Mtayarishaji

Morning Star Radio

Ijumaa, Januari 17, 2014

ANGUKO LA MARCUS GARVEY KIELELEZO CHA MTU MWEUSI KUTOJITAMBUA

Marcus Garvey


Katika kuiweka falsafa yake Garveyism hai, Marcus Garvey alihimiza wamarekani weusi chini ya umoja wao wa UNIA (Universal Negro Improvement Association) badala ya kulalama kwa watesi wao waanzishe miradi itakayowapa ajira na kuonyesha kwamba mweusi anao uwezo wakufanya yale yote watesi wao wanayoyafanya.

Miradi walioianzisha ni pamoja na Makampuni ya uchapaji wa magazeti, Migahawa, vituo vya afya, Vituo vya mashine za kuoshea nguo, kumbi za mikutano na Shirika la kwanza la Watu weusi la Meli lililojulikana kama Black Star Line mwaka 1919.

Shirika la meli mbali na kulianzisha kufanya biashara na kutoa ajira lilikuwa na lengo jingine la kuwarudisha watu weusi barani Afrika (Back to Africa Movement). Mwaka 1920 ikiwa ni mwaka mmoja toka kuanzishwa shirika la meli, UNIA chini ya Garvey waliitisha kongamano la kwanza la kimataifa la watu weusi mwezi mzima wa August lililopewa jina la “The First International Convention of the Negro Peoples of the World”. Kongamano lilijumuisha weusi toka Marekani, Canada, Amerika Kusini na Afrika Magharibi.

Kutokana na ushawishi wa Garvey, Wamarekani weusi wengi walianza kujiunga na umoja wa UNIA na walipoanzisha shirika la meli serikali ya Marekani ilistuka na ikaanza mipango ya kuwahujumu akina Garvey chini ya kitengo cha Upelelezi cha Marekani cha Bureau of Investigation kwa sasa ni FBI.

KUKAMATWA, KUFUNGWA NA KURUDISHWA JAMICA

Utengenezaji wa kesi unaonyeshwa kwenye memo ya FBI iliyoandikwa na J. Edgar Hoover, msaidizi wa Mwanasheria mkuu wa Marekani mwaka 1919 kwamba hakuna ushahidi wowote unaonyesha kwamba Garvey ametenda makosa yanayoweza kuifanya serikali ya shirikisho kumtia hatiani kisha kumrudisha kwao Jamaica.

Mwaka 1919 FBI waliajili mashushu wa kwanza weusi James Edward Amos, Arthur Lowell Brent, Thomas Leon Jefferson, James Wormley Jones, and Earl E. Titus ambao kazi yao ilikuwa kujiunga na umoja wa Garvey wa UNIA kupenyeza vibaraka wengine ili waweze kupata ushaidi wowote wa kumfungulia kesi Garvey na kumrudisha kwao Jamaica.

HUJUMA DHIDI YA GARVEY

Wakati wa ununuzi wa meli UNIA chini ya Garvey walimtuma mwanachama na mhandisi wa umekaniki wa meli mweusi Kpt. Joshua Cockburn kwenda kuikagua meli ili waweze kushauliana kuhusu bei ya manunuzi ya meli yao ya kwanza iliyojulikana kama Yarmouth. Mhandisi huyo alishafanywa kibaraka wa FBI hivyo alirudisha ripoti ya ukaguzi wa meli kwamba ni nzuri wakati akijua ni mbovu ilipagana vita ya kwanza ya dunia.

Katika manunuzi ya meli bei alitaja mara sita zaidi ya bei halisi ya meli hiyo. Bei halisi ya meli ilikuwa haizidi dola 25,000 lakini yeye alimwambia Garvey kwamba bei yake ni dola 165,000 na umoja wa UNIA ukalipa bei hiyo. Mhadisi Kpt Joshua Cockburn alilipa dola 25,000 na iliyobaki akaweka mfukoni. Haya yote aliyafanya akiwa na mgongo wa FBI.

Meli ya pili The "S. S. Shadyside” ilinunuliwa kwa dola 200,000 gharama isiyostahili kwa mtindo kama ule wa meli ya kwanza kwa weusi wanaotumwa kukagua na kushauriana bei kuongeza dau lao na huku wakijua meli ni mbovu. Meli hii ilizama kwenye mto wa Hudson ikiwa na abiria weusi wamarekani.

Baadhi ya wafanyakazi wa meli wengi walifanywa vibaraka wa FBI hivyo kwa maelekezo ya FBI walipewa vitu vya kuweka kwenye injini za meli ili ziharibike. Meli ya tatu "S. S. Antonio Maceo" ililipuka injini kutokana na hujuma hizo.

Wafanyakazi wa meli hawakuzisimamia vizuri mfano meli ya Kwanza Yarmouth ilipakia mizigo kwenda Cuba kabla ya vikwazo bila vibali vya kuifanya itie nanga. Muda wote ilikaa kwenye mwambao bila kutia nanga matokeo yake vitu vikaharibika. Na hili pia linahusishwa na FBI kwa kuwapa maelekezo watu waliokuwa kwenye mamlaka ya kufanya hivyo.

Miaka mitatu toka shirika la meli kuanzishwa weusi wakaliua wenyewe, likafilisika. Shirika likawa mhanga wa kubambikiziwa bei na wahandisi, wizi wa wawakilishi na maofisa wa UNIA bila kusahau hujuma za FBI. Biashara nyingine pia weusi walikuwa wanafuja mali zake. Hapa FBI wakaanza kutengeneza kesi kumtia hatiani Marcus Garvey.

Februari mwaka 1922 Marcus Garvey alitangaza kusitishwa kwa shughuli za Black Star Line baada ya FBI kumfungulia mashtaka ya njama za kutapeli kwa njia ya barua (mail fraud).

MASHTAKA DHIDI YA GARVEY

Garvey alishitakiwa kwa njama za kutapeli kutumia barua na kesi ya FBI dhidi yake ilijikita kwenye barua zilizokuwa zinatumwa kwa wamarekani weusi zikiwa na picha ya meli wakati meli zenyewe zilikuwa hazijanunuliwa.

Vipeperushi vilivokuwa vikitumwa vilikuwa na lengo la kuwahimiza wanachama kuchangia kuanzisha biashara na mrejesho wake kuwa asilimia ya kiasi cha mtu alichochanga. Hivyo biashara zao hazikuwa biashara kama biashara nyingine kampuni kutangaza kuuza hisa bali watu wanaoamua kuanzisha umoja ili kujiinua kiuchumi na mambo mengine ya kijamii.

FBI waliandaa mashaidi weusi na kuwatengenezea ushaidi watakaoutoa mahakamani kuonyesha kwamba ile miradi ilikuwa ya Marcus Garvey ili kuweza kumuhukumu Garvey. Wengine walikuja kusema kwamba walilaghaiwa na FBI wakati huo tayari Garvey anatumikia kifungo gerezani cha miaka mitano.

Mwendesha mashtaka msaidizi wa New York ndiye alikuwa shahidi namba moja wa FBI na ikumbukwe kwamba mwendesha mashtaka huyo ndiye alikuwa mwanasheria wa kampuni iliyowauzia akina Garvey meli ya kwanza. Alikuwa akijua mchezo wote uliochezwa na Kpt Joshua Cockburn wa kuwauzia meli mbovu na bei mara 6 ya gharama ya kawaida.

KUFUNGWA NA MWISHO WA HARAKATI ZAKE

Alifungwa mwezi wa 6 mwaka 1923 miaka mitano na lakini alianza kutumikia kifungo chake mwaka 1925 baada ya rufaa zake kutupwa. Alipewa msamaha na rais mwaka 1927 na kurudishwa Jamaica. Huo ndio ukawa mwisho wa harakati zake. Badae aliamia Uingereza na kufariki mwaka 1940 jijini London.

Anguko lake ni kutokana na watu weusi kutojitambua kama ilivyo sasa kwenye nchi nyingi za kiafrika. Wachambuzi wa historia wanasema harakati zake ndo zilimhukumu na si mashtaka ya ulaghai.


Chanzo: tudadisiforums

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni