TANGU Anguko la Edeni, wanadamu
wamezidi kudhoofika. Ulemavu, upunguani,
ugonjwa, na mateso yanayowapata
wanadamu vimekilemea zaidi na zaidi kila kizazi
kilichofuata, na watu wengi sana wamelala usingizi
wasiweze kujua sababu za matatizo
hayo. Hawatafakari na kuona ya
kwamba wao wenyewe wanayo hatia, kwa kiwango
kikubwa, kwa hali ya kusikitisha ya
mambo yalivyo. Kwa kawaida wanamlaumu Mungu
kwa mateso yao,
na kumwona Mungu kama ndiye chimbuko la misiba yao. Walakini ni
kule kutokuwa na kiasi, kwa sehemu
kubwa au ndogo, ambako ndiko kumekuwa msingi wa mateso yote haya.
Hawa hakuwa na kiasi katika tamaa
zake alipounyosha mkono wake kuchukua tunda la mti ule uliokatazwa.
Kujifurahisha nafsi karibu kumetawala kabisa ndani ya mioyo ya wanaume na
wanawake tangu Anguko lile. Hasa uchu wa chakula umeendekezwa, nao wametawaliwa
nao, badala ya kutawaliwa na akili. Kwa ajili ya kuiridhisha tamaa ya kuonja,
Hawa alivunja amri ya Mungu.
Alikuwa amempa kila kitu ambacho
mahitaji yake yangetaka, lakini hakutosheka. Tangu hapo, wana wake na binti
zake walioanguka wamefuata tamaa za macho yao
na kuonja. Kama Hawa, wameyapuuza makatazo aliyotoa Mungu, nao wameifuata njia
ile ya uasi, nao, kama Hawa, wamejigamba kuwa matokeo yake yasingekuwa ya
kutisha kama yalivyoogopwa.
Mwanadamu hajazijali sheria
zinazotawala maumbile yake, na ugonjwa umekuwa
ukiongezeka taratibu. Sababu
imefuatiwa na matokeo. Hajatosheka na chakula kile
kinachomletea afya tele; bali
ameiridhisha ladha yake hata kwa hasara ya afya yake.
Mungu ameweka sheria zinazotawala
maumbile yetu. Tukizivunja sheria hizi, basi, hapana budi tutapaswa kulipa
adhabu yake.
Sheria za maumbile yetu haziwezi
kuvunjwa kwa ufanisi zaidi kama kwa njia ya kuyajaza matumbo yetu na chakula
kile kisichofaa kwa afya, kwa sababu ya sisi kuwa na uchu mbaya sana wa
chakula. Kula kupita kiasi, hata chakula kile cha kawaida, hatimaye
kutaviharibu viungo vya kuyeyusha chakula; walakini kula chakula kingi mno,
kisichofaa kwa afya, huzidisha sana
ubovu wa mwili. Afya ni lazima itaathirika tu.
Jamii ya kibinadamu imezidi sana kuiendekeza nafsi,
mpaka karibu afya yote imetolewa
kafara juu ya madhabahu ya tamaa
mbaya ya uchu wa chakula. Wakazi wale wa ulimwengu ule wa kale walikuwa hawana
kiasi katika kula na kunywa. Walitamani na kula nyama, ijapokuwa Mungu alikuwa
hajawapa ruhusa kula chakula cha nyama. Walikula na kunywa kupita kiasi, na
tamaa zao za ufisadi hazikuwa na mipaka. Wakajitoa wenyewe kushiriki katika
ibada ya sanamu yenye kuchukiza mno.
Walitumia nguvu kuwashambulia watu
na kuwaua, tena walikuwa wakatili sana,
na waovu mno hata Mungu hakuweza kuwavumilia zaidi. Kikombe chao cha uovu
kilikuwa kimejaa, na Mungu akaisafisha nchi kutokana na uchafu wake kwa
gharika. Watu walipozidi kuongezeka juu ya uso wa nchi baada ya gharika ile,
wakamsahau Mungu, na kuziharibu njia zao mbele zake. Kutokuwa na kiasi kwa kila
hali kuliongezeka kwa kiwango kikubwa sana.
Bwana akawatoa watu wake kutoka Misri kwa ushindi mkuu.
Akawaongoza jangwani kuwapima na
kuwajaribu. Tena na tena akawaonyesha uweza wake wa ajabu kwa kuwaokoa kutoka
kwa adui zao. Aliahidi kuwafanya hazina yake ya pekee kama
wangeitii sauti yake na kushika amri zake. Hakuwakataza kula nyama, bali
alizuia kwa sehemu kubwa wasiweze kuipata. Aliwapa chakula kilicholeta afya
nyingi kwao. Akawanyeshea mkate wao kutoka mbinguni, na kuwapa maji safi sana kutoka katika
mwamba ule mgumu sana.
Akafanya agano nao: Kama wangemtii katika
mambo yote, basi, angewalinda wasipatwe na ugonjwa.
Lakini Waebrania wale
hawakutosheka. Wakakidharau chakula kile walichopewa kutoka
mbinguni, nao wakatamani kwamba
laiti kama wangekuwa wamerudi Misri, ambako
wangeketi kuyazunguka masufuria
yale ya nyama. Walipendelea zaidi utumwa, na hata
kifo, kuliko kukosa nyama kabisa.
Mungu, kwa hasira yake, akawapa nyama kukidhi uchu wao mbaya wa chakula, na
idadi yao kubwa sana
walikufa wakiwa wangali wanakula nyama ile ambayo walikuwa wameitamani sana.
Nadabu na Abihu waliuawa kwa moto
wa ghadhabu ya Mungu kwa kukosa kwao kuwa na kiasi katika kutumia mvinyo. Mungu
angetaka watu wake wafahamu kwamba
watapatilizwa kulingana na utii au
uasi wao. Uhalifu na ugonjwa vimekuwa vikizidi
kuongezeka kwa kila kizazi
kilichofuata. Kutokuwa na kiasi katika kula na kunywa, na
kujifurahisha kwa tamaa mbaya za
mwili, kumezifisha ganzi nguvu zetu bora za akili. Uchu wa chakula, kwa kiwango
cha kushangaza mno, umeitawala akili yetu.
Jamii hii ya kibinadamu imekuwa na
tamaa inayozidi kuongezeka ya chakula kitamu sana, mpaka umekuwa mtindo wao kulijaza tumbo
na vyakula vyote vilivyo vitamu kwa kadiri inavyowezekana. Hasa kwenye karamu
za anasa uchu huo wa chakula unaendekezwa bila kujizuia. Chakula kitamu na
chakula kinacholiwa usiku sana huliwa, vikiwa na
nyama zilizotiwa viungo vingi sana, na michuzi
mizito yenye viungo vingi, keki tamu sana,
maandazi na sambusa, aiskrimu, na kadhalika.
Wanaojidai kuwa Wakristo kwa
kawaida ndio wanaoongoza katika mikusanyiko kama
hii ya ulimwengu. Fedha nyingi sana hutolewa sadaka kwa miungu hii ya mitindo
na uchu wa chakula, katika kuandaa karamu zenye vyakula vinavyoharibu afya na
kuamsha uchu wa chakula, ati kwa njia hii waweze kujipatia fedha kiasi fulani
kwa matumizi ya kidini.
Kwa njia kama hii wachungaji pamoja
na wale wanaojidai kuwa ni Wakristo wamechangia kwa sehemu yao na kwa mvuto wao
kutoa fundisho na mfano kwa kujifurahisha kwao bila kuwa na kiasi katika kula,
na hivyo kuwaongoza watu kwenye ulafi unaoiharibu afya yao ya mwili. Badala ya
kumshawishi mtu kufikiri, na kuona faida atakayoipata, athari kwa utu wake, na
akili zake bora, ushawishi unaotolewa unaoelekea kufanikiwa sana ni ule wa kuuamsha uchu wake wa chakula.
Kujifurahisha huku kwa kukidhi uchu
wa chakula kutawashawishi watu wengi kutoa
[fedha] ambapo wasingeweza kufanya
lo lote. Ni picha ya kusikitisha jinsi gani kwa
Wakristo!Je, sadaka kama hiyo inampendeza Mungu? Ni mara ngapi zaidi zile
senti mbili
za yule mama mjane zilipata kibali
machoni pake!Wale wanaofuata mfano wake kwa dhatiwatakuwa wamefanya vyema.
Kupata mbaraka wa Mbingu ili uambatane na sadaka
iliyotolewa, kunaweza kuifanya
sadaka ya kawaida kuwa na thamani kubwa kuliko zote.
Wanaume na wanawake wanaokiri kuwa
wafuasi wake Kristo mara nyingi wanakuwa
watumwa wa mitindo, na uchu wa
chakula uletao ulafi. Wakati wa maandalizi ya
mikusanyiko hiyo ya kilimwengu,
muda na nguvu ambavyo vingetumika kwa makusudi ya juu na yaliyo bora, hutumika
kwa kupika vyakula mbalimbali visivyofaa kwa afya.
Kwa kuwa huo ndio mtindo, wengi
walio maskini, wanaotegemea kipato chao kwa kazi ya kila siku, wanajitosa kwa
gharama kubwa katika kutayarisha aina mbalimbali za keki tamu sana, vyakula
vitamu vya kuhifadhi katika makopo, maandazi au sambusa, na aina mbalimbali za vyakula
vya mtindo wa kisasa kwa ajili ya wageni wao, ambavyo vinawaletea tu madhara hao
wanaovila; na wakati uo huo fedha hizo walizokwisha kuzitumia huwa wanazihitaji
kwa ajili ya kununua nguo zao wenyewe pamoja na za watoto wao. Wakati huo
uliotumika katika kupika chakula cha kukidhi ladha kwa hasara ya tumbo,
ungetumika kwa mafundisho ya maadili na dini kwa watoto wao.
Desturi hii ya kutembeleana
inageuka na kuwa wakati wa ulafi. Vyakula na vinywaji
vyenye madhara huliwa kwa kiwango
ambacho kinavilemea sana
viungo vya kuyeyusha
chakula. Nguvu za akiba mwilini
hutumika bila sababu katika kazi ya kuyaondoa madhara hayo mwilini; na matokeo
yake ni kwamba upungufu wa nguvu husikika katika mfumo mzima wa mwili. Mibaraka
ambayo ingeweza kupatikana kwa kutembeleana kirafiki mara nyingi hupotea, kwa
sababu yule mkaribishaji wako, badala ya kufaidi mazungumzo yako, yeye
anahangaika jikoni, akiandaa mapishi mbalimbali kwa ajili yako upate kula.
Wanaume na wanawake walio Wakristo
wasingeruhusu kamwe mvuto wao kusaidia jambo hilo la kula vyakula vitamu vilivyoandaliwa
kwa njia hiyo. Hebu na uwaeleweshe kwamba lengo lako la kuwatembelea, sio
kujifurahisha kwa uchu huo wa chakula, bali ni kuongea pamoja nao, na
kubadilishana nao mawazo na hisia, ili baraka ziwe pande zote mbili. Maongezi
yawe ya kiwango cha juu, yanayojenga tabia, ili baadaye yaweze kukumbukwa kwa
hisia za furaha kuu.
Wale wanaowakaribisha wageni
wanapaswa kuandaa chakula kinachofaa kwa afya, chenye virutubisho, kitokanacho
na matunda, nafaka, na mboga za majani zilizoandaliwa kwa njia ya kawaida,
zenye ladha nzuri. Mapishi kama hayo yatahitaji kazi kidogo sana na gharama ndogo, nacho kikiliwa kwa
kiasi cha wastani, hakiwezi kumletea madhara mtu ye yote.
Kama walimwengu wanachagua kutumia
wakati wao, fedha yao, na afya yao kwa kukidhi uchu wao wa chakula, waache
wafanye hivyo, na kulipa adhabu ya kuvunja sheria za afya; bali Wakristo
wangekuwa na msimamo thabiti juu ya mambo haya, na kuutumia mvuto wao katika
njia nzuri. Wanaweza kufanya mengi katika kuzibadilisha desturi hizi za
mitindo, ambazo zinaharibu afya na roho.
Wengi wanajiendekeza na kuwa na
mazoea mabaya ya kula chakula muda mfupi tu kabla
ya saa za kulala. Wanaweza kuwa
wamekwisha kula tayari milo mitatu ya kawaida; lakini kwa vile wanajisikia wana
hali ya unyong'onyevu, kana kwamba wana njaa, basi, wanakula chakula kingine,
au mlo wa nne. Kwa kujiendekeza hivyo kuwa na mazoea haya mabaya, wamejenga
tabia, wao wanajisikia kana kwamba hawawezi kulala usingizi pasipo kula chakula
kingine kabla ya kwenda kulala. Kwa hali nyingi sababu ya unyong'onyevu huohutokana
na viungo vya kuyeyusha chakula ambavyo tayari vimekwisha lemewa mno na kazi ya
siku nzima ya kujaribu kukiondoa chakula hicho kisichofaa kwa afya ambacho kimeendelea
kuingizwa tumboni mara kwa mara kwa kujilazimisha, na kwa kiasi kingi sana.
Hivyo viungo hivi vya kuyeyusha
chakula huwa vimechoka sana,
na vinahitaji muda wa kupumzika kabisa bila kufanya kazi yo yote ili vipate
kuirejesha nguvu iliyopotea. Mlo wa pili usiliwe kamwe mpaka tumbo liwe
limepata muda wa kupumzika baada ya kuyeyusha mlo ule wote uliotangulia. Kama mlo wa tatu utahitajika kuliwa kwa vyo vyote vile,
basi, uwe mwepesi, na uliwe saa kadhaa kabla ya kwenda kulala.
Lakini kwa wengi tumbo lao lililochoka
linaweza kulalamika kuwa lina uchovu mwingi,
lakini kwao ikawa ni bure kabisa.
Chakula zaidi kinazidi kuingizwa humo kwa
kukilazimisha, nacho kinavifanya
viungo vya kuyeyusha chakula kuanza kufanya kazi yake, kufanya tena kazi yake
ile ile kwa wakati ule wa saa za kulala usingizi. Usingizi wa watu kama hao kwa kawaida huvurugika kwa kuota ndoto mbaya,
nao wanapoamka asubuhi wanajisikia wana unyong'onyevu, na kupotewa na hamu ya
kula chakula. Mfumo wote wa mwili unajisikia kuwa umepungukiwa na nguvu. Katika
kipindi kifupi tu viungo hivyo vya kuyeyusha chakula huchakaa; kwa sababu
havijapata muda wo wote wa kupumzika.
Hao wanapata ugonjwa mbaya wa tumbo
kushindwa kuyeyusha vizuri chakula, nao hushangaa kwamba ni kitu gani
kimewafanya kuwa hivyo. Sababu imeleta matokeo ya hakika. Kama mazoea haya
yataendekezwa kwa muda mrefu sana, afya
itaathirika vibaya sana.
Damu itakuwa chafu, rangi ya uso itapauka, vipele vingi vya mara kwa mara
vitatokea.
Utasikia malalamiko ya mara kwa
mara kutoka kwa watu hao kama vile kupata
maumivu ya mara kwa mara na kuwasha katika eneo la tumbo; na wakati
linapoendelea kufanya kazi, tumbo linachoka mno hata wao inawalazimu kuacha
kufanya kazi, na kupumzika. Wao huwa hawaelewi kabisa kwa nini hali ya mambo
inakuwa vile; maana, kama ukiliweka kando tatizo
hili, wao wanaonekana kuwa wanayo afya.
Wale wanaobadili milo kutoka milo
mitatu kwa siku kwenda miwili, mwanzoni
watasumbuliwa sana au kidogo na hali ya unyong'onyevu, hasa
kufikia saa ile waliyozoea
kula mlo wa tatu. Lakini kama
watavumilia kwa kipindi kifupi, unyong'onyevu huo
utatoweka.
Tumbo, tunapolala na kupumzika,
lingekuwa limemaliza kazi yake yote, ili nalo lipate
kufurahia kupumzika, sawasawa na
sehemu nyingine za mwili. Kazi hiyo ya kuyeyusha
chakula isingeendelea kwa kipindi
cho chote cha saa za kulala usingizi. Baada ya tumbo,
ambalo limelemewa mno, kumaliza
kufanya kazi yake, huwa linachoka sana,
jambo ambalo linasababisha unyong'onyevu. Hapa ndipo wengi hudanganyika, na
kudhani kwamba ni ukosefu wa chakula unaoleta hali kama
hiyo; na bila kuliachia tumbo muda wa kupumzika, wanakula chakula tena, ambacho
kwa wakati huo huondoa unyong'onyevu huo.
Na kadiri watakavyouendekeza uchu
wao wa chakula ndivyo utakavyozidi kutaka utoshelezwe. Unyong'onyevu huu kwa
kawaida ni matokeo ya kula nyama, na kula mara kwa mara, na kula chakula kingi
mno. Tumbo linachoka sana
kwa kulifanya liendelee kufanya kazi kila wakati, likijitahidi kukiondoa
chakula ambacho hakileti afya nyingi mwilini. Vikiwa havina muda wa kupumzika,
viungo vya kuyeyusha chakula hudhoofika, na kwa sababu hiyo huleta hisia ya
"kuzirai," na hamu ya kula mara kwa mara.
Dawa wanayohitaji watu kama hao ni
kupunguza kula chakula kingi, na kutosheka na chakula rahisi cha kawaida,
wakilamara mbili, au sana sana, mara tatu, kwa siku. Tumbo halina budi
kuwa na vipindi vya kila siku vya kufanya kazi na kupumzika; kwa sababu hiyo,
kula bila kufuata utaratibu na kula katikati ya milo ni kuzivunja vibaya sheria
za afya. Tukiwa na mazoea ya kila siku na kula chakula kinachofaa, hapo ndipo
tumbo litaanza kupona taratibu.
Kwa kuwa ni desturi inayokubaliana
na uchu mbaya wa chakula, basi, keki tamu sana,
maandazi na sambusa, na chakula
kile kitamu kinacholiwa mwisho wa chakula [pudini], na kila kitu chenye kuleta
madhara mwilini hushindiliwa ndani ya tumbo. Lazima mezani
pawepo na aina mbalimbali za
vyakula, ama sivyo uchu wao wa chakula ulioharibika
hautaweza kutoshelezwa.
Asubuhi watumwa hao wa uchu wa
chakula mara nyingi hutokwa na pumzi yenye harufu mbaya na ulimi wao unakuwa na
utando. Hawafurahii afya njema, nao hushangaa kwa nini wanateseka kwa maumivu,
kuumwa kichwa, na magonjwa mengine mbalimbali. Sababu imeleta matokeo ya
hakika. Ili kuiweka afya katika hali njema,
kiasi katika mambo yote ni muhimu ----- kiasi katika kufanya kazi, kiasi katika
kula na kunywa.
Wengi ni watumwa wa kutokuwa na
kiasi hata hawawezi kubadili mwendo wao wa
kujifurahisha kwa ulafi kwa sababu
iwayo yote ile. Wangeona heri kupoteza afya yao na
kufa mapema kuliko kujizuia uchu
wao wa chakula usio na kiasi. Tena wapo wengi ambao hawajui uhusiano uliopo
kati ya kula na kunywa kwao na afya njema.
Laiti hao wangeweza kuelimishwa,
wangekuwa na ujasiri wa kuweza kuchagua kwa hiari yao kuukana uchu wao wa
chakula, na kuamua kula mara chache zaidi chakula kile ambacho peke yake
kinaleta afya mwilini, na kwa njia yao waliyochagua wenyewe kufanya
wangejiepusha na mateso mengi sana ambayo wangeweza kuyapata.
Juhudi na zifanywe ili kuhifadhi
kwa uangalifu nguvu za akiba zilizobaki mwilini kwa
kuuondolea mbali kila mzigo
ulemeao. Huenda tumbo lisiweze kupona kabisa na kuwa na afya yake, lakini kula
chakula kinachofaa kwa afya kutazuia udhaifu zaidi usitokee; na
hapana budi watu wengi watapona,
isipokuwa kama wamekwenda mbali sana
katika
kitendo cha kujiua wenyewe kwa
ulafi.
Wale wanaojiachilia wenyewe kuwa
watumwa wa uchu mbaya wa chakula, mara nyingi wanakwenda mbele zaidi, na
kujinajisi kwa kujifurahisha kwa tamaa zao mbaya za mwili,ambazo zinakuwa
zimeamshwa kwa sababu ya kutokuwa na kiasi katika kula na kunywa kwao.
Wanajiachilia tu kutimiza tamaa zao chafu mpaka afya yao
na ubongo wao huathirika vibaya sana.
Sehemu ile ya ubongo inayofikiri na kutoa hoja, kwa sehemu kubwa sana, huharibika kwa
mazoea haya mabaya.
Nimeshangazwa kuona kwamba wakazi
wa dunia hii hawajaangamizwa kama wale watu
wa Sodoma na Gomora. Nimeona iko
sababu ya kutosha kwa hali hii ya uharibifu na kifo
iliyozagaa ulimwenguni humu. Tamaa
kali mno ya mwili inaitawala akili, na kila fikira bora ya heshima huachwa kwa
ajili ya ashiki nyingi [ukware].
Uovu mkuu wa kwanza ulitokana na
kutokuwa na kiasi katika kula na kunywa. Wanaume
na wanawake wamejifanya wenyewe
kuwa watumwa wa uchu wa chakula. Nyama ya nguruwe, japokuwa ni mojawapo ya vitu
vya kawaida sana
katika maakuli, ni
mojawapo ya vitu vinavyoudhuru
mwili vibaya sana.
Mungu hakuwakataza Wayahudi kula nyama ya nguruwe kwa sababu ya kuonyesha
mamlaka yake tu, bali kwa sababu ni kitu ambacho sio chakula kinachofaa kwa
mwanadamu.
Inaujaza mwili wote na ugonjwa ule wa kuvimba
tezi shingoni, na hasa katika nchi za joto inasababisha ukoma, na magonjwa ya aina
mbalimbali. Matokeo yake juu ya mfumo mzima wa mwili katika nchi za hali hiyo
ni mabaya zaidi kuliko katika nchi za baridi. Walakini Mungu hakukusudia kwamba
nguruwe aliwe chini ya hali iwayo yote ile. Washenzi [wapagani] walimtumia
nguruwe kama chakula, na watu wa Amerika wametumia nyama ya nguruwe kwa wingi
kama sehemu ya muhimu ya maakuli yao.
Nyama ya nguruwe isingekuwa na ladha nzuri katika hali yake ya kawaida.
Inafanywa kuwa na ladha nzuri kwa kutiwa viungo vingi vya kukoleza, ambavyo
hukifanya kitu kibaya kuwa kibaya zaidi.
Nyama ya nguruwe, zaidi ya nyama
nyingine zote, huifanya damu kuwa katika hali mbaya. Wale wanaokula nyama ya
nguruwe kwa wingi bila shaka hawatakosa magonjwa. Wale wanaofanya mazoezi mengi
ya viungo nje hawayaoni sana matokeo mabaya ya
kula nyama ya nguruwe kama wale ambao karibu maisha yao
yote wanakaa ndani, na ambao mazoea yao
ni kukaa, na ambao kazi zao zinahitaji akili.
Lakini sio afya ya mwili peke yake
inayoathirika kwa kula nyama ya nguruwe. Ubongo
unaathirika, na fahamu zake kali
hupunguzwa makali yake, kwa kutumia chakula hiki
kibaya sana. Haiwezekani kabisa kwa nyama ya kiumbe
cho chote kilicho hai kuwa na afya wakati uchafu ndio sehemu ya chakula chake,
na wakati kinakula kila kitu kichukizacho. Nyama ya nguruwe imejengwa na kile
wanachokula. Kama wanadamu watakula nyama yake, basi, damu yao
na nyama yao
itanajisiwa kwa uchafu ule ulioingia mwilini mwao kupitia kwa nguruwe huyo.
Ulaji wa nyama ya nguruwe umeleta
ugonjwa wa kuvimba tezi shingoni [mafindofindo],
ukoma, na maji ya mwilini yenye
kansa (humour). Ulaji wa nyama ya nguruwe bado ungali unasababisha mateso
makali sana kwa
jamii ya kibinadamu. Uchu wa chakula ulioharibika [walio nao watu] unavililia
vitu vile ambavyo vina madhara makubwa sana
kwa afya. Laana, ambayo imeenea kwa wingi katika dunia hii, na ambayo jamii
nzima ya wanadamu imeathiriwa nayo, pia imewaathiri na wanyama.
Wanyama wamepungua ukubwa wao, na miaka
yao ya kuishi.
Kutokana na mazoea mabaya ya mwanadamu, [wanyama] wamelazimika kuteseka zaidi
kuliko ambavyo wangestahili. Kuna wanyama wachache mno ambao hawana magonjwa.
Wengi wamelazimika kuteseka sana kwa kukosa
mwanga, hewa safi,
na chakula chenye afya.
Wanapononeshwa, mara nyingi
wanafungwa karibu-karibu kwenye vibanda vidogo, wala hawaruhusiwi kufanya mazoezi,
na kufurahia hewa inayozunguka kwa wingi nje. Wanyama wengi walio dhaifu wanaachwa
kuvuta hewa yenye sumu itokanayo na uchafu ambao unaachwa katika maghala ya
nafaka na vibanda hivyo. Mapafu yao hayawezi
kustahimili kuendelea kuwa na afya kwa kipindi kirefu wakati wanavuta hewa
chafu kama hiyo. Ugonjwa unasafirishwa mpaka kwenye
ini, na mwili wote wa mnyama huyo unakuwa mgonjwa.
Anachinjwa, na kupelekwa sokoni
kuuzwa, na watu hula kwa wingi nyama hiyo yenye sumu ya mnyamahuyo. Magonjwa
mengi yanasababishwa kwa njia hii. Lakini watu hawataki kuamini kwamba nyama
ile waliyoila ndiyo imeisumisha damu yao,
na kuwaletea maumivu. Wengi hufa hasa kwa ugonjwa ulioletwa na ulaji wa nyama,
japokuwa ni hivyo, ulimwengu hauelekei kupata hekima zaidi [kujifunza]. Maadam
wale wanaokula chakula cha nyama hawaoni matokeo mara moja, huo sio ushahidi
kwamba haiwaletei madhara yo yote. Inaweza kuwa inafanya kazi yake kwa hakika
mwilini mwao, walakini kwa wakati wa sasa huenda wasiweze kuona madhara yoyote.
Wanyama huwa wanasongamana katika
magari yaliyofunikwa, nao karibu wanakosa hewa kabisa pamoja na mwanga, chakula
na maji, kisha wanasafirishwa katika hali hiyo kwa maelfu ya maili, wakiwa
wanavuta hewa itokayo katika uchafu uliolundamana; na
wanapofika mwisho wa safari yao, na kushushwa kutoka
kwenye magari hayo, wengi
wanakuwa katika hali ya nusu kufa
kwa njaa, kukosa hewa, na kuwa katika hali ya kufa,
nao kama wangeachwa peke yao wangeweza kufa
wenyewe. Lakini mchinja nyama
anamaliza kazi hiyo, na kuiweka
nyama hiyo tayari kuuzwa sokoni.
Damu yao
inakuwa imechemka sana,
na wale wanaokula nyama hiyo wanakula sumu.
Wengine hawaathiriki mara moja,
wakati wengine wanashambuliwa na maumivu makali,
nao hufa kutokana na homa,
kipindupindu, au ugonjwa mwingine uwao wote siojulikana. Wanyama wengi sana wanauzwa kwa ajili ya soko la mjini ambao
wanajulikana kabisa na wale waliowauza kuwa ni wagonjwa, na wale wanaowanunua
kwa ajili ya kuuza nyama yao
sokoni sio kwamba siku zote hawajui juu ya hali hiyo. Hasa katika miji mikubwa
jambo hili hufanyika kwa kiwango kikubwa, na wale wanaokula nyama hiyo hawajui
kwamba wanakula nyama ya wanyama wenye magonjwa.
Baadhi ya wanyama wanaoletwa
machinjioni wanaonekana kutambua kile kitakachotokea kwao, nao wanakuwa wakali sana, na kuwa na wazimu
hasa. Wanachinjwa wakiwa katika hali hiyo, na nyama yao hutayarishwa kuuzwa sokoni. Nyama hiyo ni
sumu, nayo imewaletea wale walioila kiharusi, kifafa au degedege, madhara ya
ubongo yanayomfanya mtu kupoteza uwezo wa kusikia maumivu, kutenda, au kufikiri
(apoplexy)), na kifo cha ghafula. Lakini sababu ya mateso yote hayo haisemwi
kuwa inatokana na ulaji wa nyama.
Wanyama wengine wanatendewa
kikatili mno wanapoletwa machinjioni. Wanateswa hasa, na baada ya kustahimili
masaa mengi ya mateso makali mno, wanachinjwa. Nguruwe wanatayarishwa kwa ajili
ya soko hata wakati tauni iko juu yao, na nyama yao yenye sumu imeeneza
magonjwa ya kuambukiza, na vifo vingi vimefuatia.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni