Mtayarishaji

Morning Star Radio

Jumatano, Septemba 09, 2015

MASHAMBULIZI KUPITIA KOMPYUTA



HEBU wazia kundi la wahalifu wenye ustadi wa kutumia kompyuta wakitumia Intaneti kuongoza mitandao ya kompyuta walizoteka nyara. Kompyuta hizo zinazojulikana kama botnets (mitandao ya roboti), zinatoa habari za siri zenye madhara zinazolenga taifa fulani. Baada ya dakika chache, Tovuti za kijeshi, kifedha, na kibiashara za taifa hilo zinaacha kufanya kazi. Mashine za benki za kutolea pesa (ATM) pamoja na mitandao ya simu inashindwa kufanya kazi. Usafiri wa ndege unakatizwa na kompyuta pamoja na mifumo ya usalama katika kituo cha kutokeza nguvu za nyuklia inavurugwa. 

Watu wangetendaje?  

Wewe ungefanya nini?

Huenda tukio hilo likaonekana kuwa lisilo halisi. Lakini kulingana na Richard A. Clarke, aliyekuwa Msimamizi wa Kitaifa wa Usalama, Ulinzi wa Miundo-Msingi, na Kupambana na Ugaidi nchini Marekani, jambo kama hilo linaweza kufanyika kihalisi. Isitoshe, tayari kumekuwa na mashambulizi kupitia kompyuta.* Huenda hata wewe umewahi kushambuliwa.

Kwa nini mtu awashambulie wengine kupitia kompyuta? Mashambulizi hayo hufanywaje? Na kwa kuwa ni kawaida kwa mashambulizi hayo kumlenga mtu mmojammoja, unaweza kujilindaje unapotumia Intaneti?


Uwanja wa Vita Kwenye Kompyuta


Kuna sababu kadhaa zinazowafanya watu wawashambulie wengine kupitia kompyuta. Kwa mfano, magaidi au serikali zinaweza kupenya kwenye mitandao ya kompyuta ya maadui wao ili waibe siri au waharibu vifaa vinavyoongozwa na mitandao hiyo. Katika mwaka wa 2010, Waziri Msaidizi wa Ulinzi wa Marekani William J. Lynn wa Tatu alisema kwamba “maadui” wa kigeni walikuwa wamepenya mara nyingi kwenye mitandao ya kompyuta iliyo na habari za siri za Marekani na kuiba “maelfu ya mafaili . . . kutia ndani maagizo ya kutengenezea silaha, habari kuhusu mipango ya kijeshi, na habari za upelelezi.”—Ona sanduku “Mashambulizi ya Hivi Karibuni Kupitia Kompyuta.”

Wahalifu wanaotumia kompyuta hutumia njia sawa na hizo kuiba habari za kitaaluma au za kifedha kutoka kwa mitandao ya kompyuta ya makampuni na hata kompyuta za watu binafsi. Wahalifu hupata mabilioni ya dola kila mwaka kupitia biashara za ulaghai zinazofanywa kwenye mitandao.

Pia, wahalifu hao wameunganisha kompyuta nyingi sana walizoteka nyara ili waweze kutekeleza mashambulizi yao. Katika mwaka wa 2009, kampuni moja inayoshughulika na usalama wa intaneti iligundua kwamba kundi moja la “wahalifu” lilikuwa likidhibiti kisiri karibu kompyuta milioni mbili kotekote ulimwenguni, nyingi zikiwa ni za watu binafsi. Ripoti ya karibuni ya Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) linakadiria kwamba kompyuta 1 kati ya 3 zilizounganishwa kwenye Intaneti inadhibitiwa kisiri na mhalifu fulani. 

Namna gani kuhusu kompyuta yako? 

Je, mtu fulani anaweza kuidhibiti bila wewe kujua?



Maadui Wanaoshambulia Kimyakimya

Wazia tukio hili. Mhalifu fulani anasambaza programu fulani yenye madhara kupitia Intaneti. Programu hiyo inapoingia katika kompyuta yako, inapenya ndani ya programu inayolinda kompyuta yako. Programu hiyo yenye madhara inapopata eneo ambalo halijalindwa vizuri, inapenya ndani hata zaidi na kutafuta-tafuta habari muhimu katika kompyuta yote.* Kisha programu hiyo inaweza kubadilisha au kufuta mafaili yaliyo kwenye kompyuta yako, na inajituma yenyewe kama barua pepe kwenye kompyuta zingine, au kumtumia mhalifu huyo neno lako la siri la utambulisho, habari za kifedha, au habari nyingine za siri zinazokuhusu.

Wahalifu hao wanaweza kukufanya uingize virusi kwenye kompyuta yako mwenyewe! Jinsi gani? Unaweza kufanya hivyo kwa kufungua barua-pepe inayoonekana kuwa ya kawaida tu, kwa kubonyeza kiunganishi cha Tovuti fulani, kupakua na kuunganisha programu ya bure ya kompyuta, kuingiza kifaa cha kuhifadhi habari kilicho na virusi katika kompyuta yako, au tu kutembelea Tovuti yenye kutiliwa shaka. Mambo yote hayo yanaweza kuingiza programu yenye madhara kwenye kompyuta yako na kuifanya idhibitiwe kisiri na mhalifu.

Unaweza kujuaje ikiwa kompyuta yako imeshambuliwa? 
Kwa kweli inaweza kuwa vigumu kugundua. Huenda kompyuta au Intaneti ikafanya kazi polepole sana, au programu zisitende kwa njia ya kawaida, au visanduku vijitokeze ghafula vyenye ujumbe unaokuomba uunganishe programu fulani, au kompyuta yako itende kwa njia isiyo ya kawaida. Ukiona mojawapo ya dalili hizo, mwombe mtaalamu wa kompyuta achunguze kompyuta yako.


‘Fikiria Hatua Zako’


Kadiri mataifa na mtu mmoja-mmoja wanavyozidi kutegemea teknolojia ya kompyuta, ndivyo inavyotarajiwa kuwa mashambulizi kupitia kompyuta yataongezeka. Kwa sababu hiyo, mataifa mengi yanajitahidi sana kuboresha mbinu za kulinda kompyuta zao, na mataifa mengine yanapima uwezo wa mitandao yao ya kompyuta ili kuona ikiwa inaweza kustahimili mashambulizi. Lakini licha ya jitihada hizo, Steven Chabinsky, mtaalamu wa cheo cha juu wa usalama wa kompyuta wa Shirika la Upelelezi la Marekani anasema kwamba “adui aliyeazimia kabisa, hawezi kamwe—kamwe—kushindwa kupenya mfumo hususa anaolenga iwapo atakuwa na wakati wa kutosha, kichocheo, na pesa.”

Unaweza kufanya nini ili ujilinde unapotumia Intaneti?
 Ingawa huenda usiweze kujilinda kabisa unapotumia Intaneti, unaweza kuchukua hatua zifaazo ili kufanya kompyuta yako iwe salama zaidi.  Biblia inasema: “Mtu mwerevu huzifikiria hatua zake.” (Methali 14:15) Kwa kweli hilo ni shauri lenye hekima unapotumia Intaneti!.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni