Photo Cretid By: www.itmonline.org |
Watu wanapougua
wanakwenda kuonana na daktari wakitumai kupona, lakini kama ugonjwa ukiwa sugu,watu hao husema
"laiti daktari ajabu Huatuo angekuwa hai". Huyu Huatuo alikuwa mganga
wa miaka zaidi ya elfu mbili iliyopita, kutokana na uhodari wake watu
walimmsifu kuwa ni "daktari wa ajabu".
Huatuo alikuwa ni
mwenyeji wa mkoa wa Anhui, tarehe yake ya kuzaliwa haiwezi kuthibitishwa, lakini
aliuawa kabla ya mwaka 208. Inasemekana kwamba Huatuo alikuwa na afya nzuri na
alipokuwa na umri wa miaka mia moja afya yake bado ilikuwa njema. Kutokana na
maandishi ya historia, alikuwa mganga wa kienyeji na alikuwa na nafasi nyingi
za kuwa ofisa, lakini alikataa. Jemadari mkubwa Cao Cao (155-220) alikuwa na
ugonjwa wa kuumwa na kichwa kwa muda mrefu, alimwomba Huatuo amtibu, muda si
mrefu Cao Cao alipona kabisa. Tokea hapo Cao Cao alimlazimisha Huatuo aishi
naye na kutunza afya yake. Lakini siku chache baadaye Huatuo alirudi nyumbani
kwa kisingizio kuwa mkewe alikuwa anaumwa. Ingawa Cao Cao alimhimiza mara
kadhaa arudi kwake, lakini Huatuo hakurudi. Cao Cao aliamua kumtia gerezani na
baada ya muda alimwua.
Huatuo alikuwa na
elimu nyingi za tiba ambazo zinahusika na magonjwa ya maambukizi, minyoo,
wanawake na watoto, mfumo wa kupumua na ngozi, na hasa elimu ya kufa ganzi kwa
mwili mzima na upasuaji.
Huatuo alikuwa mtu
anayependwa sana na watu, kwa kiasi fulani uhodari wake katika matibabu
umeonesha maendeleo ya tiba katika miaka elfu mbili iliyopita nchini China.
Huatuo alikuwa mmoja wa watu waliotangulia kutumia dawa za ganzi duniani.
Huatuo alikuwa hodari
wa kufanya upasuaji. Aliwahi kumfanyia upasuaji msichana mmoja mwenye umri wa
miaka 20 ambaye alikuwa na kidonda kwenye goti kwa miaka minane. Huatuo
alifunika dawa ya unga kwenye kidonda baada ya kutoa kipande kimoja cha mfupa,
msichana huyo alipona baada ya siku saba. Watu wa leo wanaona kuwa kipande cha
mfupa alichotoa kilikuwa ni kipande kilichokufa. Kulikuwa na mgonjwa mwingine
mzee ambaye alikwenda kumwona, baada ya kuchunguza ugonjwa wake Huatuo
alimwambia kuwa ugonjwa wake umekuwa mkubwa na anaweza tu kufayiwa upasuaji wa
tumbo, lakini hata hivyo, anaweza kuishi kwa miaka 10 hivi, na bila ya upasuaji
pia ataishi muda huo huo, kwa hiyo ni afadhali aache upasuaji. Lakini kutokana
na usumbufu wa ugonjwa wenyewe alimwomba Huatuo amfanyie upasuaji, maumivu
yalipungua lakini mzee huyo hakuishi zaidi ya miaka 10.
Huatuo pia alikuwa
hodari wa kugundua ugonjwa kwa kuangalia sura ya mtu. Siku moja alipokuwa
katika baa, aliwaona watu kadhaa wakinywa pombe, aligundua mmoja kati yao
alikuwa na ugonjwa mkubwa, alimwambia asinywe zaidi na kurudi nyumbani haraka.
Mtu huyo alipokuwa njiani alianguka kutoka kwenye gari na baada ya kufika
nyumbani siku chache alikufa.
Watu wa leo wanatilia
maanani sana mazoezi ya kuimarisha afya. Miaka elfu mbili iliyopita Huatuo
alivuni mazoezi mepesi ili kuimarisha afya, "mchezo wa wanyama wa aina
tano" ambayo yalikuwa ni mazoezi mepesi kwa vitendo vya aina tano za
wanyama: chui, swala, dubu, nyani na ndege. Watu wanaofanya mchezo huo
wananyoosha mishipa, kuongeza mzunguko wa damu, kuongeza uwezo wa kujikinga na
maradhi. Wanafunzi wa Huatuo walikuwa wengi, na kati yao watatu walikuwa
maarufu ambao walitoa mchango mkubwa katika tiba ya Kichina. Baada ya Huatuo
kufariki, watu walimjengea mahekalu mengi kumkumbuka katika mahali alipowahi
kutoa matibabu.
Chen Sheng na Wu Guang
Wafanya Uasi
Chen Sheng na Wu Guang
walikuwa ni viongozi mashuhuri wa uasi wa wakulima, uasi ulioongozwa nao
ulikuwa mkubwa na wa kwanza katika historia ya China ambao ulizuka katika karne
ya tatu mwishoni mwa Enzi ya Qin.
Mwaka 210 mfalme wa
kwanza wa Enzi ya Qin alifariki, mtoto wake Hu Hai alirithi kiti cha ufalme.
Mfalme Hu Hai alikuwa
mpumbavu, chini ya utawala wake raia waliishi vibaya na kutozwa kodi nyingi.
Mwaka 209 mfalme Hu
Hai aliamuru wakulima 900 kwenda kulinda mji wa Yu Yang (wilaya ya Miyun karibu
na Beijing).
Chen Sheng aliteuliwa
kuwa kiongozi wa wakulima hao. Lakini walipokuwa njiani walizuiliwa na mvua
kubwa, walikuwa hawawezi kufika mji wa Yu Yang kwa wakati uliopangwa. Kutokana
sheria, wangechelewa wote wangeuawa. Chen Sheng na Wu Guang aliwaambia wakulima
kuwa ni afadhali kufanya uasi kuliko kuuawa. Wakulima hao waliwachagua Cheng
Sheng kuwa jemadari na Wu Guang kuwa msaidizi wake na kuunda jeshi la kwanza la
wakulima katika historia ya China.
Katika muda mfupi
jeshi hilo liliteka miji sita mikuu ya wilaya na popote jeshi hilo lilipopita
raia waliliunga mkono na kujiunga nalo. Jeshi hilo lilikuwa na askari wengi
siku hadi siku na kuwa jeshi kubwa lenye askari laki kadhaa.
Jeshi hilo
liligawanyika katika sehemu tatu, wakati jeshi hilo lilipokuwa na askari laki
kadhaa walianza kushambulia mji mkuu wa Enzi ya Qin.
Mfalme Hu Hai
alishikwa na hofu wakati jeshi la Cheng Sheng na Wu Guang lilipokaribia mji
mkuu, alihamisha askari laki kadhaa kuja mji mkuu na kushirikiana na jeshi la
kifalme kupambana na jeshi la uasi kutoka mbele na nyuma, na Wu Guang aliuawa.
Mwezi Desemba mwaka 209 Cheng Sheng pia aliuawa katika pambano kali na jeshi la
Enzi ya Qin.
Ingawa viongozi wa
uasi huo Chen Sheng na Wu Guang wate waliuawa, lakini askari wao walijiunga na
jeshi jingine lililoongozwa na Xiang Yu na Liu Bang na kuendelea kupambana na
jeshi la Enzi ya Qin. Mwaka 206 Enzi ya Qin iliangushwa na jeshi la uasi la
wakulima.
Wang Zhaojun
Katika historia ya
kale ya China migogoro kati ya kabila la Wahan na makabila mengine ikitokea,
ilikuwa inatatuliwa kwa vita, lakini pia iliwahi kutokea njia nyingine ya
kutatua migogoro kati ya makabila, nayo ni kumwoza binti wa mfalme kwenye
kabila jingine na kupata urafiki na kabila hilo.
Karne ya kwanza
ilikuwa ni kipindi cha Enzi ya Han. Kabila la Waxiongnu lililokuwa katika
sehemu ya kusini magharibi ya China lilikumbwa na migogoro kutokana na watemi
kugombea madaraka. Wakati huo mtemi mmoja aliyejulikana kwa jina la Han Xie
alikuja kwa mfalme wa Enzi ya Han kuomba msaada. Mfalme wa Enzi ya Han
alimkaribisha kwa ukarimu na alimsaidia kwa nafaka nyingi, na baada ya kurudi
alifanikiwa kupata utawala wa kabila la Waxiongnu.
Ili kupata urafiki wa
daima mwaka 33 K.K. Han Xie kwa mara nyingine alikuja mji mkuu kuonana na
mfalme na kuomba amwoe binti yake. Mfalme wa Enzi ya Han mara alikubali ombi
lake. Mfalme aliwaambia vijakazi wake "kati yenu atakayekubali kuwa mke wa
mfalme wa kabila la Xiongnu atakuwa binti yangu."
Kulikuwa na msichana
mmoja mwenye sura nzuri na werevu, aliitwa Wang Zhaojun. Msichana huyo alikuwa
mwerevu na kupenda kusoma, aliweza kutunga mashairi na kupiga kinanda,
alikubali kuolewa na mfalme wa kabila la Waxiongnu kwa ajili ya urafiki wa
makabila mawili.
Kwa kusindikizwa na
maofisa wa Enzi ya Han Wang Zhaojun alisafiri mbali na kufika sehemu ya kabila
la Waxiongnu. Mwanzoni maisha ya kabila hilo yalikuwa magumu kwake lakini baada
ya muda alizoea na kuishi vema na Waxiongnu.
Yanzi
Katika kitabu maarufu
cha "Rekodi ya Historia" kilichoandikwa na Simaqian, walielezwa
wanadiplomasia kadhaa mashuhuri, mmoja wao alikuwa Yan Zi aliyeishi katika
karne ya sita.
Kipindi kati ya mwaka
770 K.K. hadi 481 K.K. katika historia ya China kinaitwa kipindi cha Spring na
Autumn. Wakati huo utawala wa Enzi ya Zhou ulikuwa umeanza kudhoofika, madola
yaliyo chini ya himaya kake aylikuwa yanapigana kugombea ardhi na mwishowe
yalitokea madola kadhaa yenye nguvu kubwa, na pia walitokea wanasiasa
mashuhuri. Yan Zi alikukwa mmojawapo.
Kwa mujibu wa
maandishi ya historia, kimo cha Yan Zi kilikuwa mita moja na sentimita arobaini
tu, lakini elimu yake ilikuwa pana na alikukwa mtu mwerevu na mcheshi.
Yan Zi aliwahi kwenda
kwenye madola mengine mara nyingi akiwa mjumbe wa Dola la Qi, kati ya safari
zake, hadithi katika safari mbili alipokuwa katika Dola la Chu zilikuwa
maarufu. Mfalme wa Dola la Chu alijua yeye ni mbilikimo, alitaka kumdhihaki.
Katika safari ya kwanza alipokuwa kwenye Dola la Chu mfalme aliamuru watu wake
wamwingize mjini kutoka kwenye kilango kidogo pembeni mwa lango kubwa. Yan Zi
alielewa mfalme Chu akitaka kumdhalilisha, alikataa kabisa na kusema,
"Nikifika kwenye dola la mbwa nitaingia kwenye kilango cha mbwa, sasa
nimekuja kwenye dola la Chu nikiwa mjumbe wa dola, niwezaje kuingia mjini
kupitia kilango cha mbwa!" Walinzi walikuwa hawana budi ila kumpitisha
kutoka kwneye mlango mkubwa. Mfalme wa Chu alipokutana na Yan Zi alimwuliza kwa
makusudi: "Kwani dola la Qi linashindwa kumchagua mtu mwingine aje kwenye
dola la Chu badala yako?" Yan Zi alimjibu kwa utaratibu, "Dola la Qi
lina mazoea ya kutuma wajumbe wenye maadili mema kwenye madola yenye maadili
mema, na kutuma wajumbe wapumbavu kwenye madola ya wapumbavu. Mimi ni mpumbavu
kabisa kati ya wajumbe wote, ndio maana nimetumwa hapa."
Safari ya pili
alipokwenda kwenye dola la Chu, mfalme wa Chu alitaka kumwaibisha Yan Zi
hadharani. Wakati mfalme wa Chu alipomkaribisha kwenye chakula, ghafla askari
wawili walileta mtu mmoja aliyefungwa kamba mbele ya mfalme, wakisema mtu huyo
ni mtu wa dola la Qi, aliiba mali yao. Mfalme alimtupia macho Yan Zi akisema,
"Kwani watu wa dola la Qi walizaliwa na wezi?" Mwerevu Yan Zi mara
alikumbuka mto Huaihe uliokuwa mpaka wa madola mawili, alitumia michungwa
kumjibu mfalme: "Machungwa yaliyopatikana kwenye ukingo wa kusini wa mto
ni matamu, lakini yaliyoko kwenye ukingo wa kaskazini ni machungu, sababu
udongo wenyewe ni tofauti. Watu wanaoishi katika dola la Qi hawaibi, lakini
wanaoishi katika dola la Chu wana tabia ya kuiba, kwani ardhi ya Chu inalea
wizi?"
Mambo kama hayo
yalikuwa mengi ambayo Yan Zi aliwashinda wapinzani wake waliojaribu kumdhihaki
na kuharibu heshima ya dola lake. Alikuwa mwanadiplomasia mashuhuri katika
hitoria ya China.
Su Wu
Kuna hadithi moja
kuhusu Su Wu nchini China, nayo ni hadithi ya "Mchugaji Kondoo Su Wu".
Su Wu alikuwa mtu wa
Enzi ya Han katika karne ya kwanza. Ili kuweka urafiki na kabila la Waxiongnu
lililoko katika sehemu ya kaskazini magharibi ya China Su Wu alitumwa na mfalme
kwenda kwa Waxiongnu akiwa na zawadi nyingi, na baada ya kumaliza kazi aliyopewa
na mfalme tayari kurudi nyumbani, alibakizwa huko kwa kusingiziwa kuwa
alishiriki katika mgogoro uliotokea ndani ya kabila la hilo, na alilazimishwa
kuhaini Enzi ya Han.
Mwanzoni Su Wu
alishawishiwa kuwa ofisa kwa mshahara mkubwa, lakini Su Wu alikataa, baadaye
aliadhibiwa na Xiongnu kwa kutompa chakula na maji. Siku zilikwenda, Su Wu
alifungiwa ndani ya shimo, akiwa na kiu alikula theluji, akiwa na njaa alikula
koti lake ya ngozi. Mwishowe aliachiwa huru kutokana na nia yake thabiti ya
kutohaini Enzi yake ya Han. Lakini hakuruhusiwa kurudi nyumbani bali
alifukuziwa mbali kwenye sehemu ya baridi Siberia kuchunga kondoo, aliambiwa
kuwa ataruhusiwa kurudi nyumbani pindi kondoo dume akizaa.
Su Wu alifukuziwa
kando ya ziwa la Baikal na kuchunga kondoo kwa miaka nenda miaka rudi, nywele
zikawa na mvi na ndevu zikawa nyeupe.
Aliishi kwenye ziwa la
Baikal miaka 19. katika muda wa miaka zaidi ya kumi mfalme aliyemfukuzia
alikufa, na mfalme wake wa Enzi ya Han pia alifariki, aliyeathiri kiti cha
ufalme alikuwa mtoto wake. Wakati huo mfalme mpya alitekeleza sera mpya na
mfalme huyo mpya alimtuma mtu kumrudisha Su Wu nyumbani.
Su Wu alikaribishwa
kwa shangwe na wananchi katika mji mkuu wa Enzi ya Han, maofisa wa serikali
walimheshimu kutokana na uzalendo wake.
Guan Zhong na Bao
Shuya
Guan Zhong na Bao
Shuya walikuwa wanasiasa katika karne ya saba na walikuwa marafiki. Guan Zhong
alikuwa maskini na Bao Shuya alikuwa tajiri, na hao wawili walifahamiana na
kuamiana na hata walishirikiana kufanya biashara, kutokana na umaskini Guan
Zhong alitoa raslimali chache, lakini walipogawana faida alipewa pesa nyingi
zaidi kuliko Bao Shuya ili aweze kuwatunza jamaa zake.
Baadaye watu hao
wawili wote walishiriki katika mambo ya siasa, ambayo wote wawili
waliwafundisha watoto wawili wa mfalme wa Dola la Qi katika madola mengine
tofauti. Baadaye uasi ulitokea katika Dola la Qi, mfalme aliuawa. Baada ya
kusikia habari kuhusu kifo cha baba yao, watoto wote wawili walikimbilia
nyumbani dola la Qi ili kurithi kiti cha ufalme. Njiani mtoto Qi Huan Gong na
ndugu yake walikutana. Guan Zhong alimfyatulia mshale Qi Huan Gong ili ndugu wa
Qi Huan Gong apate nafasi ya ufalme. Mshale huo ulimkwaruza tu Qi Huan Gong
kiunoni, lakini alijidai kuwa amepigwa na kuanguka kama amekufa. Ndugu yake
alidhani amekwisha kufa, na kiti cha utawala hakika kitakuwa chake, akapunguza
mwendo wa safari. Lakini Qi Huan Gong hakuumia, aliharakisha safari yake usiku
na mchana na alifika nchini mapema kwa siku sita kuliko ndugu yake, mawaziri
walimwunga mkono awe mtawala wa dola la Qi.
Baada ya kuwa mfalme
wa dola la Qi, Qi Huan Gong aliwapokea watu wengi wenye busara hata hakuwa na
kinyongo na yule Guan Zhong aliyemfyatulia mshale na kumteua kuwa waziri wa
dola lake.
Guan Zhong alikuwa
waziri kwa miaka mingi na alitoa mchango mkubwa kwa ajili ya kuimarisha dola
lake.
Bao Shuya alipofariki,
Guan Zhong alilia sana mbele ya kaburi lake, alisema, "nilizaliwa na mama
yangu lakini aliyenielewa ni Bao Shuya!"
Mfalme Chu Zhuangwang
China ni nchi yenye
uvumilivu mkubwa, watu wanaona kuwa uvumilivu unaweza kuyeyusha fitina. Hadithi
ya "kuondoa kishungi kwenye kofia" inawafundisha watu wenye uvumilivu
watalipwa mema.
Katika kipindi cha
Spring na Autumn, karne ya saba, kulikuwa na madola mengi kwa wakati mmoja.
Mfalme wa Dola la Chu, Chu Zhuangwang alikuwa mwerevu, na chini ya utawala wake
dola hilo liliimarika sana.
Siku moja, mfalme Chu
Zhuangwang aliwakaribisha maofisa kwenye chakula na kuburudika kwa nyimbo na
ngoma. Giza lilikuwa linaingia, mfalme aliwaambia kuwasha mishumaa. Watu
walikula na kunywa kwa furaha.
Ghafla upepo ulivuma,
mishumaa ilizimika, wakati huo mke wa mfalme alisikia kuna mkono mmoja
ulimshika shika, mke wa mfalme alighadhabika akang'oa kishungi cha kofia ya
yule aliyemtomasa, akaenda kwa mfalme na kumnong'oneza, "washa mishumaa na
kuona kama nani alikosa kishungi kwenye kufia na kumwadhibu." Lakini
mfalme alipaaza sauti na kusema, "Msiwashe mishumaa, ni furaha pekee
kunywa pombe gizani." Baadaye mfalme aliwauliza maofisa, "Mnafurahia
chakula?" wote walijibu "Ndio!" Mfalme aliendelea, "kama
kweli mnafurahia chakula, basi ng'oeni vishungi kwenye kofia zenu!" wote
waling'oa. Kisha mfalme aliwaambia wawashe mishumaa. Maofisa walipoona kofia
zote zilibadilika sura wote walicheka, waliendelea kula na kunywa mpaka
kupambazuka.
Baada ya kurudi kwenye
kasri la kifalme, mke wa mfalme alihasirika sana alisema, "Wewe mfalme
unawadekeza sana maofisa, hivyo utashindwa kuwatawala." Mfalme alicheka na
kusema, "Nawakaribisha maofisa kwenye chakula kwa lengo la kuwafurahisha.
Ni jambo la kawaida kwa mtu akizidiwa na pombe na kufanya kitendo kisicho cha
kawaida. Nikimwadhibu ofisa huyo kwa jambo hilo dogo nitaharibu furaha na
kuwafedhehesha maofisa. Hilo silo lengo la kuwaandalia chakula."
Baadaye dola la Chu
lilishambulia dola la Zheng. Kulikuwa na jemadari mmoja aliyekuwa shupavu
mkubwa katika mapambano dhidi ya askari wa dola la Chu, na alifanya
mashambulizi mpaka karibu na mji mkuu wa dola la Chu. Jemadari huyo ndiye
aliyemshikashika mke wa mfalme wa dola la Chu.
Hadithi ya
"kuondoa kishungi kofiani" inawaambia watu wawe wavumilivu.
Yu Boya na Zhong Ziqi
Katika kipindi cha
Spring na Autumn, katika dola la Chu kulikuwa mwanamuziki mmoja ajulikanaye kwa
jina la Yu Boya. Huyu Yu Boya alikuwa mwerevu toka alipokuwa mtoto, na alipenda
sana muziki. Baadaye alijifunza kupiga kinanda kwa mwalimu wake Lian Cheng.
Baada ya kujifunza kwa
miaka mitatu, alikuwa mwanamuziki mashuhuri, lakini Yu Boya hakuridhika, aliona
kiwango chake kilikuwa bado si kikubwa kileleni. Mwalimu wake Lian Cheng
alifahamu Yu Boya aliyofikiri moyoni, alimwambia kwamba atamwongoza kwa mwalimu
wake ambaye ufahamu wake wa muziki ni wa juu sana. Yu Boya alikubali.
Baada ya kutayarisha
chakula cha kutosha hao wawili walipanda mashua na kufika kwenye mlima wa
Penglai. Mwalimu wake Lian Cheng alimwambaia, "Nisubiri hapa, nakwenda
kumtafuta mwalimu wangu." kisha akaondoka. Siku nyingi zilipita, lakini
mwalimu wake Lian Cheng hakurudi. Boya aliangalia bahari isiyo na mwisho na
misitu mlimani alihuzunika sana, kwa kusukumwa na moyo alipiga kinanda chake.
Muziki ulijaa huzuni, lakini tokea hapo alikuwa mwanamuziki mkubwa. Kwa kweli
mwalimu wake Lian Cheng alifanya hivyo kwa makusudi ili Yu Boya apate hisia za
kweli moyoni.
Kuishi katika kisiwa
kilichojitenga, usiku na mchana kitu alichoona ni bahari, ndege na misitu, siku
nenda siku rudi hisia zake zilibadilika na kuelewa zaidi muziki, alitunga
muziki maarufu uliowagusa mioyo wasikilizaji. Yu Boya alikuwa mwanamuziki
mkubwa, lakini watu waliofahamu muziki wake walikuwa wachache.
Siku moja Yu Boya
alisafiri kwa mashua, alipofika karibu na mlima, mvua kubwa ilinyesha,
aliegesha mashua yake kukimbia mvua. sauti ya mvua na mandhari nzuri ya ukungu
uliokuwa kwenye uso wa mto ilimsisimua, alipata msukumo wa kupiga kinanda.
Muziki alioupiga ulikuwa ni sauti kutoka moyoni mwake. Kulikuwa na mtu mmoja
kwenye ukingo wa mto akisikiliza muziki wake, mtu huyo aliitwa Zhong Ziqi.
Baada ya kusalimiana
Yu Boya alimkaribisha Zhong Ziqi ndani ya mashua yake na kumpigia muziki. Zhong
Ziqi alisikiliza kwa msisimko. Yu Boya alisema, "Katika dunia hii ni wewe
tu unayefahamu sauti ya moyoni mwangu, wewe ndiye mwelewa sauti yangu!"
Hao wawili walikuwa ndugu wa kuchanjiana.
Yu Boya aliahidiana na
Zhong Ziqi kuwa watakutana baadaye. Siku moja Yu Boya alikwenda kwa Zhong Ziqi
kama walivyoahidiana, lakini wakati huo Zhong Ziqi alikuwa amefariki. Baada ya
kusikia habari hiyo Yu Boya alikimbilia kwenye kaburi la Zhong Ziqi na kumpigia
muziki kwa huzuni kubwa, kisha alisimama na kuvunja kabisa kinanda chake. Tokea
hapo Yu Boya aliacha kabisa kupiga kinanda.
Sun Wu
Sun Wu aliyeishi
katika karne ya sita K.K. ni mtu maarufu sana nchini na duniani, kitabu chake
cha "Mbinu za Kivita za Sun Zi" kilikuwa ni maandishi makubwa ya
kivita katika China ya kale.
Sun Wu alizaliwa mwaka
551 K.K. kilikuwa ni kipindi cha Spring na Autumn katika historia ya China.
Alikuwa mtu wa dola la Qi, alipokuwa na umri wa miaka 19 alikwenda dola la Wu,
na katika kiunga cha mji mkuu wa dola la Wu (mji wa Suzhou wa leo) aliandika
kitabu chake cha mbinu za kivita na kumpa mfalme wa dola la Wu. Mfalme
alifurahi sana, lakini hakujua kama mbinu zenyewe zinaweza kutumika, alimtaka
Sun Wu afanye mazoezi kwa masuria waliokuwa ndani ya kasri la kifalme.
Sun Wu aliwagawa
masuria 180 kwa vikundi viwili na kuwateua wawili waliopendwa sana na mfalme
kuwa viongozi wa vikundi viwili, kimoja kulia na kingine kushoto, na kufanya
mazoezi.
Sun Wu alisimama
kwenye jukwaa na kuwafahamisha mpango wa mazoezi yake. Sun Wu alipiga ngoma ya
kuanzisha mazoezi. Lakini masuria walikuwa kama hawajasikia mdundo wa ngoma,
bali walichekacheka na kuchezacheza, safu zao zilivurugika, ingawa Sun Wu
aliwaasa mara kadhaa, lakini haikusaidia kitu. Kutokana na hali hiyo, Sun Wu
aliamuru kuwaua viongozi wawili.
Mfalme alipoona kweli
Sun Wu alitaka kuwaua wapendwa wake wawili alimsihi awaache. Lakini Sun Wu
hakubali ombi la mfalme, aliwaua. Kisha akaanza tena mazoezi, safari hii
masuria walifanya mazoezi kwa makini, walipiga hatua mbele na nyuma,
waliviringika na kutambaa kifudi fudi, kila mmoja alifanya vizuri. Kuona hali
hiyo mfalme alifurahi, akamteua Sun Wu kuwa jemadari.
Chini ya uongozi wa
Sun Wu jeshi la dola la Wu lilikuwa hodari sana na lilipata ushindi kila mara katika
vita vya kupigana na madola mengine.
Mwaka 482 K.K. mfalme
wa dola la Wu alikuwa mbabe kati ya madola yote kutokana na mbinu
zilizoandaliwa na Sun Wu.
Kutokana na ushindi,
mfalme alikuwa anavimba kichwa. Kwa kuona jinsi mfalme alivyokuwa, Sun Wu aliondoka
na kuishi mbali na mfalme milimani.
Kitabu cha "Mbinu
za Kivita za Sun Zi" ingawa kilikuwa na maneno elfu 6 katika makala 13,
lakini kilionesha kikamilifu mbinu zake za kivita. Kitabu hicho kilisifiwa na
watu wa baadaye kuwa ni "kitabu cha kwanza duniani kuhusu mbinu za
kivita", na kilitumika sana katika mambo ya kijeshi, kisiasa na uchumi.
Qi Jiguang
Katika mlima wa Yu
Shan mkoani Fujian kuna hekalu moja lililowekwa sanamu ya Qi Jiguang, watalii
wanapofika huko hawakosi kwenda kutoa heshima kwake kutokana na uzalendo wake
na mchango wake katika mapambano dhidi ya wavamizi.
Qi Jiguang alikuwa
jemadari katika Enzi ya Ming, alizaliwa katika ukoo wa jemadari. Kwa kuathiriwa
na baba yake, Qi Jiguang toka alipokuwa mtoto alipenda sana mambo ya kijeshi na
kuwa na nia ya kuwa mwanajeshi hodari. Wakati huo wavamizi wa Japan walikuwa
mara kwa mara wanashambulia China. Alipokuwa na umri wa miaka 17 alirithi
wadhifa wa baba yake na kuanza maisha yake ya kijeshi. Alipokuwa tu jemadari
tatizo lililomkabili lilikuwa ni mashambulizi ya Japan.
Tokea mwishoni mwa
Enzi ya Yuan na mwanzoni mwa Enzi ya Ming maharamia wa Japan mara kwa mara
walikuwa wakipora mali na kuua watu kwenye mwambao. Katika nusu ya pili ya
karne ya 15 maharamia wa Japan walikuwa wanashirikiana na wafanyabiashara
wabaya wa China kufanya uovu.
Mwaka 1555 Qi Jiguang
alitumwa kwenye mwambao, aliunda jeshi la wakulima na wachimba migodi.
Walitumia mishale na mikuki kuwaua baada ya kuwatega mitegoni.
Jeshi lake lilikuwa na
askari elfu 4, na baada ya kuwafundisha na kuwafahamisha askari mbinu za
kivita, jeshi hilo lilikuwa hodari sana, na kutokana na kuwa na nidhamu kali
liliungwa mkono na wananchi.
Mwaka 1561 maharamia
wa Japan elfu kadhaa na mashua zaidi ya mia walifanya mashambulizi katika sehemu
ya Taizhou mkoani Zhejiang. Qi Jiguang kwa haraka aliwaongoza askari wake
kupambana nao na kuwaangamiza maharamia wote.
Kutokana na juhudi za
Qi Jiguang na majemadari wengine, maharamia wa Japan walitoweka, mikoa ya
Zhejiang na Fujian ilikuwa tulivu, na uchumi ulistawi. Qi Jiguang alitoa
mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya maharamia wa Japan na alisifiwa sana
na watu wa China.
Chanzo: http://swahili.cri.cn
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni