Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatano, Machi 28, 2012

Ugonjwa na Sababbu Zake....SURA YA 2




WANAUME na wanawake, kwa kukidhi uchu wao wa chakula katika kula vyakula vilivyokolezwa sana, hasa nyama zenye michuzi mizito iliyokolezwa, na kwa kutumia vinywaji vinavyouchochea mwili, kama vile [majani ya] chai na kahawa, wanakuwa na uchu wa chakula usiokuwa wa kawaida. Mfumo mzima wa mwili unakuwa na hali ya msisimko, viungo vya kuyeyusha chakula huathirika, ubongo haufanyi kazi yake vizuri, tamaa mbaya za mwili huamshwa, na kuitawala akili. Uchu wa chakula unazidi kutokuwa wa kawaida na mgumu zaidi kuudhibiti. Mzunguko wa damu mwilini hauwi sawa, na damu huwa chafu. Mfumo mzima wa mwili huchafuka, na matakwa ya kukidhi uchu huo wa chakula huzidi kutokuwa na maana yo yote, ukivililia vitu vile vinavyouchochea mwili na
kuudhuru mpaka tabia imeharibika kabisa.

Kwa wengi uchu huo unapiga kelele sana ukitaka kupewa mmea ule uchukizao, yaani, tumbako, pamoja na pombe iliyofanywa kuwa na nguvu kutokana na michanganyo mbalimbali ya vitu vinavyogeuka na kuwa sumu na kuathiri afya. Wengi hawakomei hapo. Uchu wao ulioharibika unaita kuletewa kinywaji kikali zaidi, ambacho kina nguvu nyingi zaidi ya kuweza kuufisha ganzi ubongo. Hivyo wanajiachilia wenyewe kupita kiasi chote mpaka uchu wao huo umeutawala kabisa ubongo wao unaofikiri na kutoa hoja; na mwanadamu huyo, aliyeumbwa katika sura ya Muumbaji wake, hujiharibu mwenyewe na kuwa mbaya kuliko wanyama wa porini. Uanaume wake na heshima yake vyote pamoja
hutolewa sadaka kwa uchu wake. Ilihitaji muda kuweza kuzipoozesha fahamu za ubongo wake. Kazi hiyo ilifanyika taratibu lakini kwa hakika. Kuuendekeza uchu wake wa chakula kwa kuanza kula vyakula vile vilivyokolezwa sana, kulianzisha uchu mbaya wa chakula na kutayarisha njia kwa kila aina ya anasa, mpaka afya na akili vikatolewa sadaka kwa tamaa mbaya za mwili.

Wengi wameingia katika uhusiano huo wa ndoa kabla hawajachuma mali yo yote, wala hawajapata urithi wo wote. Hawakuwa na nguvu za kimwili, wala za kiakili kuwawezesha kuchuma mali yao wenyewe. Ni watu kama hao hasa ambao wameharakisha kuoa, nao wamejitwalia majukumu ambayo hawayaelewi sawasawa. Hawakuwa na hisia bora, zenye heshima, wala hawakuwa na wazo sahihi la wajibu umpasao mume na baba, wala kujua itakavyowagharimu kukidhi mahitaji ya familia zao. Wala hawakuonyesha hata kidogo uhalali wa kuongeza ukubwa wa familia zao kama ule waliouonyesha katika shughuli za biashara zao. Wale walio na upungufu mkubwa katika busara ya kuendesha biashara zao, na wale ambao sifa zao ziko chini sana kuhusu uhusiano wao na wengine katika ulimwengu
huu, hao ndio, kwa kawaida, wanaozijaza nyumba zao na watoto wengi; ambapo wale walio na uwezo wa kuchuma mali kwa kawaida hawana watoto wengi zaidi ya wale tu wanaoweza kuwatunza vizuri. Wale ambao wameshindwa kujitunza wenyewe wasingezaa watoto. Imetukia ya kwamba uzao mwingi wa watu kama hawa, walio watovu wa kupiga mahesabu ya gharama, huachwa kukua kama wanyama. Hawalishwi ipasavyo, wala kuvikwa nguo zinazofaa, wala hawapewi malezi ya kimwili, wala ya kiakili, na kwa hao hakuna utakatifu wo wote katika neno hili "nyumbani," iwe ni kwa wazazi wenyewe ama kwa watoto wao.

Ndoa ilikusudiwa na Mungu kuwa mbaraka kwa mwanadamu; lakini kwa mwonekano wake wa kawaida imetumiwa vibaya kwa namna ambayo imeleta laana ya kutisha. Karibu wanaume na wanawake wote, walipoingia katika uhusiano huu wa ndoa, walichofanya kilikuwa ni kujiuliza swali moja tu kama walikuwa wanapendana. Lakini wanapaswa kutambua kwamba wajibu mkubwa kuliko huo unawakalia katika uhusiano wao wa ndoa. Yawapasa kufikiria iwapo watoto wao watakuwa na afya njema kimwili, na nguvu kiakili na kimaadili. Walakini ni wachache mno waliosonga mbele wakiwa na makusudi ya juu, na fikira bora, ----- kwamba jumuia yao ilikuwa na madai juu yao ambayo wasingeweza kuyatupilia mbali kwa urahisi; kwamba uzito wa mvuto wa familia zao ungeweza kupanda au kushuka katika mizani.

Jumuia imejengwa kutokana na familia nyingi. Viongozi wa familia hizo wanawajibika kuijenga jumuia hiyo ipate kuwa na tabia nzuri. Laiti kama hao wanaoingia katika uhusiano wa ndoa pasipo kufikiri wangeteseka peke yao, uovu huo usingekuwa mkubwa, na dhambi yao kwa ulinganifu ingekuwa ndogo. Walakini taabu inayotokana na ndoa hizo zisizokuwa na furaha yo yote inawafikia watoto walio katika muungano huo. Wamewarithisha maisha ya huzuni kuu ya kudumu, na japokuwa hawana hatia yo yote, wanalazimika kuteseka kutokana na matokeo ya kutojali wengine ambayo wazazi wao wamejichagulia. Wanaume na wanawake hawana haki yo yote kufuata nia zao, au tamaa zao za kijinga katika uhusiano wa ndoa zao, na halafu kuwaleta duniani watoto wasiokuwa na hatia yo yote kuja kutambua kutokana na sababu mbalimbali ya kuwa maisha yao hayana furaha sana, na kwa hiyo
yamekuwa mzigo tu.

Kwa kawaida watoto hurithi tabia za ajabu-ajabu tu walizo nazo wazazi wao, na juu ya hayo yote, wengi wanakua pasipo kuzungukwa na mvuto ule uokoao. Mara nyingi mno wanatupwa ovyo ovyo tu kwa pamoja katika mazingira ya umaskini na uchafu. Wakiwa na mazingira hayo na mfano kama huo, unaweza kutazamia nini kutoka kwa watoto hao watakapofikia umri wa kufanya mambo yao wenyewe, kama sio kushuka chini zaidi katika mizani ya ubora wa maadili kuliko vile walivyokuwa wazazi wao, na kasoro zao kwa kila hali kuonekana wazi zaidi kuliko zile za wazazi wao? Kwa hiyo kundi hilo limezidumisha kasoro zao, na kuwaletea watoto wao laana kwa umaskini, utaahira, na unyonge. Watu kama hao wasingestahili kuoana, au, angalau, wasingewaleta [duniani] watoto wasiokuwa na hatia kuja kushiriki taabu zao, na kuwarithisha kasoro zao wenyewe, pamoja na hali
mbaya inayozidi kuongezeka toka kizazi hata kizazi, ambayo ni sababu kuu moja ya uharibifu wa tabia na afya uliowapata wanadamu.

Kama wanawake wa vizazi vilivyopita wangekuwa wamefanya mambo yao kwa kutafakari sana, wakitambua fika ya kwamba vizazi vijavyo vingekuwa bora, ama kuwa duni kulingana na hatua yao ambayo wangeichukua, basi, wangekuwa wamechukua msimamo thabiti, ya kwamba wasingekubali kuunganisha maisha yao na wanaume wale waliopenda tamaa zisizokuwa za kawaida, kama vile kutumia vileo, na tumbako, vitu ambavyo ni sumu ya kufisha ifanyayo kazi yake taratibu, ikiudhoofisha mfumo mzima wa mishipa ya fahamu, na kuziharibu nguvu bora za akili. Kama wanaume hao wangeendelea kushikamana na tabia hizo mbaya, basi, wanawake wangeamua kuwaacha waendelee na useja wao kwa furaha, wakifurahia wenzi wao hao [yaani, vileo na tumbako] waliojichagulia wenyewe. Wanawake wasingejiona kuwa wana thamani ndogo kiasi hicho hata kuweza kukubali kuunganisha maisha yao yote na wanaume ambao wameshindwa kabisa kuzitawala tamaa zao, lakini
ambao furaha yao kuu imo katika kula na kunywa, na kutimiza tamaa za kinyama za miili yao. Wanawake siku zote hawajafuata kama vile akili zao zinavyowasukuma, bali wamefuata tamaa zao. Kwa kiwango kikubwa hawajajisikia kuwa wanao wajibu unaowakalia, katika kufanya muungano wao wa maisha ambao ungetia muhuri juu ya watoto wao kwa kuwapatia kiwango cha chini cha maadili, na tamaa ya kukidhi ufisadi wao, kwa hasara ya afya yao na hata maisha yenyewe. Mungu atawashikilia kuwa wanahusika kwa kiwango kikubwa kwa afya ya mwili na tabia za kimaadili ambazo
zitaweza kurithiwa kwa njia hiyo na vizazi vijavyo.

Wanaume na wanawake walioiharibu miili yao kwa tabia za uasherati, wameziharibu na akili zao pia, na kuziharibu fahamu zao kali za kiroho. Wengi katika kundi hili wameoana, na kuwaachia watoto wao urithi wa aibu wa udhaifu wao kimwili pamoja na maadili mabaya. Kukidhi tamaa za mwili za kinyama, na ashiki mbaya sana, imekuwa ndiyo tabia iliyo dhahiri ya watoto wao, ikirithiwa toka kizazi hata kizazi, ikizidisha taabu ya wanadamu kwa kiwango cha kutisha, na kuharakisha uchakavu wa miili ya wanadamu. Mara nyingi wanaume na wanawake ambao wamekuwa na miili dhaifu na wale walio wagonjwa, wamejifikiria kwa uchoyo wao kupata furaha yao tu katika tendo la ndoa. Jambo hili hawajalifikiria kwa makini kulingana na kanuni bora na kuu, wakitafakari yale ambayo wangetarajia watoto wao kuyapata, ambayo si mengine ila ni upungufu wa nguvu za mwili na akili, mambo ambayo yasingeweza kuiinua juu jamii, bali kuizamisha chini zaidi.

Wanaume dhaifu mara kwa mara wamependwa na wanawake wanaoonekana kuwa wana afya njema, na kwa sababu ya kupendana wenyewe, waliona kwamba wanao uhuru kabisa kuweza kuoana, pasipo kufikiria kwamba kwa kuunganika kwao, hapana budi, mwanamke huyo angekuwa ndiye mtesekaji hasa, kwa sababu ya yule mumewe mgonjwa. Kwa hali nyingi mume aliye mgonjwa anaendelea kupata afya njema, wakati mke wake anashiriki ugonjwa wake. Mume anaishi kwa kunyonya sana nguvu zake [mwanamke], na mara [mwanamke huyo] anaanza kulalamika kuwa afya yake inazidi kupungua. Mume huyo anaongeza siku zake kwa kupunguza siku za mke wake. Hivyo wale wanaooana wanafanya dhambi kwa kufikiria kirahisi afya na uzima aliowapa Mungu kutumika kwa utukufu wake.

Laiti kama wale wanaoingia hivyo katika uhusiano wa ndoa wangekuwa wanahusika wao tu, dhambi hii isingekuwa kubwa sana. Watoto wao wanalazimika kuteseka kwa ugonjwa waliourithi. Kwa njia hiyo ugonjwa umedumishwa toka kizazi hata kizazi. Na wengi wanamlaumu Mungu kwa mzigo huu mzito wa huzuni ya kibinadamu, ambapo ni njia zao mbaya za maisha zilizowaletea matokeo hayo ya hakika. Wameitupia jumuia kizazi cha watu waliodhoofika, nao wamechangia sehemu yao katika kuichakaza jamii ya wanadamu, kwa kuufanya ugonjwa huo uwe wa kurithi, na kwa njia hiyo kuzidi kuongeza mateso kwa wanadamu.

Sababu nyingine ya kupungua nguvu kimwili na kushuka maadili ya kizazi hiki cha sasa inatokana na wanaume na wanawake wanaooana kupitana sana umri. Mara kwa mara hutokea kwamba wanaume wazee ndio wanaochagua kuoa wake vijana. Kwa kufanya hivyo, maisha ya mume huyo yanarefushwa, wakati mkewe anajisikia kupungukiwa na nguvu ile aliyomgawia mume wake mzee. Haujawa wajibu wa mwanamke ye yote kujitoa mhanga maisha na afya yake, hata kama alikuwa anampenda sana mtu aliye na umri mkubwa kuliko wake, hata kama yeye kwa upande wake alijisikia kuridhika na kitendo chake cha kujitoa mhanga. Angepaswa kuyazuia mapenzi yake. Alikuwa na mambo ya hali ya juu ya kufikiria kuliko kutafuta mapenzi yake tu. Angepaswa kufikiria kwamba, endapo watoto wangezaliwa nao, je, hali yao kiafya ingekuwaje? Tena ni vibaya zaidi kwa vijana
wanaume kuoa wanawake wanaofikiriwa kuwa na umri mkubwa sana kuliko wao. Mara nyingi watoto wanaozaliwa kutokana na muungano kama huo, mahali ambapo umri unatofautiana sana, hawana akili sawasawa. Pia wanakuwa na upungufu katika nguvu zao za mwili. Katika familia kama hizo mara kwa mara zimeonekana tabia mbalimbali za ajabu, na mara nyingi ni tabia zile zinazosikitisha. Watoto hao mara nyingi hufa mapema; na wale wanaopevuka, kwa hali nyingi, wanao upungufu wa nguvu kimwili na kiakili, pamoja na maadili mema.

Baba, akiwa na nguvu zake za ubongo zinazopungua, kwa nadra huwa amejitayarisha kuilea vizuri familia yake changa. Watoto hawa wanazo tabia za ajabu, ambazo daima zinahitaji maongozi ya kuzisahihisha, vinginevyo wataangamia hakika. Hawapati elimu ipasavyo. Kutokana na umri mkubwa wa baba, malezi yao mara nyingi mno huwa ya kugeuka-geuka tu na ya harara. Yeye anakuwa na hisia zinazobadilikabadilika, ----- wakati mmoja huwa anawadekeza sana, na wakati mwingine anakuwa mkali sana bila sababu. Katika baadhi ya familia kama hizo, kila kitu ni kibaya tu, na jambo hilo huzidisha hali mbaya nyumbani. Hivyo kundi la viumbe hao hutupwa ulimwenguni na kuwa mzigo mzito kwa jamii. Kwa kiwango kikubwa wazazi wao walihusika na tabia zilizokuzwa na watoto
wao, ambazo zinarithiwa toka kizazi hata kizazi.

Kama wangetumia akili zao, bila shaka, wangejua kwamba udhaifu wao wa kimwili na kiakili utakuwa ndio urithi wa watoto wao, hivyo wale wanaozidi kuongeza idadi ya watoto wao ni wavunjaji wa amri sita za mwisho za Sheria ya Mungu, ambayo inafafanua wajibu wa mwanadamu kwa mwanadamu mwenzake. Wanatoa mchango wao katika kuzidisha udhaifu wa jamii ya kibinadamu, na kuizamisha chini zaidi jamii hiyo, kwa mantiki hiyo wanamdharau jirani yao. Kama Mungu anazifikiria hivyo haki za majirani zetu, je! hataujali uhusiano huo ulio wa karibu sana na mtakatifu? Iwapo hata shomoro  mmoja haanguki chini pasipo Yeye kujua, je! hatawajali watoto wanaozaliwa duniani, wakiwa wagonjwa kimwili na kiakili, wakiteseka maisha yao yote kwa kiwango kikubwa au kidogo? Je, hatawataka wazazi watoe hesabu kwa akili alizowapa, ambazo wamezitupa nyuma yao [wameacha
kuzitumia], na kuwa watumwa wa tamaa ya mwili, wakati matokeo yake ni kwamba vizazi
vijavyo havina budi kuwa na alama ya upungufu wao kimwili, kiakili, na kimaadili?

Zaidi ya mateso hayo wanayowapa watoto wao, hawana fungu lo lote la kuliachia kundi hilo dogo
linalotia huruma, isipokuwa huo umaskini tu. Hawana uwezo wa kuwasomesha, na wengi wao hawaoni umuhimu wake, wala wasingeweza kupata muda kama wangetaka wa kuwalea, kuwafundisha, na kuwapunguzia urithi mbaya waliowarithisha kwa kadiri iwezekanavyo. Wazazi wasingeongeza ukubwa wa familia zao kwa haraka ila kwa kujua kwamba watoto wao hao wanaweza kuwatunza vizuri na kuwasomesha. Mtoto mikononi mwa mama yake mwaka nenda mwaka rudi ni ukatili mkubwa sana kwake. Tendo hilo hupunguza, na mara nyingi huharibu, furaha katika familia hiyo, na kuzidisha huzuni nyingi katika nyumba hiyo. Linawanyima watoto wao matunzo, elimu, na furaha, mambo ambayo wazazi wangejisikia kuwa wanawajibika kuwapa watoto wao.

Mume huwa anakivunja kiapo chake cha ndoa, na wajibu ule alioagizwa kufanya katika Neno la Mungu, wakati ule asipoijali afya na furaha ya mke wake, kwa kumwongezea mizigo na masumbufu kwa kuzaa watoto wengi. "Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda kanisa, akajitoa kwa ajili yake.... Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea kanisa."

Tunaliona agizo hilo takatifu kuwa karibu linapuuzwa kabisa, hata na wale wanaokiri kuwa ni Wakristo. Po pote unapoweza kutazama, utawaona wanawake waliopauka rangi, walio dhaifu, wachovu sana, waliovunjika moyo, wenye majonzi, na waliokata tamaa. Kwa kawaida wanafanya kazi nyingi kupita kiasi, na nguvu zao za akiba hupungua sana kwa kuzaa watoto mara kwa mara. Ulimwengu umejazwa na vinyago vya wanadamu wasiokuwa na thamani yo yote kwa jamii. Wengi wana upungufu wa akili, na wengi walio na talanta za kuzaliwa nazo hawazitumii kwa manufaa yo yote yale. Hawajawa waungwana, na sababu moja kuu ni kwamba watoto wamezaliwa kwa haraka mno kuliko wanavyoweza kuwalea vizuri, nao wameachwa kukua kama wanyama.

Hapana budi watoto wa umri huo pamoja na wazazi wao wanateseka kutokana na adhabu ya kuzivunja sheria za afya. Njia ile wanayoifuata tangu utotoni iko kinyume daima na sheria za maumbile yao. Wanalazimika kupokea urithi wa kusikitisha wa ugonjwa na udhaifu kabla ya kuzaliwa kwao, uliosababishwa na mazoea mabaya ya wazazi wao, ambayo yataweza kuwaathiri [watoto hao] kwa kiwango kikubwa au kidogo katika maisha yao yote. Hali hii mbaya ya mambo inafanywa kuwa mbaya zaidi kwa kila njia na wazazi wale wanaoendelea kuifuata njia hiyo mbaya katika malezi ya kimwili ya watoto wao wakati wa utoto wao.

Wazazi wanaonyesha ujinga wa kushangaza, kutojali, uzembe, inapohusu afya ya kimwili ya watoto wao, nao mara nyingi huharibu nguvu kidogo ya akiba iliyobaki ndani ya mtoto huyo mchanga aliyedhulumiwa, na kumfanya aweze kuingia kaburini mapema. Mara kwa mara utawasikia wazazi wakiomboleza juu ya amri ya Mungu ambayo imewapokonya watoto wao kutoka mikononi mwao. Baba yetu aliye mbinguni ni mwenye hekima mno kuweza kutufanyia sisi mabaya. Hafurahii kabisa kuona viumbe vyake vikiteseka. Maelfu wamepata uharibifu kwa maisha yao yote kwa sababu wazazi wao hawajaishi kulingana na sheria za afya. Wamefuata tamaa zao, badala ya kufuata ushauri wa busara wa akili zao na huku daima [mawazoni mwao] wakiwa na picha ya afya ya watoto wao kwa siku zijazo. Kusudi kuu la kwanza katika kuwalea watoto linalopaswa kufikiriwa ni kwamba wawe na
afya njema ya mwili, ambayo, kwa sehemu kubwa, itaandaa njia kwa malezi yale ya akili na kimaadili. Afya ya kimwili na kiroho vimeungana kwa karibu sana. Ni mzigo mkubwa jinsi gani wa uwajibikaji unaowakalia wazazi tunapotafakari kwamba njia ile wanayofuata kabla ya kuzaliwa watoto wao inahusika sana na ukuzaji wa tabia yao baada ya kuzaliwa kwao.




Watoto wengi wanaachwa kukua bila uangalizi zaidi kutoka kwa wazazi wao kuliko ule ambao mkulima anautumia kwa wanyama wake. Akina baba hasa ndio mara nyingi wanayo hatia kwa kuonyesha kutoijali sana hali ya wake na watoto wao kuliko ile wanayoionyesha kwa ng'ombe wao. Mkulima mwenye huruma atachukua muda fulani kutafakari namna awezavyo kuitunza vizuri sana mifugo yake, naye ataangalia hasa kwamba farasi wake wenye thamani hawatumikishwi sana, hawalishwi kupita kiasi, au hawalishwi wanapokuwa na joto jingi mwilini, ili wasije wakafa.

Atachukua muda fulani kuitunza mifugo yake, isije ikaumia kwa kuiacha bila kuitunza, au kwa kuiweka juani kwa muda mrefu, au kwa njia nyingine yo yote ya kuishughulikia, na mifugo yake michanga inayozidi kuongezeka ili isije ikapungua thamani yake. Ataangalia muda wa kila siku wa kuwalisha, naye atajua kiasi gani cha kazi wanaweza kumudu kufanya pasipo kuwadhuru. Ili kulifikia kusudi hilo,
atawapa chakula kile tu kiletacho afya nyingi, kwa vipimo vinavyofaa, na kwa vipindi vilivyowekwa. Kwa kufuata hivyo uongozi wao wa akili, wakulima wanafanikiwa kuhifadhi nguvu za wanyama wao. Endapo mapenzi ya kila baba kwa mke wake na watoto yangelingana na uangalifu ule alio nao kwa ng'ombe wake, kwa kiwango kile ambacho maisha yao yana thamani kubwa kuliko wanyama wale, basi, pangekuwa na matengenezo kamili katika kila familia, na taabu hizo za kuhuzunisha zinazowapata wanadamu zingepungua sana.

Uangalifu mkubwa unapaswa kuonyeshwa na wazazi katika kuandaa vyakula viletavyo afya kwa ajili ya watoto wao. Na kwa hali iwayo yote ile wasingeweka mbele ya watoto wao chakula ambacho akili yao inawafundisha kuwa hakileti afya njema mwilini bali kinaleta uchafuzi katika mfumo mzima wa mwili, na kuviharibu viungo vya kuyeyusha chakula. Wazazi hawajifunzi [kwa kuangalia] sababu na matokeo yake kuhusiana na watoto wao, kama vile wanavyofanya kwa wanyama wao, tena huwa hawafikiri ya kwamba kule kufanya kazi kupita kiasi, kula chakula mara tu baada ya kufanya zoezi la nguvu, au wakati mtu anapokuwa amechoka sana na kuwa na joto jingi mwilini, kutaweza kuathiri afya ya mwanadamu huyo, sawasawa tu kama vile itakavyoathirika afya ya wanyama, na hali kama
hiyo itaweka msingi wa afya iliyoharibika kwa mwanadamu, kama vile ilivyo kwa wanyama.

Kama wazazi wenye watoto wanakula chakula mara kwa mara, bila [kufuata] utaratibu wo wote, na kwa wingi mno, hata kama ni chakula kile kiletacho afya nyingi mwilini, basi, afya ya mwili itaathirika; lakini kuongezea kwa hilo, kama aina ya chakula hicho haifai, na kimepikwa kwa mafuta mazito ya wanyama (grease) na viungo vya kunukia (spices) ambavyo haviyeyushwi tumboni, basi, matokeo yake yatakuwa na madhara mabaya sana mwilini. Viungo vya kuyeyusha chakula vitalemewa sana, na viungo hivyo vilivyochoka sana havitaachiwa hata nafasi ndogo ya kupumzika na kurejesha nguvu yake, na viungo hivyo muhimu vitachakaa mara moja, na kuharibika. Kama uangalifu huo na utunzaji wa utaratibu wa kuwalisha unafikiriwa kuwa ni wa muhimu kwa wanyama, basi, mambo yayo hayo ni ya muhimu zaidi kwa wanadamu, walioumbwa kwa sura ya Muumbaji wao, kwa vile wao wana thamani kubwa zaidi kuliko wanyama walioumbwa.

Katika hali nyingi, baba huwa anatumia akili kidogo, na uangalifu mdogo kwa mke wake na mtoto wao kabla hajazaliwa, kuliko vile anavyoonyesha kwa ng'ombe wake wenye watoto tumboni. Mama, katika hali nyingi, anaachwa kufanya kazi ngumu toka asubuhi mpaka usiku, damu yake ikizidi kupata moto sana wakati anapoandaa vyakula mbalimbali visivyofaa kwa afya ili kukidhi ladha iliyoharibika ya familia yake pamoja na wageni. Afya yake ingepaswa kutunzwa vizuri sana. Maandalizi ya chakula kinachofaa kwa afya yangehitaji karibu nusu ya gharama na kazi iliyofanyika, nacho kingekuwa na lishe bora zaidi.

Mara nyingi mama anaachwa kufanya kazi kuliko uwezo wake, kabla ya kujifungua watoto wake. Mizigo na masumbuko yake ni shida mno kumpunguzia, na kipindi kile ambacho kwake kingekuwa cha mapumziko kabisa, huwa kipindi kimojawapo cha uchovu kutokana na kazi nyingi, huzuni, na kununa kwake. Kutumia nguvu nyingi mno kufanya kazi kwa upande wake, humfanya awanyime watoto wake watakaozaliwa lishe ile aliyoiweka Mungu katika maumbile yake, na kwa kuifanya damu yake iwe ya moto sana, anaifanya damu yake kuwa mbaya na chafu. Mtoto hunyang'anywa nguvu zake za mwili na akili. Baba na ajifunze njia ya kumfanya mke wake awe na furaha. Asingerudi nyumbani kwake akiwa na uso uliokunjamana. Kama ana matatizo yo yote kazini kwake, basi, asimsumbue mkewe na mambo kama hayo, isipokuwa kama kweli ni lazima kushauriana na mke wake. Mkewe anayo masumbufu na majaribu yake mwenyewe yanayomsumbua, na kwa huruma
angesamehewa asiongezewe mzigo mwingine wo wote usiokuwa wa lazima.

Mara nyingi mno mama huyo anakutana na ukimya baridi kutoka kwa baba. Endapo mambo yote hayaendi vizuri kama vile ambavyo yeye angetaka, basi, anamlaumu mke na mama, wala hayajali masumbufu ya mkewe na majaribu yake ya kila siku. Wanaume wanaofanya hivyo wanakwenda kinyume na matakwa na furaha yao wenyewe. Mama anakatishwa tamaa. Tumaini na uchangamfu huondoka kwake. Anafanya kazi yake kama mashine, akijua kwamba ni lazima ifanywe, na jambo hilo mara moja huleta kupotea kwa afya ya mwili na ya akili. Watoto wanaozaliwa kwao huteseka kwa magonjwa mbalimbali, na Mungu anawashikilia wazazi hao kuwa wanahusika kwa kiwango kikubwa; kwa maana yalikuwa ni yale mazoea yao mabaya yaliyoingiza ugonjwa huo katika miili ya watoto wao
waliokuwa bado hawajazaliwa, ambao chini ya ugonjwa huo wanalazimika kuteseka maisha yao yote. Baadhi yao huishi kwa kipindi kifupi tu wakiwa wamelemewa na mzigo wao wa udhaifu. Mama anaangalia maisha ya mtoto wake huyo anapolazimika kufumba macho yake na kufa; na mara nyingi anamwona Mungu kuwa ndiye chanzo cha mateso hayo yote, ambapo kusema kweli wazazi wenyewe ndio wauaji hasa wa mtoto wao huyo.

Baba na akumbuke kwamba anavyomtendea mke wake kabla ya kuzaliwa mtoto wake ataathiri kimwili tabia ya mama wakati wote wa kipindi hicho, naye atahusika na tabia atakayokuwa nayo mtoto huyo baada ya kuzaliwa kwake. Akina baba wengi wamekuwa na wasiwasi wa kuchuma mali kwa haraka hata wamesahau kufikiria mambo makuu; wengine kwa uhalifu wao wameacha kuwajali akina mama na watoto wao, na mara nyingi mno maisha yao wote wawili yametolewa mhanga kwa tamaa nyingi ya kulundika mali. Wengi hawapati adhabu kali pale pale kwa vitendo vyao vibaya, nao hulala usingizi [huzubaa] wasijue matokeo ya njia yao. Hali ya mke wakati mwingine huwa sio nzuri kuliko ile ya
mtumwa; na wakati mwingine yeye [mwenyewe] ana hatia, sawa na ile ya mumewe, kwa kutapanya nguvu za mwili ili kupata fedha za kumwezesha kuishi kama wanavyoishi watu wa siku hizi. Ni dhambi kwa watu kama hao kuzaa watoto; maana watoto wao watapungukiwa nguvu kimwili, kiakili, na kimaadili, nao watachukua chapa ile ile ya wazazi wao ya umaskini, ubahili, na uchoyo, na ulimwengu utateseka kwa ubahili wao.

Ni wajibu wa wanaume na wanawake kutumia akili kuhusu kazi zao. Wasingemaliza nguvu zao zote bila sababu; maana kwa kufanya hivyo, hawaleti mateso tu juu yao wenyewe, bali, kwa makosa yao, wanaleta wasiwasi, uchovu, na mateso juu ya wale wawapendao. Ni nini kinachomfanya mtu afanye kazi kiasi hicho? ----- Utovu wa kiasi katika kula na kunywa, tamaa ya kupata mali, vimewashawishi wengi kutokuwa na kiasi katika kufanya kazi zao. Uchu wa chakula ukidhibitiwa, halafu chakula chenye afya tu kikiliwa, kutakuwa na uokoaji mkubwa sana wa matumizi hata wanaume na wanawake
hawatalazimika kufanya kazi kuliko uwezo wao, wala kwa njia hiyo kuzivunja amri zile sita za mwisho za Yehova, ambazo zinaamuru wajibu wa mwanadamu kwa mwanadamu mwenzake, wala kwa njia hiyo kujiweka wenyewe mahali ambapo haiwezekani kwao kumtukuza Mungu katika miili yao na roho zao, vyote hivyo ambavyo ni mali yake. Iwapo, katika haraka yao ya kuwa matajiri, wanatumia nguvu zao nyingi kuliko kawaida, na kuvunja sheria za maumbile yao, basi, wanajiweka wenyewe katika hali ambayo hawawezi kumpa Mungu huduma yao kamilifu, na kwa ajili hiyo wanaifuata njia ya dhambi. Mali iliyopatikana kwa njia hiyo inapatikana kwa kujitoa mhanga mno.

Mara kwa mara kazi ngumu na masumbuko humfanya baba awe na harara, akose subira, na kuwa mkali. Hauoni mwonekano wa kuchoka alio nao mke wake, ambaye amefanya kazi kwa kutumia nguvu zake hafifu kwa nguvu kama yeye alivyofanya kwa kutumia nguvu zake nyingi zaidi. Anajiachia mwenyewe kuharakishwa na kazi, na katika wasiwasi wake wa kuwa tajiri, anapoteza ile maana ya uwajibikaji wake kwa familia yake, naye hawezi kupima kwa haki uwezo wa mkewe wa kustahimili. Mara nyingi anapanua shamba lake, akihitaji kusaidiwa, jambo ambalo linaongeza kazi ya nyumbani. Mke anatambua kila siku ya kuwa anafanya kazi nyingi mno kuliko uwezo wake, lakini anaendelea tu kufanya kazi, akifikiri kwamba kazi hiyo haina budi kufanywa. Daima anaendelea kuufikia wakati ujao,
akichota nguvu zake ambazo angezitumia wakati ujao kwa matumizi ya sasa, naye anaishi kwa mtaji [wa nguvu] uliokopwa; na wakati ule atakapozihitaji nguvu hizo, atakuwa hanazo, na kama hatapoteza maisha yake, basi, mwili wake utaharibika kiasi cha kutoweza kupona tena.

Kama baba angeijua sheria ile ya maumbile, basi, angeweza kuelewa vizuri zaidi wajibu wake na kazi zake. Angeona kwamba amekuwa na hatia ya kuwa karibu kuwaua watoto wake, kwa kuacha mizigo mingi sana kuja juu ya mama, na kumlazimisha kufanya kazi kuliko uwezo wake kabla ya kuwazaa, ili kuchuma fedha kwa ajili ya kuwaachia. Wanawalea watoto hao katika maisha yao yote wakiwa wanateseka, na mara nyingi wanawalaza mapema kaburini, wasiweze kutambua hata kidogo kwamba njia yao mbaya ndiyo iliyoleta matokeo hayo ya hakika. Ni bora jinsi gani kumlinda mama wa watoto hao ili asifanye kazi ya kuchosha sana, wala kuwa na wasiwasi kimawazo, na kuwaacha watoto kurithi afya njema ya mwili, na kuwapa nafasi ya kupambana na maisha pasipo kutegemea mali ya baba yao, bali ile inayopatikana kwa nguvu zao wenyewe! Uzoefu watakaoupata utakuwa wa thamani kwao kuliko kurithi nyumba na mashamba yaliyonunuliwa kwa hasara ya afya ya mama na watoto.

Linaonekana kuwa ni jambo la kawaida kabisa kwa wanaume wengine kuwa na hasira, uchoyo, ukali, na uonevu. Hawajajifunza kamwe fundisho la kujitawala nafsi zao, wala hawatajizuia kuwa na hisia zao za kijinga, pasipo kujali matokeo yanayoweza kutokea. Watu kama hao watalipwa maradufu kwa kuwaona wenzi wao wakiwa dhaifu na kuvunjika moyo, na watoto wao wakiwa na tabia zile zile za ajabu zinazochukiza.

Ni wajibu wa kila mume na mke waliooana kuwa na bidii kwa kutoziumbua hisia za kila mmoja wao. Wangejizuia wasiwe na mwonekano wo wote wa kunung'unika, wala hasira kali. Wangejifunza mambo madogo na makubwa yanayochangia furaha ya kila mmoja wao, wakionyesha upole kwa kukumbuka kutoa shukrani kwa matendo mema waliyotendewa pamoja na heshima ndogo ndogo. Mambo haya madogo yasipuuzwe; kwa maana ni ya maana kwa furaha ya mume na mke kama vile kilivyo chakula katika kuhifadhi nguvu za mwili. Baba amtie moyo mke na mama ili apate kuutegemea upendo wake. Maneno ya upole, uchangamfu, kumtia moyo kutoka kwake [mume] ambaye amemkabidhi furaha ya
maisha yake yatakuwa na msaada mwingi sana kwake kuliko dawa nyingine yo yote; na mionzi ya mwanga ya furaha iletwayo na maneno ya faraja kama hayo itaingia ndani ya moyo wa mke na mama, na kuakisi mionzi ya furaha yake mwenyewe juu ya moyo wa baba.

Mume siku zote atamwona mkewe kuwa amechoka kwa shughuli nyingi na kudhoofika, akigeuka na kuwa mzee mapema, kwa kusumbuka kutayarisha chakula ili kukidhi ladha yake [mume] iliyoharibika. Mume anautosheleza uchu wake wa chakula, naye anakula na kunywa vitu vile vinavyochukua muda mwingi na kazi nyingi kuviandaa ili vipate kuliwa mezani, vile vilivyo na mwelekeo wa kuwafanya wale wanaovila vyakula hivyo visivyofaa kwa afya kuwa wepesi kushtuka na kukasirika. Ni shida kwa mke na mama kukosa kuumwa kichwa, na watoto nao huathirika kutokana na matokeo ya kula chakula hicho kisichofaa kwa afya, na kunakuwa na ukosefu mkubwa wa uvumilivu na upendo kati ya wazazi na watoto wao. Wote wanateseka kwa pamoja; maana afya yao imetolewa mhanga kwa tamaa mbaya ya uchu wa chakula. Mtoto, kabla ya kuzaliwa kwake, anakuwa ameambukizwa ugonjwa na uchu wa chakula usiofaa kwa afya. Harara, machachari, na kukata tamaa kunakodhihirishwa na mama huyo kutapigwa chapa na kuonekana katika tabia ya mtoto wake.

Kama akina mama, katika vizazi vilivyopita, wangalikuwa wamejielimisha wenyewe juu ya sheria zinazotawala maumbile yao, wangekuwa wameelewa kwamba nguvu yao ya afya ya mwili pamoja na hali ya maadili yao, na akili zao, kwa sehemu kubwa vingeonekana ndani ya watoto wao. Ujinga wao juu ya somo hili, ambalo linagusa mambo mengi mazito, ni uhalifu. Wanawake wengi wasingestahili kamwe kuwa mama wa watoto. Damu yao ilijazwa na ugonjwa wa kuvimba tezi shingoni (scrofula), nayo ilikuwa imerithiwa kutoka kwa wazazi wao, na ilizidi kuchafuliwa kwa mtindo wao mbaya wa maisha. Akili imepungua nguvu yake sana, na kuwa mtumwa wa kuzitumikia tamaa za kinyama za mwili. Watoto wanaozaliwa na wazazi kama hao wamekuwa watesekaji wakubwa, wala hawana
faida kubwa kwa jamii.

Hii ndiyo sababu kuu kuliko zote ya udhaifu wa mwili wa vizazi vilivyotangulia, wake na mama, ambao huenda wangekuwa na mvuto wenye manufaa katika jamii kwa kuinua kiwango cha maadili, hawaonekani katika jamii kutokana na shughuli zao za nyumbani ambazo ni nyingi mno, kwa sababu ya mitindo yao ya mapishi ya kisasa ambayo inaathiri afya, na pia kama matokeo ya kuzaa watoto mara kwa mara. Mama amelazimika kuendelea kupata mateso yasiyokuwa ya lazima, afya yake imepungua sana, na akili yake imedhoofika kutokana na nguvu nyingi sana zinazochotwa kutoka kwenye akiba yake. Watoto wake wanateseka kwa sababu ya udhaifu wake kimwili, na kwa kushindwa kuwasomesha, basi, jamii inakuwa imetupiwa watu maskini wasiokuwa na faida yo yote.

Kama mama hao wangekuwa wamezaa watoto wachache tu, na kama wangekuwa waangalifu kula chakula kile tu kitakachoihifadhi afya ya mwili na nguvu ya akili, ili kwamba maadili na akili vipate kuutawala mwili wa kinyama, basi, wangekuwa wameweza kuwasomesha vizuri sana watoto wao ili wawe na manufaa hata kuweza kuwa mapambo yanayong'aa kwa jamii yao.

Endapo katika vizazi vilivyopita wazazi, kwa kusudi thabiti, wangekuwa wameuweka mwili wao kuwa mtumwa wa akili, na endapo wangekuwa hawajaziachia akili zao kutawaliwa na tamaa za kinyama za mwili, basi, katika kizazi hiki pangekuwa na watu walio tofauti kabisa juu ya uso wa dunia hii. Na endapo mama, kabla ya kujifungua mtoto wake, angekuwa daima amejitawala mwenyewe, akiwa anatambua fika ya kuwa anagawa chapa ya tabia yake kwa vizazi vijavyo, basi, hali ya jamii ya leo isingekuwa imeshuka sana katika maadili ya tabia.

Kila mwanamke anayekaribia kuwa mama, haidhuru mazingira yake yaweje, angejitahidi daima kuwa na mwelekeo wa furaha na kuridhika, akijua kwamba kwa juhudi yake yote kuelekea upande huo atalipwa mara kumi katika hali bora, kimwili na kimaadili, ya watoto wake. Wala hayo si yote. Kwa mazoezi anaweza kujizoeza mwenyewe kuwa na mawazo ya furaha, na kwa njia hiyo kuufanya moyo wake uwe na hali ya furaha, na uweze kuakisi roho yake ya uchangamfu kwa familia yake, na wale anaoshirikiana nao. Na kwa kiwango kikubwa sana afya yake itazidi kuongezeka. Nguvu itaongezwa kwenye chemchemi zake za uzima; damu yake haitaenda kigoigoi mwilini mwake, kama vile ambavyo ingekuwa endapo angejiachia na kukata tamaa na kununa. Afya yake kiakili na kimaadili inatiwa nguvu kwa ukunjufu wa moyo wake. Nguvu ya nia yake inaweza kuzuia mawazo ya moyo wake, tena itathibitika kuwa ndicho kitulizo kikuu cha mishipa yake ya fahamu. Watoto wanaodhulumiwa nguvu ile ya uhai ambayo wangepaswa kuirithi kutoka kwa wazazi wao wanahitaji uangalifu mkubwa kuwatunza. Kwa kuangalia kwa karibu-karibu zile sheria zinazotawala maumbile yao, hali nzuri zaidi ya afya inaweza kuimarishwa.

Kipindi kile mtoto mchanga anachoendelea kunyonyeshwa na mama yake ni nyeti sana. Akina mama wengi, wakiwa wanawanyonyesha watoto wao wachanga, wamejiachia kufanya kazi kupita kiasi, na kuifanya damu yao iwe ya moto sana wanaposhughulika na mapishi jikoni; na kwa njia hiyo unyonyeshaji huo umeathirika vibaya sana, sio tu kutokana na hali ya uchafuzi wa lishe wanayoipata kwa kunyonya maziwa ya mama hao, bali damu yao pia inasumishwa kutokana na lishe isiyofaa kwa afya kutoka kwa maziwa ya mama hao, ambao mfumo wote wa miili yao umechafuliwa, kwa njia hiyo kuweza kuathiri chakula cha watoto hao. Mtoto mchanga anaathirika pia kulingana na hali ya moyo wa
mama yake. Kama hana furaha, ni mwepesi kupata wasiwasi, ana harara, anafoka mara kwa mara, basi, lishe anayoipata mtoto huyo mchanga kutoka kwa mama yake itakuwa inawaka moto, mara nyingi ikisababisha msokoto wa tumbo (colic), mshtuko, na, mara nyingine, kusababisha kifafa au hamaki.




Kwa wastani tabia ya mtoto huathirika pia kutokana na aina ya lishe anayoipata kutoka kwa mama yake. Basi, ni muhimu jinsi gani kwamba mama, anapomnyonyesha mtoto wake mchanga, aweze kuitunza hali ya moyo wake kuwa ya furaha, akiwa na udhibiti kamili juu ya moyo wake. Kwa kufanya hivyo, chakula cha mtoto hakiathiriwi, tena hali ile ya utulivu, kujitawala, anayokuwa nayo mama huyo katika kushughulika na mtoto wake inachangia sana katika kuufanya moyo wa mtoto huyo mchanga kuwa na mwelekeo mzuri. Kama mtoto mchanga anashtuka-shtuka, anakuwa mwepesi kuwa na wasiwasi, basi, hali ya mama ya uangalifu, usiokuwa na haraka, itakuwa na mvuto wa kumtuliza na kumweka sawa; kisha ndipo afya ya mtoto huyo mchanga itakapoendelea kuwa nzuri zaidi na zaidi. Watoto wachanga wamedhulumiwa sana kwa kuwatendea isivyokuwa sawa. Kama wana machachari, kwa kawaida huwa wanalishwa ili kuwafanya wanyamaze, ambapo, katika hali nyingi, kuwapa chakula kingi mno, kunakotokana na tabia mbaya ziletazo madhara ambazo akina mama hao wanazo, ndiyo hasa sababu ya machachari hayo. Kuwapa chakula zaidi hufanya mambo kuwa mabaya zaidi; kwa maana tumbo lilikuwa limejazwa tayari na chakula kingi mno.

Watoto hao huwa wanalelewa toka uchanga wao kwa kuwaendekeza uchu wao wa chakula, nao wanafundishwa ya kuwa wanaishi kwa ajili ya kula. Mama anachangia sana katika ujenzi wa tabia za watoto wake wakati wa utoto wao. Anaweza kuwafundisha kuutawala uchu wao wa chakula, ama anaweza kuwafundisha kukidhi uchu wao wa chakula, na kuwafanya wawe walafi. Mara nyingi mama anapanga kumaliza kiasi fulani cha kazi kwa siku nzima; na watoto wanapomsumbua, badala ya yeye kutumia wakati fulani kuzituliza huzuni zao ndogo ndogo, na kuwafanya washughulike na mambo mengine, yeye anawapa kitu fulani cha kula, ili kuwafanya watulie. Jambo hilo linafanikiwa kulitimiza kusudi hilo kwa muda mfupi tu, lakini hatimaye hufanya mambo yawe mabaya zaidi. Matumbo ya
watoto hao hushindiliwa na chakula wakati hawana haja hata kidogo ya kutaka kula chakula. Kinachotakiwa hasa ni kwa mama huyo kutumia wakati wake kidogo na kuwasikiliza. Lakini yeye anaona kabisa kuwa wakati wake ni wa thamani mno kuweza kuutumia kwa kuwafurahisha watoto wake. Pengine ni kuipanga vizuri nyumba yake kwa njia inayopendeza ili wageni wakija wamsifu, tena pengine ni kupika chakula cha mitindo ya kisasa, hayo ndiyo mawazo yanayopata kipaumbele kichwani mwake kuliko furaha na afya ya watoto wake.

Kutokuwa na kiasi katika kula na kufanya kazi huwadhoofisha wazazi, mara nyingi huwafanya wawe na machachari, na kuwafanya wasiweze kufaa kutekeleza wajibu wao kwa watoto wao. Mara tatu kwa siku wazazi na watoto hukusanyika kuizunguka meza iliyojaa vyakula mbalimbali vya mitindo ya kisasa. Utamu wa kila chakula ni lazima uonjwe. Pengine mama amefanya kazi ngumu hadi amepata joto jingi mwilini mwake na kuchoka sana, naye hayuko katika hali ya kula hata chakula chepesi sana mpaka kwanza apate muda fulani wa kupumzika. Chakula hicho alichosumbuka kukiandaa hakifai kabisa kwake kwa wakati uwao wote ule, bali kinavilemea viungo vyake vya kuyeyusha chakula
hapo damu yake inapokuwa ya moto sana na mwili mzima kuchoka. Wale wanaozidi kuzivunja sheria za maumbile yao watalazimika kulipa adhabu wakati fulani katika kipindi cha maisha yao.

Kuna sababu nyingi kwa nini duniani humu kuna wanawake wengi wenye machachari, wanaolalamika kwamba matumbo yao hayayeyushi chakula vizuri, pamoja na kuwa na msururu wa uovu mwingine unaoambatana nalo. Sababu imefuatiwa na matokeo ya hakika. Haiwezekani kwa watu walio na utovu wa kiasi kuwa wavumilivu. Wengi huwa hawaonekani kuelewa uhusiano uliopo kati ya akili na mwili. Kama mfumo mzima wa mwili umeathirika kwa kula chakula kisichofaa, basi, ubongo na neva huathirika, na mambo madogo tu huwaletea kero wale walioathirika hivyo. Matatizo madogo kwao ni milima mirefu ya matatizo. Watu walio na hali kama hiyo hawafai katika kuwalea vizuri watoto wao. Maisha yao yatakuwa hayana mipaka; mara nyingine watawadekeza sana watoto wao, na mara nyingine watakuwa wakali sana, wakiwakaripia watoto wao kwa mambo madogo mno yasiyostahili hata kuyaangalia.

Mara kwa mara mama anawatuma watoto wake kwenda mbali naye kwa sababu anadhani hawezi kustahimili makelele yao yanayosababishwa na michezo yao ya furaha. Lakini bila jicho la mama yao kuwa juu yao kukubali ama kutokubali michezo yao kwa wakati unaofaa, tofauti kati yao mara nyingi hutokea. Neno moja tu kutoka kwa mama lingewaweka wote kuwa sawa tena. Wanachoka upesi na kutaka mabadiliko, nao huenda barabarani kujifurahisha; na watoto safi hao, wasio na hatia mioyoni mwao wanaswagwa kwenda kujiunga na makundi mabaya, na huko mawasiliano machafu yanayonong'onezwa masikioni mwao huharibu mwenendo wao mwema. Mama mara nyingi hulala usingizi [huzubaa] asijue wanachopenda watoto wake, mpaka hapo atakapoamshwa kwa uchungu
hapo atakapouona uovu wao. Mbegu mbaya zilipandwa katika mioyo yao michanga zikileta matumaini ya mavuno mengi. Na kwake linakuwa ni jambo la kumshangaza kuona kwamba watoto wake wana mwelekeo wa kutenda mabaya. Wazazi wangeanza kwa majira yake kuweka ndani ya mioyo michanga kanuni nzuri na sahihi. Mama anapaswa kuwa na watoto wake kwa wakati mwingi kwa kadiri inavyowezekana, tena anapaswa kupanda mbegu za thamani mioyoni mwao.

Wakati alio nao mama kwa njia ya pekee ni mali ya watoto wake. Wanayo haki kuutumia wakati wake kuliko wengine wawezavyo kuupata. Katika hali mbalimbali akina mama wameacha kuwaadibisha watoto wao, kwa sababu jambo hilo lingeweza kuwachukulia muda wao wote ambao wanadhani unapaswa kutumika katika idara ya mapishi, au katika kushona nguo zao wenyewe, pamoja na zile za watoto wao, kwa kufuata mitindo ya kisasa, kukuza kiburi katika mioyo yao michanga. Ili kuwafanya watoto wao watukutu kutulia, wanawapa keki, au vitu vitamu kama kashata (candies), karibu kwa saa yo yote ya siku, na matumbo yao yanajazwa na vitu vinavyodhuru bila kufuata utaratibu wa saa za kula. Nyuso zao zilizopauka hushuhudia ukweli kwamba mama zao wanafanya kila wanaloweza kuharibu nguvu za akiba zilizobaki za watoto wao wanyonge. Viungo vya kuyeyusha chakula huwa vinalemewa kila wakati, wala havipewi muda wa kupumzika. Ini linaanza kupoteza nguvu yake ya kufanya kazi, damu inakuwa chafu, na watoto wanakuwa dhaifu na wepesi kukasirika, kwa sababu wao ndio watesekaji hasa kutokana na utovu wa kiasi; na haiwezekani kwao kuwa na uvumilivu.

Wazazi wanashangaa kwamba watoto siku hizi ni vigumu sana kuwaongoza kama ilivyokuwa zamani, ambapo, kwa hali nyingi, ni uhalifu wao katika uongozi wao uliowafanya watoto kuwa hivyo. Aina ya chakula wanacholeta mezani pao, na kuwashawishi watoto wao kukila, hicho ndicho kinachochochea daima tamaa zao za kinyama, na kuzidhoofisha nguvu zao za maadili na kiakili. Watoto wengi sana wanakuwa na ugonjwa wa kusikitisha wa tumbo lao kushindwa kuyeyusha chakula vizuri tangu ujana
wao kutokana na mwenendo mbaya wa wazazi wao walioufuata kuelekea kwa watoto wao. Wazazi hao watatakiwa kutoa hesabu kwa Mungu kwa kuwatendea hivyo watoto wao. Wazazi wengi hawawapi watoto wao mafundisho juu ya kujizuia (self-control).

Wanawaendekeza kwa kukidhi uchu wao wa chakula, na kujenga tabia za watoto wao za kula na kunywa kama tamaa zao zinavyotaka tangu utotoni. Hivyo ndivyo watakavyokuwa katika tabia zao za kawaida wakati wa ujana wao. Tamaa zao hazikuzuiwa; nao wanapoendelea kukua kuelekea uzeeni, hawatakidhi tabia zile tu za kawaida za utovu wa kiasi, bali wataendelea mbele zaidi katika kujifurahisha kwa tamaa zao. Watajichagulia wenzi wao wenyewe, japokuwa ni wafisadi. Hawawezi kustahimili zuio lo lote kutoka kwa wazazi wao. Watajiachilia kabisa na kutimiza tamaa mbaya za miili yao, wala
hawatathamini sana usafi wa maisha, wala maadili mema. Hii ndiyo sababu kuna usafi wa maisha kidogo sana pamoja na maadili mema miongoni mwa vijana wa siku hizi, na hiyo ndiyo sababu kuu kwa nini wanaume na wanawake hawajisikii hata kidogo kuwajibika kutoa utii wao kwa Sheria ya Mungu [Amri Kumi]. Wazazi wengine hawajizuii nafsi zao kabisa. Hawautawali uchu wao mbaya wa chakula, wala hasira zao kali sana; kwa ajili hiyo, hawawezi kuwalea watoto wao kuukana uchu wao wa chakula, wala kuwafundisha kujizuia nafsi zao.

Akina mama wengi wanaona ya kwamba hawana muda wa kuwafundisha watoto wao, tena ili kuwaondolea mbali, huwapeleka shuleni. Chumba cha darasa ni mahali pa shida kwa watoto wale waliorithi miili yenye afya mbaya. Vyumba vya madarasa kwa kawaida havijajengwa kwa kuzingatia afya, bali kwa kuzingatia gharama ndogo. Vyumba havijapangwa kwa namna ambayo vinaweza kuwa na vitobo vya kuingizia na kutolea hewa, kama ambavyo ingetakiwa kuwa, bila kuwaacha watoto kupata mafua makali. Na viti navyo kwa nadra sana vimetengenezwa ili watoto waweze kukaa kwa raha, na kuiweka miili yao midogo katika hali sahihi ya kukaa ili kuhakikisha kwamba mapafu yao na moyo vinafanya kazi zao kiafya. Watoto wadogo wanaweza kukua wakiwa na umbo liwalo lote, nao
wanaweza kuwa na maumbo yenye afya kwa kufanya mazoezi ya viungo yanayofaa na kuweka miili yao katika hali nzuri ya kukaa. Ni kuharibu afya na maisha ya watoto kuwafanya wakae juu ya viti vigumu, vilivyotengenezwa vibaya, kwa masaa matatu hadi matano kwa siku, wakiwa wanavuta hewa chafu inayotokana na pumzi nyingi za watoto wengi waliomo humo. Mapafu yao dhaifu yataathirika; tena ubongo, ambao ndilo chimbuko la nguvu ya neva za mwili wote, unadhoofika kwa kutumika sana kabla viungo vya ubongo huo havijakomaa vya kutosha kuweza kustahimili uchovu huo.

Katika chumba hicho cha darasa kwa hakika msingi umewekwa kwa magonjwa ya kila aina. Lakini, zaidi hasa, ubongo ambao ni kiungo chororo mno kuliko viungo vyote, mara nyingi umepata madhara ya kudumu kwa kutumika kupita kiasi. Mara nyingi hali hiyo imesababisha uvimbe unaowasha ubongoni, halafu maji-maji (dropsy) ndani ya kichwa, na kifafa, kikiambatana na matokeo yake ya kutisha. Na maisha ya watoto wengi yametolewa mhanga na mama zao wenye kutaka makuu. Kuhusu watoto wale ambao wameonekana kuwa na afya ya mwili ya kutosha kuweza kustahimili hali hiyo, wako wengi ambao miilini mwao wanabeba matokeo hayo kwa maisha yao yote. Nguvu ya mishipa ya fahamu ubongoni mwao hupungua sana hata wanapofikia utu uzima inakuwa haiwezekani kwao kuweza kustahimili mazoezi mengi yanayohitaji kutumia akili. Nguvu ya baadhi ya viungo vyororo vya ubongo huonekana kuwa imetumika yote.

Sio tu afya ya kimwili na kiakili ya watoto inayohatarishwa kwa kupelekwa kwao shuleni wakiwa na umri mdogo sana, bali pia wanapoteza tukiangalia upande ule wa maadili. Wamekuwa na fursa ya kufahamiana na watoto ambao hawakuwa na adabu njema. Walitupwa katika jamii ya walio na lugha chafu na wakorofi, waongo, wanaoapa ovyo, wezi, na wadanganyifu, na wale wanaofurahia kugawa maarifa yao ya kutenda maovu kwa wale walio na umri mdogo kuliko wao wenyewe. Watoto wadogo, wakiachwa peke yao, wanajifunza mabaya kwa haraka kuliko kujifunza yaliyo mema. Tabia mbaya zinakubaliana sana na moyo wa asili, na mambo yale watoto hao wanayoyaona na kuyasikia wakati
wangali wachanga na utotoni yanazama kabisa na kukaa katika mioyo yao; na mbegu hiyo mbaya iliyopandwa katika mioyo yao michanga itaota, nayo itakuwa miiba mikali ya kuiumiza mioyo ya wazazi wao.

Katika kipindi cha kwanza cha miaka sita au saba ya maisha ya mtoto uangalifu maalum ungetolewa kwa ajili ya kumlea kimwili kuliko kwa kumlea kiakili. Baada ya kipindi hiki, kama afya ya mwili wake ni nzuri, basi, elimu ya pande zote mbili ingeangaliwa. Utoto uchanga unaendelea hadi kufikia umri wa miaka sita au saba. Mpaka kufikia kipindi hicho, watoto hao wangeachwa huru kama wana-kondoo kutangatanga ndani ya nyumba, na uani kwa furaha inayobubujika mioyoni mwao, wakirukaruka kwa kuzungusha kamba kichwani na kurandaranda huku na huko, wakiwa hawana wasiwasi wo wote wala shida Wazazi, hasa akina mama, wangekuwa ndio waalimu pekee wa mioyo hiyo michanga ya watoto. Wasingewaelimisha kutokana na vitabu. Kwa kawaida watoto watakuwa wadadisi katika kujifunza viumbe vya asili. Watauliza maswali kuhusu vitu wanavyoviona na kuvisikia, na wazazi hao wangeutumia vizuri muda huo kuwafundisha, na kwa uvumilivu wao kuyajibu maswali yao madogodogo. Kwa njia hii, wanaweza kumshinda adui, na kuimarisha mioyo ya watoto wao kwa kupanda mbegu njema mioyoni mwao, wasiache nafasi yo yote kwa maovu kuotesha mizizi yake humo. Mafundisho ya mama yaliyojaa upendo kwa umri huo mdogo ulio mwepesi kudhurika ndiyo yanayohitajiwa na watoto hao ili kujenga tabia zao.

Fundisho la kwanza kwa watoto ni kuwafundisha kujikana tamaa yao ya chakula. Ni jukumu la akina mama kuyashughulikia mahitaji ya watoto wao kwa kuituliza mioyo yao kufanya mambo mengine, badala ya kuwapa chakula, na kuwafundisha kwa njia hiyo kuwa kula chakula ni dawa ya kutibu magonjwa yote ya maisha. Kama wazazi wangekuwa wameishi kiafya, na kuridhika na chakula rahisi, basi, gharama nyingi zilizotumika zingekuwa zimeokolewa. Baba asingelazimika kufanya kazi kuliko
uwezo wake ili kukidhi mahitaji ya familia yake. Chakula cha kawaida chenye virutubisho kisingekuwa na mvuto ule usiofaa unaouchochea mfumo wa neva na kuziamsha tamaa za mwili za kinyama, na kuleta chuki na harara. Kama angekuwa amekula chakula kile tu kilicho cha kawaida, kichwa chake [ubongo] kingekuwa safi, neva zake zingetulia, tumbo lake lingekuwa katika hali bora zaidi ya afya kuliko ilivyo sasa. Lakini hata sasa, katika kipindi hiki cha mwisho, tunaweza kufanya kitu fulani ili kuboresha hali yetu ya afya. Kuwa na kiasi katika mambo yote ni jambo la muhimu. Baba mwenye kiasi hatalalamika endapo haoni vyakula vingi vya aina mbalimbali mezani. Njia hii ya kuishi kiafya
itaboresha hali ya afya ya familia kwa kila njia, na kumpa nafasi mke na mama kutumia muda fulani kwa ajili ya watoto wake. Fundisho kubwa la kujifunza kwa wazazi litakuwa kutafuta jinsi gani wanaweza kuwalea vizuri sana watoto wao ili wawe na manufaa katika ulimwengu huu, na mbinguni baada ya hapa. Wataridhika kama watawaona watoto wao wakiwa na mavazi safi ya kawaida, yaletayo raha kuyavaa, yasiyokuwa na nakshi na mapambo; tena watajitahidi kwa dhati kuona kwamba [watoto wao] wanalo pambo lile la ndani, pambo la roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

Kabla baba huyo Mkristo hajaondoka nyumbani kwake na kwenda kazini kwake, ataikusanya familia yake kumzunguka, akiinamisha kichwa chake mbele za Mungu, atawaweka katika ulinzi wa Mchungaji Mkuu. Kisha ndipo ataenda kazini kwake kwa upendo na baraka za mke wake, pamoja na upendo wa watoto wake, mambo ambayo yataufanya moyo wake kuchangamka saa zote za kufanya kazi yake. Na mama yule aliyeamshwa na kuuona wajibu wake anatambua mzigo uliowekwa juu yake wa watoto
wake wakati baba hayupo. Atajisikia ya kwamba anaishi kwa ajili ya mume na watoto wake. Kwa kuwalea watoto wake ipasavyo, akiwafundisha tabia ya kuwa na kiasi na kujizuia, tena akiwafundisha wajibu wao kwa Mungu, anawatayarisha kuwa na manufaa katika ulimwengu huu, na kuziinua juu kanuni za maadili katika jamii, na kuiheshimu na kuitii sheria ya Mungu [Amri Kumi]. Kwa uvumilivu na uthabiti mama huyo mcha Mungu atawafundisha watoto wake, akiwapa mstari juu ya mstari, kanuni juu ya kanuni, sio kwa njia ya ukali na kuwalazimisha, bali kwa upendo; na kwa upole atawaongoa. Watayafikiria mafundisho yake hayo ya upendo, nao kwa moyo wa furaha watayasikiliza maneno yake ya mafundisho.

Badala ya kuwafukuza mbele yake ili asipate kusumbuliwa na kelele zao, wala kuudhiwa na kule kutaka kwao kwingi ili awaangalie, atajisikia ya kwamba wakati wake usingetumika vizuri zaidi kuliko katika kuwabembeleza na kuugeuzia kando utukutu wao, na mioyo yao yenye shughuli nyingi kwa kuwapa jambo fulani la kuwaburudisha, au kazi nyepesi za kufurahisha. Mama huyu atalipwa maridhawa kwa juhudi zake hizo za kuvumbua mambo ya kuwaburudisha watoto wake.

Watoto wadogo wanapenda kuwa pamoja na kushirikiana. Kama jambo la kawaida, hawawezi kufurahi wakiwa wenyewe peke yao; na mama angejisikia kwamba, katika hali nyingi, mahali panapowafaa watoto wake, wanapokuwa nyumbani, ni katika chumba kile anachokaa mwenyewe. Hapo ndipo anapoweza kuwaangalia kwa juu juu, na kuwa tayari kusahihisha tofauti ndogo ndogo zinazojitokeza, wanapomwomba kufanya hivyo, na kusahihisha tabia zao potovu, au mwonekano wa uchoyo au hasira kali, naye anaweza kwa njia hiyo kuipa mioyo yao mwelekeo kwenda upande ule ulio mzuri. Kile wanachokifurahia watoto wanadhani mama atakifurahia, nalo ni jambo la kawaida kabisa kwao kumwomba ushauri wake katika mambo yao madogo yanayowatatiza. Tena, mama asiuumize moyo
wenye hisia kali wa mtoto wake kwa kulifanya jambo hilo kuwa halina maana, ama kwa kukataa kusumbuliwa na mambo madogo kama hayo. Kile ambacho kinaonekana kuwa kidogo kwa mama ni kikubwa kwa watoto wake. Neno moja la kuwaongoza, au onyo, kwa wakati unaofaa litakuwa la thamani kubwa. Mtazamo unaoonyesha kukubali, neno lile la kutia moyo, au kusifu, kutoka kwa mama, mara nyingi litautupa mwonzi ndani ya mioyo yao michanga kwa siku hiyo nzima.

Elimu ya kwanza ambayo watoto wangepaswa kupokea kutoka kwa mama wakati wangali wachanga ingehusu afya yao ya mwili. Wangeruhusiwa kula chakula kile tu kilicho cha kawaida, cha aina ile iwezayo kuwaweka katika hali njema kiafya; na hicho kingeliwa kwa wakati maalum uliopangwa, sio zaidi ya mara tatu kwa siku, na milo miwili ingekuwa bora zaidi kuliko mitatu. Watoto wakilelewa vizuri, watajifunza upesi kwamba hawawezi kupata kitu cho chote kwa kulia au kufanya machachari. Katika kuwalea watoto wake, mama huyo mwenye busara hatafanya mambo kwa kufuata raha yake ya sasa, bali kwa faida yao ya baadaye. Na kwa mwisho huu, atakuwa amewafundisha somo muhimu la kutawala uchu wao wa chakula, na kujinyima ili wapate kula, kunywa, na kuvaa kwa kuzingatia afya yao.

Familia ile iliyolelewa vizuri, impendayo na kumtii Mungu, itakuwa na ukunjufu na furaha kila siku. Baba anaporudi kutoka kazini, hataleta matatizo yake nyumbani. Atajisikia kwamba nyumbani, na familia yake, ni mambo matakatifu mno kuweza kuyaharibu kwa kuleta matatizo yake ya kusikitisha. Alipoondoka nyumbani hakumwacha nyuma Mwokozi wake wala dini yake. Vyote viwili alivifanya wenzi wake. Mvuto mzuri wa nyumbani mwake, mbaraka wa mke wake, na upendo wa watoto wake, huufanya mzigo wake kuwa mwepesi; naye anarudi nyumbani akiwa na amani moyoni mwake, pamoja na ukunjufu, na maneno ya kuwatia moyo mkewe na watoto wake, ambao wanamngojea kwa furaha
kumkaribisha. Wakati anapoinamisha kichwa chake pamoja na familia yake katika madhabahu ile ya maombi ili kumshukuru Mungu kwa ulinzi wake kwake mwenyewe na kwa wapendwa wake kwa siku nzima, malaika wa Mungu hurukaruka juu ya chumba hicho, na kuyachukua maombi hayo ya dhati ya wazazi hao wanaomcha Mungu mpaka mbinguni, kama manukato mazuri, ambayo hujibiwa kwa njia ya baraka zinazowarudia.

Wazazi wawasisitizie watoto wao kwamba ni dhambi kutafuta ladha ya chakula kwa madhara ya tumbo lao. Wangeweka katika mioyo yao dhana ya kwamba kwa kuzivunja sheria za maumbile yao wanatenda dhambi juu ya Muumba wao. Watoto waliolelewa kwa jinsi hiyo hawatakuwa wagumu kuwazuia. Hawatakuwa na harara, hasira za vipindi, nao watakuwa katika hali bora zaidi ya kuyafurahia maisha yao. Watoto kama hao watakuwa wepesi kuelewa wajibu wao kimaadili. Watoto waliofundishwa hivyo kusalimisha mapenzi na matakwa yao kwa mapenzi yale ya wazazi wao watakuwa wepesi na rahisi zaidi kuyakabidhi mapenzi yao kwa Mungu, nao watanyenyekea na kutawaliwa na Roho wa Kristo. Ni kwa nini wengi wanaojidai kuwa ni Wakristo wanayo majaribu mengi ambayo yanalifanya kanisa kubeba mzigo mzito, sababu ni kwamba hawakulelewa ipasavyo wakati wa utoto wao, nao kwa sehemu kubwa waliachiwa kujenga tabia zao wenyewe. Tabia zao
mbaya, na mwelekeo wao wa ajabu na wa kusikitisha haukusahihishwa. Hawakufundishwa kuyasalimisha mapenzi yao kwa wazazi wao. Maisha yao yote ya Kikristo yanaathirika kutokana na malezi yao wakati wa utoto. Wakati ule hawakuzuiwa. Walikuwa hawajaadibishwa, na sasa, katika maisha yao ya Kikristo, ni vigumu kwao kujisalimisha kwa yale maongozi safi ya Neno la Mungu. 
Yawapasa wazazi kutambua wajibu unaowakalia wa kuwalea watoto wao kwa kuzingatia maisha yao ya kidini.Wale wanaouona uhusiano wao wa ndoa kama mojawapo ya maagizo matakatifu ya Mungu yanayolindwa na sheria yake takatifu [Amri Kumi], watatawaliwa na maongozi bora ya akili zao. Kwa makini watafikiria matokeo ya kila haki inayotolewa na uhusiano huo wa ndoa. Hao wataona ya kwamba watoto wao ni johari za thamani walizokabidhiwa na Mungu ili kuzitunza, kuondoa sura ile inayoparuza kutoka katika asili yao kwa njia ya malezi bora, ili mng'aro wake upate kuonekana. Watajisikia ya kwamba wako chini ya uwajibikaji mzito sana wa kuzitengeneza tabia zao [watoto] ili katika maisha yao wapate kutenda mema, wapate kuwa mbaraka kwa wengine kwa nuru yao, na ulimwengu upate kuwa bora zaidi kwa kuishi kwao ndani yake, na hatimaye wafae kwa maisha yale ya juu zaidi, katika ulimwengu ule ulio bora ili wapate kung'aa mbele zake Mungu na mbele za Mwana-Kondoo milele hata milele.

Itaendelea....

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni