Neno la Kilatini lenye maana ya utamaduni ni Cultura
ambalo lina usuli wake katika neno colere, linalo maanisha
"kulima") Neno hili lina fafanuzi nyingi. Kwa mfano, mnamo mwaka
1952, Alfred
Kroeber na Clyde
Kluckhohn walikusanya orodha ya vijelezi 164 vya neno
"utamaduni" katika kazi yao: Culture:a Critical Review of Concepts
and Definitions. Hata hivyo, neno "utamaduni" linatumika
kimsingi katika njia tatu zifuatazo:
- Maonjo ya hali ya juu katika sanaa, vilevile hujulikana kama utamaduni wa juu
- Mkusanyiko wa maarifa ya kibinadamu, itikadi na tabia ambao hutegemea sana uwezo wa kuwasilisha mawazo na mafunzo ya kijamii kiishara
- Ni jumla ya mitazamo, kaida, malengo na maadili yanayotambulisha asasi, shirika au kikundi Fulani
Dhana hii ilipoibuka
kwanza katika karne ya kumi na nane na kumi na tisa barani Ulaya, ilimaanisha
mchakato wa kulima au kuboresha kilimo au kilimo cha mboga. Katika karne ya
kumi na tisa dhana hii ilimaanisha kuboreshwa kwa mja kupitia kwa elimu na hali
kadhalika ilimaanisha kutekelezwa kwa maazimio ya kitaifa au maadili. Katikati
mwa karne ya kumi na tisa, wanasayansi wengine walitumia dhana ya utamaduni
kurejelea uwezo wa kiubia wa binadamu.
Katika karne ya
ishirini, "utamaduni" ilijitokeza kama dhana ya kimsingi katika somo
la Anthropolojia. "Utamaduni" ulihusisha mambo yote yaliyomhusu
binadamu ambayo hayakufungamana na matokeo ya kimaumbile. Dhana ya utamaduni
katika Anthropolojia ya Kimarekani ilikuwa na maana mbili:
(1) Uwezo
wa kibinadamu wa kuainisha na kuwasilisha tajiriba za kibinadamu kiishara na
kutenda mambo kiubunifu; na
(2) Namna
mbalimbali watu wanaoishi katika sehemu mbalimbali ulimwenguni huainisha na
kuwasilisha tajiriba zao za maisha na kutenda mambo kiubunifu. Kufuatia vita
vya pili vya dunia, dhana hii ilipata umaarufu ingawa na fafanuzi
tofautitofauti katika taaluma kama vile sosholojia, Mafunzo ya utamaduni,
saikolojia ya mipangilio na mafunzo ya usimamizi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni