Mtayarishaji

Morning Star Radio

Ijumaa, Oktoba 12, 2012

USIKU WA MWISHO DUNIANI

Photo by: lolamouse.

 
(SOMA DANIELI 5 YOTE)

Moyo wa mwanadamu umejaa upumbavu. "Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wametenda uovu wa ufisadi na kuchukiza, Hakuna atendaye mema" (Zab.53:1). Watu wanaopenda kufanya
dhambi huamua kumfutilia mbali Mungu katika mawazo yao, mafundisho yao, na maisha yao. Biblia inasema huo ni upumbavu. Kwa sababu Mungu yuko kweli, na watu kama hao watawajibika kwa vitendo vyao viovu. Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba hatujifunzi kutokana na yale yaliyowapata watangulizi wetu.
Tunataka kujionea wenyewe.

Siku moja mfalme Belshaza (mjukuu wa Nebukadreza) alifanya karamu kubwa ya ulevi kwa ajili ya wakuu wake elfu. Hakujua kwamba karamu yake hiyo ilikuwa ya mwisho, na ya kwamba Mungu wa
mbinguni alikuwa ameiona hata kabla haijafanywa (Yer. 51:37-40,57-58). Na usiku ule karamu ile ikawa ya aina yake; lakini wahusika hawakuweza kuamka asubuhi yake; walikuwa maiti. Belshaza hakujifunza kutokana na mambo yaliyompata babu yake Nebukadreza (Dan. 5:18-23). Alikuwa anajua yote hayo lakini kwa kiburi kabisa akafanya yaliyomchukiza Mungu wa Mbinguni. Makosa makubwa aliyoyafanya ni haya:

Kosa lake la kwanza ni kutumia vyombo vitakatifu kunywea pombe (Dan. 5:1-3). Hakuweka tofauti kati ya vyombo vya kawaida vya kutumia na vyombo vitakatifu vinavyotumika kwa kazi maalum ya Mungu. Jinsi gani siku hizi wachungaji hawawafundishi washiriki wao kuweka tofauti hiyo? "Makuhani [wachungaji] wake
wameihalifu sheria yangu [Amri Kumi], wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu [kama nguruwe, panya, na kadhalika] na vitu vilivyo safi [kama ng'ombe, mbuzi, kondoo], nao wamefumba macho yao, wasiziangalie Sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao" (Eze. 22:26). 

Kutokutambua vitakatifu ni kosa la kufisha. Sabato [Jumamosi] ni takatifu (Mwa.2:2,3; Kut. 20:11; Isa. 58:13,14). Jumapili si takatifu; ni siku ya kazi (Eze. 46:1). Siku ya ibada aliyoiweka Mungu kwa wanadamu wote ni Sabato [Jumamosi] na itakuwa hivyo milele zote (Isa. 66:22,23). Zaka (sehemu ya kumi ya mapato yetu) ni takatifu (Law. 27:30-33). Kuitumia kwa matumizi yetu ya kawaida ni kumwibia Mungu (Mal.3:8-11). Wevi hawataurithi ufalme wa Mungu (1 Kor. 6:9,10). Kumtegemea mchungaji wako badala ya kusoma Biblia mwenyewe ni hatari kubwa!

Kosa lake la pili ni kunywa divai [pombe] (Dan. 5:4a). Tulijifunza katika somo la kwanza lililohusu vyakula na vinywaji kwamba pombe inaudhuru sana mwili wetu, na ya kwamba wale wanaouharibu mwili wao kwa pombe au kwa njia nyingine yo yote wataharibiwa (1 Kor. 3:16,17). Pombe ina sumu ya alkoholi
ambayo inaathiri mishipa ya fahamu, ubongo, moyo, nyama za mwili, na kadhalika. Sio suala tu la kulewa linalohusika, bali ni ile sumu iliyomo. Wengi hata wakinywa pombe nyingi hawalewi; lakini sumu inafanya kazi miilini mwao na kuiharibu. Hivyo wale wasemao kunywa pombe kidogo tu wasingeweza kusema hivyo kuhusu sumu ya panya. Sumu kidogo tu yatosha kuua mtu au kuuathiri mwili (Mithali 23:29-35). Biblia inailinganisha sumu iliyomo katika pombe na sumu ya nyoka aitwaye "fira" (Mithali 23:31,32).
 
Ni sumu mbaya sana. Biblia inasema walevi [wanaolewa na wasiolewa] hawataurithi ufalme wa mbinguni (1 Kor. 6:9,10). Kosa la tatu la Belshaza ni lile la kuisifu miungu badala ya Mungu wa mbinguni (Dan. 5:4b). Neno lasema, "BWANA asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema BWANA" (Yer. 9:6).

Si kwamba Belshaza alikuwa hamjui Mungu wa mbinguni alipokuwa anaisifu miungu yake pamoja na wakuu wake, kilikuwa ni kiburi chake sugu kilichomfanya afanye hivyo. Je! wewe unamsifu nani? Wakati sherehe imefikia kilele chake, wamelewa na kuanza kusifu wanawake na miungu yao, kiganja cha mkono kisichotoka
damu kikaanza kuandika ukutani. Jasho jembamba likawatoka. Pombe yote ikayeyuka kichwani. Hofu kuu ikawashika, wasijue la kufanya. Wataalam wakaitwa ili wayasome maandiko yale; hawakuweza. Ndipo malkia, mke wa Nebukadreza, akaingia na kuwaambia habari za Danieli jinsi alivyomtafsiria ndoto babu
yake. 

Danieli akaitwa. Akamshutumu Belshaza kwa kiburi chake, licha ya kujua fika yaliyompata babu yake. Akasoma maandiko yale ukutani: "MENE (HESABU), MENE (HESABU), TEKELI (MIZANI), NA PERESI (MGAWANYO). Na tafsiri ya maneno hayo ni hii; MENE, Mungu ameuhesabu ufalme wako na kuukomesha. TEKELI, Umepimwa katika mizani nawe umeonekana kuwa umepunguka. PERESI, Ufalme
wako umegawanyika, nao wamepewa Wamedi na Waajemi" (Dan.5:25-28). Ilikuwa imetabiriwa mapema kwamba milango ya kuingilia mjini itaachwa wazi na maji ya mto yatakaushwa (Isa. 45:1; 44:27). Hivyo ndivyo alivyofanya Koreshi aliyeyaongoza majeshi ya Wamedi na Waajemi usiku ule. Milango ya mto
haikufungwa usiku ule. Wakaingia na kumwua mfalme na viongozi wake waliokuwamo mle. Ulikuwa ni usiku wa mwisho kwao.

Mungu anayapima mataifa katika mizani na kukomesha ufalme wao kama apendavyo. Vile vile anampima mtu mmoja mmoja katika mizani ile ya mbinguni (Amri Kumi) na kuandika mbele ya jina lake "umepunguka" au "umetimilika katika yeye" (Kol. 2:10). Hiyo ndiyo kazi anayofanya Kuhani wetu Mkuu, Yesu Kristo, mbinguni tangu mwaka wa 1844. Karibu sana kesi ya kila mmoja wetu itakatwa kwa milele. Akimaliza kazi yake ya upatanisho au hukumu atatamka maneno haya ya kutisha: "Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi
kutakaswa" (Ufu.22:11). Hukumu hiyo itakatwa kabla ya kuanguka mapigo yale 7 ya Ufunuo 16. Katika pigo la mwisho atakuja kuwachukua watu wake na kuwaangamiza waovu wote.

Mkulima yule tajiri aliyevuna mavuno mengi asijue pa kuyaweka, alifikiri kwamba atakuwa na maisha marefu sana ya raha mbele yake (Luka 12:16-21). Usiku ule akajiambia mwenyewe, "Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi" (Luka 12:19). Maskini
yule, alipolala usiku ule hakuamka, aliuawa. Yule mlinzi mtakatifu asiyeonekana aliyeandika ukutani Babeli, akatamka kwa tajiri huyo maneno haya, "Usiku huu wa leo wanataka roho yako!

Vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?" (Luka 12:20). Ndugu yangu, leo ndiyo siku ya wokovu (2 Kor. 6:2). Kesho si yako (Yak. 4:13-16). Amua leo kumpokea Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wako. Achana na ulevi na dhambi zote. Ukimpokea atakupa uwezo wa kushinda dhambi (l Kor. 15:57; Yuda 24,25).
Usiku wa mwisho duniani kwako na kwangu unaweza kuwa ni usiku huu wa leo. "Basi jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi na masumbufu ya maisha haya, siku ile ikawajia kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia" (Luka 21:34,35). Siku moja ulimwengu wote unaojifurahisha katika anasa mbalimbali za dhambi hautaweza kuiona asubuhi; watakuwa maiti, hawatazikwa, wala kuliliwa (Yer. 25:32-37). Itakuwa karamu ya mwisho Mungu atakayowafanyia ndege (Ufu. 19:17,18).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni