Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Januari 22, 2013

Lamu Kisiwa Ambacho Kimedumu Bila Kubadilika



Na mleta habari wa AMKENI! kutoka KENYA.

UPEPO mwanana wenye chumvi ulipiga matanga ya turubai, na kusukuma mbele meli ndogo ya mbao. Juu kwenye sitaha, akishikilia mlingoti, mlinzi alitazama hadi upeo wa macho ili aone nchi kavu, akikaza macho yake kutazama tu Bahari ya Hindi. Ilikuwa karne ya 15 W.K., na mabaharia hawa walikuwa wanatafuta kisiwa cha Lamu.

Dhahabu, pembe za tembo, vikolezo, na watumwa—Afrika ilikuwa na vyote. Wakivutiwa na hazina za Afrika na hamu ya kuvumbua, wanaume jasiri walisafiri kwa mashua hadi kwenye pwani ya Afrika Mashariki kutoka nchi za mbali. Mabaharia walivumilia bahari zilizochafuka na pepo za ghafula wakitafuta hazina. Walifunga safari ndefu, wakiwa wamesongamana ndani ya meli za mbao.

Mabaharia hao pamoja na meli zao dhaifu walipata bandari yenye kina iliyokingwa na mwamba-tumbawe walipofika juu katikati ya pwani ya Afrika Mashariki, palipo na kikundi kidogo cha visiwa, jamii-visiwa ya Lamu. Walipofika hapa mabaharia hao waliweza kupakia upya merikebu zao maji safi na chakula.

Kufikia karne ya 15, kisiwa cha Lamu kilikuwa kituo cha kibiashara chenye mafanikio. Mabaharia Wareno waliofika katika karne ya 16 walikuta wafanya-biashara matajiri waliovalia vilemba vya hariri na kanzu kubwa-kubwa. Wanawake waliokuwa wakitembea-tembea kwenye barabara nyembamba walijiremba kwa bangili za dhahabu mikononi na kwenye vifundo na kujipaka marashi. Kandokando ya maegesho, meli za matanga zikiwa matanga yake ya pembe tatu yamekunjwa zilielea majini, huku zimejazwa pomoni bidhaa za kupelekwa nchi za kigeni. Watumwa waliofungwa pamoja na kuwekwa katika vikundi, walingoja kuingizwa kwenye majahazi.

Wavumbuzi wa mapema wa Ulaya walishangaa kupata usafi wa kiafya wa hali ya juu na usanifu-majengo katika Lamu. Nyumba za mjini zinazokabili bahari zilijengwa kwa matufali ya matumbawe yaliyochongwa kwa mkono katika machimbo ya mawe ya karibu, na milango mizito ya mbao, iliyochongwa kwa uangalifu mwingi, ililinda njia zao za mwingilio. Nyumba zilipangwa vizuri katika safu zilizokusudiwa kupitisha upepo mwanana wa baharini kwenye barabara nyembamba na kutuliza watu kutokana na joto kali.

Nyumba za watu waliokuwa matajiri zaidi zilikuwa kubwa na zenye nafasi ya kutosha. Bafu zilikuwa na maji safi ya mfereji yaliyopitishwa kwa mifumo ya kale ya mabomba. Vilevile mfumo wa kuondoa takataka ulikuwa wenye kuvutia na wa hali ya juu kuliko wa nchi nyingi za Ulaya wakati huo. Mifereji mikubwa iliyochongwa kutoka kwa mawe, iliteremka kuelekea baharini na kubeba maji machafu hadi kwenye mashimo yaliyochimbwa mchangani yaliyokuwa mbali na vyanzo vya maji safi. Matangi ya maji yaliyotengenezwa kwa mawe yaliyokuwa na maji safi ya kutumiwa nyumbani yalikuwa na samaki wadogo waliokula mabuu ya mbu, na hivyo kupunguza idadi ya wadudu hao wanaouma.

Kufikia karne ya 19, majahazi ya baharini yalipata pembe za tembo, mafuta, mbegu, ngozi za wanyama, kaka la kobe, meno ya kiboko, na watumwa wengi kutoka Lamu. Hata hivyo, baada ya muda, ufanisi wa Lamu ulianza kudidimia. Tauni, kushambuliwa na makabila jirani yenye uhasama, na vikwazo kwa biashara ya utumwa vilifanya Lamu ididimie kibiashara.

Kuchunguza Wakati Uliopita
Kusafiri kwa mashua hadi kwenye bandari ya Lamu leo ni sawa na kuchunguza wakati uliopita. Upepo huvuma bila kukoma kutoka Bahari ya Hindi iliyo kubwa ya rangi ya samawati. Mawimbi mepesi ya feruzi huosha fuko zenye mchanga mweupe. Majahazi ya mbao ya muundo wa kale hunyiririka kandokando ya pwani, huku matanga yake yenye umbo la pembetatu na ya rangi nyeupe yakifanana na vipepeo wanaopuruka. Yakiwa yamepakiwa samaki, matunda, nazi, ng’ombe, kuku, na abiria, yaelekea kwenye bandari ya Lamu.

Gatini, michikichi inayovuma kwenye upepo mwanana wenye joto hutokeza kivuli kidogo kwa wanaume wanaopakua shehena kutoka kwenye meli za mbao. Soko limejaa pilikapilika za watu wenye kelele wanaofanya biashara ya kubadilishana bidhaa. Wafanya-biashara hao hawatafuti dhahabu, pembe za tembo, au watumwa, bali ndizi, nazi, samaki, na vikapu.

Chini ya kivuli cha mwembe mkubwa, wanaume wanasokota kamba ndefu za makonge na kushona matanga ya vitambaa yanayoendesha majahazi yao ya mbao. Barabara ni nyembamba na zimejaa watu wanaoelekea kila upande. Wafanya-biashara waliovalia kanzu ndefu kubwa-kubwa waita watu kutoka kwenye maduka yao yasiyo na mpangilio, wakiashiria wateja waje na kujionea bidhaa zao. Punda, anayejikaza kuvuta mkokoteni wa mbao uliojaa magunia mazito ya nafaka, apita katikati ya watu wengi. Wakazi wa Lamu waelekea kutoka upande mmoja wa kisiwa hadi mwingine kwa miguu, kwa kuwa hakuna magari ya kusafiria kisiwani. Njia pekee ya kufika kisiwani ni kwa kutumia mashua.

Jua lifikiapo upeo katikati ya mchana, wakati huonekana kuwa umesimama. Katika joto kali, ni watu wachache ambao hutembea, na hata punda husimama bila kusonga wakiwa wamefunga macho yao kabisa ili kujituliza na joto hilo.

Jua lianzapo kushuka na halijoto kupungua, kisiwa hicho chenye utulivu hujaa utendaji. Wafanya-biashara hufungua wazi milango yao mizito iliyochongwa kwa mbao ili kuanza biashara, na taa zao zitaendelea kuwaka hadi usiku wa manane. Wanawake huosha watoto wao na kuwasugua kwa mafuta ya nazi mpaka ngozi zao zinaanza kung’aa. Wanawake huanza kutayarisha chakula wakiwa wamekalia mikeka iliyofumwa kwa makuti ya nazi. Hapa wanawake bado hupika kwa kutumia mafiga, wakitayarisha vyakula vyenye ladha tamu vya samaki waliokolezwa vikolezo vyenye kunukia vizuri na wali uliopikwa kwa tui. Watu ni wenye urafiki, wakarimu, na wapole.

Ijapokuwa Lamu haina fahari kama zamani, utamaduni wa Kiafrika wa zamani uliokuwako kabla ya karne ya 20 ungali unasitawi hapa. Chini ya jua la kitropiki, maisha yanaendelea kama yalivyokuwa karne nyingi zilizopita. Ukiwa hapa unaweza kuona mambo ya kale na ya wakati wa sasa pia. Kwa kweli, Lamu imeokoka enzi iliyopita kwa njia ya kipekee, ni kisiwa ambacho kimedumu bila kubadilika.

Ziara Yetu LAMU
  Hivi karibuni, tulizuru Lamu tukiwa kikundi, lakini hatukuwa tumeenda kununua au kuuza vitu. Tulienda kuwatembelea akina ndugu na dada zetu Wakristo, Mashahidi wa Yehova wenzetu. Ndege yetu ndogo ilisafiri kuelekea kaskazini juu ya pwani ya Kenya yenye mawemawe. Chini kabisa, kulikuwa na mawimbi shwari kwenye pwani iliyo na misitu mingi ya kitropiki yenye ukingo wa mchanga mweupe. Kisha, kwa ghafula, tuliona jamii-visiwa ya Lamu ikimetameta kama vito kwenye bahari ya feruzi. Kama tai mkubwa wa Afrika, tulizunguka visiwa hivyo kisha tukatua kwenye barabara ya ndege katika bara. Tulishuka, tukatembea kwenye ukingo wa maji, na kupanda jahazi la mbao ili kutusafirisha hadi Lamu.

  Ilikuwa siku nzuri yenye jua, na upepo wa bahari ulikuwa na joto na uliburudisha. Tulipokaribia kisiwa hicho, tuliona kwamba gati ilikuwa imejaa watu furifuri. Wanaume wenye nguvu waliinua mizigo mizito kutoka kwenye mashua, na wanawake walibeba mizigo yao kwa kuisawazisha barabara vichwani. Tukiwa tumebeba mizigo yetu, tulipenya katikati ya umati wa watu na kusimama chini ya kivuli cha mchikichi. Baada ya dakika chache, ndugu zetu Wakristo walituona, na tulikaribishwa kwa uchangamfu kwenye makao yao yaliyo kisiwani.

  Tuliamka vyema asubuhi kabla ya jua kuchomoza ili kukutana na akina ndugu na dada ufuoni. Safari ya kuhudhuria mikutano ya kutaniko ilikuwa ndefu na ingechukua muda wa saa kadhaa. Tulikuwa tumejitayarishia maji ya kunywa, kofia pana, na viatu vinavyofaa kwa safari. Kulipoelekea kupambazuka, tulifunga safari hadi bara, ambapo mikutano ilifanyiwa.

  Akina ndugu walichukua fursa ya kuhubiria watu waliokuwa mashuani, na hadi tulipofika, tulifurahia mazungumzo fulani ya Biblia na kuangusha magazeti kadhaa. Barabara isiyokuwa na watu ilikuwa na joto na vumbi. Tulipokuwa tunatembea kichakani, tulishauriwa kuwa macho kwa sababu ya wanyama wa mwituni, kutia ndani tembo waliovuka barabara pindi kwa pindi. Akina ndugu walikuwa na furaha na uchangamfu huku tukitembea polepole mahali tulipokuwa tunaenda.

  Punde si punde, tuliwasili kwenye kijiji kidogo ambapo tulikutana na wengine wa kutaniko waliokuwa wametembea kutoka mbali. Kwa sababu ya umbali, mikutano minne ya kutaniko ingefanywa siku hii moja.
  Mikutano ilifanywa katika shule ndogo iliyojengwa kwa mawe yasiyo laini, bila milango au madirisha yaliyokamilishwa kwa ustadi. Ndani ya darasa moja, 15 kati yetu tuliketi kwenye benchi nyembamba na kufurahia programu nzuri inayotegemea Biblia, iliyokuwa yenye kutia moyo na kufundisha. Hakuna aliyebabaishwa na joto kali lililokuwa likitoka kwenye paa ya mabati juu ya vichwa vyetu. Wote walifurahi kuwa pamoja. Baada ya saa nne za mikutano, tuliagana kisha kila mtu akaenda zake. Kufikia wakati tuliporudi Lamu, jua lenye rangi ya kidhahabu lilikuwa likitua kwenye upeo wa macho.

  Jioni hiyo, kwenye baridi ya usiku, tulifurahia mlo sahili pamoja na familia za Mashahidi wanaoishi Lamu. Katika siku zilizofuata tulitembea pamoja nao katikati ya barabara nyembamba zenye kujipinda, tukihubiri na kutafuta watu walio na njaa ya kweli ya Biblia. Tulitiwa moyo na bidii na ujasiri wa ndugu na dada hao wachache.

  Hatimaye siku ilifika ambapo tulihitaji kuondoka. Akina ndugu walitupeleka ufuoni, na tukaagana kwa huzuni. Walituambia kwamba walitiwa moyo na ziara yetu. Tulijiuliza ikiwa walijua jinsi walivyokuwa wametutia moyo! Tuliporudi bara, punde si punde tulipanda ndege yetu ndogo. Tulipopaa juu kabisa angani, tulitazama chini na kuona kisiwa maridadi cha Lamu. Tulifikiri juu ya imani yenye nguvu ya akina ndugu wanaoishi huko, umbali wanaosafiri ili kuhudhuria mikutano, na bidii na upendo walio nao kwa ajili ya kweli. Zamani za kale unabii ulirekodiwa katika Zaburi 97:1: “BWANA ametamalaki, nchi na ishangilie, visiwa vingi na vifurahi.” (Italiki ni zetu.) Kwa kweli, hata kwenye kisiwa cha mbali cha Lamu, watu wanapewa fursa ya kushangilia katika tumaini kubwa zaidi la paradiso ya wakati ujao chini ya Ufalme wa Mungu.—Imechangwa.

SOURCE: CLICK HAPA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni