Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatano, Februari 20, 2013

TEKNOHAMA - UTUNZAJI WA SOFTWARE NDANI YA KOMPYUTA


Photo credit by: http://www.wipro.com

 
Kifaa kifahamikacho kama hard disk (ukanda sumaku kwa lugha ya Kiswahili) ndicho ambacho hutunza software katika kompyuta. Kifaa hiki hutunza kumbukumbu zote zinazohusiana na habari zote tangu zilipotengenezwa isipokuwa kama zikifutwa na mtumiaji. System software na application software zote hutunzwa ndani ya kifaa hiki. Zote hizi huonekana kama mkusanyiko wa mafaili (files) ambayo huwa na majina maalum kulingana na kazi inayofanya. Mafaili haya huwa yamepangiliwa katika mfumo maalum unaorahisisha mawasiliano na kuondoa muingiliano. Kama ambavyo unaweza kutunza maji ndani ya pipa lenye ujazo wa lita mia tano, ndivyo ambavyo software hutunzwa katika hard disk na kuoneshwa kipimo chake ambacho hujulikana kwa jina la Bytes au kwa kifupi B. hii ina maana kuwa ndani ya hard disk kuna nafasi ambayo inaruhusu utunzaji wa data na habari pamoja na software.

Utunzaji wa data na habari katika hard disk huongozwa na maelekezo mama (system software) ambayo ndiyo hupanga ukubwa wa kila data au software nyingine na jinsi zitakavyokaa kulingana na matakwa ya mtumiaji. Kipimo cha Bytes kina vipimo vingine vikubwa vilivyo juu yake, kama ambavyo tumezoea kupima uzito kwa kutumia aidha gramu, kilogramu, na tani. Vivyo hivyo kuna vipimo vilivyo juu ya Byte na ambavyo ni Kilobyte, Megabyte, Gigabyte na Terabyte. Byte 1 ni sawa na kuhifadhi herufi au namba moja; yaani herufi kama A au F na namba kama 0 au 7 huchukua nafasi ya Byte 1 katika hard disk. Vipimo vingine hutokana na vipimo hivi:

Kilobyte 1 ni sawa na Byte 1000, Megabyte 1 ni sawa na Kilobyte 1000 na Gigabyte 1 ni sawa na Megabyte 1000. Kwa maana hiyo kadiri kipimo kinavyokuwa kikubwa inamaanisha kuwa kuna mafaili yenye ukubwa mkubwa katika kompyuta. Kwa maana hiyo kadiri hard disk inavyokuwa na nafasi kubwa ndivyo inavyokuwa na uwezo wa kutunza data. Kama ukienda dukani utaambiwa kuwa kompyuta hii ina hard disk yenye 120 GB kwa mfano au 40 GB. Kwa kawaida hapa anakuwa anazungumzia uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu wa kompyuta unayotaka kununua. Kumbuka kuwa hard disk hupimwa kwa kutumia kipimo cha Gigabyte au GB kwa kifupi. Hii inamaaniiha kuwa; kwa mfano; kompyuta yenye hard disk ya 40 GB ni sawa na 40,000 MB ambayo ni sawa na 40,000,000 KB au 40,000,000,000 Bytes. Hii ni sawa na kuweza kubeba herufi au namba bilioni 40!

Uhusiano kati ya RAM na Hard Disk
Software zote hutunzwa katika hard disk pindi kompyuta inapokuwa imezimwa. Hii ni pamoja na data zote ambazo mtumiaji amezihifadhi. Pindi unapowasha kompyuta unaziamuru software na data zote zilizotunzwa katika hard disk ziamke na kuanza kufanya kazi au kutumika. Data hizi na software zote huelekea mahala pengine kabisa nje ya hard disk ambako zinaweza kuonwa na kufanya kazi au kutumika kulingana na matakwa ya mtumiaji. Sehemu hii ambayo ni kama uwanja wa kufanyia kazi hufahamika kama Random access memory yaani sehemu ya kutunzia kumbukumbu na maelekezo yote yanayohusiana na ufanyaji kazi wa kompyuta. sehemu hii huhitaji umeme ili iweze kufanya kazi. Bila umeme data na software zote haziwezi kukaa mahali hapa na hurudi katika hard disk pindi umeme unapokatika au unapoizima kompyuta. kwa hiyo tunaweza kusema kuwa RAM ni kama sehemu ya kutunzia kumbukumbu na maelekezo yote kwa muda; kwa kimombo (temporary storage area).

Maoni 1 :

  1. Safi sana Bwana Mtayarishaji. Bila shaka wenye kuitafuta elimu hii ya kompyuta watakuwa wameelimika. Uwe na wakati mwema Mkuu.

    JibuFuta