Nafsi ni neno la mkopo kutoka Kiarabu. Linatumika kusisitiza dhati ya mtu (k.mf. "Mimi nafsi yangu"). Hivyo linatumika kutafsiria neno la Kilatini "persona" (kwa Kiingereza "person") ambalo linamtofautisha binadamu (kama kiumbe wa pekee) na wanyama wote na kumpa haki zake za msingi. Tofauti hiyo ilisisitizwa hasa na dini ya Uyahudi iliyomtambua mtu (mwanamume na mwanamke vilevile) kuwa sura na mfano wa Mungu. Ni msamiati muhimu wa ustaarabu wa Magharibi, unaotumika sana katika saikolojia, sheria, falsafa, teolojia n.k. Maendeleo makubwa katika kuuelewa yalipatikana wakati wa mabishano ndani ya Ukristo kuhusu fumbo la Yesu na Utatu.
Binadamu
Binadamu ni neno linalomaanisha "Mwana wa Adamu", anayeaminiwa na dini za Uyahudi, Ukristo na Uislamu kuwa ndiye mtu wa kwanza. Kisayansi jina hilo linaweza kutumika kwa maana ya Homo Sapiens ili kumtofautisha na viumbe wengine wa jenasi Homo ambao wa mwisho wao (Homo Neanderthalensis) walitoweka miaka 35,000 hivi iliyopita. Wanadamu wote walioko leo hii ni spishi ileile na tofauti zinazoonekana kati ya maumbile ya watu katika sehemu mbalimbali za dunia ni kidogo tu. Utafiti juu ya DNA umethibitisha kwamba binadamu wote wametokana na watu waliokuwepo Afrika Mashariki tangu miaka 200,000 hivi iliyopita. Kwa namna ya pekee, upimaji wa DNA ya mviringo, ambayo kila mmoja anarithi kwa mama tu, unaonyesha kuwa binadamu wote waliopo duniani wanachanga mama mmoja aliyewahi kuishi miaka 130,000 hivi iliyopita. Halafu upimaji wa DNA ya mstari, hususan kromosomu Y, ambayo kila mwanamume anarithi kwa baba tu, umeonyesha kuwa wanaume wote waliopo duniani wanachanga baba mmoja aliyewahi kuishi miaka 70,000 hivi iliyopita, kidogo kabla ya watu wa kwanza kuhama bara la Afrika na kuenea Asia kufuatia pwani za Bahari ya Hindi.
Kutoka bara la Asia, watu walienea kwanza Australia na Ulaya, halafu Amerika toka kaskazini hadi kusini. Hatimaye, katika karne ya 20 watu walikwenda kukaa kwa muda katika bara la Antaktika kwa ajili ya utafiti. Ingawa binadamu ana undugu mkubwa wa kibiolojia na sokwe na viumbe vingine, ustawi wake hauna mfano, kiasi cha kufanya wengi waamini tofauti iliyopo inadai kuelezwa kwa uwemo wa roho ndani ya mwili wake; roho ambayo dini hizo zinasadiki imetiwa na Mungu moja kwa moja. Kadiri ya Biblia, binadamu ameumbwa “kwa mfano wa Mungu” (Mwa 1:27), mwenye roho isiyokufa. Ameshirikishwa naye ukuu juu ya viumbe vyote vinavyoonekana. Yeye tu ni nafsi, anaweza kujifahamu, kujitawala, kujitolea na kupendana na wengine. Basi, anapaswa kulinda hadhi hiyo asitawaliwe na tamaa za kila aina. Akifanya hivyo anatimiza mpango wa Mungu juu yake na kupendana naye. Utotoni anasukumwa tu na haja za umbile lake, ambazo ni muhimu kwake na anazilenga bila ya kuhitaji juhudi.
Lakini akikua anaanza kutambua tunu za maadili na dini, ambazo ni njema, ni muhimu kwa zenyewe na zinamdai azifuate kwa nia imara hadi afikie lengo. Kwa bidii za kudumu za namna hiyo anamlenga hasa Mungu, wema mkuu. Anapopitia misukosuko ya ujana asikubali kushindwa na vionjo wala asikate tamaa, kwa kuwa Mungu amemuumba atawale hata nafsi yake na mwili wake. “Mungu aliona kila kitu alichokifanya, na tazama ni chema sana” (Mwa 1:31). Hata hivyo, baada ya dhambi ya asili anadaiwa bidii katika kutekeleza tunu ili wema alionao uzae matunda. Basi, apanie kukuza wema aliojaliwa ili kesho awe mtu bora kama mzazi, raia, kiongozi wa dini na jamii n.k. Penye nia pana njia hata ya kuelekea utakatifu utakaokamilika katika uzima wa milele. Binadamu amekabidhiwa na Mungu dunia, lakini hasa amekabidhiwa nafsi yake mwenyewe. Itamfaa nini kujua na kutawala ulimwengu, asipojijua na kujitawala kweli? Karne XX imeleta maendeleo makubwa katika elimunafsia (= saikolojia). Hivyo anaweza kutambua vizuri mema na mabaya yaliyomo ndani mwake.
Lakini akitaka kujifahamu haitoshi asikilize mafundisho hayo au kusoma vitabu vingi juu yake. Anahitaji kuishi katika mazingira bora ambapo ajisikie nyumbani, huru na mtulivu kwa kupendana na wenzake, kusikiliza watu wanaomfahamu (hasa walezi wake) wanasema nini juu yake, kujipatia muda wa kutulia peke yake na kujifikiria kulingana na maneno yao, kujichunguza kwa makini kuanzia miaka ya utotoni. Kwa kuwa utu unategemea urithi, mazingira na utashi wa kila mmoja, anapaswa kuchunguza hayo yote yaliyochangia kumjenga. Mara kwa mara ajitenge na watu na shughuli ili kutathmini tena maisha yake, kupima maono yake na kuweka maazimio ya kufaa, bila ya kusahau kwamba uhai wake ni fumbo, kwa kuwa unamtegemea Mungu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni