Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Februari 07, 2012

UTIMILIZO HALISI



Sasa mbele yetu tunayo orodha ya tabia maalum tisa, ambazo zimetolewa toka katika sura ya saba ya Danieli, ili kuifafanua pembe ile ndogo. Kuna mamlaka moja tu katika historia yote ambayo inapatana kabisa na maelezo yaliyotolewa hapa. Kwa shida mno ishara yo yote katika hizo inaweza kutumika kwa mamlaka nyingine, isipokuwa ni UPAPA peke yake. Kanisa Katoliki peke yake linatimiza mambo yote yanayoitambulisha pembe hiyo ndogo ambayo yametajwa katika Danieli 7. Hebu na tuangalie kwa haraka na kuona kwa wazi jinsi jambo hilo linavyotekelezwa.



KWANZA kabisa, UPAPA ulitokea katika eneo la Ulaya Magharibi, katikati kabisa ya eneo la Dola ya Rumi ya Kipagani ----- katika RUMI yenyewe.



PILI, ulizuka baada ya mwaka 476
B.K. wakati Mfalme Justinian alipomteua Papa kuwa mtawala wa KISIASA na wa KIROHO wa ulimwengu wote. Haya ni mambo ya kweli ya historia ambayo yanaweza kuhakikishwa Kutoka katika chimbuko la mamlaka yo yote ile ya kihistoria.



TATU, Upapa ulipotokea ulipingwa na makabila matatu ambayo yalikuwa yametawala baada ya kuangushwa kwa Dola ya Kirumi. Wavandali (Vandals), Waostrogothi (Ostrogoths), na Waheruli (Heruli) walikuwa ni mamlaka zenye imani ya Arius (Arian powers) ambao kwa Nguvu zao zote walipinga kuzuka kwa Kanisa Katoliki. Majeshi ya Warumi yakayang'oa kabisa na kuyaangamiza makabila hayo matatu. La mwisho katika hayo matatu liliangamizwa katika mwaka ule ule wa 538 B.K., wakati RUMI YA KIPAPA ilipoanza kutawala dunia.



NNE, Katika mfumo wake, Kanisa Katoliki lilikuwa na MTU akiliongoza.



TANO, Upapa ulikuwa ni UFALME ULIO TOFAUTI na falme zile nyingine za kisiasa zilizoutangulia. Ulikuwa ni MAMLAKA YA KIDINI NA KISERIKALI ambayo iliitawala dunia yote. Hakuna mamlaka iliyofanana kabisa na hiyo ambayo ilipata kuonekana ulimwenguni kabla ya wakati ule.



Sasa tunaiangalia tabia yake ya SITA ----- ile ya kunena maneno makuu na makufuru dhidi yake Aliye juu. Je, Upapa unatimiza maelezo hayo? Tunahitaji tu kukumbushwa Kwamba Kanisa Katoliki limejitwalia lenyewe UWEZO WA KUSAMEHE DHAMBI. Kuhusu maneno yake makuu, hebu ninukuu kutoka katika makala ya F. Lucii Ferraris, iliyo katika kitabu cha PROMPTA BIBLIOTHECA CANONICA JURIDICA MORALIS THEOLOGICA. Kitabu hiki kilichapishwa mjini Roma, na kimeidhinishwa na ensaiklopidia ya Kikatoliki. Sikiliza madai haya: "Papa ni mkuu mno, naye ametukuzwa sana, kiasi kwamba yeye si mtu tu, bali kama ilivyo, yeye ni Mungu na Aliye Badala ya Mungu (Vicar of God). Kama ilivyo, PAPA NI MUNGU DUNIANI. Mfalme mkuu wa wafalme, mwenye uwezo mwingi." Gombo la VI, uk.25-29. Haya ni maneno machache tu ambayo Biblia inasema kuwa ni makufuru. UPAPA unatimiza ishara zote za utambulisho na
hivyo kuwa ile PEMBE NDOGO.



Sasa tunakuja kwenye kitambulisho cha SABA, tunaona ya kwamba HISTORIA inaunga mkono unabii huu kuhusu MATESO YA PAPA. Kila mmoja anayejua habari za Kizazi kile cha Kati (Middle Ages) Zama za Giza anafahamu fika ukweli kwamba mamilioni ya watu waliteswa kikatili mno na kuuawa na Mahakama Maalum za Kikatoliki (Inquisitions). Kutoka katika kitabu kilichoandikwa na Kadinali wa Kikatoliki, ambacho pia kimeidhinishwa na Kanisa Katoliki, tunasoma hivi: "Kanisa Katoliki... lina hofu kuu ya kumwaga damu. Hata hivyo, linapokabiliwa na UZUSHI HERESY... LINALAZIMIKA KUTUMIA NGUVU, kutoa adhabu ya kupigwa viboko mwilini, na KUTESA. Linaunda mahakama kama ile ya Inkwizisheni (Inquisition).



Linatumia SHERIA ZA SERIKALI kulisaidia... Lilifanya hivyo hasa katika karne ile ya 16 kuhusiana na WAPROTESTANTI... Katika nchi ya Ufaransa, chini ya wafalme Francis I na Henry II, katika nchi ya Uingereza chini ya Malkia Mary Tudor, Kanisa Katoliki liliwatesa wazushi." Maneno haya yamenukuliwa kutoka katika kitabu cha 'THE CATHOLIC CHURCH, THE RENAISSANCE AND PROTESTANTISM', uk.182-184. Tunaweza kuongeza semi nyingi kama hiyo kutoka kwa wanahistoria, Wakatoliki na Waprotestanti, zinazoelezea MATESO YA KUTISHA ya mamlaka ya kipapa juu ya Waprotestanti. Kwa njia hiyo tunaweza kuona utimilizo kamili wa maelezo haya ya pembe ndogo. 

Ishara ya NANE, kama ilivyotolewa katika fungu la ishirini na tano, inahusu jaribio lile la kubadili Sheria ya Mungu Amri Kumi. Je, jambo hilo linahusika na Upapa?



Tafadhali zingatia haya: Kanisa Katoliki limeondoa Amri ya Pili kutoka katika vitabu vyake vya mafundisho ya dini na Katekisimu zake, kwa sababu inashutumu IBADA YA SANAMU. Kisha Amri ya Kumi imegawanywa sehemu mbili ili waendelee kuwa na Amri Kumi. Walakini mbili zinakataza KUTAMANI, na hakuna hata moja inayokataza IBADA YA SANAMU. Kwa njia hii, Upapa UMEAZIMU UMEFIKIRIA kubadili Sheria ya Mungu, lakini bila mafanikio. SHERIA YA MUNGU HAIWEZI KUBADILISHWA

Mwishowe, tunakuja kwenye ishara ile ya TISA ya kitambulisho chake, ambayo inatuambia hasa muda ambao mamlaka hii ya Upapa ingeyatumia mamlaka yake juu ya dunia hii. Tuligundua kwamba ingetawala kwa miaka 1260.



Je, jambo hilo linakubaliana na kumbukumbu za historia? Kumbuka, ya kwamba tumeona jinsi Upapa ulivyoanza utawala wake, kwa amri ya Justinian, katika mwaka wa 538 B.K.. Tukihesabu kuja upande wetu miaka 1260 kuanzia mwaka huo tunaletwa kwenye mwaka wa 1798. Katika mwaka uo huo Jenerali wa Kifaransa, Berthier, aliongoza majeshi yake kuingia mjini Roma na kumng'oa Papa Pius wa VI Kutoka kwenye kiti chake cha enzi. Alichukuliwa uhamishoni, na mali zote za Kanisa zikataifishwa zikanyang'anywa. Uongozi wa Serikali ya Kifaransa ulitoa amri kwamba pasingekuwa na Askofu mwingine wa Roma kamwe. Kwa kadiri ulimwengu ulivyohusika, na kwa mwonekano wa nje, Kanisa Katoliki lilikuwa limekufa. Baada ya miaka 1260 kamili, kwa kutimiza unabii huu, likapoteza utawala wake juu ya dunia hii. Hivyo pointi hii ya mwisho imetimizwa kwa wazi kabisa katika Upapa, na katika Upapa peke yake.

Kuthibitisha na kujionea maelezo zaidi ya haya click HAPA

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni