Sifa za mtu aliyekomaa
1. Anayatambua mambo yalivyo. Anajitambua na kuwatambua wengine walivyo. Anatambua matukio pia katika sifa na kasoro. Anatambua yale anayoyaweza na yale asiyoyaweza. Hana wivu wala hofu. Anapima hali mbalimbali bila ya kufumba macho mbele ya mambo yasiyompendeza bali anatumia akili akabiliane nayo.
2. Anakubali hali ilivyo. Anajikubali na kuwakubali wengine walivyo.
Akiona kasoro hachukii, bali kwanza anakubali hali ilivyo, halafu
anajitahidi kuirekebisha iwezekanavyo. Hata akishindwa anakubali na
kuvumilia. Vilevile anaweza kuyakubali mabadiliko na mambo mapya bila ya
hofu, kwa kuwa anapima yote bila ya kufadhaika kwa kusema, “Itakuwaje?”
3. Anawajibika. Hangoji kuambiwa kila mara afanye nini na vipi, bali
anaona mwenyewe anavyotakiwa kutenda, halafu anaamua kwa moyo ayatende.
Ndiyo sifa kuu ya mtu aliyekomaa kweli: ana mwongozo wa maisha ndani
mwake. Anazingatia pia kanuni za jamii na kusikiliza mashauri, lakini uamuzi wake unatoka ndani.
4 Anajiongoza kwa kuzingatia tunu alizojichagulia. Anaelekeza maisha yake upande fulani alivyoazimia. Katika kuamua la kufanya anafuata tunu hizo, si mkondo kama wanavyofanya kondoo.
5. Anahusiana vema na watu kwa sababu anawakubali, anawaheshimu na kuamini wanaweza kutenda mema. Anaelewa shida zao na kuwatimizia. Anawafanya wajisikie raha na kutokeza sifa zao. Mwenyewe anajisikia salama na kuwafanya washinde hofu zao na hivyo wakomae kwa urahisi zaidi.
6. Anafanikisha mipango. Ana mawazo ya kushangaza kwa kuwa mitazamo
yake ni mipana na ya ndani zaidi. Mipango na miradi yake ni mingi,
lakini haogopi kujaribu wala kushindwa, kwa kuwa anatambua mambo yalivyo
na yanavyoweza kurekebishwa. Hivyo mara nyingi anafaulu kufanya mambo
yawe alivyotaka. Mambo yaliyo magumu kwa wengine, kwake ni rahisi.
7. Anajiendeleza aishi kwa ukamilifu. Anatumia vizuri vipawa vyake vyote. Anafurahia mambo mbalimbali ya maisha na kufaidika nayo ili azidi kujiendeleza
Pande mbalimbali za ukomavu wa mtu
1. Wa maono • anakubali maono yake bila ya kutawaliwa nayo; • anaweza kuyajulisha
ili kusaidiwa; • anakabili magumu bila ya kuyaepa wala kuhangaika mno; •
si mtu wa kujikinga kila mara.
2. Wa nafsi: • anasikiliza wengine, hatimaye anaamua mwenyewe bila ya wasiwasi mkubwa mno; • anaweza kubadili uamuzi wake akipata habari mpya; • anasema ukweli na kuchukua jukumu la uamuzi wake; • anapokea uamuzi wa wengine.
3. Wa jamii:
• anaona wema wa wengine, asijifanye lengo la yote; • anafungamana vema
na wengine; • ana marafiki wa kufaa; • hawategemei mno ndugu zake; •
anafuata taratibu za jumuia; • analinganisha mahitaji yake na ya kikundi chake; • yuko tayari kutimiza sheria halali hata zisipompendeza • anafanya kazi hata ngumu kwa utulivu.
4. Wa maadili: • anapokea mawazo mazuri na kuyaishi; • anafuata malengo yake kwa sababu anayo ya kufaa; • anatimiza busara, haki, nguvu na kiasi; • yuko imara katika imani, tumaini na upendo.
5. Wa roho: • anafungamana vema na Mungu, malaika na watakatifu; • anamtegemea Mungu na kutimiza matakwa yake; • anaelewa wito wake, anauthamini na kudumu kwa hiari kuuitikia
Mambo yanayozuia ukomavu
Binadamu anakusudiwa kukomaa, lakini hafanikiwi sikuzote. Tunawaona watu waliolemaa upande wa mwili, lakini wengi zaidi wamelemaa upande wa nafsi. Sababu ni kwamba mtu akikosa haja zake za msingi hawezi kustawi. Haja hizo zina nguvu sana, nazo zisipotimizwa zinamuacha mtu kilema.
Mambo yanayompata hata akalemaa kinafsi yanaelezwa na mviringo ufuatao usioelekea popote:
1. Hatimiziwi haja za nafsi, ambazo ni za msingi kama zile za mwili, hivyo zisipotimizwa yanaanza matatizo.
2. Hajisikii vizuri, hata kama ni mtoto au haelewi, kwa kuwa mtu akihisi hapendwi, hatakiwi, hayuko salama, basi anajisikia vibaya mpaka ndani.
3. Anapatwa na wasiwasi unaofanya nafsi isistawi, hata kama mwili
unaendelea kukua. Ndiyo sababu anashindwa kushirikiana vizuri na watu au
anajitenga nao kwa kuona hawampi anayoyahitaji.
4. Kutokana na hofu
hashiriki vizuri katika mambo yote. Anatambua kwamba akibaki peke yake
hapati nafasi ya kupendwa, lakini anashindwa kukabili hofu yake.
5. Matokeo yake ni kwamba anajihisi hastahili kutimiziwa haja zake.
Hatimaye anaweza akajichukia kama kwamba ndiye anayesababisha watu
wasimtimizie haja zake.
6. Anafadhaika asijue la kufanya mbele ya matatizo hayo. Anashindwa
kupata jibu kuhusu haja zake kutimizwa kesho: ikiwa leo hapati
anayoyahitaji hata kwa watu wenye wajibu kwake, je, atayapata lini?
7. Anafuata njia za kujikinga
na hofu hizo kusudi asiendelee kufadhaika. Moja ya njia hizo ni
kusukuma ndani kabisa mwa nafsi yake yale yasiyompendeza yasielee tena
katika kumbukumbu; lakini kadiri mambo hayo yalivyoshindiliwa ndani
yanamvuruga na kujitokeza kwa matendo na maneno yasiyotarajiwa. Njia
nyingine ya kujikinga ni kutokubali hali halisi, yaani kukataa kukabili
jambo la hatari au lisilopendeza. Njia nyingine ni kuhamisha dhihirisho
la ono fulani (hasira, chuki n.k.) limlenge mtu tofauti na yule anayekusudiwa. Njia nyingine ni kuishi katika ndoto za mchana
badala ya kuwazia hali halisi: mtu anajichorea akilini picha ya
ulimwengu mwingine ambapo mambo yanakwenda anavyotaka, hata akaamini
ndio wa kweli. Njia nyingine tena ni kujitafutia visingizio ili
kutosikia aibu
moyoni: mtu anaweza akafikia hatua ya kumshtaki mwenzake kwa kosa
alilolifanya mwenyewe. Njia ya mwisho ni kudai kwamba wengine ndiyo
wenye hali aliyonayo mwenyewe asiikubali.
8. Kwa kuwa njia hizo hazimtimizii haja zake, hazimsaidii ila
zinamtuliza kijuujuu tu kwa muda, yaani zinafunika matatizo yake badala
ya kuyatatua. Mtu amejikinga isivyofaa, basi shida
inabaki palepale. Hivyo mviringo usioelekea popote umekamilika kwa
kurudia namba moja: mtu anahitaji bado kupendwa, kukubaliwa, kuthaminiwa
na kuwa salama. Nani atamsaidia?
Dalili za mtu asiyekomaa
1. Anapurukusha tu na kulipua kazi mpaka asimamiwe.
2. Hatimizi vizuri wajibu wake kwa jumla, ni mtegezi.
3. Anachekacheka na kucheza wakati usiofaa.
4. Ana kiburi cha kitoto.
5. Hajui kujiheshimu wala kuwastahi wengine.
6. Ni mbishi, pia kwa makusudi, tena mlalamishi.
7. Hajui kulinda siri za nyumbani, ni mchongezi.
8. Hajali maonyo, anayachukua kimzaha.
9. Hakubali maoni ya wengine.
10. Si mnyofu wala hajui kujieleza wazi alivyo.
11. Anaogopa kutoa mawazo yake mbele ya watu.
12. Haamui kwa utashi imara.
13. Anafuata mkumbo.
14. Katika kuwapenda wenzake ana ubaguzi.
15. Anajipendekeza na kujipendea.
16. Anadai kubembelezwa na kufarijiwa.
17. Hana [[uvumilivu wala moyo mkuu.
18. Anatunza kinyongo.
19. Anakata tamaa kwa urahisi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni