Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumanne, Aprili 12, 2011

SIKU YA KWANZA

Ningesema mengi leo, lakini haikuwa mara yangu ya kwanza kuijiwa na huyu mtu, mawazoni kulijaa fikra na picha tofauti na nilivyomuona husika mwenyewe; nikidhani ni miongoni mwa washenzi niliowahi kuwasikia na wengine kuwaona katika filamu za ulaya.

Leo ni siku ya pili napita eneo hili nikiwa peke yangu na kila mara nimekuwa nikijiuliza kama inaweza tokea siku moja ama zaidi ya moja, yaani kwamba siku mbili zikaungana na kuwa moja.

Ukweli uliojificha machoni pake ni dhihirisho la taabu alioipitia katika makuzi na maisha – najisikia kufanya jambo zaidi lakini akili haijatanabaisha.

Ni kweli kwamba kila siku nimekuwa na kawaida ya kusikiliza muziki laini wa ala tofauti na ilivyokuwa siku zilizopita, pengine labda ugeni wa jambo ninalotaka kuingia!

Au ndio ule usemi unatimia kwamba kila jambo na wakati wake? Kwa hiyo huu ni wakati wa kusikiliza ala za muziki laini…mhfuu!. Si hivyo...

Hayo ni mawazo tu ambayo maswali yake hakuna anayeweza kubaini jibu kwa haraka ingawa kuna kila dalili ya mwelekeo.

Upendo ni kitu kingine kabisa mtu asikwambie. Nikimnukuu mwimbaji mmoja wa nyimbo za injili katika moja ya mashairi ya nyimbo zake anaelezea juu ya upendo!

“…upendo wako bwana wanishangaza, jinsi viumbe wa baharini waishivyo, ndege wa angani wasiolima wala kuvuna na kila kitambaacho juu ya ardhi, milima na mabonde, mimea ya kondeni na kila aina ya zao.

Bwana wanishangaza kwa huruma. Nauliza: Upendo ni kitu gani? Ewe mwanadamu wa sasa.”

Wimbo huo unanifanya nijiulize ili niwe na uhakika na maamuzi yangu, isije kuwa ni ndoto tu pengine nipo katika usingizi wa pono mara baada ya shughuli kubwa ya kusimamia uchukuaji wa magari ya baba bandarini.

Hata hivyo upendo wa Mungu ni tofauti na upendo wa mwanadamu, leo hii tunaweza kutofautiana mitazamo na kusiwepo na mawasiliano tena kwa sababu ya kukwaruzana, migongano ama kwa sababu ya migogoro.

Hii ni kawaida ya binadamu sisi, mimi huyu na wewe huyo. Unaweza pia kuzungusha shingo na kuelekeza macho yako kwa kila anayepita jirani yako ama aliyejirani. Ndiyo kawaida ya binadamu sisi.

Alieleta majivuno, kujisikia, chuki, fitina katushika kweli kweli!! Na wengi tumejiunga katika mtandao wake pasipo kuelewa, cha ajabu hafanyi matangazo ya ofa kama zilivyo kampuni za mawasiliano hapa Duniani…!!!

Wanaojisajiri humo kila siku ni wengi!!! Ni wengi kweli kweli!!.

**************************************************************

SIKU YA KWANZA NI SIMULIZI INAYOGUSA MAISHA HALISI YA BINADAMU, NI KIPENGELE KITAKACHOKUWA KINAKUIJIA KILA JUMANNE.

**************************************************************

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni