Katika
kumkumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na
kuzienzi kazi za kimapinduzi alizozifanya kwa maslahi ya taifa letu na
watu wake, kila mtanzania mzalendo atakubaliana nami kwamba katika
kipindi kifupi sana cha miongo miwili historia imetuonyesha kwamba mambo
mengi aliyoyasimamia Mwalimu yalikuwa sahihi ingawa yametelekezwa.
Maandiko
ya Mwalimu kuhusu Azimio la Arusha, siasa ya ujamaa na kujitegemea,
elimu, afya, kilimo, viwanda, reli, bandari, ustawi wa maisha ya
wananchi, utu, haki sawa kwa wote, nk na mafanikio yake yanauonyesha
umahiri aliokuwa nao katika kubuni mikakati ya kulikomboa taifa, ingawa
wapo vibaraka waliolishwa kasumba ya kibeberu, ambao wanazibeza kazi za
Mwalimu kwani zinasuta dhamira zao juu ya ustawi Tanzania na watu wake.
Katika ulimwengu wa sasa tunashuhudia mataifa yanatikiswa na mengine yameangushwa na kumegwa vipande vipande na magaidi na
majasusi ambao wamevunja ngome za ulinzi na usalama wa mataifa hayo.
Mamilioni ya watu wasiokuwa na hatia wameuwawa. Duniani kote mapambano
dhidi ya magaidi na majasusi yanaendelea kwa siri na wazi ili kulinda
uhai wa watu na mali zao na ustawi wa mataifa. Hali hii si ngeni.
Imekuwepo kwa miaka yote. Kwa Tanzania, Mwalimu Nyerere aliliweka mwanzo
kabisa suala la usalama wa taifa ambao kimsingi ndio uhai wa Tanzania.
Katika kumkumbuka Mwalimu nitaidurusu kazi aliyoifanya ya kuimarisha na
kuulinda usalama wa taifa, pia nitatoa maoni yangu ya nini kifanyike
katika juhudi za kuimarisha usalama wa nchi yetu katika ulimwengu huu wa
kigaidi na kijasusi.
Historia inaonyesha kuwa Tanzania chini ya
Mwalimu Nyerere ilianzisha sera ya kutetea na kusimamia haki watu
duniani kote pamoja na kuongoza harakati za kupigania uhuru wa Afrika.
Kwa kuwa harakati hizi zililenga kumkomboa mwafrika aliyenyonywa na
kukandamizwa na mabeberu, mataifa makubwa yenye maslahi yake katika nchi
za kiafrika yaligeuka kuwa hasimu mkubwa kwa Tanzania na yalitumia kila
mbinu za kijasusi na kigaidi kutaka kulihujumu taifa letu na hata
kuipindua serikali. Tanzania ya Nyerere ilikuwa macho na iliwadhibiti
magaidi na majasusi kutoka kwa makaburu wa Afrika Kusini, serikali ya
Ian Smith ya Rhodesia, serikali za kikoloni za Kireno wote hawa
wakiungwa mkono na mataifa makubwa ya magharibi. Majasusi kutoka kwa
Nduli Idd Amini nayo yalithibitiwa. Hali ya sasa ya ugaidi na ujasusi
duniani na tishio lake kwa usalama wa Tanzania yetu inafanana na hali
tuliyokumbana nayo wakati huo. Mbinu za magaidi na majasusi ni zilezile
-- kujipenyeza kwa siri na kuujua udhaifu wa mfumo wa ulinzi na usalama
na wapi pa kupiga kwa urahisi -- na malengo yao ni yaleyale -- kutia
hofu, kuuwa watu na kuhujumu miundo mbinu ili kutimiza malengo yao ya
kisiasa.
Nini kiliifanya Tanzania kuushinda ugaidi wa ujasusi?
Jibu ni mfumo imara wa ulinzi na usalama ambao ulikuwa ni jukumu la
kila mtanzania -- mfumo wa shina la nyumba kumikumi. Hapa neno shina
lilimaanisha pia maofisi na maeneo yote ya kazi, starehe nk ili mradi
upo mkusanyiko wa watu. Jukumu la usalama wa taifa halikuwa jukumu la
vyombo vya usalama peke yake. Watu walilelewa hivyo na kuishi hivyo.
Kila raia alikuwa ni askari katika kaliba yake. Mfumo huu imara
aliounzisha Mwalimu Nyerere uliifanya Tanzania kuwa na ngome imara ya
kuwadhibiti maadui wa ndani na nje na kudumu katika amani. Kila
waliothubutu kuingia nchini kufanya ujasusi na ugaidi walikamatwa na
kurejeshwa makwao. Kila mpango wa kijasusi na kigaidi ndani ya nchi
ulijulikana na kudhibitiwa mapema. Hii ni kutokana na ukweli kwamba,
KIITIKADI (kijamaa), watanzania walitambua kuwa Tanzania ilikuwa na
maadui wa ndani na nje na kwamba utayari wetu, mshikamo na ushirikiano
wetu katika kuilinda nchi yetu ndiyo ilikuwa ni silaha yetu kubwa. “Moyo
kabla silaha” yalikuwa ni maneno ya hamasa kutoka kwa Mwalimu. Idara ya
Usalama wa Taifa ilitanda kila kona ya nchi si kwa maana ya maofisa
kutoka “Idara ya Usalama Taifa” bali kila raia mwema, mzalendo, mwenye
nia safi juu ya nchi yetu alikuwa ni mwanaidara. Kwa kujipanga sawasawa
kimkakati tuliwashinda maadui. Tanzania ilibaki salama na hatimaye nchi
za Angola, Namibia, Msumbiji, Zimbabwe na Afrika Kusini zilipata uhuru
wake.
Tanzania ya sasa bado inao maadui wa ndani na nje na
inakabiliwa na changamoto kubwa sana katika kukabiliana nao.. Lakini la
kusikitisha ni kwamba suala la usalama wa taifa linaonekana kuwa ni
suala la vyombo vya ulinzi na usalama tu. Haya ni matokeo ya kutelekezwa
kwa mfumo wa usalama tuliokuwa nao baada ya kulitumbukiza taifa katika
mfumo wa uliberali mamboleo. Tanzania ya katika mfumo mpya wa uliberali
mamboleo ikasahau kwamba bado inao maadui wa ndani na nje. Tanzania
ikacha milango na madirisha wazi na hata paa ikaezua. Mfano ni wahamiaji
haramu wanaingia na kutoka Tanzania wapendavyo. Twiga na ukubwa wake
anapitishwa uwanja wa ndege. Majengo marefu yamejengwa karibu sana na
Ikulu jambo ambalo ni hatari sana kwa Usalama wa Taifa. Kisa? Eti
wameweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Ajabu sana! Tanzania ikawa kituo
cha madawa ya kulevya. Ujangili na wizi wa kutumia silaha ukashamiri.
Silaha za kivita zikatapakaa kila pembe ya nchi. Uhujumu uchumi ukawa ni
njia kuu ya kujitajirisha. Tanzania ikaendeshwa na rushwa. Rushwa
kidogo inawasahaulisha wenye dhamana athari za wahamiaji haramu (rejea
hotuba ya Rais Kikwete akihitimisha ziara mkoani Kagera:
youtube.com/watch?v=Pxsbyi82uxM)
au madawa ya kulevya kwa taifa na vizazi vyetu. Matokeo yake tukaupa
kisogo mfumo wetu mzuri na imara wa ulinzi na usalama wa taifa kuanzia
shina la nyumba kumikumi, kwenda kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya
kijiji au mtaa, kamati ya ulinzi na usalama ya kata, wilaya, mkoa hadi
ngazi ya taifa.
Tukumbuke kwamba katika shina ndipo
anakopatikana adui wa ndani na nje. Tunaanzia kidogo kwenye wilaya.
Lakini nguvu zetu zote tumezielekeza kwenye ngazi ya taifa na mkoa.
Kwamba kupitia kwenye kamati za ulinzi na usalama za taifa, mkoa na
wilaya Tanzania iko salama. Kwa kweli tunajidanganya. Katika shina ndipo
kila mmoja wetu anamfahamu jirani yake na nyendo zake na hata siri
zake. Kupitia ufahamu huu taifa linaweza kumdhibiti yeyote yule kabla ya
kuleta madhara uraiani au katika vyombo vya ulinzi na usalama. Hata
kwenye nchi zenye teknolojia ya hali juu ambazo zimetandaza kamera kila
kona na kufuatilia nyenendo za watu kwenye mitandao ya simu na intanet
kama Marekani na Uingereza, mambo yakiwazidia huwa wanarudi kwenye
mashina ili kukabiliana na hujuma za kigaidi na kijasusi. Nchi kama Cuba
ambayo bado inautumia mfumo huu wa shina na imeweza kuwepo mpaka leo
licha ya kuwa karibu sana hasimu wao mkubwa tena mwenye nguvu sana --
Marekani. Haiingii mtu Havana akafanya ugaidi na ujasusi. Ni ngumu sana
tena sana. Wachina wana mfumo huu wa shina. Hapenyi mtu pale.
Nitumie
fursa hii kusema kwamba katika kumuenzi Mwalimu basi turejeshe na
tuimarishe mfumo huu wa usalama kuanzia kwenye shina. Kiitikadi (maana
itikadi ndiyo inayozaa uzalendo) wananchi wahamasishwe na kushirikishwa
zaidi katika usalama wa taifa katika mashina yote nchini na taarifa zao
zisivujishwe kwani kufanya hivi ni kuhatarisha maisha yao hasa pale
wanapotoa taarifa kuhusu watu wenye uwezo mkubwa kifedha. Mwaka 2010
nilikutana na mzee mmoja mkazi katika mojawapo ya vijiji vinavyozunguka
jiji la Mwanza akaniambia kuwa kuna wakati aliitikia wito wa serikali wa
kutoa taarifa polisi za wanaomiliki silaha za moto kinyume cha sheria
lakini alipotoa taarifa hizo kesho yake wale aliowataja wakamwendea na
kumtisha kweli. Hayo ndiyo matokeo ya mambo kuendeshwa kwa rushwa. Kwa
hiyo tuwe na mtandao wa siri mpana na maalum wa upashanaji habari za
kiusalama kuanzia ngazi ya shina ambao utaiwekea Tanzania ngome imara
kwamba anapoingia muhamiaji haramu, gaidi, jasusi kwenye kaya au eneo
fulani, shina linakuwa na taarifa hizo zinafikishwa kwenye vyombo husika
haraka iwezekanavyo. Au raia mwema akishuku au kuwa na taarifa kwamba
mtu fulani katika kaya, ofisi, au kundi fulani ana nyenendo za kutiliwa
mashaka, basi habari zake zipelekwe kwenye vyombo husika mara moja na
uchunguzi wa kina ufanyike haraka ili kuujua ukweli na kumdhibiti kabla
hajafanya madhara. Tukifanya hivi tutaudhibiti vilivyo ugaidi na hujuma
za jiasusi za aina yeyote. Tusisubiri CIA na FBI ambao kimsingi hawako
kwa ajili ya maslahi ya Tanzania yetu.
Wapo wanaoweza kusema
mfumo huo wa kuwa macho kuanzia kwenye shina unaifanya Tanzania
itawaliwe kipolisi (police state) na kwamba unawaminya uhuru watu. Jibu
kwa wasemao hivi ni kwamba hakuna kitu kinachoitwa UHURU-HURU. Uhuru
usio na mipaka wala wajibu haupo. Uhuru wa watu kuachwa wakapanga
mipango ya kigaidi na kijasusi ya kuhujumu nchi ni uhuru wa kuleta
maangamizi. Kama taifa hatuwezi kukubali kuona watu wasio na hatia
wanauwawa. Kwa hiyo, mfumo huu wa kiusalama katika mashina ni njia
sahihi, nyepesi na ya uhakika ya kupata taarifa za magaidi na majasusi
na kuwadhibiti. “Kinga ni bora kuliko tiba,” wahenga wetu walisema. Kwa
mfumo huu tutawadhibiti wauza madawa ya kulevya. Tutawadhibiti
majangili. Tutawakamata wakwepa kodi. Tutajua nani ni nani, yuko wapi,
na afanya nini katika kulihujumu taifa na tutachukua hatua katika wakati
muafaka kumdhibiti na kutokomeza uovu wake. Na teknolojia simu za
mkononi katika mfumo maalumu itatusaidia sana wananchi katika kufikisha
taarifa kwa vyombo husika ili mradi tu siri za watoa taarifa
hazivujishwi na vyombo husika. Pia tuangalie uwezekano kurejesha sheria
ya kizuizini ili mradi iwepo haki, uadilifu, udhibiti na ulinganifu
katika kuitumia ili isije kutumika kuwanyamazisha watu. Katika
kumkumbuka Mwalimu tujadili kwa mapana na marefu na kujikumbusha
historia ya nchi yetu na mafanikio yake na umuhimu wa mchango wa
wananchi katika usalama wa taifa letu. Na wala asikudanganyeni mtu kuwa
vita baridi ilikwisha. Bado ipo tena ni hatari zaidi. Kwa mfumo wa shina
wa kuwashirikisha wananchi Tanzania itakuwa salama na amani yetu
itadumu.
Mungu ibariki Tanzania.
Mungu udumishe uhuru na umoja wetu.
Ndugu yenu,
Amani Millanga.