Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Januari 22, 2013

BAHARI SAYARI YA MARS



Na Leon Bahati

WANASAYANSI wa anga kwa muda mrefu wamekuwa wakitafuta uwezekano wa maisha katika sayari nyingine, mbali na dunia. Kuna imani kuwa kwenye sayari hizo, huenda zikapatikana raslimali nyingi kwa urahisi kuliko duniani ambako binadamu wameishi mamilioni ya miaka hadi sasa.

Wataalamu hao wa anga wamekuwa wakifanya hivyo kwa muda sasa na moja ya mambo muhimu waliyoangalia ni upatikanaji wa maji. Popote maji yanapopatikana, wanaamini maisha yanawezekana.Moja ya sayari ambayo wamekuwa wakiichunguza kwa miaka mingi sasa ni Mars, ambayo ni ya nne kutoka kwenye jua. Dunia ni ya tatu.

Sababu kuu za kuichagua sayari hii tofauti na zingine ni kwamba, hali ya hewa inatofautiana kidogo sana na ya dunia. Sayari nyingine kama Mercury na Venus, zipo karibu zaidi na jua na hali ya joto iko juu kiasi kwamba hali ya maisha inaweza kuwa taabu. Mars ambayo wanasayansi wanaipa jina la sayari nyekundu, ipo karibu na dunia, hivyo ni rahisi kufika iwapo wanasayansi watathibitisha iwapo maisha yanawezekana huko.

Wanaiita sayari nyekundu kwa sababu eneo kubwa la uso wake ni wa rangi nyekundu, tofauti na nyingine zilizomo kwenye mfumo wetu wa sayari. Hakuna mwanasayansi ambaye amethubutu kusafiri hadi kwenye sayari hiyo kutokana na ugumu wa kupata vyombo vya kuaminika, vinavyoweza kusafirisha watu kutoka duniani hadi Mars na kurudi salama.

Hata hivyo, hilo siyo tatizo kwa sababu wakibaini mazingira mazuri, utengenezaji wa vyombo hivyo hauwezi kuwapa taabu. Kazi ya uchunguzi imekuwa ikifanywa kwa vyombo maalumu ambavyo havina watu lakini, vina uwezo wa kuleta mawasiliano duniani.

Pia wanatumia viona mbali katika mchakato huo kuchunguza hali ilivyo kwenye sayari hii, ambayo kumekuwapo na hisia kwamba huenda waliwahi kuishi viumbe hai mamilioni ya miaka iliyopita lakini baadae mazingira yakabadilika na kuwa mabaya.

Uchunguzi unaonyesha kuwa, sayari hii ina mabonde mengi ambayo yanakila dalili kuwa awali yalikuwa yanatiririsha maji kama ilivyo mito hapa duniani. Kwa muda mrefu, wanasayansi wamekuwa wakiichukulia sayari hiyo kuwa na mazingira ya jangwa yanayotokana na ukame wa muda mrefu.
 

WAGUNDUA MAJI

 
Mwezi januari 2009 wanasayansi hao walikuja na maelezo kwamba sayari hiyo ina kiwango kikubwa cha maji na mengi yapo mita chache kutoka uso wake. Mmoja wa wanasayansi waliochunguza sayari hiyo ni Profesa Jay Melosh wa Chuo Kikuu cha Purdue, nchini Marekani.

Yeye alisema uchunguzi huo umewapa imani kwamba siyo tu kwamba Mars ina maji bali kuna viumbe wadogo, mfano wa jamii ya bacteria ambao wanaendelea kuishi humo hadi leo hii. Ni uchunguzi ambao waliamini una matumaini tofauti na taarifa za uchunguzi ulizopita na kizuri zaidi pia ni kubaini moja ya miezi yake miwili, maji yapo kwa wingi zaidi.

Miezi inayoizunguka sayari ya Mars ni Demos na Phobos. Phobos ndio mwezi uliogundulika kuwa na kiwango kikubwa cha maji na ndio ulio karibu zaidi na sayari hiyo. Kwa sababu hiyo, wanaamini kwamba maisha yakianza kwenye sayari ya Mars, kuna uwezekano pia wengine wakahamia kwenye mwezi huo wa Phobos.

Taarifa za uwepo wa maji kwenye sayari hii zilitolewa kwenye mkutano wa wanasayansi wanaochunguza anga za mbali, uliofanyika Austria Juni mwaka 2009. Moja ya dalili za uwepo wa maji ni vimondo ambavyo vimekuwa vikianguka kwa wingi kwenye uso wa sayari hiyo. Mtaalamu wa Uhandisi na Mambo ya Anga, Profesa Kathleen Howell alisema picha walizopiga maeneo ambayo vimondo vimegonga uso wa Mars, zilionesha dalili kama za mtu aliyetupa jiwe kwenye eneo lenye tope.

“Sehemu kimondo kilipoigonga sayari ya Mars, aina ya kitu kama tope kiliruka na kusambaa pembeni,” anasema Profesa Howell. Hali hiyo wakaitafsiri kuwa maji yaliyokaribu na uso wa sayari hiyo yaliruka pamoja na udongo wakati, kimondo kilipozama ndani na kusambaa pembeni.
 

HALI IKOJE?

 

Utafiti huo unaashiria kwamba, sayari hiyo ina bahari kubwa iliyoenea chini kwa chini kwenye miamba mita chache kuingia ndani. Milipuko ya volkano ya miaka mingi iliyopita ni kiashirio kingine kwamba, sayari hii ina maji. Uchunguzi unaonyesha kwamba mlipuko huo uliandamana na maji.

Ripoti ya utafiti huo ambao ulichapishwa pia na jarida la Geology, unaonesha kuwa kiwango cha maji kilichopo Mars kinakadiriwa kuwa sawa au kimezidi kile kilichopo hapa Duniani. “Kimsingi, kiwango cha maji tunayoyazungumzia kinalingana ama ni zaidi ya kile kilichopo kwenye uso wa dunia,” Alisema Kiongozi wa Jopo la Wanasayansi hao, Profesa Francis McCubbin, ambaye pia ni Mtaalamu wa Anga Chuo Kikuu cha Mexico.

“Si jambo la kushangaza kwamba, kwenye sayari hii waliwahi kuishi viumbe hai miaka iliyopita,” alisema Profesa Howell na kuongeza:  “Tatizo tutakalokabiliana nalo ni iwapo tayari muda umepita sana kiasi cha kutotambua vyema hali hiyo.  “Lakini, hata kama hautapatikana uthibitisho wa kisayansi wa viumbe kuwahi kuishi miaka iliyopita, jambo muhimu ni uwezekano wa kiumbe kuweza kuishi kwa sasa.”  
 

HATARI KWENYE MARS!


Hatari iliyopo ni kwamba, ni moja ya sayari ambayo imekuwa ikigongwa mara kwa mara na vimondo vinavyoanguka. Ni vimondo vichache sana ambavyo viliwahi kutua kwenye uso wa dunia. Vinapoanguka kuelekea uso wa dunia hukabiliwa na safari ndefu na kutokana na mwendo mkali wa mwanguko, hujikuta vinapata msuguano mkali na hewa, ambao husababisha joto kali linaloimomonyoa udongo hadi inakwisha.

Sayari hii ambayo ipo karibu na ukanda wa vimondo, uso wake una makovu mengi yanayoashiria athari za vimondo vyenye ukubwa tofauti vilivyotua. Vimondo hivi ndivyo vimeweka wazi dalili za kuwapo kwa maji kwenye sayari hii ambayo uso wake unaonekana kama vile jangwa, kwa kutokuwa na miti na ishara ya ukame wa muda mrefu.
 
DALILI ZAONYESHA KUNA VIUMBE HAI
 JE, NI HATUA NZURI YA UWEZEKANO WA BINADAMU KWENDA KUISHI?

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni