HEBU wazia kundi la wahalifu wenye
ustadi wa kutumia kompyuta wakitumia Intaneti kuongoza mitandao ya
kompyuta walizoteka nyara. Kompyuta hizo zinazojulikana kama botnets (mitandao
ya roboti), zinatoa habari za siri zenye madhara zinazolenga taifa
fulani. Baada ya dakika chache, Tovuti za kijeshi, kifedha, na
kibiashara za taifa hilo zinaacha kufanya kazi. Mashine za benki za
kutolea pesa (ATM) pamoja na mitandao ya simu inashindwa kufanya kazi.
Usafiri wa ndege unakatizwa na kompyuta pamoja na mifumo ya usalama
katika kituo cha kutokeza nguvu za nyuklia inavurugwa.
Watu
wangetendaje?
Wewe ungefanya nini?
Huenda tukio hilo likaonekana kuwa
lisilo halisi. Lakini kulingana na Richard A. Clarke, aliyekuwa
Msimamizi wa Kitaifa wa Usalama, Ulinzi wa Miundo-Msingi, na Kupambana
na Ugaidi nchini Marekani, jambo kama hilo linaweza kufanyika kihalisi.
Isitoshe, tayari kumekuwa na mashambulizi kupitia kompyuta.* Huenda hata wewe umewahi kushambuliwa.
Kwa nini mtu awashambulie wengine
kupitia kompyuta? Mashambulizi hayo hufanywaje? Na kwa kuwa ni kawaida
kwa mashambulizi hayo kumlenga mtu mmojammoja, unaweza kujilindaje
unapotumia Intaneti?
Uwanja wa Vita Kwenye Kompyuta
Kuna sababu kadhaa zinazowafanya watu
wawashambulie wengine kupitia kompyuta. Kwa mfano, magaidi au serikali
zinaweza kupenya kwenye mitandao ya kompyuta ya maadui wao ili waibe
siri au waharibu vifaa vinavyoongozwa na mitandao hiyo. Katika mwaka wa
2010, Waziri Msaidizi wa Ulinzi wa Marekani William J. Lynn wa Tatu
alisema kwamba “maadui” wa kigeni walikuwa wamepenya mara nyingi kwenye
mitandao ya kompyuta iliyo na habari za siri za Marekani na kuiba
“maelfu ya mafaili . . . kutia ndani maagizo ya kutengenezea silaha,
habari kuhusu mipango ya kijeshi, na habari za upelelezi.”—Ona sanduku “Mashambulizi ya Hivi Karibuni Kupitia Kompyuta.”
Wahalifu wanaotumia kompyuta hutumia
njia sawa na hizo kuiba habari za kitaaluma au za kifedha kutoka kwa
mitandao ya kompyuta ya makampuni na hata kompyuta za watu binafsi.
Wahalifu hupata mabilioni ya dola kila mwaka kupitia biashara za ulaghai
zinazofanywa kwenye mitandao.
Pia, wahalifu hao wameunganisha
kompyuta nyingi sana walizoteka nyara ili waweze kutekeleza mashambulizi
yao. Katika mwaka wa 2009, kampuni moja inayoshughulika na usalama wa
intaneti iligundua kwamba kundi moja la “wahalifu” lilikuwa likidhibiti
kisiri karibu kompyuta milioni mbili kotekote ulimwenguni, nyingi zikiwa
ni za watu binafsi. Ripoti ya karibuni ya Shirika la Ushirikiano wa
Kiuchumi na Maendeleo (OECD) linakadiria kwamba kompyuta 1 kati ya 3
zilizounganishwa kwenye Intaneti inadhibitiwa kisiri na mhalifu fulani.
Namna gani kuhusu kompyuta yako?
Je, mtu fulani anaweza kuidhibiti bila
wewe kujua?
Maadui Wanaoshambulia Kimyakimya
Wazia tukio hili. Mhalifu fulani
anasambaza programu fulani yenye madhara kupitia Intaneti. Programu hiyo
inapoingia katika kompyuta yako, inapenya ndani ya programu inayolinda
kompyuta yako. Programu hiyo yenye madhara inapopata eneo ambalo
halijalindwa vizuri, inapenya ndani hata zaidi na kutafuta-tafuta habari
muhimu katika kompyuta yote.*
Kisha programu hiyo inaweza kubadilisha au kufuta mafaili yaliyo kwenye
kompyuta yako, na inajituma yenyewe kama barua pepe kwenye kompyuta
zingine, au kumtumia mhalifu huyo neno lako la siri la utambulisho,
habari za kifedha, au habari nyingine za siri zinazokuhusu.
Wahalifu hao wanaweza kukufanya
uingize virusi kwenye kompyuta yako mwenyewe! Jinsi gani? Unaweza
kufanya hivyo kwa kufungua barua-pepe inayoonekana kuwa ya kawaida tu,
kwa kubonyeza kiunganishi cha Tovuti fulani, kupakua na kuunganisha
programu ya bure ya kompyuta, kuingiza kifaa cha kuhifadhi habari
kilicho na virusi katika kompyuta yako, au tu kutembelea Tovuti yenye
kutiliwa shaka. Mambo yote hayo yanaweza kuingiza programu yenye madhara
kwenye kompyuta yako na kuifanya idhibitiwe kisiri na mhalifu.
Unaweza kujuaje ikiwa kompyuta yako
imeshambuliwa?
Kwa kweli inaweza kuwa vigumu kugundua. Huenda kompyuta
au Intaneti ikafanya kazi polepole sana, au programu zisitende kwa njia
ya kawaida, au visanduku vijitokeze ghafula vyenye ujumbe unaokuomba
uunganishe programu fulani, au kompyuta yako itende kwa njia isiyo ya
kawaida. Ukiona mojawapo ya dalili hizo, mwombe mtaalamu wa kompyuta achunguze kompyuta yako.
‘Fikiria Hatua Zako’
Kadiri mataifa na mtu mmoja-mmoja
wanavyozidi kutegemea teknolojia ya kompyuta, ndivyo inavyotarajiwa kuwa
mashambulizi kupitia kompyuta yataongezeka. Kwa sababu hiyo, mataifa
mengi yanajitahidi sana kuboresha mbinu za kulinda kompyuta zao, na
mataifa mengine yanapima uwezo wa mitandao yao ya kompyuta ili kuona
ikiwa inaweza kustahimili mashambulizi. Lakini licha ya jitihada hizo,
Steven Chabinsky, mtaalamu wa cheo cha juu wa usalama wa kompyuta wa
Shirika la Upelelezi la Marekani anasema kwamba “adui aliyeazimia
kabisa, hawezi kamwe—kamwe—kushindwa kupenya mfumo hususa anaolenga
iwapo atakuwa na wakati wa kutosha, kichocheo, na pesa.”
Unaweza kufanya nini ili ujilinde
unapotumia Intaneti?
Ingawa huenda usiweze kujilinda kabisa unapotumia
Intaneti, unaweza kuchukua hatua zifaazo ili kufanya kompyuta yako iwe
salama zaidi. Biblia inasema: “Mtu mwerevu
huzifikiria hatua zake.” (Methali 14:15) Kwa kweli hilo ni shauri lenye hekima unapotumia Intaneti!.