Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatatu, Machi 28, 2011

JE, UNAJUA YANAYOTOKEA?


Huyu ni dada, ni mwandishi wa vitabu na mtunzi wa filamu. Kisa hiki ni simulizi ambayo ni sehemu ya maisha yake yaliyotokea halisi.

NA KWA KWELI KISA HIKI PIA NI SALAAM KWA WALE WOTE WALIOFIWA NA NDUGU JAMAA NA MARAFIKI KAMA AMBAVYO HIVI SASA KUNA MWANABLOG MWENZETU WA http://ruhuwiko.blogspot.com AMEONDOKEWA NA MDOGO WAKE.

Nikiwa na miaka 6 nilichukuliwa na kulelewa na mama ambaye nae alikuwa na watoto tayari. Niliona nimepata mkombozi baada ya kufiwa na mama yangu mzazi. Mama aliyenichukua alikuwa na kijana mdogo ambaye kiumri tulilingana, nilisoma na kijana huyo darasa moja la kwanza mpaka la saba. Kitu ambacho sitaweza kusahau maishani mwangu na ambacho sipendi kabisa kukisikia tena wala kukiona na pia huwa nasikitika nikiona mtu anafanya ni kumnyanyasa mtu ambaye hana hatia.

Yote ni kwa sababu niliyapitia maisha hayo. Nakumbuka nilipokuwa darasa la tano mpaka namaliza darasa la saba sikuweza kufika kwa kuwahi hata siku moja kuingia darasani mapema kama ilivyo desturi ya shule niliyokuwa nikisoma. Ratiba ilikuwa ni kupanga mstari saa moja na dakika ishirini, saa mbili kamili masomo yalianza. Kwa kumbukumbu zangu nakumbuka nilikuwa nikiingia darasani saa tatu kasoro dakika kumi, ambapo mara nyingi mwalimu aliyekuwepo kwenye zamu ya kipindi alinigombeza na nilihahikisha walimu wote walijua nini kilichopelekea mimi nichelewe kuwahi darasani.

Yote niliyopitia ni kwa sababu ya kutekeleza wajibu nilioachiwa na mama ambaye alinichukua kunilea. Kila siku kabla sijaenda shuleni ilinipasa kuamka asubuhi kwa ajili ya kuosha gari la mama, kupiga pasi nguo za mama za kuendea kazini na pia kuchota maji ya kutumia nyumbani. Kwa maana ndani yalikuwa hayatoki kwa hiyo nilikuwa nachota kwenye nyumba ya jirani na kupandisha nayo juu ghorofani ambapo tulikuwa tukiishi. Kuchemsha nyama au maharage tayari kwa kuyaunga kwa ajili ya mlo wa mchana ndizo kazi nilizopaswa kukamilisha kwanza ndipo niondoke kwenda shule, piga picha.

Pamoja na kufanya kazi zote kama mtoto wa nyumbani nilijiona nikinyanyasika, kwa maana sikuweza kulala mpaka nimalize kazi zote mara nyingi nililala si chini ya saa sita usiku. Nilihuzunika kwa maana sikuwa na ndugu wa kunionea huruma na mara nyingi nilikuwa nikipigwa bila sababu ya msingi. Nilitamani kufahamu mahali palipokuwa na vituo vya kulelea yatima ili niende nikaishi huko, lakini sikufanikiwa kupaelewa kwa maana nilikuwa ni mdogo na niliogopa kuuliza walionizidi umri na kuhofia wangerudi kumweleza mama aliyekuwa akinilea.

Niliendelea kuishi kwa kuvumilia huku nikimwomba mungu anilinde pia aweze kunikutanisha na ndugu zangu ambao walikuwa mbali nami. Moyoni niliwaza sana kama mama aliyeamua kunichukua kwa kusudi la kunilea mbona aligeuka kuwa katili na adui yangu kwa kunipiga na kunitukana kwa kuniita kenge kila kukicha!

Namshukuru mungu alinipigania na maumivu yote niliyaona ya kawaida. Nakumbuka siku moja nilienda kubatizwa, nami nilifundishwa kanisani kuishika sabato kwa maana siku hiyo si ya kufanya kazi yoyote. Asubui niliachiwa maagizo na mama mlezi ya kwamba ifikapo jioni nikaange samaki kwa ajili ya mlo wa usiku nilimwitikia vyema. Nilijiandaa kwenda kanisani ambapo mchana wa siku hiyo nilibatizwa.

Nilimaliza shughuli za kanisani na kurudi nyumbani, nilijilaza kidogo kitandani na kupitiwa na usingizi. Kama ujuavyo usingizi baadae niliamka saa moja kasorobo na kuanza kuandaa mapishi. Wakati huo mama hakuwepo nyumbani ila alirudi muda huo na kunikuta katika maandalizi, bila kuniuliza chochote alininyanyua mashikio juu na kuanza kunipiga bila kuhitaji maelezo. Nilisononeka sana kwa maana nilikuwa nimetoka kuzaliwa upya (kubatizwa), namshukuru mungu kwa neema yake kwa sababu ameniumbia moyo msafi hata hivyo nilijisikia amani sana.

Niliendelea na mapishi ya kukaanga samaki bila ya kuwa na kinyongo ingawa nilikuwa nimeumizwa sana kichwani kwa kupigwa na mwiko mkubwa, moyoni nilijua kama ningekufa siku ile ile; Hakika ningeingia mbinguni moja kwa moja bila kuwa na mawaa, maana ndio siku niliyokuwa nimetoka kumkiri bwana kuwa mwokozi wa maisha wangu. Mama mlezi alikuwa akipenda sana kunituma nyakati za usiku kwenda dukani au wakati mwingine kwenda kununua bia sehemu moja inaitwa jeshini.

Siku moja nikielekea kumchukulia mama bia majira ya usiku kijana mmoja ambaye alikuwa akiishi si mbali na nyumbani kwetu alinikamata na kunibaka, niliumia sana na niliogopa kumweleza mama kwa maana nilijua kningemweleza ingekuwa mwisho wangu wa kuishi pale kwake. Nilivumilia na kwenda kununua bia huku nikiwa na maumivu na kurudi nyumbani nikawa kimya bila kumweleza mtu yeyote.


Nikiwa darasa la sita nilifanya urafiki na kijana ambaye alikuwa akisoma shule tofauti na ninayosoma, siku moja kulikuwa na pati akanialika niende, kwa kuwa jirani na nyumba yetu kulikuwa na sherehe nilishindwa kuondoka na kubaki kusheherekea hapo. Nakumbuka alikuja kwenye sherehe na kunichukua, tuliondoka na kusimama muda mrefu njiani tukiongea. Kumbe kuna kijana ambaye ni jirani yetu alikuwa anatuchungulia mahali tulipokuwa tumesimama.

Jack alirudi nyumbani na kumweleza kaka kuwa niko mitaa ya mbali na si kwenye pati halafu akasisitiza kuwa kuna jambo nilikuwa nafanya ambalo si zuri kwa jamii. Nilipomaliza kuongea na boyfriend nilirudi nyumbani moja kwa moja, bila kujua hili wala lile nilimkuta kaka akiwa amekusanya fimbo kibao za mti wa mpera, aliponiona tu alianza kunicharaza.

Nililia na kuomba msamaha na kukubali kweli nilikuwa na boyfriend. AMbapo niliamriwa siku inayofuata nimwite huyo kijana aje nyumbani ama la angemweleza mama, nilikubali kufanya hivyo. Boyfriend alifika nyumbani na kuomba msamaha ambapo kaka alimweleza ahakikishe ananifundisha masomo na niyaelewe vyema. Nilistaajabu maamuzi ya kaka. Namshukuru mungu kwa kunipa mtu ambaye alinionea huruma na pia aliumia aliponiaona mie mtu baki kwake nikipotea May God rest him in peace.

Nilimpenda sana kaka yangu huyo ambaye alikuwa ni mtoto wa mama mlezi, mara nyingi aliporudi likizo alikuwa akinisaidia kazi zote na nikawa nalala mapema na pia nilipata na muda wa kusoma. Maagano yafanywapo yapaswa kukumbukwa. Nikiwa darasa la saba, tukiwa tumekaa na Boyfriend kwenye bustani ya shule siku ya jumapili tuliwekeana maagano kwamba tutakapokuwa wakubwa tutaoana pia mungu akipenda tutaenda ulaya tukaishi hukohuko.

Namnukuu:

Boyfriend; Nikimaliza sekondari nitaenda kusoma ulaya na nikirudi nitakuletea zawadi ya saa, utanivumilia kunisubiri mpaka kipindi hicho?

Mimi: Ndiyo nitakusubiri, lakini na mimi ningekuwa na uwezo natamani ningeenda nawe tukasome tukimaliza tuoane tuishi hukohuko.

Boyfriend: Ngoja nikasome nikirudi nifanye kazi nikipata pesa

tutakuwa tunaenda kutembea ulaya, ukitaka tutaishi hukohuko.

Boyfriend: Akiwa ameshika wembe, alinichanja kwenye kidole nae pia akajichanja tukanyonyana vidole vyenye damu, “tutapendana siku zote hatutaachana”.

Nilishindwa kuvumilia kuishi kwa mama mlezi hasa baada ya kunipiga na kuniamuru nizibue choo ambacho hata siku moja mama huyo hakuwai kuita fundi kukitengeneza, Na pia cha ajabu alisusa kuongea nami, jambo jingine ni kwamba alipohitaji kitu alimtuma rafiki yake ambaye alikuwa amemtembelea kutoka Arusha.

Mara nyingi niwapo darasani nilijawa na mawazo ya kutoroka nyumbani lakini sikupata wazo la wapi ningeenda kuishi, ilipokuwa ikikaribia muda wa kurudi nyumbani moyo ulikuwa ukiniuma kwa uwoga, kwa kweli mama aliyenilea alikuwa ni mkali sana, hata niliposikia akipiga honi ya gari roho ilinilipuka kwa uwoga. Nakumbuka kabla mama yangu hajaaga dunia alikuwa na kanga moja iliyokuwa imeandikwa MTUMAINI CHA NDUGU HUFA MASKINI.

Niliukumbuka usemi huo ingawa kiumri nilikuwa mdogo sana kuwaza mambo hayo makubwa. Niliamua kukata shauri la kuondoka nyumbani pale nilipokuwa nikilelewa. Nililala siku mbili nikitafakari ni jinsi gani niondoke kwenye maisha ya mashaka yale, ndipo siku moja ya jumatatu nilipokusanya baadhi ya nguo zangu na kwenda kuzificha juu ya nyumba yetu kisha nikaelekea shuleni.

Nilipofika shuleni muda wa mapumziko niliwatuma wanafunzi wenzangu wawili waende nyumbani wapande ghorofani juu wakanichukulie nguo zangu nilizokuwa nimeficha eneo hilo. Wakaenda, wapolirudi wakanieleza kuwa hawakukuta nguo yoyote, niliwaangalia kwa mshangao!! nikaendelea na masomo. Muda wa kwenda nyumbani ulipofika, mapigo ya moyo yalinidenda mbio,

…niliwaza “leo sirudi nyumbani natoroka, lakini nitakwenda wapi?” nilitembea hadi kwenye kituo cha basi posta ambapo niliomba nauli kwa wapita njia na kupanda daladala na kuelekea Kinondoni kwa mmoja wa rafiki zake marehemu mama.

Maisha yangu yalikuwaje baadae…….!!!!!!!!!

Maisha ni wewe unavyoyaendesha kila siku, maisha ni wewe unavyoyakubali yakukabili, Maisha mazuri yasiyo na tabu wala hayatakuletea bughudha katika moyo wako ni kumtii mungu na kuyafuata matakwa yake kwa jina lake hautataabika….

…sikiliza sauti yake na uitii…!!!Maoni 4 :

 1. Bwana Mcharia, watoto wengi wanaishi kwenye maisha hatarishi na ya manyanyaso kama huyu dada. Wanapata shida, lakini wanakosa mtu wa kuwasaidia.

  Huyu dada ameandika kitabu gani na kinapatikanaje?

  JibuFuta
 2. Dada Margaret! Kwanza kabisa napenda kukupa HONGERA kwa ujasiri wako Habari yako imenigusa yaani imeingia pamtima kabisa maana uliyopitia dadangu haupo peke yako. wapo wengi sana na mmoja wapo huyu aandikaye haya maoni. Nilipokuwa nasoma chozi lilikuwa likinidondoka sio kwa uchungu tu bali pia kwa ujasiri wako, uvumilivu na utu pia. Sio wengi wanakuwa na uvumilivu kama uliokuwa nao.
  Ningependa sana kuwasiliana na wewe kwani naona kuna kitu baina yetu kinanifanya niweze kuwasiliana nawe. J vitabu vyako/vyake alivyoandika naweza kupata jina au wapi vinapatikana?. Ahsante kaka Macharia kwa kutushirikisha katika simulizi hii.

  JibuFuta
 3. Asante kwa hii Mkuu!

  Na asante kwa kunifahamisha mdada huyu Margaret Obange

  JibuFuta
 4. Msijali wote, ndio jukumu tuliloamua kuwa nalo la kuelimishana na kuambizana mambo mbalimbali yanatusibu sisi na marafiki,majirani,ndugu na hata jamaa zetu.

  Kiukweli HIO NDIO KWELI YENYEWE.

  JibuFuta