti ikafanya kazi polepole sana, au programu zisitende kwa njia ya kawaida, au visanduku vijitokeze ghafula vyenye ujumbe unaokuomba uunganishe programu fulani, au kompyuta yako itende kwa njia isiyo ya kawaida. Ukiona mojawapo ya dalili hizo, mwombe mtaalamu wa kompyuta achunguze kompyuta yako.

‘Fikiria Hatua Zako’

Kadiri mataifa na watu mmoja-mmoja wanavyozidi kutegemea teknolojia ya kompyuta, ndivyo inavyotarajiwa kuwa mashambulizi kupitia kompyuta yataongezeka. Kwa sababu hiyo, mataifa mengi yanajitahidi sana kuboresha mbinu za kulinda kompyuta zao, na mataifa mengine yanapima uwezo wa mitandao yao ya kompyuta ili kuona ikiwa inaweza kustahimili mashambulizi. Lakini licha ya jitihada hizo, Steven Chabinsky, mtaalamu wa cheo cha juu wa usalama wa kompyuta wa Shirika la Upelelezi la Marekani anasema kwamba “adui aliyeazimia kabisa, hawezi kamwe—kamwe—kushindwa kupenya mfumo hususa anaolenga iwapo atakuwa na wakati wa kutosha, kichocheo, na pesa.”

Unaweza kufanya nini ili ujilinde unapotumia Intaneti? 

Ingawa huenda usiweze kujilinda kabisa unapotumia Intaneti, unaweza kuchukua hatua zifaazo ili kufanya kompyuta yako iwe salama zaidi. (Ona sanduku “Jilinde!”) Biblia inasema: “Mtu mwerevu huzifikiria hatua zake.” (Methali 14:15) Kwa kweli hilo ni shauri lenye hekima unapotumia Intaneti!


Mashambulizi kupitia kompyuta yamekusudiwa hasa kubadilisha, kukatiza, au kuharibu kabisa mifumo ya kompyuta au mitandao au habari au programu ambazo kompyuta huhifadhi au kusambaza.—Baraza la Kitaifa la Utafiti la Marekani linaeleza.

Katika mwaka wa 2011, wahalifu wa kutumia kompyuta wangeweza kutumia zaidi ya udhaifu 45,000 unaojulikana ili waweze kupenya katika kompyuta nyingine. Kwa kutumia udhaifu huo, wahalifu hao wanaweza kuingiza programu yenye madhara (malware) katika kompyuta za watu binafsi bila watu hao kujua.


Wahalifu wa kutumia kompyuta wameunganisha kompyuta nyingi sana walizoteka nyara. Kulingana na shirika la OECD, kompyuta 1 kati ya 3 zilizounganishwa kwenye Intaneti, inadhibitiwa kisiri na mhalifu fulani


MASHAMBULIZI YA HIVI KARIBUNI KUPITIA KOMPYUTA

  2003: Programu ya kompyuta yenye madhara inayoitwa Slammer ilisambaa haraka sana kwenye Intaneti na kushambulia kompyuta 75,000 hivi kwa dakika kumi tu. Utendaji wa Intaneti ukawa wa polepole sana, Tovuti zikaacha kufanya kazi, mashine za benki za kutolea pesa (ATM) zikashindwa kufanya kazi, usafiri wa ndege ukakatizwa, na kompyuta pamoja na mifumo ya usalama katika kituo cha kutokeza nguvu za nyuklia ikavurugwa.

  2007: Mfululizo wa mashambulizi kupitia kompyuta ulilenga Estonia na kuathiri mifumo ya serikali hiyo, vyombo vya habari, na hata benki. Mengi ya mashambulizi hayo yaliyotoka kwenye mifumo ya kompyuta zilizotekwa nyara (botnets) yaliathiri kompyuta zaidi ya milioni moja zilizoshambuliwa katika nchi 75 kwa kuzifanya zitume ujumbe mwingi wa uwongo wa kuomba habari.

  2010: Programu ya kompyuta yenye madhara na tata sana inayoitwa Stuxnet ilishambulia mifumo inayoendesha kituo cha kutokeza nguvu za nyuklia nchini Iran.


Programu za kompyuta zenye madhara hujinakili zenyewe kutoka kompyuta moja hadi nyingine kupitia Intaneti na programu za aina hiyo hupewa majina kama vile Slammer.

JILINDE!

 1. Weka programu za kuzuia virusi (antivirus), programu za kutambua programu za upelelezi (spyware-detection), na mfumo wa ulinzi (firewall) katika kompyuta yako. Hakikisha kwamba programu hizo pamoja na programu kuu ya kuendesha kompyuta yako inaboreshwa kwa ukawaida.

 2. Fikiria kwa uzito kabla ya kufungua viunganishi (links) au viambatanisho (attachments) vinavyotumwa kwenye barua-pepe au ujumbe wa haraka—hata ule unaotoka kwa marafiki. Jihadhari hasa ikiwa ujumbe huo unatoka kwa mtu usiyemfahamu na unaomba habari za kibinafsi au neno la siri.

 3. Usinakili au kutendesha programu za kompyuta kutoka katika vyanzo usivyovijua.

 4. Tumia neno ya siri la utambulisho lenye angalau herufi nane na utie ndani namba na ishara kadhaa, na uwe na zoea la kubadili neno hilo kwa ukawaida. Tumia maneno tofauti-tofauti ya siri kwa ajili ya kila akaunti yako.

 5. Fanya biashara kwenye Intaneti na mashirika yenye kuaminika ambayo yana mifumo salama.

 6. Usitoe habari zako za siri au za akaunti zako unapotumia vifaa ambavyo havijaunganishwa kwa nyaya [Wi-Fi], kama vile vinavyopatikana katika sehemu za umma.

 7. Zima kompyuta yako wakati ambapo huitumii.

 8. Uwe na kawaida ya kunakili habari zako, na uzihifadhi mahali salama.


Vituo vya intaneti salama vina ishara fulani, kama vile ishara ya kufuli na “https://” kwenye kisanduku cha anwani. Herufi “s” inamaanisha salama (secure).

Fanya yote uwezayo ili kujilinda unapotumia Intaneti

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni